UCHU

KASHESHE

Ilikuwa yapata saa tatu na nusu usiku wakati Willy na Bibiane walipokuwa wakijiandaa kuelekea Kibumba, walivalia sare za Msalaba Mwekundu huku wakiwa wamebeba silaha mbalimbali ndani ya mifuko ya nguo na mikoba waliyokuwa wamebeba yenye alama ya Msalaba Mwekundu. Walibeba silaha zote za hatari yakiwemo mabomu ya kisasa yaliyotolewa na Bibiane.

Willy alikuwa amevaa saa iliyoendana na yale mabomu akiwa tayari kuyatumia wakati wowote wakati wa safari yao. Walipofika kwenye gari na kufungua mlango ili waweke mikoba yao tayari kwa safari, mara moja Meja Kasubuga alijitokeza akitoka gizani akiwa ameshika bastola yake mkononi akawauliza. "Mnakwenda wapi Willy, hamkusikia maagizo ya Col. Rwivanga kwamba msifanye chochote wala msiende Kibumba mpaka mtakapowasiliana nae kesho, haraka ya nini Willy?, mimi sintaruhusu muondoke".

"Sisi hatuendi Kibumba Meja, tuko hapa hapa sehemu ya mpakani ili kufanya utafiti wa hali ya usalama katika maeneo hayo", Willy alijibu.

"Siamini, huenda mnataka kuvunja amri ili mvuke mpaka, hilo sintaruhusu na nimeamru kikosi changu hapa kiwazuie msiondoke hapa hotelini mpaka hiyo asubuhi, mimi nina amri zangu. Willy naomba tafadhali rudini ndani tusije tukavunjiana heshima kwa kuwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi mpaka Col. Rwivanga atakapofika hapa", Meja Kasubuga alionya.

Willy na Bibiane waliangaliana, maana wao walikuwa wameamua kuendelea na kazi yao usiku ule. Hawakuona sababu ya kusubiri kesho yake kwani wao walikuwa na mipango yao tofauti ambayo haikuwahusu akina Col. Rwivanga. Nia yao ilikuwa kuwasaka Col. Gatabazi, Nkubana na Jean. Wakati lengo la Col. Rwivanga na jeshi la RPF ilikuwa kuliangamiza jeshi zima la Akazu.

"Naona kama hutuamini Meja, hakuna tatizo tutarudi ndani tukalale", Willy alijibu kwa sauti ya unyonge sana.

"Samahani bwana Willy, mimi natii amri niliyopewa na wakubwa wangu wala msijaribu kunitoroka maana hiyo haiwe.....", kabla hajamaliza kusema sentensi hiyo, milio ya bunduki aina ya AK 47 ilisikika upande mwingine wa hoteli.

"Tumeingiliwa", Meja Kasubuka alisema huku akikimbia kuelekea sehemu ulipotokea mlipuko huku akitoa amri kwa wanajeshi wake kujitokeza tayari kwa mapambano dhidi ya wavamizi.

II

Wakati Jean na wenzake wanatoka Goma kuelekea Kibumba saa moja na nusu ya jioni ile, Nkubana akiwa na kikosi cha askari shupavu wenye mafunzo thabiti wapatao thelathini hivi, walielekea mpakani kutafuta habari za Willy na Bibiane, kwani walikuwa na hisia kuwa lazima wangewatafuta kwa vile Bibiane aliijua mipango yao yote. 

Nia ya Nkubana ilikuwa kupeleleza ili amuwahi Willy kabla Willy hajawawahi, maana hii ndio sheria ya mchezo wao huu. Nkubana na kikosi chake walipofika mpakani upande wa Zaire ilikuwa yapata saa mbili na nusu na ndipo walipoelezwa na vikaragosi wao waliokuwa wamejipenyeza ndani ya vikosi vya jeshi la RPF pale Gisenyi kuwa mtu mgeni aliyekuwa amefikia pale Meridien Hotel alikuwa ofisa wa Msalaba Mwekundu na mkewe.

"Huyo mkewe alifananaje?", Nkubana aliuliza kwa shauku.

"Afande, ni mwanamke mrembo ajabu, utanisamehe afande lakini kusema kweli nilipomwangalia yule mwanamke mara moja nilizini afande, ni mzuri sanasana chotara yule?", askari alijibu huku mawazo yake yakiwa yamerudi kwa yule mwanamke na kuanza kumfikiria huku mwili wake unasisimka.

Hata Nkubana alipokuwa anakieleza kile kikosi chake. "Watu wetu wamefika yafaa tupange mipango madhubuti tuwashambulie na kuwakamata hai kama bosi alivyoagiza", yule askari hakusikia kabisa mpaka Nkubana alipomshitua tena. Wewe vipi, una tatizo la kifafa", maana alianza kutetemeka.

"Hapana afande, hapana, nafikiri ukame umetuathiri sana mawazo".

"Ukame gani, wewe ni mwehu nini?, hetu tufahamishe huyu jamaa na mkewe wanakaa upande upi pale hotelini?".

Yule askari alieleza kila kitu kwa ufasaha jinsi hotelini ilivyo na akawaelekeza namna ya kuingia mpaka kwenye chumba walichofikia akina Willy bila kushukiwa na askari wa RPF waliokuwa wakilinda eneo hilo.

"Inapofika saa tatu mara nyingi askari wengi wanaondoka kuelekea mpakani na wale wanaobaki mara nyingi wanakuwa upande wa Ziwa. Hivyo itabidi tuvuke mpaka kabla ya saa tatu na nitawaonyesha sehemu salama ya kupita, halafu tutajibanza sehemu mpaka hapo askari wengi watakapotawanyika kuelekea kwenye malindo ya usiku halafu ndipo tutavamia kwani askari watakaobaki tutaweza kuwamudu", yule kikaragosi alielekeza.

"Maelezo yako ni safi sana, unafikiri kutakuwa na askari kama wangapi, yaani watakaokuwa wamebaki kwa ajili ya kulinda hoteli?", Nkubana alihoji.

"Hawawezi kuzidi hamsini pamoja na mimi, maana leo ni zamu yangu kulinda hoteli", yule askari alieleza.

"Ulikuwa ulinde upande gani?", Nkubana aliuliza kwa shauku.

"Unande ule niliokueleza kuwa tutapita halafu tujibanze maana askari anayelinda sehemu hiyo ni mtu wetu, anajuwa kila kitu", yule askari alibainisha.

Nkubana alimwangalia kwa makini yule askari na akaridhika kuwa alisema ukweli na akamwamini.

"Kwanza nenda na askari wangu mmoja mkavinjari, halafu mrudi. Kama kila kitu kiko tayari na mambo shwari ndipo tutaanza kazi", Nkubana aliwatuma ili kuwa na uhakika wa mambo na kuthibitisha maneno ya yule askari alivyoeleza. Baada ya wale askari wawili kuondoka. Nkubana alibaki akiwaweka sawa askari wake tayari kwa kuishambulia hoteli ya Meridien-Izuda ili waweze kuwakamata Willy na Bibiane.

Wale askari waliporudi na kumweleza Nkubana kuwa mambo yalikuwa shwari na vilevile kupata habari kuwa yule mtu wa Msalaba Mwekundu na mke wake walikuwa wamelala baada ya safari ndefu habari hizi zilimfurahisha sana Nkubana, akafikiri kuwa angeweza kumteka Willy na Bibiane wakiwa wamelala na huenda wakiwa wanafanya mapenzi. Alisikia hasira inampanda na palepale akakiamru kikosi chake. "Haya sasa tunakwenda kazini".


ITANDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru