GISENYI
II
Ilipofika
saa nne asubuhi JKS alikuwa tayari ameshapata kibali kutoka kwa Rais ili
aweze kwenda Uingereza kwa matibabu. Daktari alikuwa ameiandikia serikali barua kufanya haraka na kila
njia JKS aondoke siku ileile kwani alihisi kuendelea kusubiri kungeweza
kumletea shinikizo la damu lenye nguvu kubwa ambalo huenda wao wasingeweza kumsaidia kabisa.
Ni barua hii
ya Daktari iliyomfanya Rais akubali kutoa kibali harakaharaka na kuamru kuwa
ifikapo jioni ile JKS awe ameondoka kwenda Uingereza kwa matibabu. Hadi saa saba
mchana Wizara ya Afya ilikuwa imefanya mipango yote na ikawa wamempatia
usafiri kuondoka na ndege ya shirika la ndege la Uingereza usiku ule.
JKS alikataa
kusindikizwa na maofisa wa serikali kwa kisingizio kuwa atapokelewa na watoto
wake walioko mjini London, Uingereza ambao alisema watamwangalia kwa karibu
zaidi wakati wa matibabu yake. Bila watu kujua, alifanya mipango yake mwenyewe
ili usiku uleule aweze kuunganisha ndege kwenda hadi Geneva, Uswisi, kitu
ambacho alifanikiwa. "Hakika Willy Gamba hataniweza, nikirudi na mapesa
yote yale, hakika naamini ataiona dunia na ardhi ya Tanzania chungu", JKS
alijisemea mwenyewe huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio.
.............................................................................................................................
III
Wakati Willy
na Bibiane wanaondoka Kigali kuelekea Goma, saa kumi na mbili asubuhi. Col.
Gatabazi na Nkubana walikuwa wanapokelewa na Col. Marcel Bazimaziki na kikundi
cha wanajeshi wa jeshi la Zaire kikiongozwa na Meja Massamba kwenye mpaka wa
nchi hizo za Rwanda na Zaire.
"Pole
sana na safari, ulipokaribia kufika Gisenye natumaini umepita ile njia yetu na
nadhani hukupata shida", Col. Bazimaziki aliwasalimia kuwapa wageni wake
mkono huku kila kikundi cha askari kikijiweka sawa kutoa heshima kwa gwaride
rasmi lililoandaliwa kwa ajili ya Col. Gatabazi ambaye kama walivyokuwa
wameelekezwa kuwa baada ya muda si mrefu ndiye atakuwa kiongozi wa Rwanda.
"Safari
ilikuwa safi kabisa na hizi Benz ni gari imara sana ha hata kile kinjia
tulichopita hatukupata taabu sana. Asante kwa kutuma mtu wa kutuongoza, maana
tungeweza kubabaika kufika hapa", Col. Gatabazi alijibu.
"Jean
tulizungumza kwenye simu yetu aliyoleta hivi karibuni ya Satellite. Sasa
mawasiliano ni mazuri sana kati yake na sisi. Hata kabla ya kuja kukupokea
tulizungumza nae, alikuwa akielekea uwanja wa ndege, nae tayari amepanda ndege
na imeondoka Paris tangu saa kumi na mbili.
"Anatumia
ndege yake ile ya Falcon, atakuwa hapa saa kumi na mbili jioni, maana atapitia
Kinshasa kuonana na viongozi wa serikali kule, mkutano utafanyika uwanja wa
ndege ili waweke msimamo, halafu watakuja na Jenerali Kasongo ili kuangalia
hali pamoja na wewe mwenyewe ukiwepo ili mkiridhika na hali kazi ianze",
Col. Bizimaziki alieleza na kisha Col. Gatabazi akaelekea kwenye gwaride ili
apokee heshima zake kutoka kwa kikundi cha wanajeshi wa Zaire.
Baada ya
kupokea heshima na kukagua gwaride. Col. Gatabazi na wenyeji wake waliamua
kuondoka kuelekea Kibumba kwanza na kisha jioni ndio waelekee Goma kwenda
kuonana na Jean na maofisa wengine wa juu.
"Acheni
hilo gari hapa mpakani, hakuna matatizo askari wa jeshi la Zaire wapo
wataliangalia maana kule kwenye makambi lazima kwenda na magari ya jeshi la
Zaire ndio idara na taasisi za Kimataifa zinazoshughurikia wakimbizi haziwezi
kushituka", Col. Bizimaziki alieleza.
"Sawa,
vipi minong'ono kwamba watu wetu wanajitayarisha kuishambulia tena Rwanda huku
wakitumia kinga ya wakimbizi?", Col. Gatabazi aliuliza.
"Usijali
kabisa kuhusu hilo, serikali ya Zaire itakanusha vikali huku sisi tumetia pamba
masikioni. Na kama ujuavyo kiongozi wa baraza la Akazu, Anatoile Kabuga.
Alitusihi tusisikilize propagada za vyombo hivi isipokuwa tujiimarishe kijeshi
tayari kwa kuikomboa nchi yetu kutoka kwa wavamizi wa Kitutsi. Kwanza nilitaka
kusahau, vilevile Bwana Kabuga anakuja pamoja na Jean ili maamuzi yaweze
kufanyika, ameeleza kuwa mjumbe mwingine wa Akazu ambaye anaweza kufika ni John
Ngeze ambaye sasa yuko Afrika Kusini, lakini ameambiwa apande ndege ya shirika
la ndege la Afrika Kusini inayoingia mjini Kinshasa saa sita na kama akiwahi
atawasubiri pale uwanjani na wao wakiwahi watamsubiri|.
"Lo,
kumbe tutakuwa na mkutano mkubwa", Col. Gatabazi alinena.
"Wakati
umefika kwa wewe Col. Gatabazi kuchukua nchi kutoka mikononi mwa wavamizi wa
Kitutsi. Siri zote za adui yetu unazijua, nguvu ya RPF yote unaijua, ya kijeshi
na kisiasa. Sasa nini kitazuia?, wao hawajui nguvu yetu wanafikiri tunacheza.
Utaenda sasa hivi kujionea mwenyewe salaha za kisasa, magari, vifaru. Tuna
silaha ambazo zina uwezo wa kupiga masafa marefu hadi kilomita mia mbili, na
kuna mafunzo makali yanayoendelea kutoka kwa askari wale tuliowakodi kutoka
Afrika Kusini na wana kazi kubwa na vijana wetu wana ari kubwa maana wanajua
tusiposhika nchi tena maisha yao yako hatarini. Ni kweli kama ulivyosikia
wakimbizi tumewazuia kurudi ili siku tutakapoamua kuanza kazi ndiyo siku ambayo
wakimbizi wote wanaume tutaandamana nao. Wakirudi wakati huu uhalali wa
kuivamia tena Rwanda hatutakuwa nao. Hii vurugu ya wakimbizi kwanza inaficha
mambo yote tunayoyafanya, pili itatupa uhalali na nguvu za kuvamia. Rafiki zetu
wote watasema. "mlitaka wafanye nini, yaani mamilioni ya watu yabaki kuwa
wakimbizi nje ya nchi yao", Col. Bazimaziki alieleza, kisha wakaelekea
kwenye kambi.
Walipofika
huko kambini walitumia muda mrefu kuangalia aina mbalimbali za silaha za kisasa
kabisa, mafunzo makali ya kijeshi, ari ya vijana wa Kihutu, hasa wale
Intarahamwe waliotaka siku hiyohiyo kwenda kuvamia Inyenzi na kurejesha
madaraka yao. Kutokana na aina ya silaha walizonazo na mafunzo waliyokuwa
wakipata na moto waliokuwa nao wa kutaka kupigana na adui. Col. Gatabazi
aliamini kabisa kuwa wakisaidiwa na Wahutu waliokuwa ndani ya Rwanda ushindi
ulikuwa wao asilimia mia. Col. Gatabazi alipandwa na mori akatamani kama vita
vingeanza saa ile. Kisha, wakaondoka kuelekea Goma.
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment