UCHU


 

XII

"Saa ngapi sasa?" Bibiane alimwuliza Willy Gamba.

"Imefika saa sita na nusu sasa", Willy aliMjibu. 

Walikuwa tayari wana saa moja ndani ya kambi hii ya kijeshi na bado walikuwa hawajapata tatizo lolote. Sasa ndio walikuwa wanaanza kutega mabomu kwenye bweni la mwisho ili baada ya hapo kama itawezekana watafute namna ya kutoka nje, kwani mabomu waliyokuwa wameyatega na kuyaprogramu kwa saa ya Willy ili kuyalipuwa lazima wawe mbali, maana yalikuwa na uwezo wa kuharibu kambi nzima na vitu vyote vilivyomo kama yangefanya kazi kama ilivyotarajiwa. Wakati wanafikiri hivi, ghafla taa za kiwanja cha ndege zikawashwa.

"Aha, kumbe ule ni uwanja wa ndege!" Willy alinong'ona.

"Ndio, unafikiri zile ndege za kijeshi zinaruka kutokea wapi!", Bibiane ambaye naye hapo awali alikuwa hajui uwanja ulikuwa wapi, alijibu.

"Kwanini wanawashwa taa wakati huu?", Willy alijiuliza.

Wakiwa wameduwazwa na kitendo hiki na wakiwa sasa wameondoka kwenye ukuta wa bweni la mwisho na kujibanza kwenye kivuli cha lori kubwa la jeshi lililokuwa limeegeshwa pale, Bibiane alijibu. "Huenda ndege za kivita zinatolewa ili zikashambulie mahali ama ndege ya Jean inataka kutua".

"Nafikiri hilo la pili ni sawa. Hii itakuwa raha sana mimi kukutana uso kwa uso na huyu bwana yako", Willy alikejeli Bibiane akafadhaika.

"Si bwana yangu tena, bwana yangu ni wewe Willy, maana wewe ndiyo uko na mimi sasa, sema, fanya kila unachotaka nifanye", Bibiane alijibu kwa sauti ya mahaba. Willy alimwangalia, kisha akamshika na kumbusu.

Mara wakasikia king'ola na askari wakatoka na kuanza kuelekea kwenye kiwanja cha ndege.
"Hapa kuna hatari, nafikiri wametushitukia", Willy alisema huku ile kengere yake ya hadhari ikilia kichwani mwake. Kisha akaendelea. "Kinachotokea hapa ni sisi kutoka ndani ya kambi hii. Wataanza kutusaka sasa hivi".

Mara tena wakasikia mwungurumo wa ndege na magari sita aina ya Landrover ya wazi yakiwa yamebeba askari yakielekea karibu na uwanja, yalipokaribia yakasimama. Kisha, yakafika magari mengine mawili aina ya Landcruiser GX nayo yakasimama pale vilevile kusubiri ile ndege itue. Pale kwenye uwanja mkubwa, vikosi vya askari vilizidi kujipanga kwa ajili ya mapokezi.

Ile ndege ilipotua watu wanne walitoka ndani ya Landcuiser zilizokuwa zimesimama kando na kusogea karibu ili kuilaki ile ndege. Wakiwa bado wamefichwa na kivuli cha lile Lori walitumia viona mbali vyao na kuwaangalia kwa makini wale watu waliotoka kwenye yale magari.

"Yule aliyetangulia ni Col. Marcel Bazimaziki, huyu ndiye kamanda mkuu wa majeshi yote ya Akazu. huyo wa kushoto ni Kapten Nkubana aliyekutoroka Kigali, ndiye aliyetumwa kuniua, kumbe naye keshafika huku. Wa kulia ni kamanda Morris huyu ni mkuu wa vikosi vya kukodiwa ambavyo vinafundisha majeshi ya Akazu. Huyu wa nyuma simfahamu".

Ndege ilisimama na milango ikafunguliwa na watu wakaanza kutoka. Jean ndiye alikuwa wa kwanza kutoka ndani ya ndege hii.

"Aha huyu ndiye Jean nafikiri?", Willy aliuliza.

"Bila shaka huyo ndiye Jean, ambaye ndiye mzizi wa fitina katika Rwanda. na yule anayemfuatia ni Anatoile Kabuga, huyo ndiye kiongozi wa Akazu, anayefuata ni Jenerali Kasongo, kamanda wa majeshi ya Rais wa Zaire, rafiki mkubwa wa Jean, anayetokea sasa pale mlangoni ni Col. Gatabazi na huyo anayetokea mwisho simfahamu, maana sijawahi kumuona", Bibiane alieleza.

"Asante, sijui bila wewe ingekuwaje, umefanya kazi yangu iwe rahisi kiasi fulani".

"Ni kweli, lakini ungetumia njia nyingine, wewe si wa kushindwa jambo".

Baada ya kutoka ndani ya ndege, kundi la Jean liliingia ndani ya zile Landcruiser wakaondoka huku wakisindikizwa askari kwa ulinzi mkali.

"Unadhani watakuwa wanaelekea wapi sasa?", Willy alimuuliza Bibiane.

"Sijui, nilitegemea huenda wanataka kuzungumza na vikosi vilivyofanya gwaride pale uwanjani, lakini wameondoka moja kwa moja kuelekea upande ambao ndiko kuna lango kuu. Huenda wanakwenda kupumzika kwa kamanda Morris, nyumba na ofisi ya kamanda Morris iko juu ya hicho kilima, huwezi kuona ukiwa hapa kwa vile kumefichika kwa miti", Bibiane alieleza.

Kati ya magari yaliyobeba askari moja halikuendelea na msafara isipokuwa lilielekea kwenye gwaride. Gari hilo lilipofika hapo lilisimama na watu waliotoka ndani walikuwa Nkubana na askari wengine watano. Kisha Nkubana akaanza kuhutubia hilo gwarinde na kikosi kimoja wapo kikapiga hatua moja mbele na vingine vikatawanyika. Willy na Bibiane hawakuelewa nini kilikuwa kinaendelea.

"Lililopo ni sisi kuondoka hapa kambini haraka iwezekanavyo. Vinginevyo tutakamatwa hata kabla hatujamaliza kazi iliyotuleta", Willy alieleza.

"Mimi bila kummaliza huyu Jean siendi kokote ng'o", Bibiane alijibu kwa hasira.

"Lazima ufahamu kuwa hatuwezi kukabiliana na watu wote hawa, lazima kutumia akili ya ziada, wewe unajua katika kazi yetu hii swala ni kuendelea kuishi; lazima uhakikishe unajilinda ili ubaki salama. Hapa tukitaka kuanza mapambano ni sawa na kujinyonga sisi wenyewe. Pili ili tuweze kulipua mabomu tuliyotega ni lazima tutoke nje kabisa ya eneo hili, la sivyo sisi pia tutakuwa tumejiteketeza pamoja na adui", Willy alimuasa Bibiane kisha wakaona wale askari wa kikosi wanakabidhiwa silaha na kuelekea kwenye seng'enge ya ua wa kambi.

"Ehe, umeona kazi hiyo, hawa jamaa wanategemea tutakuja hapa, lakini hawajui kama tumeingia ndani na kazi imefanyika", Willy alieleza.

"Lakini wakifika pale tulipoingilia lazima watajuwa tuko ndani", Bibiane alijibu.

"Ndio sababu nikasema tutafute njia tutoke humu ndani", Willy alisisitiza.

Wakati wote Willy alikuwa akipanga mbinu za kuweza kutoka ndani ya kambi hii wakiwa salama.

"Hebu nifuate tuangalie hali ikoje upande wa lango kuu", Willy alimwambia Bibiane.

"Kule hatuwezi kupita, afadhari tuwahi palepale mahali tulipotumia mwanzo", Bibiane alisema na Willy akamuunga mkono na kuona alikuwa na mawazo sahihi hivyo, haraka haraka wakaelekea sehemu waliyokuwa wameingilia, huku askari wa doria wakizidi kujipanga na kupewa silaha ili kuzidi kujipanga kando ya ua huu wa seng'enge wakiwa tayari kulinda kambi yao. Ile tembetembea ya hawa askari kiasi fulani iliwasaidia sana akina Willy na Bibiane kutobainika mapema kwani walikuwa wamevaa mavazi ya kijeshi kama wale askari. Nkubana na watu wake waliweka ulinzi mkali upande la lango kuu wakiamini kuwa Willy angeweza kujaribu kuingia pale kambini kwa kutumia lango kuu. 

Hakuna askari wala kiongozi katka kikosi chicho aliyefikiri kuwa adui wangeweza kupitia sehemu nyingine yoyote kwani waliamini kwamba hakuna kitu ambacho kingeweza kupita ua ulioizunguka kambi hii. Hivyo, hata hawakuweka askari kuzunguka ua ilikuwa ni kwa hadhari tu. Kumbe kitu ambacho hawakujua ni kwamba teknolojia yotote inaweza kushindwa na teknolojia nyingine yenye maarifa ya juu zaidi. Willy alikuwa ndani na tayari alikuwa ametega mabomu kila upande. 

ITAENDELEA 0784296253 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU