KASHESHE
XIII
Huyu Willy
Gamba lazima atakuwa kaingia hapa, hatujui kapita njia ipi na yuko sehemu
gani?", Nkubana alimwambia Col. Gatabazi kwa njia ya radio.
"Haiwezekani, hakikisha kwanza",
Col. Gatabazi alijibu kwa hofu.
"Hakika
ni yeye Willy Gamba, tumekuta sehemu imechimbwa chini ya ua mita kama tatu hivi
kwenda chini, hata hatujui imetumika nini kuchimba ardhi. Kwa maana hiyo,
tumeanzisha operesheni kali ya kumsaka ndani na nje ya kambi, japokuwa hatuna
uhakika kama bado yuko ndani ama ametoka. Hakika mtu huyu ni hatari sana,
itabidi kuongeza ulinzi katika eneo hilo hususan mahali mlipo, nitatuma askari
zaidi kuimarisha ulinzi hapo", Nkubana aliahidi.
"Kuna
madhara yoyote kafanya huyo Willy", Col. Gatabazi alihoji kwa wasiwasi.
"Mpaka
sasa hakuna, tumekagua sehemu zote ni salama isipokuwa hapa kwenye ua
palipochimbwa ardhi, ni sehemu hii tu".
"Nani
kagundua eneo hilo limechimbwa na muda gani umepita toka hali hiyo
itokee", Col. Gatabazi aliuliza tena kwa shauku.
"Niko
hapa katika eneo husika afande", Nkubana alijibu. Baada ya ukimya wa
sekunde kadhaa akaendelea. "Askari wetu mmoja wa doria aliyepangwa kulinda
eneo hili la ua anasema haiwezi kuwa zaidi ya dakika kumi na tano hivi
zilizopita. Nafikiri bado hajaingia ndani, anasubiri ama ameona ndege wakati
mnaingia, anaweza kuwa anajipanga kujaribu kuanzisha mashambulizi. Ujue yuko
pamoja na Bibiane ambaye anaijua sehemu hii vizuri sana".
"Bibiane
anataka kulipa kisasi, kwa hiyo lazima watakuwa wanaelekea hapa baada ya kuona
tumetua kwa ndege, ongeza ulinzi, nafikiri umebashiri sawasawa", Col.
Gatabazi alijibu.
Baada ya
kuzungumza na Nkubana kwa radio, Col. Gatabazi aliwafahamisha wenzake kuhusu
maelezo ya Nkubana. "Huyu mtu ni hatari sana, lazima atakuwa anaelekea
hapa, nimeagiza ulinzi uongezwe zaidi. Nia yake ni kutuangamiza sisi kwani
Bibiane atakuwa amemweleza yote kuhusu uongozi wetu. Naomba wote tuwe katika
hadhari, huyu mtu ananitia wasiwasi maana anaonekana amepania ni mjuzi na
haogopi kitu. Watu wa aina hii ni hatari sana", Col. Gatabazi alieleza.
"Hapa
hawezi kuingia, ajaribu aone moto, hii itasaidia kumkamata kirahisi maana
nyumba hii inalindwa na mitambo maalumu ya kisasa, kuna kamera zimetegwa eneo
hili. Na tunaweza kuona sehemu zote zinazoizunguka nyumba hii kwa mara moja,
kwenye chumba chetu kuna vifaa vya kuangalia usalama wa nyumba hii, kuna
televisheni nne ambazo zinaangalia mzunguko wa eneo hili kwa umbali wa kilomita
moja. Hii ina maana hata sehemu ya upande huu wa kambi tunaona. Halafu pale
kambini kuna mitambo kama hii, sijui imekuwaje hawakuweza kumuona!",
Kamanda Morris alieleza kwa mshangao.
"Hebu
twende kwenye hicho chumba chako", Jean ambaye pia alianza kuingiwa na
hofu, alieleza. Wakaelekea kwenye chumba cha mawasiliano na usalama wa kambi
hiyo.
Walipoingia
ndani ya chumba hiki waliwakuta askari kama sita hivi waliokuwa wakisimamia
kuendesha ile mitambo ya ulinzi mle ndani. Wakiwa ndani waliweza kuona picha za
maeneo yote yaliyozunguka ile nyumba, waliwaona pia askari waliokuwa wakilinda
eneo hilo. Kwa kweli, kulikuwa na askari wengi kila mahali wakiwa tayari
kupambana na adui kwa njia yoyote. Kupitia mitambo hiyo waliweza kuwaona askari
wengine zaidi wakiongezeka na kujipanga kwa ulinzi zaidi.
Kwa vile
kambi hii inao komandoo zaidi ya mia tano waliofuzu vizuri mafunzo yao, hii
ilimpa jeuri Jean na Col. Gatabazi kuwa na imani kuwa hakuna adui anayeweza
kuleta rabsha mbele ya vijana hao ambao pia walikuwa sehemu ya ulinzi wakati
huo.
"Kukitokea
kitu chochote cha hatari, sisi tutakuwa wa kwanza kukiona hata kabla ya askari
wa hapo nje hawajakiona. Tumeweka taa kali za ulinzi ili eneo hili lionekane
kama mchana na kamera zetu zichukue picha kwa ufasaha zaidi", Kamanda
Morris aliwaeleza na kufanya wageni wake waridhike na maelezo hayo na kuamini
kuwa hakuna madhara.
"Lakini
ikitokea bahati njema Willy Gamba akamatwe, huyu atakuwa mfungwa mikononi
mwangu, msimuue tafadhari, nileteeni hapa nimle nyama taratibu. Nasisikia
kuonja nyama yake", Jean aliagiza.
"Na
Bibiane?", Col. Gatabazi aliuliza huku akimwangalia Jean.
"Huyu
nitapenda kufanya naye mapenzi kwa mara ya mwisho kabla hajaenda ahera",
Jean alijibu huku uso wake ukionyesha uovu wa ajabu na mate yakimjaa mdomoni.
"Huyu
mtu ni mgonjwa", Col. Gatabazi alijisemea moyoni.
"Tunaweza
kuendelea na mkutano", Jean aliagiza baada ya kujiridhisha na hali ya
usalama wa kambi, wakarudi kwenye chumba cha mkutano walikokuwa Kamanda Morris,
Bizimaziki na wataalamu wengine wa kijeshi waliokodishwa, waliendelea kuwaeleza
jinsi mipango ya mashambulizi ilivyokuwa imepangwa.
Meza moja
ilikuwa na ramani ya nchi za Zaire, Rwanda na Burundi na baadhi ya nchi zote za maziwa makuu
zikitumiwa kuonyesha jinsi ambavyo jeshi la Akazu lilivyojiandaa kusonga mbele
katika kuivamia Rwanda, wakitumia askari wa miguu, magari ya kisasa ya kivita, vifaru, makombora
ya masafa mafupi na marefu pamoja na ndege za kivita, yote ni kuivamia nchi hiyo kijeshi.
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment