UCHUNGUVU YA RUSHWA

V

Baada ya Col. Gatabazi kuvaa nguo vizuri, walichukua silaha mbalimbali na fedha zilizokuwa pale ndani. Wote walivaa mavazi ya kijeshi na kutumia gari ndogo aina ya MB 230E, ambalo awali Nkubana alikuwa amepewa na Col. Gatabazi kwa ajili ya Operesheni ya usiku. Gari hii ni mojawapo ya magari yaliyokuwa yameachwa na viongozi wa serikali iliopita, baada ya kukimbia mji wa Kigali, wakati RPF inaingia madarakani.

Nkubana alikaa kwenye usukukani kwa ajili ya kuendesha gari, Col. Gatabazi akakaa upande wa kulia, maana gari hili lilikuwa na usukani upande wa kushoto.

"Aha, kumbe gari limejaa mafuta kwenye tenki".

"Ndio, nilijaza kwa sababu kama hizihizi kama dharura itatokea", Col. Gatabazi alijibu.

"Tuchukue njia gani?", Nkubana aliuliza.

"Najua sasa hivi wataanza kututafuta. Hivyo, twende na barabara kubwa iendayo Ruhengeri. Kwa vile bado mawasiliano ni shida kati ya vikosi, tunaweza kupata bahati tukafika Gisenyi kabla habari zetu hazijaenea. Kwa vile vikosi vya RPF vinanifahamu na kuniheshimu njiani hatutaulizwa wala kupata tatizo lolote, watajua kuwa niko kazini. Kwa hiyo tutumie barabara kubwa mpaka Ruhengeri, halafu moja kwa moja mpaka Gisenyi, halafu tutavuka mpaka na kuingia Goma. Upande ule Jean ameshafanya mipango, hatutakuwa na shida. Nimemweleza amweleze Mkuu wetu wa Majeshi Col. Marcel Bazimaziki atukute mpakani"Col. Gatabazi alieleza.

"Sasa hivi ni saa sita na robo, itatuchukua masaa kama manne kwa gari hii, kwa hiyo saa kumi na moja alfajiri tutakuwa Goma?", Nkubana aliuliza huku akitia gea na kuondoa gari kwa kasi kuelekea Goma.

NGUVU YA RUSHWA

VI

Baada ya Jean kumweleza JKS mambo yote yaliyokea Kigali, palepale JKS usingizi ulimtoka. Aliona na kuamini kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wake. Ndoto zake za kuwa Rais wa Tanzania zilianza kuyeyuka mfano wa seluji. Hakujua afanye nini. Aliamini kuwa Willy Gamba akipata habari zake kuwa yuko kwenye mtandao wa kuisaliti Afrika haitamchukua zaidi ya siku mbili kabla mambo yake hayajabainika na kuanikwa hadharani.

JKS alimjua vizuri Willy Gamba alivyokuwa makini na hodari katika kufanya kazi zake. Alifikiri asubiri Willy arudi kwanza nchini ndio amkabiri yeye mwenyewe au aieleze serikali ya Tanzania kilichokuwa kinafanyika Rwanda. Aliona kashifa kubwa inakuja mbele yake. Ingawaje Rais wa sasa wa Tanzania alikuwa rafiki yake mkubwa, lakini ingekuwa vigumu sana kuizuia kashifa hii, maana vyombo vya habari vingemmaliza kabisa. Kisha, akakumbuka kuwa alikuwa na mapesa mengi ambayo Jean alimwekea kwenye akaunti zake katika mabenki ya huko Uswisi na Cyprus.

Baada ya kutafakari kwa muda mrefu huku jasho jembamba likimtoka. JKS akaamini kuwa mapesa hayo yangeweza kuzuia kashifa hii kwa kuwanunua wamiliki wote wa vyombo vya habari Tanzania kama Radio, magazeti na taasisi zingine kama polisi, usalama wa Taifa na idara zingine nyeti za serikali ambazo zingeonekana kumletea madhara kwenye safari yake ya kuelekea Ikulu.

"Watanzania karibu wote wana njaa, nitawanunua kwa mapesa tu. Hapo ndipo Willy atajuwa jeuri na nguvu ya pesa. Hakuna mtu atakayemsikiliza tena Willy Gamba, mimi nitaendelea na mambo yangu bila hofu. Uchu wangu wa kuwa Rais wa Tanzania utafanikiwa", JKS alijisemea mwenyewe huku akiwa amelala mfano wa mtu aliyeko katika usingizi mnono akiota ndoto.

Hivyo, baada ya kutafakari hili na lile kwa mapana na marefu, JKS aliamua kuwa atamfuata Rais ili amuombe ruhusa na kusafiri kwenda Ulaya kwa ajili ya kuangaliwa afya yake kwa madaktari wake walioko Uingereza, na angemwambia daktari mkuu wa Hospitali ya Muhimbili atoe ushauri wa haraka. Akiwa amejiwekea malengo kuwa akifika Ulaya akusanye mapesa yake halafu ndipo ajue kitu cha kumfanyia Willy Gamba aliyemwona mchawi wa safari yake ya kuelekea Ikulu ya Tanzania.

JKS aliamini kuwa akiwa na mapesa mkononi, ataweza kufanya chochote atakavyo. Akapiga moyo konde, akamkumbuka tena Willy Gamba moyo wake ukapata maumivu makali, akahisi mtu huyu ni mchawi. Hata hivyo akaapa kuwa hatarudi nyuma.

ITAENDELEA 0784296253
Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru