UCHU

BIBIANE

II

Willy Gamba alimkuta Col. Rwivanga anakula chakula. Alipomuona Willy alionekana kufurahia "Nimekusubiri sana mpaka nikaamua bora niendelee na chakula maana ni zaidi ya saa nne sasa na unajuwa mimi nakula mara moja tu kwa siku, njaa ilikuwa inauma sana", Col. Rwivanga alijitetea.

"Usijali Kamanda", Willy alijibu huku akielekea jikoni kuchukua sahani na kisha akaketi kwenye meza pamoja na Col. Rwivanga na kupakuwa chakula.

"Hiki chote kilikuwa chako peke yako", Willy alimkejeli Col. Rwivanga.

"Hapana, nilijuwa tu utanikuta nakula", Col. Rwivanga alijibu huku akicheka. Willy alichota kijiko cha kwanza na kukitia mdomoni, chakula kilikuwa wali na mchemsho wa nyama.

"Lo, mpishi ni wewe?".

"Kwani vipi?".

"Kitamu sana chakula hiki", Willy alijibu.

"Wapi, na wewe una njaa vilevile, upishi wangu mimi ni mchemsho tu".

"Hapana si njaa ila wali umepikwa vizuri na nyama ya mchemsho, napenda sana mimi", Willy alieleza.

"Ehe vipi huko, umewakuta?".

"Bwana nimewakuta wale mapadri na nimewekwa shule hasa, na sasa hivi naijua historia ya utawala wa nchi vizuri sana kuanzia kabla ya ukoloni".

"Wacha bwana".

"Nakuambia wale mapadri wanaijua nchi hii kuliko viganja vya mikono yao", Willy alimweleza Col. Rwivanga, kisha akamgusia kwa muhtsari mambo muhimu aliyoelezwa.

"Kumbe hili swala la Akazu hata hawa wazee wanalifahamu sana?", Col. Rwivanga aliuliza baada ya maelezo ya Willy.

"Sana, na wamesema bila hawa watu kukamatwa hakuwezi kuwa na amani katika nchi hii".

"Hilo ni kweli kabisa na sisi tunalijua na ninafikiri ndio walio nyuma ya hili swala la kutaka kukuua maana hawa watu wana mahusiano dunia nzima na pesa nyingi. Hivyo, tunajua wanajipanga kuja kutuhujumu, hilo tunajua. Ila hatujui kwa sasa hivi wanafanya shughuli zao kutoka wapi. Nia yetu imekuwa ni kuimarisha serikali yetu, halafu ndipo tuangalie habari yao", Col. Rwivanga alieleza.

"Ni sawa, lakini mimi nafikiri jambo hili mgelishughulikia sasa hivi wakati bado nao wamechanganyikiwa, lakini mkisubiri watakusanya nguvu halafu itakuwa shida tena", Willy alishauri.

"Kutokana na matokeo ya siku hizi mbili nasi tumeshituka sana, maana inaonekana hawa watu bado wana watu ndani ya serikali yetu na wameanza kutuhujumu. Kama unavyosema, nasi tumeamua kulishughulikia mara moja swala hili na tutakuwa na mkutano na makamanda wote wa jeshi pamoja na baraza la mawaziri kesho saa moja na nusu asubuhi", Col. Rwivanga alieleza.

"Hivyo itakuwa vizuri. Ingawaje mimi kazi iliyonileta haikuwa ya mapambano, lakini kwa sababu wao ndio wamenianza na mimi naomba ruksa yako unilinde mbele ya wakubwa wako, kwani nataka nami kwa kiasi fulani nijuwe habari ya watu hawa na vipi wameamua kutaka kuniangamiza. La maana hasa nataka nijuwe nani hasa anahusika na kutaka kuniua mimi. Hilo Col. Rwivanga ningependa sana unipe hiyo nafasi nifanye kazi yangu", Willy alijieleza.

"Ni sawa lakini tungeomba na sisi utufahamishe kila hatua unachofanya ili tuweze kukusaidia itakapobidi kwani ukweli ni kuwa kazi hii ni yetu na wala si yako", Col. Rwivanga alijibu.

"Asante Col. Rwivanga. Vipi yule msichana wa jana usiku, Bibiane umepata habari zake?".

"Ahaa, ndio nilikuwa nakusubiri nikueleze. Hivi usingewahi ungenikuta nimeshaenda kumfuata. Huyu msichana inasemekana ni mkalimani, anajuwa lugha kama nane hivi na amekuwa akifanya kazi serikalini kama mkalimani hivyo, alikuwa akisafiri na Rais au mawaziri ama maafisa wakubwa wa serikali wanaposafiri nje ya nchi na vilevile ndiye aliyekuwa mkalimani wa serikali kama wageni wasiojuwa kifaransa wakija nchini hapa. Inasemekana wakati wa mauaji yeye hakuwepo. Alikuwa Nairobi, lakini ni kati ya watu wa kwanza kabisa kurudi na amekaa katika nyumba yake aliyokuwa akiishi toka zamani mtaa uleule wa Silas Biniga, lakini nyumba ya nne mbele kwenye kona watu wamekuwa hawana wasiwasi nae kwani inasemekana ana asili ya Kitutsi ingawa ni chotara na uzuri wake watu wengi wameuchukulia tu kuwa huenda ni chakula ya wazee. Kwa hivyo hakuna ambaye amediliki kumgusa. Hivyo nataka nikajuwe habari zake", Col. Rwivanga alieleza.

"Hapana, usiende wewe, maana wewe ni afisa wa ngazi za juu na unajulikana hapa la pili wewe ni mwanajeshi. Kazi hii ni ya mpelelezi kama mimi. Tatu, nina kisasi naye. Naomba uniachie, usiku huu lazima nitapambana naye kama bado yuko hapa mjini na nitakujulisha habari zake baadae".

"Sawa Willy, kazi kwako, mzee naye alinieleza ndio zako hizo ikibidi msichana au mrembo".

"Zamani siyo sasa, sasa nimestaafu maana nimeoa lakini kwa msichana kama yule ambaye hatishiki na mtu kuuawa, nataka mimi mwenyewe nijuwe habari zake. Habari ulizonazo ni kwamba bado yuko mjini?".

"Jioni hii ameonekana akiendesha gari lake aina ya MB 190E. Na hilo ni gari lake hata kabla ya mauaji na kabla sisi hatujaingia hapa. La ajabu si sisi wala si Intarahamwe aliyegusa gari lake, ni jambo la kushangaza na limefanya nitaka kujuwa huyu binti vipi mambo yake".

"Basi niachie maMBO yake utayapata. Si bure huyU binti ni mtu hatari, na hatari sana".

ITAENDELA 0784296253   


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru