KASHESHE

X

Willy na Bibiane walitambaa chini kwa chini kama nyoka na hatmaye wakayafikia majengo yaliyokuwa upande wa pili kutoka sehemu waliyotokea.

"Haya ni maghala ya kuhifadhia silaha, ni makubwa sana yana silaha nyingi za kisasa na vifaa vya kila aina vya kijeshi, zikiwemo silaha mpya za kisasa kabisa kwa ajili ya vita", Bibiane alieleza.

"Itabidi tuingie ndani kwanza ndio tutajua cha kufanya", Willy alieleza.

"Mlango uko upande ule kabisa, yaani unatazamana na majengo ya upande ule kabisa, ambako ndiko kuna ofisi na nyumba za kulala askari. Ulinzi upande ule ni mkali sana na lango la upande ule linafunguliwa kwa chombo maalumu ambacho kinahifadhiwa kwa mmoja wa makamanda wa juu wa jeshi lao", Bibiane alieleza.

"Kuta za maghala haya zimejengwa kwa teknolojia gani, au wametumia nini kujenga, tofali za simenti ama mabati?", Willy aliuliza.

"Kampuni moja ya Afrika Kusini iitwayo Super Frame ndiyo iliyojenga maghala haya pamoja na mabanda yote unayoyaona tena kwa muda wa mwezi mmoja tu. Kila kitu kililetwa hapa kwa helkopita kubwa zilizokodishwa kutoka Urusi na hapa waliunganisha tu hizi kuta na kuezeka. Wakati wa joto  kuta zake zinaleta ubaridi na wakati wa ubaridi kuta hizi zinaleta joto, hivyo sijui zimetengenezwa kwa teknolojia gani?", Bibiane alijibu.

"Nimeelewa, baada ya hayo maelezo yako, teknolojia hii imetoka Marekani na inatumika kwa kujenga nyumba za gharama nafuu, lakini zenye kudumu kwa muda mrefu hata zaidi ya matofali ya saruji", Willy alijibu.

"Wewe kuna kitu usichokijua katika Ulimwengu huu", Bibiane alitania kisha akaendelea. "Sasa tunafanyaje Bwana kujua?".

"Utaona, sasa hivi tutaingia ndani", Willy alijibu kisha akafungua na kupekua kwenye mkoba wake, akatoa kifaa kimoja kilichofanana na kalamu lakini hiki ni kinene kidogo. alikifungua akatoa mfuniko wa mbele na kukifungua tena nyuma, baada ya kukifungua zilitoka betri mbili ndogo sana, Willy akazikagua kuona kama ziko sawa, kisha akazirudisha.

"Haya, rudi nyuma hiki chombo kinatoa miale aina ya leza bimu na hii miale ina nguvu za ajabu na miale hii inakata huu ukuta utadhani kisu ndani ya siagi, rudi nyuma yangu kabisa", Willy alisema Bibiane akarudi nyuma kwa hofu.

"Nasubiri kuona", Bibiane alitania.

"Subiri utaona japokuwa umeingiwa na hofu, lakini usiogope maana hapa hakuna ujanja zaidi ya kumuomba Mungu".

Willy alisukuma nyuma ya kile chombo kama mtu anavyosukuma kalamu wakati anataka kuandika, na mara moja miale myekundu ilijitokeza Willy akaielekeza kwenye ukuta na taratibu alikata saizi ya mlango sehemu ile walipokuwa, alipomaliza akakizima kile kifaa chake.

"Mbona hujakata chochote?", Bibiane aliuliza.

"Subiri kidogo, hii ni sawa na sayansi inayotumiwa na madaktari siku hizi kupasua mwili wa binadamu, wewe uko wapi mama, wenzio twaelekea karne ya ishirini na moja, karne ya sayansi na teknolojia wewe bado upoupo tu. Siku hizi mtu anafanyiwa opresheni, anapasuliwa tumbo, halafu baada ya saa moja anarudi nyumbani mwenyewe na haoni sehemu iliyopasuliwa", Willy alimkoga Bibiane aliyekuwa anashangaa.

Willy aliiangalia saa yake kisha akaufungua mkoba wake akatoa kitu kama bawaba kisha akaipachika kwenye ukuta kikanasa.

"Hiyo ni sumaku?", Bibiane alihoji.

"Ndiyo, inashika kitu chochote hata kama ni mbao".

"Ama kweli wewe mkali Willy, sikutegemea kabisa".

"Au vipi", Willy alijibu. Huku akiitumia ile bawaba alivuta taratibu na ile sehemu ikachomoka na kuacha uwazi wenye ukubwa wa mlango.

Willy na Bibiane walijikuta wanaangalia ndani ya ghala kubwa sana lililojaa silaha.

"Ingia sasa, mbona kama umepigwa na radi!" Willy alimweleza Bibiane.

"Bado nashangaa, hakika mambo uliyonionyesha ama kweli ujuzi huzidiana", Bibiane alijibu huku akiingia ndani ya ghala la silaha.

Willy akitumia chombo kingine kwa kukishikanisha na ile bawaba, ile bawaba ilitoka akaiweka upande mwingine wa kipande cha ukuta alichokuwa amekata, kisha na yeye alipoingia ndani ghala alivuta kile kipande cha ukuta kwa nguvu zake zote na kukipachika mahali pale tena. Mtu yeyote angepita pale kwa macho tu bila darubini asingejua kuwa pale pamekatwa. Bibiane hakuna na neno la kusema isipokuwa kuangalia ile sehemu tu.

"Wewe ni mkali kwelikweli", Bibiane alirudia kusema.

"Kwa mambo mengi si hili tu", Willy alisema kwa kumwemwesa.

wakiwa ndani Willy alishangaa kuona ghala kubwa sana la silaha. Kwa vile taa zilikuwa zikiwaka kwa ndani hawakuamini macho yao. Hata Bibiane hakujuwa kuwa Akazu walikuwa wamejiimarisha kiasi hiki. Mara ya mwisho Bibiane kufika hapa ilikuwa kama miezi mitatu iliyopita na katika hii miezi mitatu silaha nyingi, yakiwemo makombora ya masafa marefu na mafupi, vifaru, ndege aina ya MIG 21 na 23. mizinga, magari ya kivita, helkopita za kivita zilikwishaletwa eneo hili! Hakika ilikuwa ajabu na kweli.

"Hawa watu wanajipanga kupigana na Rwanda tu ama nchi nyingine jirani?", Willy aliuliza kwa mshangao.

"Nia yao ni kupigana na serikali ya Rwanda basi, hakuna kingine", Bibiane alijibu na kuongeza. "ila wanataka kuyapiga majeshi ya RPF kipigo kitakatifu, wasijejaribu tena mara baada ya kufukuzwa Rwanda".

"Fedha za kununulia vifaa hivi vyote watakuwa wamepata wapi?", Willy aliuliza.

"Miaka yote hii unafikiri walikuwa wakifanya nini?, wamewaibia wananchi mali zao zote. Akazu na Jean ni matajiri ajabu. Wana uhusiano na Rais wa Zaire na kiongozi wa waasi wa UNITA kule Angola. Almasi za Angola na Zaire dalali wake ni Jean. Sasa wewe fikiria wana utajiri wa kiasi gani?", Bibiane alijibu.

"He, sasa nimekuelewa mama".

"Kila kitu kilipangwa kwa ustadi wa hali ya juu. Hii ingewezekana kuchukua silaha zao kwa kutumia muda mfupi sana kwama wangeshambuliwa. Willy aliamini kuwa hii kweli ilikuwa kazi ya askari wa kukodishwa kwani hakika hili lilikuwa ghala la silaha lililotayarishwa na kupangwa na watu wenye ujuzi wa juu sana.

Willy na Bibiane walitembea kwa hadhari lakini kwa haraka wakijificha ndani ya vivuli vya zile silaha. Waliziangalia silaha hisi kiasi kwamba walianza kusahau kilichowaleta hapa.

"Unayaona makombora haya Willy", Bibiane alimwonyesha Willy makombora yaliyotengenezwa Urusi. Kisha akaendelea. "Haya makombora ni aina ya SAM 16 yalitekwa na majeshi ya Ufaransa wakati wa vita vya Ghuba, Februari 1991 na kupelekwa kwenye maghala ya silaha huko Ufaransa lakini kutokana na mahusiano wa karibu kati ya Jean na viongozi w ngazi za juu wa Ufaransa waliamua kumuuzia Jean makombora hayo. Katika makombora haya yamo yaliyotumika kuipiga ndege iliyokuwa imewabeba marais wa Rwanda na Burudi Aprili 6, 1994. Ni Jean na Akazu ndio waliamru rais auawe kwa sababu alikuwa ameanza kwenda kinyume na maagizo yao wakati wa mkutano wa Arusha, nakumbuka niliwahi kukueleza".

"Kama ndivyo, basi hawa Akazu na Jean ni wabaya kwelikweli, sasa naamini", Willy alisema huku hasira zikimpanda dhidi ya watu hawa.

"Lililobaki sasa ni kuziteketeza silaha hizi zote, naamini kuwa jeuri na nguvu ya Jean na Akazu tutakuwa tumeimaliza", Bibiane alieleza.

"Mkuki wa nguruwe, kwa binadamu mchungu, itabidi sasa tutumie yale mabomu yako aliyokuletea Jean, maana kazi kama hii ndio saizi yake", Willy alishauri.

"Unafikiri kwanini nilisema tuyachukue, nilijua. Kwanza ni madogo, na pili yana nguvu kubwa ya ajabu. Ghala kubwa kama hili, matano au sita yanaliteketeza kabisa na hakibaki kitu. Hili senduku linatosha kuiteketeza Kigali nzima. Nia ya Akazu ilikuwa wakishindwa mpango huu basi waiteketeze Kigali nzima na vyote vilivyomo bila kujali maisha ya watu", Bibiane alieleza.

Willy alimwangalia Bibiane kwa jicho kali, baada ya kutafakari akaelewa kwanini Willy alibadilika vile, ikamlazimu Bibiane kubadili maneno. "Haya tuyatege, nafikiri ulikuwa unasoma maelezo sasa unajua nini cha kufanya".

"Bila shaka", Willy alijibu sasa akiwa makini tayari kwa kazi. Kwa hesabu zake alitega mabomu ambayo alihakikisha angeteketeza kila kitu ndani ya lile ghala. Bila kushitukiwa walitoka kwa kupitia sehemu ileile na kisha wakairudishia ile sehemu ya ukuta kiasi kuwa hakuna ambaye angefikiria kuwa kuna mtu aliyewahi kupitia pale.

"Umesema kama ukitumia hii saa ya kulipua haya mabomu unatakiwa kuwa umbali gani, nina maana haya mabomu tuliyotega", Bibiane aliuliza huku wakiambaa na ukuta kuelekea kwenye mabweni ya kulala askari.

"Umbali usizidi kilomiota moja", Willy alijibu.

 ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru