UCHU

 BIBIANE

IV

Wakati Willy anafika nyumbani kwa Bibiane. Col. Gatabazi alikuwa akifunguliwa lango la mbele nyumba hiyo akatoka na kuondoka akihofia matatizo aliyokumbana nayo kwa Luteni Biniga. Willy alichukuwa hadhari kubwa sana maana alichukuwa vifaa vya kazi si mchezo. Kwa vile nyumba ya Bibiane ilikuwa kwenye kona ya barabara mbili, Willy alibana kwenye kona moja na kuchungulia mbele ya nyumba na kuona lango likifunguliwa. Alimuona mtu mmoja akitoka na kukatisha barabara na kuelekea kwenye uchochoro na kutokomea. Willy alirudi nyuma kidogo na kuhisi kuwa sehemu ile ndiyo ilikuwa nyuma ya nyumba hii. Kwa hadhari sana alikwea ukuta uliozungishiwa vyuma vilivyochongoka juu. Kwa vile Col. Rwivanga alimweleza kuhusu hilo. Willy alikuwa amejitayarisha vizuri kabisa kwa lolote. Alikwea na kuchungulia ndani, baada ya kuangaza vizuri macho yake aliweza kuona kivuli cha mtu amebana kwenye ukuta wa nyumba hii karibu na upande wa pale alipokuwa yeye. Mtu huyu alikuwa amebeba bunduki kubwa. Hivyo, Willy alihisi ni mlinzi wa pale nyumbani.

Baada ya muda kidogo, Willy alimuona mtu mwingine anakuja akitokea upande wa mbele kuja upande huu ambao huyu mwingine alikuwa amebana. Willy alijining'iniza juu ya ukuta kwa nje ili asionekane huku macho yake yakiwa usawa wa ukuta. Yule mtu alikuja moja kwa moja mpaka usawa wa yule mwingine alipokuwa amesimama.

"Unataka sigara?", yule aliyekuja eneo hilo alimuuliza mwenzake.

"Sitaki, hao jamaa ndani si wamalize mambo yao haraka ili waondoke na sisi twende zetu, maana hapa tunapoteza muda na huku kazi yenyewe bado", yule wa pili ajibu.

"Mbona kama una wasiwasi, vipi unaogopa?".

"Kwanini nisiogope, mimi si binadamu bwana?".

"Acha woga wewe, wajuwa Kaisari alisema watu waoga mara nyingi hufa kabla ya tarehe ya vifo vyao kufika, komaa mtoto wa kiume", mwenzake alisema kwa kujiamini.

"Bwana, hebu nenda kalinde sehemu yako na umwambie huyo Nkubana aharakishe kutoka sehemu hii".

Baada ya kuelezwa, yule mtu aliyekuja sehemu hii kutoka mbele aliondoka kimyakimya kurudi kule alikotoka huku mwenzake akimsindikiza. Willy akatumia nafasi hiyo. Kama tumbili aliukwea ule ukuta haraka sana. Kufumba na kufumbua akaruka juu ya vile vyuma na kujitosa ndani bila hata kusababisha kishindo na kujibanza kwenye ukuta. Kwa vile Willy alikuwa amevaa nguo nyeusi pale alipokuwa amejibanza ilibidi umsogelee karibu sana ndipo uweze kumtambua maana upande huu wa nyumba hapakuwa na mwanga. Mara akamsikia yule mlinzi akirudi upande wake, kutokana na mazungumzo aliyokuwa ameyasikia alihisi hawa nao bila shaka walikuwa kundi lilelile kama alilopambana nalo kwa Luteni Biniga. Bila shaka walikuwa wamekuja kwa malipo kwa huyu mwanamke. Willy alijitayarisha na kujibanza kwenye ukuta utafikiri buibui. Yule mtu alikuja akinyata taratibu utafikiri alikuwa amehisi kitu. Willy alikuwa amebana kwenye kona kabisa ya upande wa pili wa nyumba. Huyu mtu alipofika hapo tu, kama Simba anapomrukia Swala, Willy alimtia kabali kwa nguvu zake zote. Yule mtu hakuweza hata kuguna maana kabali ile ilikuwa kali, na huku akitumia utaalam kumuua kimyakimya kwa kumnyonga, Willy alimuua yule mtu. Kisha, alimvuta mpaka kwenye ua wa nyumba na kumvua shati, akavua lake na kuvaa la yule mtu kwani ukubwa wa mwili na urefu walikuwa wanalingana. Akatwaa silaha yake ya AK 47 'Machinegun' ya Kirusi na kuelekea mbele.

Alipofika kwenye kona ya mbele, Willy alimuona yule mtu mwingine akichungulia dirishani, si mbali na aliposimama Willy. Willy alikohoa kidogo na yule mtu akageuka kuangalia. Alionyesha ishala ya kumwita. Na yule, akijuwa fika kuwa alikuwa mwenzake, alikuja haraka bila hadhari. Alipokaribia, na kwa ajili ya giza aliamini ni yule mwenzake, alianza kusema, "Huko ndani naona mambo yanaa...", kabla hajamalizia sentesi yake, Willy alimrukia na kumpiga karate ya shingo na kumuua palepale. Alianguka chini kwa kishindo, na Willy alipomrukia pale chini akammaliza. Baada ya Willy kumkagua alimkuta na Bastola mbili, moja yenye kiwambo cha sauti na nyingine ya kawaida. Vilevile alimkuta na kisu ambacho ukikibonyeza kinachomoka na kutoka urefu wa nchi tisa. Kile kisu kilikuwa silaha hatari sana ikitokea watu wanapigana huku mmeshikana. Willy alijihisi mtu mwenye bahati kwani silaha kama hii kama ingebidi kumenyana bila kujuwa kuwa mtu anayo anakuondoa duniani haraka sana.

Sasa Willy alikimbia mbele kuangalia kama kulikuwa na mtu mwingine, lakini hakukuwa na kitu. Alipozunguka upande mwingine tena hakuna kitu. Kisha akachukua dakika chache kuhakikisha kuwa hakuna hatari nyingine, na alipohakikisha ndipo alipokwenda pale dirishani alipokuwa anachungulia yule mtu wa pili. Dirisha lile lilikuwa sebuleni na lilikuwa wazi kidiogo. Pazia la dirisha lilikuwa limerudishiwa kidogo kiasi kwamba ungeweza kuona ndani na kusikia maneno yote yaliyokuwa yanazungumzwa.

Willy alishangazwa kuwaona wanaume watatu na mwanamke mmoja ambaye mara moja alimtambua kwani alikuwa Bibiane. Hawa wanaume wote walikuwa wametoa Bastola zao wakizungumza na yule mwanamke. Wawili walikuwa wamesimama na mmoja ameketi kwenye kiti kilichokuwa kinaangaliana uso kwa uso na alichoketi Bibiane.

"Nakwambia hivi, sisi tumetumwa kuja kukuua na huyo huyo bwanako Jean. Faida yako kwake imesisha sasa wewe ni mzigo na yeye hataki kubeba mzigo", yule aliyeketi alimweleza yule mwanamke huku akionyesha kwenye sura yake maudhi na usongo wa ajabu.

"Wewe unatania. Jean! hawezi kusema hivyo. Kwa yote niliyomtendea na jinsi tunavyopendana, Xavier sema jingine kama wewe na Col. Gatabazi mmeamua kuniua basi niuweni, msimsingizie Jean, Jean ni wangu wa kufa na kuzikana", Bibiane alijibu huku akionyesha sura ya hofu maana aliwajuwa hawa jamaa ni wauaji.

"Wanawake ni watu wa ajabu. Epa", yule mtu ambaye Bibiane alimwita Xavier alimwita mmoja wa wale waliosimama.

"Eee", yule mtu alijibu kwa woga vilevile.

"Siku zote nakwambia wanawake ni wajinga, wewe huamini. Huyu anafikiri eti Jean alikuwa anampenda, Jean alikuwa anamtumia tu kama chombo. Kwanza alikuwa anakutumia kwa mambo yake ya kazi zake za kumwingizia pesa na pili, anapokuwa huku Afrika alikuwa akijisaidia kutimiza haja zake za kimwili; hata siku moja hajawahi kukupenda. Pale tu wewe na Col. Gatabazi mlipomweleza kuwa wewe umemwona Willy Gamba na Willy Gamba kukuona mara moja alijuwa Willy Gamba atakutafuta na akikupata utatoa siri, na ukitoa siri si ndiyo mambo yetu yameisha! kwa hiyo, mara moja ametoa hukumu ya kifo kwako na sisi tumekuja kutekeleza amri. Kwa kweli ni uhalibifu kwa kiumbe kizuri kama wewe kuuawa, lakini wewe sasa ni mzigo kwetu nasi hatubebi mzigo," Xavier alieleza.

Kwa maelezo haya Bibiane alijua kweli hukumu imetoka kwa Jean na huo ndio ulikuwa mwisho wake. Pamoja na ujuzi wake wote wa kupigana hakuthubutu mbele ya Xavier na wenzake kwani aliwajuwa vizuri, walikuwa wabaya mara kumi yake, na alijuwa kuwa hao hawabembelezeki hivyo, alikata tamaa na hasira zikampanda dhidi na Jean na machozi yakaanza kumtoka.

"Ukionana naye mwambie atakufa kifo kibaya sana. Nami naamini kuwa huyo Willy Gamba anayemuogopa kweli ndiye atakayenilipia kisasi", Bibiane alisema huku akitetemeka kwa hasira.

Xavier alisimama na kurudisha kiti chake nyuma. Bibiane naye akataka kusimama. "Hapana, kaa hapohapo, usilete ujanja hapa. Huyo Willy baada ya muda si mrefu mtaonana ahera, nasikia huko watu huonana tena. Hamtapishana zaidi ya masaa mawili na yeye atakuwa marehemu kama wewe".

Willy, ambaye alikuwa anasikia na kuona yote haya akiwa dirishani, alipoangalia usoni mwa yule aliyeitwa Epa, akajuwa huyu ndiye akayemuua Bibiane. Aliangalia nafasi aliyokuwa, akajuwa angeweza kumpiga risasi Epa na yule mwingine, lakini si Xavier. Kwa vyovyote Xavier angemmaliza Bibiane, lakini hakukuwa na njia. Hawa walikuwa ni wauaji wataalam, tena huenda wa kulipwa. Hivyo, ilikuwa ni afadhali kwake kupambana na mmoja kuliko watatu na kwa maajabu ya Mungu angeweza kumponyesha Bibiane ambaye akili yake ilimweleza kuwa angeweza kuwa mtu muhimu kwake.

Xavier alimkonyeza Epa. Yeye akavuta kiti na kuanza kugeuka. Bibiane akafumba macho, lakini kabla Epa hajafyatua risasi, palepale Willy akiwa dirishani na mikono yake yote ikiwa na Bastola, alimpiga risasi ya kichwa Epa na yule mwingine kifuani, na Bibiane akajirusha nyuma ya kiti, Nkubana kama umeme akamimina risasi dirishani. Lakini Willy alikuwa tayari amejitupa chini na kujiviringisha na kisha kuchukua AK 47 akamimina risasi kama hamsini hivi kumtia kiwewe Nkubana. Haya mambo yote yalitokea haraka sana kama kufumba na kufumbua. Nkubana alipoangalia akajuwa Epa na Karekezi walikuwa wamekufa na hakujuwa wamezungukwa na watu wangapi. Alijirusha kwenye dirisha upande wa pili ambalo lilikuwa la kioo kitupu na kuangukia nje na kisha kujiviringisha tena. Bibiane alichukua Bastola iliyodondoka kutoka kwa Epa na kujaribu kumpata Xavier lakini naye alijitosa nje akaurukia ukuta wa mbele kwa nanma ya ajabu na kuangukia uapnde wa barabarani. Willy alipokimbia upande ule wa pili ili kumuwahi Nkubana alikuwa amechelewa, Xavier naye alikuwa ndio anaishia baada ya kuruka ule ukuta.

Bibiane alipoinuka pale alipokuwa amejitupa kumfuata Xaviar akajikuta anaangalia kwenye mdomo wa AK 47.

"Tupa silaha yako mama, uko chini ya ulinzi", Willy alimweleza Bibiane.

"Aheri ya Musa kuliko ya Firauni, Bila shaka wewe ni Willy Gamba".

"Naamini wewe ni Bibiane".

Willy alimshika mkono Bibiane na bila hata kumwelezana wanaelekea wapi, wakakimbia kwa tahadhari kuwa kutoka eneo hilo kabla askari na watu wengine hawajafika kuangalia kilichotokea hapo kwani mlio wa risasi za Ak 47 ulikuwa umetikisa eneo hilo na kusikika vibaya sana wakati huo wa usiku.

ITAENDELEA COL. NI AFISA WA JESHI MWENYE CHEO CHA KANALI 0784296253  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru