UCHU

BIBIANE

Ilikuwa yapata saa nne usiku wakati Willy Gamba alipokuwa akielekea nyumbani kwa Col. Rwivanga, akitokea Centre Christus. Walikuwa wamekubaliana na Col. Rwivanga kuonana baada tu ya Willy kutoka kwa Mapadri. Wakati anakaribia kukata kona kuingia Barabara inayoingia sehemu ya Kimihurura ili aelekee nyumbani kwa Col. Rwivanga alipitwa na gari nyingine aina ya Landrover 110, lililokuwa likienda kasi sana na kama asingekuwa makini katika uendeshaji wangeweza kumgonga maana pamoja na kuonyesha ishara ya taa kuwa anahitaji kuingia kushoto lakini gari hilo lilipita kasi bila kujali ishara ya taa.

"Hawa wanajeshi ndio sababu hupata ajali mara kwa mara, uendeshaji wao ni wa ovyo sana", Willy alijisemea moyoni na kisha akakata kushoto kuelekea nyumbani kwa Col. Rwivanga.

"Endesha kwa tahadhali Felician, tungeweza kumgonga yule mtu ikaleta balaa hata kabla hatujaanza kazi. Kazi yetu ni kummaliza Willy Gamba na wala si kugonga magari ya watu ovyo", Xavier Nkubana alikaripia Felician.

Nkubana na wenzake waliwasili jioni ile mjini Kigali kwa ndege ya serikali ya Tanzania ambayo iliwasili na ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliofika kuchunguza tukio la kulipuliwa kwa ndege ya Tanzania iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya ndege ya Tanzaiar. Ndege hii iliwaleta maafisa kutoka idara ya usalama wa anga, mambo ya nje, polisi na waandishi wa habari. Nkubana na wenzake walifanyiwa mpango na kupanda ndege hii kama wafanyabiashara wa kinyarwanda waishio Tanzania walikuwa wakirudi nyumbani Rwanda kuangalia hali ya nchi ilivyo kwa wakati huu ili kama ikiwezekana waanzishe biashara tena kati ya Tanzania na Rwanda. Waliingia Rwanda bila tatizo lolote na kupokelewa vizuri na viongozi wa serikali ya Rwanda na kupelekwa kwenye Hoteli ya Des Mills Collines. Kwa vile walijulikana kama wafanyabiashara, baada ya kufikishwa hotelini waliachwa ili waendelee na mambo yao, na wale maofisa wa serikali ya Tanzania wakaanza kushugulikiwa na wenzao kuhusu mambo ya hotelina mambo mengine ya kiusalama.

Baada ya kuchukuwa vyumba na kuoga. Nkubana aliondoka na kuelekea nyumbani kwa Co. Gatabazi na kuwaacha wenzake wakipumzika, kwani ratiba yao ya kazi ilikuwa usiku ule ule. Ilikuwa yapata saa moja hivi Nkubana alipowasili nyumbani kwa Col. Gatabazi aliyekuwa akimsubiri.

"Karibu sana", Col. Gatabazi alimkumbatia Nkubana kwani walikuwa hawajaonana kwa muda mrefu.

"Asante, naona mambo mazuri", Nkubana alijibu.

"Mambo mazuri gani haya! Mambo yatakuwa mazuri baada ya sisi wenyewe kuchukuwa madaraka ya nchi hii. Kila siku nasikia uchungu moyoni kuona 'Inyenzi' inazidi kujiimalisha hapa. Lazima mambo yafanyike haraka kabla hawajajizatiti sawasawa, karibu ndani", Col. Gatabazi alijibu huku akiwa ameushikilia mkono wa Nkubana kisha akamwongoza kuelekea sebuleni.

"Utakunywa nini?", Col. Gatabazi alimuuliza.

"Nipe chai kama ipo".

"Tena na mimi sasa hivi nilikuwa nakunywa chai", Col. Gatabazi alijibu na kwenda kuchukuwa chupa ya chai na vikombe viwili vya chai, wakakaa mezani pale sebuleni.

"Karibu".

"Asante sana". Nkubana alichukua kikombe chenye chai na kuanza kunywa.

"Ehee, hamkupata tatizo lolote?".

"Wewe unacheza na mipango ya JKS nini?, atakapokuwa Rais wa Tanzania na wewe hapa mbona tutakula kuku mpaka tuchoke! Tumekuja kwa heshima zote na kupokelewa na 'Inyenzi', na kutupeleka mpaka hotelini. Wangeweza hata kutulipia hoteli lakini sisi tumekataa maana tumekuja kama wafanyabiashara hivyo ni vizuri kujitegemea", Nkubana alijibu.

"Vijana wako katika hali nzuri?".

"Wako na moto kama nini, maana wanataka kumaliza kazi usiku huuhuu, na baada ya hapa tunaelekea Bukavu tukasaidie kupanga mapambano dhidi ya 'Inyenzi', JKS ametueleza mipango yote nasi tumeafiki".

"Hiyo safi, lakini kwanza mambo ya hapa. Huyu Willy Gamba ni mtu hatari kabisa. Inabidi tumfanyie mkakati mzuri. Siyo mtu wa kawaida", Col. Gatabazi alieleza lakini kabla hajajendelea Nkubana alimkata kauli.

"Yaani huna maana sisi watu watano ambao ni sawa na jeshi zima la askari shupavu, bado una wasiwasi? Hivi umesahau kuwa sisi ni makomandoo, tupe mipango tujuwe yuko wapi, kazi ingine tuachie sisi wenyewe", Nkubana alijigamba.

"Imebidi nikutahadharishe kwanza, msije mkamwendea kwa pupa. Ni lazima tupange mipango mathubuti. Inabidi kwanza kueleza nyendo zake kutokana na upelelezi niliofanya toka mambo yaliyotokea juzi usiku", Col. Gatabazi alijibu.

"Sawa endele", Nkubana alijibu huku akionyesha kuwa Col. Gatabazi alikuwa anazidi kupoteza muda kwani anaamini hakuna mtu. Hata awe wa uwezo wa aaina gani asingeweza kutamba mbele ya kikosi chake.

Nkubana alikuwa kati ya askari waliopatiwa mafunzo ya kijeshi na kijasusi kwa pamoja. Alikuwa na cheo cha Meja Jeshini lakini aliingia hata katika kambi za RPF huko Uganda na kuchukuwa habari na ndiye ambaye mara nyingi aliifanya RPF isifanikiwe katika mashambulizi yake kwani yalijulikana mapema. Inasemekana mauaji yote yaliyofanywa kwa watu na wanajeshi waliokuwa wakitoa habari kwa RPF yalifanywa na yeye. Alikuwa jasiri na shupavu lakini uso wake kila siku utadhani wa padri hata namna yake ya kusema akiwa na watu wa kawaida. Pia inasemekana kuwa 'Akazu' walimchagua kufuatilia maofisa ambao baadaye waliwafundisha Intarahamwe, na kuwapa amri kumi ili wazieneze kwa Wahutu. Mhutu yeyote ambaye asingezifuata na kuzitekeleza basi auawe hapohapo.

Na hizi amri kumi za Wahutu zilikuwa kama ifuatavyo.

1. Kila Mhutu ajue kuwa mwanamke wa Kitutsi kokote aliko, yuko kwa manufaa ya watutsi. Kwa       hiyo mtu yeyote atakayeoa, kufanya urafiki au kumwajiri mwanamke wa Kitutsi kama mfanyakazi wake au mkewe basi Mhutu huyo ni msaliti, lazima auawe.

2. Kila Mhutu ajue kuwa ni mwanamke wa Kihutu tu anjayefaa kama mke, kama rafiki na kama mfanyakazi wake ofisini.

3. Wanawake wote wa Kihutu lazima wewe imara na wawahamasishe waume zao, kaka zao na watoto wao wa kiume kumchukia Mtutsi.

4. Kila Mhutu lazima ajue kuwa Mtutsi yeyote si mwaminifu katika biashara. Hivyo, Mhutu anayefanya biashara na Mtutsi, anayewekeza fedha zake au za serikali katika kampuni za Kitutsi, anayekopesha ama kukopa kwa Mtutsi, anayewasaidia wafanyabiashara wa Kitutsi ni msaliti, anatakiwa kuuawa.

5. Kazi zote za juu katika siasa, utawala, uchumi, jeshi na usalama lazima wapewe Wahutu.

6. Katika sekta ya elimu (walimu, watoto wa shule na nguo), lazima wengi wawe Wahutu.

7. Jjeshi la Rwanda liwe kwa Wahutu tu. Na mwanajeshi haruhusiwi kuona Mtutsi.

8. Wahutu waache kuwaonea huruma Watutsi, unyama unyama tu dhidi ya Watutsi.

9. Wahutu popote walipo duniani lazima wawe na umoja kwa kila njia na wajaribu kuzima propaganda za Watutsi na kuungana katika kuwaangamiza Watutsi.

10. Mapinduzi ya kijani ya mwaka 1959 na itikadi za Kihutu lazima zifundishwe kwa kila Mhutu. Na Mhutu yeyote anayemwonea Mhutu mwenzake kwa kueneza itikadi hizi basi huyo Mhutu auawe, maana ni msaliti.

Kwa kutumia askari wa vikosi alivyovifundisha Nkubana alihakikisha kuwa amri hizi zinatekelezwa na zinachochea chuki ya Wahutu dhidi ya Watutsi kama alivyoagizwa na Akazu.

Huyu ndiye Nkubana, mtu jasiri, aliyehitimu katika shule mbalimbali za kijeshi, kijasusi na kikomandoo ulimwenguni, lakini mafunzo yake yote yalikuwa ya dhamira moja tu, ya kuhakikisha kuwa utawala wa Kihutu uliokuwa madarakani unaendelea kutawala milele na milele kwa njia moja tu kuhakikisha Watutsi wote wanafyekwa ili wasiwepo tena duniani. Hivyo, kwake mtu yeyote aliyemuunga mkono Mtutsi lazima afe na yeyote aliyesaidia Mhutu basi yeye Nkubana alimsaidia kwa lolote. Hivyo ndivyo walivyoweza kuelewana na kundi la Jean kwani lilikuwa upande wa Akazu. Na habari za Willy Gamba kuwa alikuwa anajaribu kuharibu mipango ya Wahutu kurudi madarakani, zilimuudhi sana na kusikia hasira isiyo kifani dhidi ya Willy Gamba.

"Lazima usiku huu huu afe", Nkubana alijishitukia amesema kwa hasira hata Col. Gatabazi aliyekuwa ameanza kueleza mipango akashituka. Akashtuka.

"Haya sasa endelea, huyu mtu ameniudhi sanasana, tayari hukumu yake ya kifo imeshapita".

Col. Gatabazi ilibidi aanze upya kumpa mipango ya usiku ule kama walivyokuwa wamepanga na Jean na JKS.


ITAENDELEA 0784296253    

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU