PROFESA MUHONGO AJIONDOA MWENYEWE NISHATI NA MADINI



Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (aliyeshika tama pichani), ametangaza kujiuzulu rasimi wadhifa huo, Jijini  Dar es Salaam leo, kufuatia kashfa nzito ya uchotaji wa Sh. Bilioni 306, zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, inayowakabiri yeye na wenzake.
.
Waziri Muhongo amelazimika kutangaza kujiuzulu leo ikiwa ni siku chache tu kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mjini Dodoma. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema Profesa Muhongo amepita uzito wa kashfa hiyo dhidi yake na kulazimika kujiuzulu kukwepa maswali mengi ya Wabunge.

Sakata hilo ambalo lilimlazimu Rais Jakaya Kikwete kumuondoa aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye awali aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye na Waziri mwenzake Profesa Muhongo, hawawezi kujiuzulu kwa sababu Rais Kikwete atawashangaa kwani anawategemea sana katika majukumu yake.

Pamoja na majigambo hayo ya Profesa Tibaijuka, Rais Kikwete alitangaza kumuondoa kwenye Baraza lake la  Mawaziri, akidai kuwa maelezo na jinsi alivyopokea mapesa hayo kupitia kwenye akaunti yake vinatia shaka, Hata hivyo Rais Kikwete alikimweka Waziri Muhongo kiporo.

Kitendo cha Rais Kikwete kutangaza kuwa Waziri Muhongo amewekwa kiporo, kilichukua sura mpya baada ya wana harakati na wapenda demokrasia nchini, walidai kuwa kiporo cha Profesa Muhongo kilikuwa kimechacha.
 
Uchunguzi wa kina uliofanywa na MPIGANAJI, umebaini kuwa Wabunge bila kujali itikadi ya vyama vyao walikuwa wamejipanga kumshambulia Profesa Muhongona kumshinikiza aachie ngazi. Ni wazi kuwa shinikizo la Wabunge limemsukuma Profesa huyo kuachia ngazi kabla ya kurudi Bungeni.

Kuahirishwa kwa Bunge mjini Dodoma, mwishoni mwa mwaka jana ni kama kulileta ahuweni kwa Mawaziri hao, kwani mijadala yote ya nchi ilisimama huku wabunge wengine wakiwatetea wasiochie ngazi wengine wakisema wezi hao waondoke.

Baada ya kuahirishwa Bunge Mjini Dodoma, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alitangaza kujiondoa mwenyewe na nafasi hiyo kuwa wazi kwa muda kabla ya Rais Kikwete kumteua Mwanasheria Mkuu Mpya.

Hata hivyo, baada ya Profesa Tibaijuka kuwekwa kando na Rais Kikwete, alirudi kwao, mkoani Kagera kama shujaa wa vita akisindikizwa na msururu mrefu wa magari zaidi ya mia moja, ambayo baadhi ya wapenda maendeleo ya nchi yao, walisema mafuta yaliyotumika kwenye msafara huo yangeweza kujenga Maabara za shule kadhaa mkoani humo.

Sasa watanzania wanasubiri kuona, nani ataingia kwenye baraza la mawaziri nani atatoka, kufuatia tetesi na uvumi kuwa Rais Kikwete anapanga kuliwekea viraka baraza hilo.  

Profesa Muhongo ni Waziri wa tatu kujiuzulu kutoa Wizara ya Nisati na Madini, wengine ni Ibrahimu Msabaha, aliyejiuzulu kutokana na sakata la RICHMOND na Wiliam Mganga Ngereja.

WATANZANIA KAZI TUNAYO.... IMEANDIKWA NA MPIGANAJI

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU