UCHU

BIBIANE

III

Baada ya Col. Gatabazi kumwelezea mipango yote kama walivyokuwa wamepanga na Jean, Nkubana aliomba gari ili akawachukuwe wenzake na kuanza kazi ya kumsaka Willy. Col. Gatabazi aliwapa gari aina ya Landrover 110 ya Jeshi ambayo hutumika kwa ajili ya wageni wa Serikali. Kwa sababu ya kazi maalum iliyokuwa ikiwakabili, kutokana na unyeti wa kazi hiyo, Col. Gatabazi aliwaachia gari hilo waendeshe wenyewe. Nkubana alikwenda, moja kwa moja akawaamsha wenzake, baada ya mazoezi makali, walioga na kupata chakula pale hotelini, kisha wakaanza kazi ya kupeleleza habari za Willy Gamba. 

Kutokana na maelezo waliyokuwa wamepewa na Col. Gatabazi, mara moja walijua kuwa Willy yuko Meridien Hoteli, mara baada ya kupata namba ya chumba chake cha kulala waliamua kwanza wakafanye shughuli nyingine ili wasubiri wakati mzuri wa kupambana na Willy Gamba ambaye pia walikuwa wakimhofia kwa kiasi fulani.

Baada ya kupanga vyema mipango yao ya kuhakikisha wanamuua Willy Gamba usiku huo. Walirudi hotelini wakapata kinywaji kidogo kwa ajili ya kujiweka safi. Ilipotimia saa nne hivi usiku wakaamua kwenda kwa wote kwa Col. Gatabazi kwa ajili ya mikakati ya ziada. Ni wakati huo walipokuwa wakielekea kwa Col. Gatabazi ndipo walipokaribia kuligonga gari la Willy Gamba bila wao kujuwa kuwa ndiye mtu anayepanga kumuangamiza usiku huo.

Kwa kasi ileile, gari hilo liliingia nyumbani kwa Col. Gatabazi, aliyekuwa nje ya nyumba yake akitafakari jinsi Willy alivyokuwa akiwanyima usingizi. alipowaona akawapokea kwa tabasamu kisha akawaongoza hadi kwenye sebule ya nyumba yake.

"Vipi mmepata habari zozote kuhusu Willy Gamba?", Col. Gatabazi aliwauliza baada tu ya kuketi kwenye makochi.

"Habari za Willy zote tunazo, huyo tutaanza biashara yake, atakuwa marehemu baada ya saa sita usiku", Nkubana alijibu kwa majidai na kujiamini.

"Nasema tena lazima muwe makini sana, huyo mtu ni hatari sana, na amri ni kwamba mara hii isishindikane, akionekana tu ua mara moja", Col. Gatabazi alisisitiza.

"Col. tafadhali usitutishe na huyo mtu wako, atakuwa hatari gari mbele yetu! Vipi una matatizo nini Col. Gatabazi?", Nkubana alijibu kwa mshangao huku vijana wake wote wanne wakicheka kwa dharau.

"Acha wasiwasi mzee, kazi ya Willy hesabu imeisha, amezoea kucheza na wafanzi leo atakutana na waalimu wa kazi", Felician alimhakikishia Col. Gatabazi.

"Ehe, Bibiane umemtaarifu kuwa tutakwenda nyumbani kwake leo?", Nkubana aliuliza.

"Bibiane ana taarifa zenu, na wakati ndio huu, twendeni basi mara moja, hiyo gari acheni hapa maana anakaa ileile nyumba yake", Col. Gatabazi alijibu.

"Ahaa, kweli gari tuache tu hapa, tutalipitia wakati wa kwenda mjini", Felician alijibu.

"Haya twendeni anatusubiri, lakini mjuwe kutokana na mipango ilivyo mimi nitawaacha pale nyinyi mtaendelea nae", Col. Gatabazi aliwaelza.

"Sawa hamna tabu", wote walijibu kwa pamoja na kuondoka kuelekea kwa Bibiane.


ITAENDELEA 0784296253   

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru