UCHUGISENYI

VIII

Willy Gamba na Bibiane walisafiri salama kutoka Kigali mpaka Gisenyi bila kukutana na kituko cha aina yoyote Barabarani. Lile gari lenye alama ya Msalaba Mwekundu liliwafanya wasafiri bila kupata usumbufu na habari zilikuwa zimetumwa mapema na wale askari watatu waliotumwa kutangulia mbeke ili lile gari la maofisa wa Msalaba Mwekundu lisibugudhiwe. 
Walipofika Ruhengeri walipumzika huku kila mmoja wao akili yake ikifanya kazi jinsi ya kukabiliana na jambo lililokuwa mbele yao. 

Baada ya mapumziko ya saa moja hivi, Willy na Bibiane waliendelea na safari yao na kuwasili Gisenyi saa nane za mchana. Moja kwa moja walikwenda Hoteli Meridien-Izuba, ambako walipanga kuonana na maofisa ambao Col. Rwivanga alikuwa amewapasha habari waonane nao na wawape habari kamili kuhusu uhalifu unaofanywa huko Gisenyi na Kibumba, ili kama walikuwa wamebahatisha kupata habari zozote wazipate hapo.

Meridien Hoteli Izuza ilikuwa moja ya hoteli nzuri sana ingawa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda vilikuwa vimeiathiri kidogo hoteli hii, lakini ilibaki kuwa safi pamoja na misukosuko ilivyokuwa sehemu hii. Ikiwa kwenye ufukwe wa Ziwa Kivu, mpakani mwa Zaire, huku kwa mbali ukiangalia milima ya volkano ya Virunga, kweli Meridien-Izuda palikuwa mahali pazuri sana pa kupumzika.

"Umepapenda hapa?", Bibiane alimuuliza Willy Gamba.

"Mbona wewe unapenda kusoma mawazo yangu?", Willy aliuliza.

"Ubaya uko wapi Willy, fikiri kama tungekuwa tunakuja hapa kwa ajili ya mapumziko na si hii kazi ya hatari, huoni kuwa ingekuwa raha sana, mimi naona tungestarehe sana", Bibiane alijibu.

Huku akitabasamu Bibiane alitoa mkoba wake ndani ya gari huku Willy akijibu. "Sawa mama umeshinda".

Baada ya gari la Msalaba Mwekundu lililokuwa likitumiwa na Willy na Bibiane kusimama, askari wanne walielekea kwenye gari hilo, walipofika karibu mmoja wao moja kwa moja akauliza. "Natumaini nyinyi ni Bwana na Bibi George Mambo wa Msalaba Mwekundu kutoka Makao Makuu Nairobi?".

"Bila shaka", Willy alijibu bila kusita huku Bibiane amejikausha utafikiri kweli alikuwa mke wake, baada ya kutambulishwa vile, Willy alitambua kuwa huyu mwanamke alikuwa kweli amefundishwa vizuri mambo ya upelelezi maana Willy hakumweleza mapema jinsi ambavyo wale askari wangetambulishwa hapa. Kazi yote hii ilikuwa imefanywa na Col. Rwivanga.

"Kamanda Kasubuga anawasubiri pale ofisini kwake", yule askari alimweleza Willy Gamba.

"Twende", Willy alimweleza Bibiane.

"Hapana, wewe nenda tu, mimi nitakusubiri hapa", Bibiane alijibu na Willy akaelewa maana na sababu ya Bibiane kubaki pale, akafurahi moyoni kuwa kweli alikuwa amepata mshirika katika kazi.

Kamanda Kasubuga alikuwa mtu mwenye rika la Willy na baada ya Willy kuingia ofisini kwake aliinuka kwenye kiti alichokuwa amekaa akisoma faili moja hivi, huku akitabasamu akamlaki Willy.

"Karibu sana", Kamanda Kasubuga alimkaribisha Willy.

"Asante", Willy alijibu huku wakishikana mikono na Kamanda Kasubuga alimwonyesha ishara yule askari aliyemleta Willy awape faragha kidogo, yaani aondoke awaache peke yao.

Baada ya yule askari kutoka Kasubuga alisema, Lo! Bwana Willy Gamba ni wewe huyu, Sifa zako na wewe mwenyewe hufanani. Col. Rwivanga amenieleza yote na mimi nikamweleza kuwa nimekusikia sana nilipokuwa Tanzania. Mimi nimefanya kazi na Jeshi la Tanzania na vyeo vyangu vyote mpaka hiki cha umeja nimevipata nikiwa Tanzania".

"Alaa! nashukuru sana", Willy alijibu na kuketi kwenye kiti.

"Oke, bila kupoteza wakati, habari kutoka kwa kijana wetu ambaye juzi tu tumeweza kumnunua kutoka katika jeshi la Zaire linalolinda mpaka na sisi zinaeleza kuwa leo hii yapata saa kumi na mbili na nusu asubuhi waliwasili watu wawili upande ule wa Zaire na kupokelewa kwa heshima zote za kijeshi na kisha wakaondoka kuelekea kwenye makambi ya wakimbizi kule Kibumba. Baada ya maelezo ya jinsi wale watu walivyofanana tulielewa mara moja kuwa mmoja wao alikuwa Col. Gatabazi. Hivyo, Col. Gatabazi kafika na yuko Kibumba", Meja Kasubuga alieleza.

"Hizo ni bahari njema sana, sasa ngoja na sisi tupumzike halafu giza likiingia na sisi tutakwenda Kibumba", Willy alijibu huku Meja Kasubuga akimwemwesa.

"Sawa mzee, ila tumewawekea chumba kimoja maana ni mimi tu ninajua wewe ni nani, hawa askari wengine wote wanajua kweli wewe ni afisa wa Msalaba Mwekundu na kwamba kwa vile unajua utakaa Rwanda kwa muda mrefu umekuja na mke wako", Meja Kasubuga alimweleza Willy.

"Hapa taabu", Willy alijibu kwa mkato.

"Safari ya Kibumba, tumeagizwa na Mkuu wetu kuwa tufuatane, maana siku zote nimetaka kuvuka na kikosi changu cha hapa lakini nimekuwa nakatazwa, lakini leo nimeamriwa tufuatane wote, sijui safari itakuwa saa ngapi?".

"Sijui, tutaangalia wakati huo si na wewe unakaa hapa hapa hotelini?".

"Ndiyo mzee, niko chumba namba 110, nyie mtakuwa nambari 220 kwenye vyumba vinavyofuata".

"Sawa", Willy alijibu na kuaga. Aliporudi pale kwenye gari alimkuta Bibiane anapiga soga na wale askari.

"Tupelekeni chumba namba 220", Willy aliwaeleza wale askari.

Askari mmoja aliingia ndani ya gari baada ya kushusha mizigo yao, akawapeleka kwenye banda lililokuwa na chumba nambari 220. Yule askari alipoondoka Bibiane akasema, "Kwa vile kuna kitanda kimoja tu wewe utalala ng'ambo ile na mimi ng'ambo hii".

"Lo, kumbe ulikuwa unajidai bure, sasa umeanza masharti".

"Si tulisema kazi kwanza?", Bibiane alijibu huku akifunga mlango kwa funguo na kuanza kuvua nguo huku akiendelea kusema, "mimi nitaoga kwanza.

"Sawa mama", Willy alijibu huku mawazo yake yakiwa tayari yameanza kupanga mipango ya usiku ule. "Tukimaliza wote kuoga tuitishe chakula kidogo halafu tupumzike angalau kwa masaa mawili ndipo safari ya Kibumba ianze", Willy alimwambia Bibiane.

"Amri itatoka kwako baba, mimi kazi yangu ni kutii amri tu", Bibiane alijibu huku sasa akiwa amevua nguo zote pale kitandani.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru