UCHUGISENYI

Ilikuwa yapata saa kumi na mbili alfajiri wakati Willy Gamba na Bibiane walipokuwa wakiondoka nyumbani kwa Bibiane kuelekea Goma, nchini Zaire. Baada ya Bibiane kwenda kulala usiku na kumwacha Willy akimpa habari Col. Rwivanga kuhusu yote aliyoelezwa na Bibiane, usiku, uleule Willy na Col. Rwivanga waliamua kwenda haraka kumkamata Col. Gatabazi nyumbani kwake, baada ya kuchunguzi wa kina waligudua kuwa nyumba hiyo imefungwa na hakuna mtu. Mara moja Col. Rwivanga akahisi kuwa Col. Gatabazi alikuwa ameelekea kwenye majeshi yake huko Kibumba karibu na Goma kama ambavyo walikuwa wameelezwa na Bibiane. Hivyo, waliafikiana kuwa asubuhi na mapema Willy aondoke na Bibiane kwenda Goma, kuwasaka Col. Gatabazi, Nkubana na Jean.

Wakati huo Col. Rwivanga alikuwa akijiandaa kwenda kutoa taarifa za uhalifu huo kwa serikali ya RPF ili iandae jeshi la kushambulia sehemu ya Kibumba na kuliangamiza jeshi la Akazu pamoja na Jean kabla halijaishambulia Rwanda tena. Hivyo, Willy Gamba na Col. Rwivanga walirudi nyumbani na Willy akatafuta usingizi wa saa moja kwa ajili ya kujiweka sawa. Ilipofika saa kumi na moja alifajiri Willy alimuamsha Bibiane ili waanze safari.

Willy akilipokuwa akijipumzisha, Col. Rwivanga alitoka usiku huo kwenda kumwona mkuu wa shirika la Msalaba Mwekundu ambaye alikuwa rafiki yake na kumwomba gari. Col. Rwivanga alipewa gari ya Msalaba Mwekundu aina ya Toyota Land Cruser GX ambalo alipanga Willy na Bibiane walitumie kwenda mpakani kwenye kambi ya wakimbizi ya Kibumba. Vilevile Col. Rwivanga aliwatanguliza vijana wake watatu askari wa kikosi maalumu cha upelelezi kutoka jeshi la RPF ili wawahi kufika Gisenyi na kutoa taarifa za Col. Gatabazi kwa makamanda wa RPF walioko Gisenyi. Pia alituma taarifa ya siri kwa Meja Tom Kabarisa, kiongozi wa waasi wa Banyamulenge kikundi kilichokuwa kikipigana kupinga serikali ya Zaire, kilichokuwa na makao makuu yake sehemu za milimani, karibu na mji wa Goma. Hawa Banyamulenge walikuwa ni watu wa asili wa Kitutsi ambao walihamia miaka mingi eneo hili na Mashariki mwa Zaire kutokana na misukosuko ya muda mrefu ndani ya Rwanda.

Kwa muda mrefu watu hawa waliishi kama wananchi wa Zaire, lakini miaka ya hivi karibuni serikali ya Zaire ilianza kuwabagua kiasi cha kuwanyima haki hata ya kupiga kura na kisha kuwataka wahame maeneo waliyokuwa wakiishi ndani ya Zaire ili warudi kwao Rwanda. Lakini walikataa katakata kutii amri hii ya serikali ya Zaire na kuanzisha kikundi chao cha wapiganaji ili kiweze kulinda maslahi yao. Kikundi hiki kilikuwa na mahusiano mazuri na maofisa wa jeshi la RPF. Wakati na baada ya mauaji ya Watutsi na Wahutu kukimbilia eneo hili la Ziwa Kivu, uhusiano wa Banyamulenge na uongozi wa RPF uliimarika zaidi kwa sababu za kiusalama kwa pande zote mbili.

"Mimi niko tayari kwa safari, lakini naomba tupite pale nyumbani kwangu ili nipate nguo za safari ya namna hii na nyenzo nyingine ambazo zinaweza kutusaidia katika safari yetu", Bibiane ambaye alikuwa ametokea chumbani na kujiegemeza kwenye ukuta alisema.

Willy na Col. Rwivanga waliokuwa wanapanga mikakati huku wameupa mgongo ule upande wa chumba waligeuka na kumwangalia. Alfajiri hii Bibiane alionekana mrembo hata zaidi ya jana yake.

Willy na Col. Rwivanga walitazamana tena na kutabasamu huku macho ya Col. Rwivanga yakimweleza Willy kuwa. "Haya kazi unayo".

"Mmenisikia?", Bibiane aliuliza tena.

"Sawa", Willy alijibu kisha kama amekumbuka kitu akahoji, "Lakini sijui kama pale kwako tutaweza kuruhusiwa kuingia".

"Tutaenda wote", Col. Rwivanga alijibu.

Kisha Col. Rwivanga alimmalizia Willy maelezo na mipango yote, wakaondoka kuelekea nyumbani kwa Bibiane.

Kwa vile kulikuwa bado hakujapambazuka, walipofika nyumbani kwa Bibiane ilibidi Col. Rwivanga atoke na kujitambulisha kwa askari wapatao wanne waliokuwa wamejitokeza baada ya kusikia mwungurumo wa gari. Kisha lango la mbele lilifunguliwa wakaingiza gari ndani. Baada ya maelezo mengine mafupi, Bibiane aliruhusiwa kuingia ndani.

"Karibuni", Bibiane aliwakaribisha Willy na Col. Rwivanga ndani.

Bibiane aliingia chumbani na kuwaacha Col. Rwivanga na Willy sebuleni. Nyumba ilikuwa bado kabisa haijakaguliwa. Hivyo, kila kitu kilikuwa kimebaki kama kilivyokuwa isipokuwa maiti za wale tu ndizo zilikuwa zimeondolewa.

"Willy njoo", Bibiane alimwita Willy chumbani kwake. Willy na Col. Rwivanga waliangalia na kutabasamu, baada ya sekunde kadhaa Col. Rwivanga alimuonyesha Willy ishara aende chumbani kama alivyoitwa.

Willy alipoingia chumbani alimkuta Bibiane anavaa suluali lakini sehemu ya juu yote ilikuwa bado iko wazi yaani hajavaa kitu hata sidiria.

"Hatuna muda wa kukaa hapa hivyo itabidi unisaidie vitu vingine ili tuweze kuondoka mapema", Bibiane alimwambia Willy ambaye alikuwa kama amepigwa na butwaa. Hakika msichana huyu alikuwa mzuri, umbo lake jinsi alivyoumbika hutaamini kama alizaliwa kutoka tumboni kwa mwanamke isipokuwa alishushwa kutoka juu. Hakukuwa na maelezo ya kutosha kueleza urembo wa msichana huyu bali ujitahidi kumtafuta ili uthibitishe mwenyewe kama Willy alivyojionea.

Usinitie majaribioni", Willy alisema huku akirudisha mlango.

"Aaa mshirika, mapigo yangu nikitaka utayaweza?. Kazi kwanza mambo mengine baadaye. Nimekuita kwa sababu hatuna muda wa kukaa hapa nataka kukuonyesha kitu", Bibiane alisogea kwenye ukuta akabonyeza sehemu na ukuta ule ukafunguka. Willy alishangazwa kuona kumbe ule haukuwa ukuta isipokuwa kabati la siri lililojificha likiwa na zana mbalimbali za kazi za kisasa kabisa.

"Pale mwisho kuna makasha mawili makubwa yameandikwa 'hatari', yatoe", Bibiane alimwambia Willy huku akichukua sidiria na kuendelea kuvaa.

Willy aliyatoa na kuyaweka chini.

"Fungua", alisema huku akiendelea kuvaa. Willy alipofungua alikuta ni mabomu aina ambayo hakuwahi kuyaona wala kuyatumia kabisa.

"Haya ni mabomu aina ya teknolojia ya kisasa kabisa, ambayo Jean aliniletea siku chache tu zilizopita, akanielekeza niyahifadhi mpaka nitakapopata maelekezo zaidi. Lakini yule mtu wa DOSE aliyeleta silaha hizi alinieleza jinsi zinavyotumika na kweli ni aina ya mabumu ya kisasa na hatari sana", Bibiane alieleza huku akivaa viatu na kutengeneza nywele zake. Alimweleza Willy jinsi mabomu hayo yanavyofanya kazi na kumalizia. "Hayo mabomu mawili yana uwezo wa kulipua nusu ya mji wa Kigali, na kwa kutumia saa hii ninayokupa unaweza kulipua mji wa Kigali huku umeketi mahali unakunywa chai.

"Ili mradi tu usiwe umetega na nyumba yako au ya majirani zako", Willy alitania na wote wakacheka.

Willy alikubaliana na Bibiane kuwa waende na makasha yote mawili, maana kutokana na maelezo ya Bibiane, Jean na Akazu walikuwa wameandaa jeshi kamili kwa ajili ya kuivamia Rwanda, wakiwa na silaha kali na za kisasa kutoka Ufaransa na Afrika Kusini, huku wakitumia kisingizio cha wakimbizi. Kisha Bibiane alitoa bastola nne, mbili zikiwa ndogondogo sana alizoziweka kwenye mkoba na mbili kubwa alizomkabidhi Willy, vilevile alichukua risasi nyingi sana.

"Nafikiri sasa tuko tayari", Bibiane alisema huku akimsaidia Willy kubeba kasha moja na mfuko wake wa nguo.

"Ehe, vipi huko ndani?", Col. Rwivanga aliuliza.

Kabla Willy hajajibu Bibiane alijibu."Salama kabisa".

Wote wakacheka, kisha kwa kifupi, Willy akamweleza Col. Rwivanga kuhusu kilichokuwa ndani ya yale makasha waliyotoka nayo ndani.

Baada ya hapo, Willy na Bibiane waliingia ndani ya gari na kumtakia Col. Rwivanga heri ya kuonana, kisha wakaanza safari ambayo hawakuwa na uhakika kama mambo yangeendaje huko.

"Mungu awe pamoja nanyi, naamini atawasaidia", Col. Rwivanga aliwaaga, askari waliokuwa wakilinda nyumba ile waliwafungulia lango wakatoka na kutokomea kuelekea Kibunda.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru