GISENYI
VI
Baada ya
kupata habari hizi walikubaliana kuitisha mkutano wa dharura mnamo saa sita na nusu mchana. Rais
alipiga simu tena kwa Jenerali Bunyenyezi na kumwambia afike ofisini kwake haraka akiwa
pamoja na kiongozi wa upinzani wa Zaire, aliyekuwa akiunganisha vyama vyote vya
upinzani na ambaye askari wake waliwahi kupigana vita bega kwa bega na majeshi
ya RPF, wakati wa mapambano dhidi ya Serikali ya Rwanda ili wapate uzoefu
kutoka kwao. Bwana Mpinda ambaye nae alikuwa mjini Kigali kwa mazungumzo.
Haikuchukua
zaidi ya saa moja wote walifika ofisini kwa Rais.
"Bwana
Mpinda karibu sana. Nimekuita pamoja na Kamanda hapa ili tuzungumze kama
uliyonieleza juzi, maana naona hali imegeuka, sasa inakupendelea wewe", Rais
alicheka kidogo na wote wakatabasamu.
"Asante
sana Mheshimiwa Rais, nashukuru Mungu, kama umegeuza uamuzi wako na uko tayari
kutuunga mkono sisi", Mpinda alijibu.
"Kama
nilivyosema naona hali inakupendelea, kuna mambo ambayo yametokea na kuashiria
tulifikirie kwa makini ombi lako. Askari wako wote bado wako kwenye ardhi ya
Rwanda?", Rais aliuliza.
"Hapana
Mheshimiwa, wengine wengi bado wapo lakini baadhi yao wamevuka wapo mpakani,
wakisaidia kufundisha jeshi la Wabanyamulenge", Mpinda alimwambia Rais.
"Kamanda
Bunyenyezi, nataka basi ufanye mpango na kiongozi wa Banyamulenge nae awepo
kwenye mkutano wa saa sita na nusu", Rais aliagiza.
"Na
hilo tumelifikiria, na Col. Rwivanga ameshatuma Helikopita kwenda
kumchukua", Kamanda Bunyenyezi alijibu.
"Oh,
vizuri sana. Sasa bwana Mpinda unakaribishwa kwenye kikao saa sita na nusu, na
naomba ujieleze vizuri, na kama ukiweza kuwashawishi mawaziri na makamanda
wangu, basi utakuwa umefanikiwa. Hii ni nafasi nzuri sana kwako kwani na sisi
sasa tunalazimika kutumia mpango wako ili nasi tukidhi lengo letu. Hivyo, kazi
kwako kukishawishi kikao kama kweli una mipango thabiti ya kuweza kufanya kazi",
Rais alimalizia.
"Mheshimiwa
Rais, naenda kukaa na makamanda wangu, na kwa vile viongozi wa Banyamulenge nao
watakuwepo na wako upande wenu na wetu, basi naamini nitaweza kukiridhisha
kikao kuwa tuko tayari kufanya kweli", Mpinda alijibu.
"Haya
Bwana Mpinda kwa heri. Kamanda Bunyenyezi, wewe ngoja kidogo".
Walimtoa nje
Bwana Mpinda na wakamrudisha kwenye nyumba ya wageni ya Serikali alikokuwa
amefikia na makamanda wake. Rais na makamanda wake walipobaki nyuma,
walitafakari swala zima kwa undani. Wakaangalia jinsi ambavyo wangeweza
kufaidika kwa kuwatumia wapinzani wa Serikali ya Zaire ili waweze kutimiza
lengo lao kuwaondoa Intarahamwe na Wahutu wote wenye siasa kali pale mpakani
kwao ili wasije wakaivamia Rwanda, huku bila kulaumiwa na Jumuia ya Kimataifa
kuwa wamevamia nchi nyingine na kuwaua wakimbizi.
"Nafikiri
hii ndio nafasi yetu ya pekee kumaliza tatizo hili. Kwa hiyo, inabidi tulieleze
kwenye mkutano vizuri", Kamanda Bunyenyezi alieleza.
"Je,
hawa wapinzani na waasi wa Banyamulenge wakishindwa, itakuwaje? si siri
itavuja?", Rais aliuliza.
"Hilo
litakuwa jambo jingine, sisi tutakuwa tumetimiza lengo letu na tutakuwa
tumewaondoa na kuwamaliza kabisa hawa Intarahamwe karibu na mipaka yetu.
Tutakuwa tumewatokomeza mstuni huko Zaire. Shida na wasiwasi kwetu vitakuwa
vimemalizika kabisa. Kazi yako itabaki kujenga nchi na si kupigana tena",
Kamanda Bunyenyezi alijibu.
"Kweli,
sasa tumepata kisingizio; Mungu yuko pamoja nasi, maana chochote tungefanya
serikali ya Zaire na Jumuia ya Kimataifa visingetupa nafasi. Basi nenda
kajitayarishe, Mkutano utakuwa mgumu sana, maana najua mawaziri wengi itakuwa
vigumu kukubali", Rais alijibu.
"Asante
Mheshimiwa Rais, nafikiri watatuelewa kwa sababu hii ni kwa faida ya Taifa la
Wanyarwanda ambalo limeteseka sana, lazima wananchi wapate muda wa kupumua na
si vita kila siku", Kamanda Bunyenyezi alijibu na kueondoka kwenda
kujitayarisha.
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment