DUWE; SHUJAA ALIYETUMIA DAKIKA 15 KUPAMBANA NA MAMBA ZIWANI

Waswahili wanasema, hujafa hujaumbika, msemo huu una maana kubwa sana kwa binadamu hususan wale waliopatwa misukosuko ama majanga makubwa kama Ndugu Fidelis Duwe (pichani), mkazi wa Mbamba-Bay, Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma.

Duwe kijana shupavu mwenye mwili wa wastani uliojengeka alikumbwa na dhoruba kubwa iliyosababisha baadhi ya viungo vyake vya mwili kubaki majini wakati akikabiliana na Mamba hatari aliyemkamata ili awe kitoweo chake.

Uhodari wa Duwe umesababisha awepo kwenye historia ngumu ya watu waliobahatika kuponea kwenye tundu la sindano, unaweza kusema chupuchupu kuliwa na Mamba mwenye njaa kali. Alikamatwa na Mamba wakati akiogelea ndani ya Ziwa Nyasa, katika eneo liitwalo Zambia (siyo nchini Zambia).

Duwe anasema ilikuwa jioni, wakati alipokwenda Ziwani kwa ajili ya kuoga kama ilivyo kawaida ya wananchi wa Mbamba-Bay, wakati anapaka sabuni mwilini ghafla alinaswa na Mamba mwenye njaa kali na akaanza kumkata viungo vya mwili wake kwa meno makali.

“Baada ya kupaka sabuni, nilitaka nirudi ili niondoe sabuni mwilini, ghafla nilikamatwa na Mamba, tukaanza kushindani, wakati yeye analazimisha kunipeleka chini mimi nilikuwa najaribu kumvuta ili nisiende chini”, anasema na kuongeza kuwa alipambana na Mamba huyo kwa dakika 15.

Anasema wakati anaendelea kupambana na Mamba huyo ndani ya maji alisikia sauti za wavuvi wakipita huku wakiimba ndani ya Mtumbwi wao, bahati nzuri alizifahamu sauti zao hivyo akapiga kelele kuomba msaada.

“Waliniuliza wewe unafanya nini hapo, kuna Mamba wakali sana hapo, mimi niliwaambia kuwa hao Mamba unaosema mmoja kanikamata ndio niko naye hapa, kwanza walidhani nafanya dhihaka, lakini baada ya kutafakari walikuja na kuniokoa, Mamba akaniacha na kukimbia”, anasema Duwe.

Anasema pamoja na kuokolewa kutoka midomoni mwa Mamba, alikuwa amejeruhiwa vibaya, mikono yake yote ikiwa imekatwa mara tatu na damu nyingi zikimvuja. Hakuna alieamini kuwa atapona kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo wakati huo.

Duwe anasimulia kuwa baada ya kuokolewa kutoka majini na wavuvi aliowataja kwa majina ya Benard Mpay na Sikuzani ambaye sasa ni marehemu, alipelekwa haraka hospitali ndogo ya Mbamba-Bay, ambako alipata huduma ya kwanza na baadaye akapelekwa Liuli ambako alipata huduma ya uhakika.

Mungu alinisaidia sana, baada ya kuokolewa kutoka midomoni mwa Mamba, nilipelekwa hospitali, walinifanyia huduma ya kwanza, lakini hawakuwa na vifaa vya uhakika, bahati nzuri siku hiyo kulikuwa na Meli, ikanipeleka Liuli ambako nilipata huduma ya haraka, nikashonwa na kuungwa mifupa ya mikono yangu, leo niko hai”, anaesema na kuonyesha majeraha makubwa aliyopata mwilini.

Kuhsu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa, Duwe anasema, Malawi inajaribu kufurahisha umma, kwa kuwa hakuna asiyejuwa kuwa mpaka halisi wa nchi hizi yaani Tanzania na Malawi ni katikati ya Ziwa Nyasa. Hivyo amewataka viongozi wa nchi hizi kukaa katika meza ya mazungumzo.

Anasema ni kweli kabla ya Nyasa kuwa WIlaya, walikuwa wakipata baadhi ya huduma za jamii kwa karibu kutoka Malawi, lakini wamalawi pia walipata huduma zingine kutoka Tanzania kama ilivyo sehemu zingine zilizopakana na Tanzania.

Duwe ameiomba serikali kuongeza kasi ya miundombinu, kwani hivi sasa wananchi walioko sehemu hiyo wanapata mawasiliano ya karibu kutoka Malawi, tofauti na Tanzania hivyo likitokea jambo lolote Tanzania hawawezi kujua kama ilivyo kwa Malawi.

IMEANDIKWA NA NYAKASAGANI MASENZA 0784296253
 


MWANNDISHI MWANDAMIZI WA ZBC, MSANGU SAID AKIONGEA NA NDUGU FIDELIS DUWE, KANDO YA ZIWA NYAMA, MAHALI AMBAPO ALINUSURIKA KULIWA NA MAMBA..


SEHEMU YA ZIWA NYASA, MAHALI AMBAPO NDGU FIDELIS DUWE ALIKUWA AKIOGA KABLA YA KUKAMATWA NA MAMBA NA HATIMAYE KUOKOLEWA NA WAVUVI.


HAPA NI ZIWA NYASA,  SEHEMU YA MBAMBA-BAY KARIBU NA MPAKA WA MALAWI.


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru