UCHUKASHESHE

XIV

Wakiwa ndani ya kambi hii, Willy na Bibiane walijificha kwenye vichaka vilivyokuwa kando ya njia ambayo magari ya jeshi yalikuwa yanapita kuelekea kwenye jumba analoishi Kamanda Morris.

Walikuwa wamefanikiwa kuvuka kizuizi cha kwanza kutoka kambini bila kushitukiwa, na moja kwa moja walitumia vichaka kujificha huku wakiua askari waliokuwa wakilinda maeneo hayo, mpaka wakafika sehemu hii wakitafuta nafasi nzuri ya kuishambulia nyumba ya Kamanda Morris ili waweze kuukabiri uongozi wa juu wa Akazu.

"Ikitokea gari lisilo na askari wengi nyuma au hata likiwa na askari wawili ama watatu tulivamie na kulifanya letu ili tulitumie litupeleke kule juu bila kuwashtua walinzi. Kwa vile tumevaa sare zao tunaweza kujaribu kuingia mpaka ndani bila shida ndipo tuanze mapambano, kama tutakuwa bado hatujashitukiwa", Willy alimwambia Bibiane.

"Kama nilivyowahi kukwambia nyumba hii inalindwa kwa mitambo maalumu ya kisasa. Nje kuna kamera nne zinazopeleka picha kwenye televisheni ndani ya chumba cha udhibiti wa mitambo, ambamo kuna askari wanaangalia mitambo hii kwa zamu, kwa saa ishirini na nne kila kinachotokea nje kinaonekana kwenye televisheni hizi, kamera hizi ninafanya kazi katika mzunguko wa kilomita moja kutoka eneo la kambi. Vilevile ndani ya chumba hicho kuna vifaa vya kisasa kwa ajili ya kunanasa sauti na mazungumzo yoyote ya radio kwa radio kwa umbali wa zaidi ya kilomita mia moja. Pia wanaweza kunasa picha zinazoletwa kwa rada kama kuna kitu kinaruka sehemu hii. Hivyo, tukijaribu kufanya chochote lazima tutaonekana moja kwa moja", Bibiane alimuasa Willy.

Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, Willy alitoa kile kitochi chake chenye miali ya leza akampatia Bibiane.

"Sikia, mimi ninacho kingine, kama tutafanikiwa kuikaribia ile nyumba tutagawana njia, wewe utaelekea mashariki mimi nitapita magharibi, kitu cha kwanza kabisa ni kuua zile kamera za upande wako kwa kutumia miali ya chombo hiki. Ukiwasha tu na kuelekeza miali hii kwenye hizo kamera basi zinakufa papohapo, hazifanyi kazi tena. Harafu unaweza kukitumia haraka kukata ukuta kama tulivyofanya wakati tunaingia kwenye maghala ya silaha, Pia unaweza kukitumia chombo hiki kupofua mtu yeyeto macho. Tukifanikiwa kuifikia ile nyumba basi tuivamie na kuanza mapambano, hapo ndipo kuna kufa ama kupona. Jean na wenzake ama sisi. Tukifanikiwa tutaonana ndani, nataka umuonyeshe Jean mafunzo yote aliyokupeleka ulihitimu vizuri na unao iwezo mkubwa wa kutumia nafasi kama ulivyofundishwa".

Wakati Willy bado anaeleza waliona gari aina ya Landrover la jeshi linakuja, nyuma ya gari hilo kulikuwa na askari wawili waliokuwa wamesimama wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi kama wao.

"Gari hilo, kazi kwako Bibiane", Willy alitoa amri, na gari lilipokaribia wote walilirukia kwa nyuma na kuingia ndani bila kutoa kishindo. Wale askari wawili walikuwa wakizungumza huku wakiangalia mbele. Willy alimuonyesha ishara Bibiane, na kwa kutumia vipaji vyao vya karate, waliwavamia wale askari na kuwaua palepale na kisha kuwainamisha chini ndani ya lile gari bila kutoa kishindo cha kuwashitua wale waliokuwa mbele ya gari. Wakawalaza vizuri na kuwafunika kwa turubai lililokuwa ndani ya lile gari. 

Kisha wakajifanya ndio wale askari kwani walivaa kofia za chuma za wale askari waliowaua. Gari lilipopunguza mwendo na kusimama, Willy alitoa ishara wote wakaruka na kuelekea pande mbili tofauti. Bibiane akaelekea kulia, Willy kushoto. Kwa vile wote walikuwa wamevaa nguo za kijeshi kama wale askari wengine, hakuna aliyewashitukia. Willy aliongoza kwenye ile nyumba bila wasiwasi huku akipigiana saluti na askari wengine wa pale. Alipofika karibu kabisa na nyumba ile aliona ile kamera. Wakati Willy anaiona ile kamera ya upande huu wa kushoto, Bibiane naye alikuwa akijipenyeza upande wa kulia, akaiona ile kamera wa upande wake.

Kama vile walivyoambizana, wote walitoa zile tochi zao zenye miali ya leza na kuzielekeza kwenye kamera hizo. Macho ndani ya zile kamera yalikufa palepale na kukatisha mawasiliano ya kutuma picha za pande zote mbili kwenye televisheni. Na baada ya kufanya hivyo tu Willy alijipenyeza na kwenda kuitafuta ile kamera ya upande wa kusini.

Mle ndani ya chumba maalumu kilichokuwa na mitambo walishituka baada ya televisheni zinazopokea picha kutoka kulia na kushoto kushindwa kutuma picha.

"Tumeingiliwa, hii si bure", Kiongozi wa wale askari waliokuwa wakiendesha mitambo ndani ya chumba alisema na kwenda kumweleza Kamanda Morris. Kamanda Morris na wenzake walikuwa katikati ya mkutano wakati yule askari alipofungua mlango na kuingia ndani.

"Kuna nini?". Kamanda Morris alimuuliza kwa shauku huku kundi zima likisimama kumwangalia yule askari kwa taharuki.

"Televisheni zote za kulia na kushoto hazileti picha, inawezekana zimeharibiwa", yule askari alisema.

"Tayari yuko hapa", Col. Gatabazi alijibu na kuinuka kutoka kwenye kiti. Kabla mtu mwingine hajasema lolote, mlango ulifunguliwa na askari mwingine kutoka chumba cha kingine mitambo nae akaingia na kueleza. "Sasa kamera zote hazileti picha".

Kundi zima la Akazu na mamluki wao wakaingiwa na hofu.

"Huyu mtu ameweza kufika mpaka kutuingilia hivi kwa namna gani, Nyinyi hamna ulinzi wa kutosha hapa", Jean alifoka kwa hasira huku akionyesha hofu.

"Usitahayali Jean, lazima ufurahi kuwa mtu wetu kajileta mwenyewe na hataweza kuondoka hapa akiwa hai", Col. Gatabazi alijibu huku akielekea mlangoni na kwenda nje akifuatiwa na Kamanda Morris.

"Twende zetu tukamsake, mambo yameiva sasa", Col. Gatabazi alimwambia Kamanda Morris.

Nkubana ambaye naye alikuwa amefika kwenye eneo la nyumba hii akiwa anahisi Willy na Bibiane wangekuwa wamefika, alizunguka eneo hili kwa hadhari kubwa huku akiwachunguza kwa makini kila askari waliokuwa karibu yake, aliwaangalia machoni mwake. Kutokana na kitendo cha pale mpakani alijuwa kuwa Willy na Bibiane walikuwa wamevaa sare za jeshi sawa na wao. Wakati Bibiane anapiga miali ya leza kuua ile kamera ya kusini Nkubana alikuwa karibu nae kabisa lakini alikuwa bado hajamtambua. Ile miale ilipotoka kwenye tochi ya Bibiane na kuunguza jicho la kamera likatoa mwanga wa kati baada ya sekunde kadhaa jicho lake likaungua. 

Nkubana alisitushwa na mwanga uliotokea na kuua kamera. Akamwangalia Bibiane na macho yao yalipokutana mara moja wakatambuana. Kama umeme Nkubana alitoa bastola yake kiunoni ili awahi kummalize Bibiane. Bila hata kufikiri kuwa Bibiane alikuwa fundi zaidi, alimuelekezea ile mionzi ya leza machoni na palepale akajitupa chini kukwepa risasi, Nkubana alipiga risasi hovyo kwani alikuwa amekwisha pofuka macho na kupiga makelele, "Bibiane huyu hapa kanipofua macho".

Risasi zote alizorusha Nkubana hazikumpata Bibiane ambaye alijiviringisha na kuinuka mahali penye mlango ambao Col. Gatabazi na Kamanda Morris walikuwa wanaufungua ili kutoka nje, baada ya kumsikia Nkubana akipiga kelele. Hivyo, mlango ulipofunguliwa tu, Bibiane alijitupa pale mlangoni na kuwakumba Col. Gatabazi na Kamanda Morris, kitu ambacho hawakukitegemea na wote wakaangukia ndani huku wakifuatiwa na risasi zilizoelekezwa kwa Bibiane.

"Acheni acheni kupiga risasi, mtaleta madhara makubwa", Ofisa mmoja wa jeshi la Akazu aliamru baada ya kuona kilichotokea. Bibiane ndiye aliyekuwa wa kwanza kuinuka na alipoinuka huku katoa Bastola yake, askari mmoja aliyekuwa analinda mle ndani alimpiga kichwani kwa kitako cha bunduki; Bibiane alianguka chini na kuzirai.

Jean, aliyekuwa anaangalia yaliyokuwa yanatokea huku akiwa amezugukwa na kundi la viongozi wa Akazu na marafiki zake wa jeshi la Zaire, aliagiza, "Msimuue. Nasema mpelekeni bafuni mmwagieni maji. Kwanza mfungeni kamba, sikujua mtoto huyu ni hatari kiasi hiki. Kumbe sikupoteza fedha zangu bure nilipompeleka kwenye mafunzo ya kijeshi. Nilikuwa nasikia sifa zake tu leo nimemuona mwenyewe akiwa kazini, nimefarijika sana".

Col. Gatabazi na Kamanda Morris sasa walikuwa wamesimama huku wakiwa na hasira ya kutaka kummaliza Bibiane.

"Wewe huna akili nzuri kweli, huyu mwanamke ni mtu hatari halafu unasema umefarijika, huyu ni mtu wa kuuawa sasa hivi si mtu wa kusubiri". Col. Gatabazi alihamaki.

"Poa, Col. tulikubaliana kuwa kabla sijamuua ni lazima nifanye naye mapenzi mara ya mwisho. Hakuna mwanamke aliyewahi kuniridhisha kimwili kama huyu. Ngoja azinduke halafu nitimize ahadi yangu ndipo nitakuachia umuue", Jean alieleza. 

Willy aliposikia purukushani na milio ya risasi upande ule wa kusini na kelele alizopiga Nkubana alijua kuwa kwa Bibiane mambo tayari yameharibika. Alitumia hii vurugu na yeye akakimbilia ule upande wa kusini. Alipofika akamuona mtu anataka kubebwa ili aingizwe ndani, alikuwa haoni na hakujua yule ndiye alikuwa mtu aliyepambana na Bibiane na kupofuliwa macho. Kwa vile nia ya Willy ilikuwa kuingia ndani na kuwaangamiza viongozi wa Akazu, aliona amepata upenyo wa kuweza kufanya hivyo. Huku akijifanya kama mmoja wa askari wa pale, aliwahi na kumuondoa askari aliyekuwa anataka kumbeba Nkubana kumpeleka ndani na kumuonyesha ishara ambayo yule askari hakuelewa lakini akafikiri huenda yule ni askari mwenzake ndiye aliyeamriwa kufanya vile.

Willy alimshika Nkubana kiunoni na kumweleza. "Afande ngoja nikuongoze ndani ukapumzike, huyu mshenzi Willy atatutambua leo".

"Nia aibu kwangu, mimi Nkubana kufanywa hivi na mwanamke, mimi nia yangu ilikuwa kumuangamiza kabisa Willy kwa mikono yangu, nasikia uchungu sana", ndipo Willy alipotambua kuwa huyu aliyekuwa amemshika alikuwa Nkubana. Alifurahishwa sana na kazi ya Bibiane.
  
"Usihofu Afande, tutakulipizia, hapa huyo Willy kafika, atawezaje kutoka hapa, huyu mtu ni mwendawazimu. wakati Willy akieleza hayo walikuwa wamefika mlangoni na kuingia ndani ya sebule kubwa ya nyumba hiyo.

Bila kuhisi kuwa huyu aliyekuwa akimuongoza Nkubana alikuwa ni Willy Gamba, Col. Gatabazi alimweleza.

"Mkarishe pale kwenye kiti, halafu askari toka haraka mkamsake huyo Willy Gamba".

"Ndio Afande", Willy alijibu huku akielekea kwenye pembe nyingine ya ile sebule kulipokuwa na makochi. Wakati huo Willy alimsikia Kamanda Morris akitoa amri kwenye kipaza sauti kuwa askari wote walioko pale wapange mstari mara moja kuizunguka nyumba na kila mmoja amnong'oneze afisa wake lile neno la siri wanalotumia wakati wa usiku. Wakati huo huo Willy aliliona kundi la Akazu na Jean likizunguka meza na mmoja wao kutamka, "Nafikiri tuyaamrishe majeshi yetu yaanze kusogea, tunapoteza muda kwa huyu Willy, mtu mmoja asitupotezee muda hata kama ni hodari atakua wangapi, sanasana hawazidi mia, ndio atakuwa amefanya nini?", Kabuga alieleza.

"Namuunga mkono bwana Kabuga. Askari wachache wabaki wamshughulikie huyo Willy, wengine waanze kuelekea mpakani, huku kusubirisubiri kunaweza kutuletea madhara. Tumeshaona tuko tayari kabisa, hakuna wakati tumekuwa tayari kama wakati huu", Col. Gatabazi alieleza.

"Oke, nami nakubali, kwanza huyu Bibiane kesha fufuka?", Jean aliuliza.

Willy alikuwa amekwisha mkalisha Nkubana huku akili yake ikipiga hesabu za haraka namna ya kuwateka hawa Akazu na vibaraka wao.

"Wewe askari njoo hapa, na wewe uninong'oneze neno la siri tunalitumia usiku", Kamanda Morris alimwita Willy wakati alipotaka kutoka nje. Willy alikuwa hajui hilo neno la siri, hivyo mtego huo ulikuwa umemnasa. Karibu na Kamanda Morris alikuwepo Jean akaagiza chumba cha mitambo askari wamlete Bibiane aweze kuulizwa alipo Bibiane.

"Willy alimsogelea Kamanda Morris na ghafla alimrukia Jean na kumkaba na kuvuta kwenye ukuta, bastola kichwani kwa Jean na kusema, Jean huna haja ya kumtafuta Willy, niko hapa. Kundi zina lilisimama huku askari wote wakiwa wamepigwa na butwaa. Kamanda Morris, Jenerali Kasongo, Meja Masamba, wale askari wa kukodiwa na hata Nkubana, japo alikuwa kipofu walitoa bastola zao.

"Msifanye mchezo wowote, wekeni silaha zenu zote hapo kwenye meza, mkifanya mzaha huyu bwana yenu Jean atakuwa historia nitamwangamiza", Willy Gamba alieleza kwa ukali. Wote walijua hatari. "Na mtu asisogee hapa wala asiondoke humu ndani. Ila wamlete Bibiabe", Willy aliendelea kuamru.

"Fanyeni anavyosema", Jean alieleza huku akitetemeka huku mkojo ukimtoka chapachapa.

Kamanda Morris alitaka kutoka ili kwenda kumleta Bibiane, lakini Willy alikataa, "Mtu hatoki huku ndani, nimesema kwa lugha inayoeleweka, umenipata wewe Kaburu".

"Kampuni yenu ya mamluki naijua safari hii mmeingia hasara, mmetengeneza faida kubwa katika biashara hii, lakini leo nasema tena, safari hii mmeingia hasara".

Kamanda Morris alimwagiza askari mmoja amlete Bibiane, ambaye alikuwa tayari amepata fahamu. Na Kamanda Morris akawa amesema na neno moja ambalo Willy hakulielewa. "Umesema nini wewe kibaraka?", Willy alihoji huku macho yake yakionekana mekundu.

"Nimeita mwisho jina la yule askari", Kamanda Morris alijibu. Lakini Willy machale yalimcheza. Wakati bado anafikiria lile neno aliwahi kulisikia wapi, ghafla ukuta aliokuwa ameuegemea ukapitishwa umeme na yeye akamsukuma Jean upande mwingine na kuruka nyuma ya makochi.

Nguvu ya ule umeme ilikuwa kubwa kiasi cha kumfanya Willy kupoteza fahamu baada ya kuanguka chini. Kamanda Morris alikuwa amejiwekea usalama wa kila aina na alikuwa amemzidi Willy maarifa, mara moja kila mmoja alichukua silaha yake, na Bibiane kabla hajafanya lolote alikuwa ameshikiliwa vizuri na askari watatu.

"Mfungeni kwenye hicho kiti, sasa tutamla nyama vizuri", Col. Gatabazi aliagiza. Bwana Kabuga akiwa bado anatetemeka kwa kuwa mambo kama haya yalitokea kama miujiza alidai arudi kwenye ndege ili waondoke eneo hilo.

"Hapana, kaa uone maana ya utawala", Jean alijibu baada ya kuinuka kutoka mahali alipokuwa amedondoka na macho ya chuku akiwa ameyaelekeza kwa Bibiane aliyekuwa anafungwa kwenye kiti. Kisha, akamwendea Bibiane na kumnasa kibao, akisema "Mbio za sakafuni huishia ukiongoni, janja yako kwisha. Lakini kabla mwisho wako haujafika niliahidi nitafanya mapenzi na wewe kwa mara ya mwisho".

"Utawahi, kwani na wewe unadinda", Bibiane alijibu.

Jean alimnasa tena kibao na kusema, "Umesahau nilivyokuwa nakunyanyasa kitandani".

"Wewe ni mgonjwa na huu ndio mwisho wako", Bibiane alijibu kwa dharau.

"Unachekesha, huu ndio mwanzo wangu na mwisho wako", Jean alijibu na kugeuka nyuma, kwani wakati mawazo yake yakiwa kwa Bibiane, Kamanda Moris alileta kifaa cha umeme na kumfunga Willy kwenye kiti na kumtingishatingisha ili azinduke.

"Willy alipozinduka tu, Jean alikuwa wa kwanza kumfikia na kuanza kumpiga vibaya sana mpaka Willy akaanza kutoa damu puani.

"Wewe mwanaume gani, mpaka mwanaume mwenzako afungwe ndio umpige, si umfungue tuone nani mwanaume hapa, kati yako Jean na Willy", Bibiane alisema kwa dharau.

"Ngoja amalize hasira zake, huyu mshenzi hatufanyia mambo mabaya sana", Col. Gabatazi alidakia huku akisogea na kumchakaza Willy kwa makofi yaliyomfanya azirai tena.

"Basi inatosha, kabla hajala umeme nataka nimpe maneno yake. Nikimaliza kusema Kamanda Morris fanya kazi yako. Huyu tayari tumemhukumu kifo, na atakufa si kwa risasi bali kwa umeme, kama wahalifu waliohukumiwa kunyongwa kule Marekani.

"Kufa si tatizo, kila mtu atakufa", Willy alisema baada ya kuzinduka na kuongeza, "Ila hata mkitumaliza leo, lakini hamfiki popote".

"Wewe ni mwehu, sisi tuna jeshi la kuikamata Rwanda chini ya wiki moja, unasema nini mwehu wewe, utapata habari utakapokuwa ahera", Col. Gatabazi alitamba.

"Wewe ndiye nani", Willy aliuliza.

"Mimi ndiye Col. Gatabazi".

"Nijulishe basi kwa wengine maana kata anayehukumiwa kifo hujui majaji waliomhukumu", Willy alihoji akiwa na maana ya kuvuta muda kama kuna njia nyingine ya kujiokoa aweze kufanya hivyo.

"Huyu hapa ni Anatoire Kabuga, ndiye kiongozi wa Akazu. Najua unafahamu Akazu ni nini. Wale rafiki zetu toka jeshi la Zaire. Anayeingiza ni Col. Marcel Bizimaziki, ambaye ni kamanda wa Akazu anayesaidiwa na huyu mzungu. Kamanda Morris kutoka kampuni ya kijeshi ya Afrika Kusini. Na waheshimiwa huyu ndiye adui yetu namba moja Willy Gamba, kutoka Tanzania lakini na yeye tuna habari kuwa kazi hii anaifanya kwa kukodishwa. Hivyo, hawakilishi msimamo wa Tanzania hata kidogo katika suala hili; yeye na Kamanda Morris hawana tofauti na huyu Bibiane ni msalti kama mnavyomjua. Niliwahi kumshawishi Jean kuwa karibu sana na mwanamke akajua siri zake ni balaa kwani wao fikira zao zinatoka chini na si juu kichwani. Si watu hawa, lakini hakunisikia, sasa ona madhara aliyotufanyia", Col. Gatabazi alilalamika.

"Kazi na dawa, bila kuwa karibu na mwanamke mzuri anayekupa mapenzi vizuri huwezi kufikiri sawasawa, usisahau Col. Gatabazi hata sisi tumenufaika sana na huyu kiupmbe, mimi binafsi nilikuwa na bahati ya kufaidi mwili wake hivyo usinionee wivu, ngoja nikafaidi mara ya mwisho", Jean alijibu. Akimuonyesha ishara askari aliyekuwa karibu amfungue kamba ili ampeleke chumbani. Willy sasa fahamu zake zilikuwa zimerudi na akili yake ilikuwa ikifanya kazi ya ziada namna ya kuponyoka toka ndani ya balaa hii.

Aliona azidi kununua muda kidogo wa kuomba.

"Huenda nimefanya yote haya bila kujua undani wa suala zima hili, kwa sababu kwa akili ya mtu yeyote haya mauaji mliyofanya na kuyatekeleza yanafanya akili isikubali maana yalikuwa ya kikatili na kunyama. Kabla sijanyongwa naweza angalau kuelezwa sababu zilizowafanya mkatekeleza mauaji mabaya ya aina hii ambayo ni ya kipekee baada ya Dikteta Hitler?".

Wakati Willy anamuuliza Col. Gatabazi, Jean na Kamanda Morris walikuwana wananong'onezana na Kamanda Bizimaziki ili askari waondoke kuelekea mpakani. Willy, huku macho yakifunguka kwa shida kutokana na kipigo aliweza kuwaona jinsi wanavyonong'onezana na vilevile akaweza kuona jinsi Bibiane anavyofunguliwa kamba kutoka kwenye kiti na kupelekwa kwenye mlango uliokuwa ukielekea chumbani. Aida, alihisi Jean alikuwa anataka kufanya nini. Yote haya yalifanyika wakati Willy akiongeza kasi ya kuwaza jinsi ya kujinasua ili aweze kukamilisha kazi yake iliyomfikisha haba badala ya kukata tamaa.

Acha mimi nimjibu, wewe endelea na shughuli inayotusubiri, ambayo ni muhimu zaidi. Nimefurahi kuona kuwa huyu Willy anataka kujua sababu na sababu nitazitoa mimi", Anatoile Kabuga, Kiongozi wa Akazi, alijibu huku akiangalia saa yake iliyoonyesha kuwa ilikuwa saa nane na nusu usiku.

 
ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru