KASHESHE
VII
Ilipofika
saa tano kamili za usiku, Willy Gamba na Bibiane walikuwa tayari wamewasili
Kibumba. Bibiane alizijua vizuri njia za vichochoro za sehemu hii. Hivyo,
walifika bila tatizo lolote. Bibiane alimuonyesha Willy sehemu yalipo maghala
makubwa ya silaha ambayo baada ya Willy kuyaona, alitaka waanzishe mapambano
dhidi ya watu wakiwa kwenye maghala hayo kwani aliamini hapo ndipo nguvu kubwa
ya Akazu ilikuwa imewekwa.
"Sehemu
hii inalindwa sana", Bibiane alimwambia Willy baada ya kutoka kwenye msitu
na kuona kambi kubwa ya kijeshi ambayo ilimshangaza hata Willy.
"Walijenga
lini kambi kubwa ya jeshi kama hii?", Willy aliuliza kwa mshangao.
"Hapa
kulikuwa na kambi ya jeshi la Zaire, na Akazu walipewa kambi hii baada ya
matukio makubwa ya Rwanda, na mara moja wakaleta vifaa vyao vya kivita na
kuifanya kuwa kambi ya jeshi ya kisasa kabisa. Ina kila kitu kama unavyoona,
taa, maji, mawasiliano, yaani kuna kila kitu cha kisasa nakwambia. Hata maafisa
wa mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia wakimbizi wanapotokea hapa kwa
bahati mbaya wanaamini ni kambi ya jeshi la Zaire, maana kambi za wakimbizi
ziko kilomita moja tu kutoka hapa upande ule wa kilima, hata wakiuliza basi
huambiwa kuwa hii ni kambi ya jeshi la Zaire, na raia hawaruhusiwi kabisa kusogea
karibu na kambi hii", Bibiane alimwambia Willy, ambaye wakati huo alikuwa
ameshikwa na mshangao.
"Maghala
ya silaha ni yapi?", Willy alihoji huku akichungulia kuangalia vizuri
kambi hii akitumia kiona mbali. Bibiane alitumia nafasi hiyo kumwelekeza kila
kitu. Kwa vile kambi ilikuwa ikiwaka taa utafikiri mchana waliweza kuona kila
kitu vizuri kabisa.
"Kambi
hii yote imezungukwa na seng'enge yenye umeme wenye nguvu kubwa unaoweza kumuua
hata tembo haraka kama inzi, yaani ukigusa tu unakaushwa kwa umeme kama nyama",
Bibiane alieleza.
Willy
aliamua kwanza walifiche gari la jeshi walilokuwa wakitumia kwenye msitu ule,
wakachukua mizigo yao ya kazi na kasha wakatafuta njia ya siri kwa ajili ya kuingia
pale kambini.
"Hii
kambi inaweza kuwa na askari kama wangapi kwa kukisia kwako?", Willy
alimuuliza Bibiane.
"Eeeh…
wanafika elfu tano na zaidi, wenye mafunzo ya juu sana, wale askari wa kikosi
cha Rais wako hapa pia na askari wenye ujuzi mkubwa. Kuna makomandoo waliofuzu
vizuri kama mia tano, halafu kuna askari wa kawaida wenye mafunzo mazuri
vilevile zaidi ya elfu nne na mia tano. Hivyo, kuna askari kama elfu kumi hapa,
na ndilo tegemeo kubwa la Akazu kurudi madarakani. Lakini kusema kweli wanaweza
kushika tena madaraka, ukichukulia ari, uwezo na vifaa vya kijeshi walivyo
navyo", Bibiane alimweleza Willy.
KKwa kweli
kambi hii ilikuwa kubwa sana kiasi cha kumtia hofu Willy Gamba, kwani
hakutegemea kabisa kukutana na kambi kubwa ya adui yenye idadi kubwa ya askari kama
hii.
"Hebu
nipe muda nifikiri kabla ya kujitumbukia huko", Willy alimwambia Bibiane.
"Hatuna
muda Willy, hatuna muda kabisa kabisa, lazima ufahamu kuwa tunatafutwa na adui,
na wakihisi tuko huku hakika tumekwisha", Bibiane alilalamika wakati Willy
akimwangalia tu bila kusema kitu.
Baada ya
Willy kutafakari kwa dakika kadhaa alilazimika kumwambia Bibiane.
"Nikisema nahitaji muda wa kufikiri nina maana dakika tano tu, lakini niwe
peke yangu, naamini sasa umenielewa?", Willy alimwambia Bibiane huku
akielekea kwenye kichaka kilichokuwa hatua chache kutoka walipokuwa wamesimama.
"Kumbe
unaamini uchawi, wewe unakwenda kuloga, mimi nifanyeje sasa?", Bibiane
alimkebehi Willy.
"Jifanyie
lolote kwa imani yako", Willy alijibu huku akipotelea kwenye kichaka.
Inasemekana katika hali kama hii ya hatari Willy husali sana akimuomba Mungu. Baada
ya dakika kadhaa Willy alirudi alimkuta Bibiane akiwa amebeba silaha za kiasi
chake akiwa tayari kwa kusonga mbele kwa ajili ya mapambano dhidi ya jeshi la Akazu.
"Ehe,
sema sasa tunasonga mbele ama tunarudi nyuma kumsubiri Col. Rwivanga?",
Bibiane aliuliza.
"Tunaendelea",
Willy alijibu kwa mkato huku akitoa vifaa vyake vya kazi kwenye mkoba wake.
Willy
alibeba silaha na vifaa vilivyokuwa vimebaki, na kwa hadhari kabisa wakaanza
kuelekea kwenye ile seng'enge yenye umeme.
"Mara
nyingi ulinzi si mkali sana upande wa ua kwa kuwa wanaamini hakuna kitu
kinachoweza kuzipenya hizi seng'enge bila kufa kwa umeme, maana kila siku
wanyama wanakutwa wamejikaanga wenyewe. Vilevile, kitu chochote kinachokaribia
mita moja ishara inaonekana kwenye chumba maalum kinachodhibiti usalama wa kambi
hii kama kuna kitu kinasogelea seng'enge mara moja hatua za haraka za usalama
wa kambi zinachukuliwa.
"Yote
haya yamefanywa lini?", Willy alitaka kujua.
"Sababu
ya pesa Willy, pesa, askari wa kukodishwa kutoka Afrika Kusini ndio wameleta
vifaa na teknolojia hii iliyopo hapa kambini. Tukifanikiwa utajionea
mwenyewe", Bibiane alidokeza.
Walipokuwa
mita kumi kutoka usawa wa seng'enge walisimama na Willy alitoa kifaa maalum
kwenye mkoba wake. "Tutapita chini ya seng'enge, baada ya kuchimba
handaki".
"Itatakiwa
liwe mita mbili kwenda chini, vinginevyo tutakaushwa kama mikaa", Bibiane
alisema huku akionyesha wasiwasi.
"Hili
bomu", Willy alisema akiwa ameshika bomu dogo lenye ukubwa wa yai la kuku.
"Lina uwezo wa kuchimba handaki la urefu wa mita kumi na upana wa mita
tatu, na kina cha mita tatu unasemaje?".
"Sikupingi,
kwa teknolojia ya sasa hata mimi nimeona maajabu mengi katika vifaa vya vita,
teknolojia imeendelea sana. Haya chimba tuone".
Willy
alishika kisu na kuanza kuchimba shimo la mita moja kwenda chini, kisha
akawasha lile bomu na kulitumbukiza pale shimoni na kulifukia.
"Litalipuka
baada ya nusu dakika turudi nyuma haraka tulale chini".
"Halitasikika
baada ya kulipuka?".
"Hapana,
bomu hili limetengenezwa mahususi kwa ajili ya matumizi kama haya, ili kuziba mlio ndio sababu
tunalizika chini ya ardhi", Willy alimwambia Bibiane na kumtoa hofu.
Baada ya
nusu dakika bomu lile lililipuka na kutoma sauti kidogo, hii yote ilitokana na kazi ya Willy na kukatokea handaki zuri kwa ajili ya wao kupita bila kikwazo.
"Bwana,
hakika kazi yako nimeipenda, sasa tuingie ndani tukafanye kazi iliyotuleta,
kikwazo hiki ndicho kilikuwa kinanipa wasiwasi mkubwa", Bibiane alisema
wakati wakiingia ndani ya handaki ili wapite kwa ajili ya kuwakabiri wanajeshi
zaidi ya elfu kumi ndani ya kambi yao.
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment