UCHUKASHESHE

XI

Nkubana aliamua kuwasiliana na Col. Gatabazi kwa simu ya upepo. Alipompata alikuwa tayari amewasili Goma na walikuwa wameanza mkutano. Nkubana alieleza kwa kirefu yote yaliyotokea na kisha akashauri. "Huyu Willy Gamba hajui nguvu zetu. Hivyo, ameamua kwenda kujinyonga huko Kibumba, mimi naelekea huko kwenda kuongeza nguvu na kuwashitua makamanda wetu ili tumkamate kabla hajaleta kasheshe zake".

"Sawa, fanya hivyo, Jean anahitaji kumuona akiwa hai", Col. Gatabazi alikubaliana na Nkubana na kumweleza shabaha ya bosi wao Jean.

"Vilevile nitazungumza na makamanda hapa ili waniruhusu tupeleke jeshi mpakani kumsaidia Luteni Nyamboma kudhibiti mpaka wa Zaire, mpaka hapo amri ya kuishambulia Rwanda itakapotoka. Sisi tuko tayari, naamini uamzi utatoka haraka ili kazi ianze alfajiri ya leo. Hebu ngoja kidogo usizime radio yako", Col. Gatabazi aliwaeleza wenzake mambo yalivyokuwa Gisenyi na jinsi ambavyo Nkubana alikuwa akihisi kuwa Willy ameelekea Kibumba. Mara moja Jean alisimama baada ya kusikia habari hii ya Willy kuelekea Kibumba. Haraka alichukua radio na kutoa maagizo kwa Nkubana.

"Sikia, sisi tunakuja huko sasa hivi, tutakuja kwa ndege yangu na mimi nitaondoka. Sasa hivi bado tunawasiliana na Kamanda Bazimaziki awahi uwanja wa ndege. Waeleze wakiwakamata Willy na Bibiane wasiwaue kwanza mpaka tufike, hao ni halali yangu", Jean alitoa amri.

"Unafikiri ni busara sisi viongozi wa juu kwenda huko?", Anatoile kabuga alihoji.

"Bila shaka, huko ndiko yaliko majeshi yetu na ndiko tutakapotoa amri", Jean alieleza msimamo wake.

"Mimi pia nafikiri tuwe pale wakati wanajeshi wanaelezwa kukaa tayari kwa ajili ya kuanza vita alfajiri, hii itawaongezea mori", Jenerali Kasongo alijibu.

"Na mimi nimefurahi sana kwa uamzi huo, kuanzia sasa ofisi yetu kubwa ya kuratibu shughuli za vita itakuwa hukohuko Kibumba, maana ndiko kwenye vifaa vyote, sioni sisi tutafanya nini hapa wakati kila kitu chetu kiko kule", Col. Gatabazi alieleza kwa sauti ya juu.

"Sawa, wengi wape", Kabuga alijibu.

Kisha wakawasiliana na Col. Marcel Bizimaki, ambaye ni Kamanda wa jeshi la Akazu wakitumia njia ya simu ya satellite, wakamweleza kuwa wote walikuwa wanarudi hapo tena, kwa ajili ya kutoa mwongozo na ruksa ya kuanza mapambano dhidi ya adui alfajiri ile. Vilevile, alielezwa aweke vikosi vyake vyote kwenye tahadhari ili waweze kumsaka na kumkamata Willy Gamba akiwa hai.

"Karibuni, nitawapokea na nitawaweka kwenye nyumba ya mkufunzi wetu mkuu. Kamanda Moris ambayo ina ulinzi mkali pia inalindwa na mitambo ya kisasa ya usalama. Na mtakapokuwa pale kwake itakuwa rahisi kwenu kuona kwa macho jinsi majeshi yetu yanavyosonga mbele kupitia mitambo ya kisasa kabisa", Col. Bizimaziki alitamba.

Kundi zima liliondoka kuelekea uwanja wa ndege, likiwa tayari kuelekea Kibumba, ambako kuna umbali usiozidi dakika kumi kwa ndege, Jean alifikiria kuwa ni vizuri kuwa na ndege yake karibu, ikiwa kwa bahati mbaya kikatokea kitu na kutakiwa kuondoka ghafla na kujisalimisha aweze kufanya hivyo kwa ndege yake. Wakati wanaelekea uwanja wa ndege. Co. Gatabazi aliwasiliana tena na Nkubana. 

"Uko wapi sasa?".

"Nimekwisha kuwasili Kibumba na sasa naelekea kwenye lango kuu la kuingilia ndani, nimewasiliana nao kwa radio wananisubiri", Nkubana alimweleza Col Gatabazi.

"Sawa, kazi yako kubwa ni kumkamata huyo Willy na kikaragosi chake huyo Bibiane na uwalete kule mlimani ilipo nyumba ya Kamanda Moris, sisi tutakuwa huku muda si mrefu", Col. Gatabazi aliagiza.

"Nitafanya hivyo afande. Mara hii kaingia mkenge yeye mwenyewe", Nkubana alijibu.

"Lakini mtu huyu ni hatari sana, naomba umwambie Kamanda Bizimaziki mchukue tahadhari kubwa sana. Hata tulipofika sitaki makosa yatokee", Col. Gatabazi alisisitiza.

"Sawa afande, tutafanya hivyo, lakini mtu mmoja na mwanamke mmoja wanaweza kufanya nini mahali kwenye kambi kubwa ya jeshi kama Kibumba?", Nkubana alihoji.

"Wewe chukua hadhari ya hali ya juu huyu mtu si wa kawaida", Col. Gatabazi alisisitiza na kuzima radio.

Nkubana alifahamu kuwa viongozi wake walikuwa na mashaka na Willy, lakini Nkubana yeye hakuna na wasiwasi. Aliamini kuwa huu ndio ulikuwa mwisho wa Willy Gamba. Ulinzi na uwezo wa kambi ya Kibumba ulikuwa mkali mno, kiasi kwamba ilikuwa vigumu sana kwa mtu mmoja kuingia na kutoka salama. Gari lilisimama na kumwondoa Nkubana katika mawazo yake. Walikuwa wamefika kwenye lango kuu na kusimama kama ilivyo sheria ya kusimama na kukaguliwa kabla ya kuingia ndani ya ngome hii.

Nkubana alipoangalia saa yake ilikuwa yapata saa sita na nusu usiku.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru