UCHUGISENYI

IV

Ilikuwa saa kumi na moja na nusu jioni, Jeana na wenzake walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Goma. Baada ya kuwasiliwa, walipokelewa na Col. Gatabazi aliyesindikizwa na askari wake. Jean aliwasili akiwa pamoja na kiongozi wa Akazu, Bwana Anatoile Kabuga, Bwana John Ngeze, ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Akazu, Jenerali Kasongo, ambaye ni mshauri wa Rais wa Zaire, Meja Karongo, Mkuu wa kikosi cha jeshi linalomlinda Rais wa Zaire, Bwa, George Karikutis, ambaye ni dalali wa mamluki aliyefanya mipango yote ya kuwawezesha Jean na wenzake wa Akazu kupata askari wa kukodi.

Baada ya kuwasili uwanja wa ndege walipelekwa moja kwa moja hadi Ikulu, ambako Rais alitoa kibali Jean na wenzake wafikie kwenye jumba hilo. Ikulu hii ilikuwa ya kifahari sana. Ili uweze kuelewa kwa kifupi, vyoo, bafu na vyumba vya kulala alivyokuwa akitumia Rais vilijengwa kwa vito vya dhahabu tupu. Sasa naamini utakuwa umeelewa maana yake. Karibu na Ikulu hii kulikuwa na Jumba jingine kubwa ambalo Majemedari wa jeshi wa ngazi za juu walikuwa wakifikia. Ndani ya jumba hilo ambalo pia lilikuwa la kifahari sana, ndimo alipofikia Col. Gatabazi na wenzake. Kisha, wakaenda kukaa kwenye sebule ya kifahari ajabu. Wasichana warembo sana wapatao kumi hivi walijitokeza kwa ajili ya kutoa huduma, wakiwa wamevaa kaputula fupi, matiti nje, yaani asilimia tisini walikuwa uchi.

"Hivi ndivyo mzee anavyoishi hapa duniani Jean, hapa panaweza kuwa peponi ukitaka. Mzee ameyafanya maisha yake hapa duniani kuwa sehemu ya peponi. Hivyo, na wewe onja pepo kidogo ukiwa hapa", Jenerali Kasongo alimweleza Jean, ambaye wakati huo alikuwa akitikisa kichwa, maana pamoja na utajiri wake mkubwa usio kifani alikuwa hajawahi kukalia viti na meza za kahawa vilivyotengenezwa kwa dhahabu tupu, ukiacha sehemu za kukaa ambazo zilivishwa kwa ngozi ambazo hata yeye hakuwahi kuziona kabisa duniani.

Huku wale wasichana wakiendelea kuwahudumia, kila mmoja alikuwa amejichagulia mrembo wa kumhudumia, wakileta vinywaji vya kila aina vilivyokuwa ndani ya jumba hilo. Baada ya muda mazungumza yalianza.

"Ehe, hebu Nkubana tueleze ilikuwaje hata huyu Willy Gamba akachafua mipango yetu namna hii, maana inaniuma sana kufikia hatua ya Bibiane kuwa mikononi na mshenzi huyu. Hebu tueleze", Jean aliuliza kwa hasira.

Huku akitetemeka Nkubana alieleza jinsi mambo yalivyokuwa huku wote wakimsikiliza kwa makini sana, kisha akamalizia kwa kusema, "Tulichukua tahadhali ya kila aina, lakini nafikiri huyu Willy Gamba alikuwa na bahati kuliko sisi. Katika biashara kama hii yetu, wakati mwingine ni bahati tu inaweza kukusaidia", Nkubana alijitetea.

"Unafikiri huyu mtu ana mipango gani sasa?", Jenerali Kasongo aliuliza.

"Sijui, lakini naamini Bibiane anaweza kumleta huku. Hizi ni hisia zangu, maana Bibiane atakuwa na uchungu wa kutaka kulipiza kisasi na siri zetu zote anazijua. Hivyo, atataka amtumie Willy Gamba baada ya kuona umahiri wake, alipize kisasi", Nkubana alijibu.

"Mbona hiyo itakuwa raha, maana nitaua ndege wawili kwa jiwe moja, Col. Bazimaziki na Meja Massamba, moja ya kazi zenu ni kuweka kikosi imara chenye wapiganaji jasiri cha kuweza kuwakamata hawa watu wawili, nataka Nkubana akiongoze kikosi hicho, Nkubana, ukiweza kuwakamata usiwaue hao ni halali yangu. Nataka niwafanyie kitu ambacho wakiwa ahera wasinisahau milele", Jean aliamru.

"Sawa bosi", Nkubana alijibu hku Col. Bazimaziki na Meja Massamba wakiitikia kwa vichwa vyao.

"Ratiba ikoje?", Jean alimuuliza Col. Gatabazi.

"Nafikiri kwanza twendeni wote tukaangalie hali ya vikosi vyetu ilivyo, hasa hapa Kibumba, maana mtapata mwanga baada ya kuona jinsi tulivyojiandaa tayari kwa vita. Tumetuma habari kwa vikosi vyetu vingine vilivyoko karibu na Bukavu, navyo vijiweke tayari. Ile simu moja kati ya simu nne za Satellite ulizoleta tuliwapelekea na sasa tunawasiliana vizuri sana kati ya hapa na sehemu zingine zote ambako kuna vikosi vyetu, lakini kwa kuwa nguvu yetu kubwa iko hapa nafikiri twende mara moja Kibumba mkajionee wenyewe, kwani ni kilomita thelathini tu kutoka hapa Goma. Halafu tukirudi tutakula chakula hapa na baadaye kidogo tutaanza mkutano wetu. Mimi naamini kuwa mkishaona kama nilivyoona mimi mkutano wa leo utaruhusu tuanze uvamizi leoleo", Col. Gatabazi alimalizia.

Wote walikubaliana naye. Kabla hawajaondoka alichukua simu ya Satellite akapiga simu Tanzania. Nia yake ilikuwa kumpata JKS ili ampatie habari za wakati ule kuhusu nyendo za Willy Gamba kama alikuwa amezipata kutoka kwenye vyanzo vyake vya habari. Kwa mshangao alipata habari kutoka kwa mke wa JKS kuwa alikuwa ameumwa ghafla na kuondoka jioni ile Tanzania kuelekea Uingereza kwa ajili ya matibabu. Na mama huyo alieleza kuwa mumewe aliondoka kwa ndege ya shirika la ndege la Uingereza. Mara moja Jean alihisi kuna tatizo. huku akitingisha kichwa huku wengine wakimwangalia kwa kustaajabu, Jean aliwaambia wenzake wote wamsubiri nje.

Walipotoka nje Jean alipiga simu zingine tatu zilizomchukua dakika kama kumi hivi na baada ya kuzipiga aliagua kicheko kwa sauti mpaka askari aliyekuwa karibu akashangaa akifikiri kuwa huyu mzungu alianza kupata uchizi kwa kucheka peke yake hivi. Jean alipoangalia saa yake ilikuwa yapata saa moja na nusu jioni, hivyo aliungana na wenzake wakaondoka kuelekea Kibumba. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru