KASHESHE
XVI
Anatoile Kabuga alimwangalia Willy kwa jicho baya sana, alimuona kuwa ndiye kikwazo na adui wao namba moja kwa kuwachelewesha Inyenzi na washirika wao kushika madaraka ya nchi ya Rwanda. Hata hivyo aliamini kuwa hakuna mtu mwingine zaidi ya Willy atakayeweza kupena na kuingia katika ngome yao.
"Nitakupa
historia kidogo", Anatoile Kabuga alianza kumweleza Willy Gamba.
"Willy Gamba, lazima ufahamu kuwa sehemu hii ya Maziwa Makuu katika Afrika watu wa kwanza wa asili ni wabantu.
Wabantu ndio walioishi eneo hili la Maziwa Makuu kwa karne nyingi sana tena wakiishi kwa
raha mstarehe bila migogoro wala matatizo mpaka walipokuja watu wenye asili ya
Kihemetiki ambao baada ya kufika eneo hili walianza kuleta chokocoko, vita wakitokea
Kaskazini na Mashariki mwa Afrika. Kwa ufupi, Watutsi wamo kwenye kundi hilo.
Tangu wafike katika sehemu hii amani imekosekana kabisa. Karne mbili zilizopita
walianza kuweka Ufalme wao katika eneo hili baada ya vita vikali na wabantu wa
sehemu hii na kuwashinda. Waliweka wafalme wao waliowaita wafalme wa Kihima
ambao walitawala kutoka Bahari ya Hindi mpaka Atlantiki, sehemu ambayo sasa ni
Zaire, Rwanda, Burundi, Tanzania, Uganda na Kenya", alinyamaza kidogo
kisha akaendelea.
"Willy
Gamba. Nitakueleza kwa kifupi sana maana hatuna muda wa kupoteza. Lakini kwa
sababu wao walikuwa wachache na wakawa wanaendeleza utawala wa mabavu na
unyanyasaji kwa wabantu ambao ndio waliokuwa wengi, hali inayoendelea mpaka
sasa, mapigano ya kuukataa utawala huo yaliendelea sehemu zote, hatmaye ufalme
huo ukaangushwa katika sehemu zingine na kubaki sehemu ambayo sasa ni Rwanda na
Buurundi. Na hali hii iliendelea mpaka wakati wa Ukoloni ambapo katika Rwanda
utawala wa ukandamizazi wa Watutsi dhidi ya Wahutu na wabantu ambao ndio wengi
katika Rwanda, uliendelea. Miaka yote hii mpaka vita vya pili vya dunia Watutsi
wachache waliendelea kutawala na kuwanyanyasa Wahutu wakihakikisha kuwa
hawapati elimu, madaraka na hata mali. Ni mpaka juzi tu, mwaka 1957, Wahutu
walipojikomboa na kushika madaraka, na hawa Inyenzi wakakimbilia nchi jirani
ikiwemo Tanzania. Wakati wa utawala wetu tulijaribu sana kuwaweka karibu lakini
siyo wote waliotaka kutawaliwa na walio wengi sababu wao walijiona wana hadhi
ya juu kuliko sisi. Vilevile, waliapa kuwa lazima watatafuta njia mbadala
warudi kututawala maana sisi ni watumwa wao. Na kwa taarifa yako kila Mtutsi
anamuona kila Mbatu kama mtumwa wake. Ndivyo wanavyokuona wewe hata kama
unawasaidia kwa sababu wewe ni Mbantu na ndivyo wanavyoniona hata mimi. Sasa
basi tatizo kubwa lilikuja wakati nchi jirani ilipopata kiongozi mwenye asili
hiyohiyo ya Kitutsi, na akawa na nguvu na akaahidi kuwasaidia Wahutu ili wautoe
utawala wa wabantu katika Rwanda, Yaani watu wenye asili ya Kitutsi tu ndio
watawale sehemu hii ya maziwa makuu ikiwemo Zaire, Rwanda, Burundi, Tanzania,
Uganda na Kenya. Sisi tulipopata habari hizi tukajua eneo lote hili la maziwa
makuu halitapata amani ikiwa hawa Watutsi wanazidi kuzaliana na kuwa wengi eneo
hili. Njia pekee ya kuleta amani ni kuhakikisha mmewaua waume, wake kwa watoto,
ili kuua kabisa nguvu yao. Leo hawa tusipowaangamiza nakueleza wewe Willy Gamba,
Tanzania haitakuwa na amani na wala Zaire, Uganda na Kenya hawana amani maana
hawa wana asili ya kujipanua. Ni watu hatari ajabu, na kama mngejuwa kuwa hawa
ni watu wa kuteketezwa kabisa hata mmoja asionekane katika sehemu hii".
"Ngoja
nikukata kauli, umesema watu wengi katika eneo hili la maziwa makuu ni wabantu,
hawa Watutsi wachache watatawala vipi", Willy aliuliza huku akisogeza
vidole vya mkono wake wa kulia kujaribu kama vingeweza kuifikia saa yake
aliyovaa mkono wa kushoto.
"Unasema
nini, tunavyozungumza nani anatawala Rwanda, Burundi na Uganda, watu wengi
katika nchi hizi ni watu gani, sisi wabantu, sasa nini kitawashinda kutawala
Zaire, Tanzania na Kenya kama wameweza katika nchi hizo, njia pekee ni
kuwateketeza ili waishe, wasiendelee kutunyanyasa na kuleta vita vya mara kwa
mara katika eneo letu. Hawa na Wayahudi hawana tofauti. Ngoja nikwambie Willy
Gamba, hawa Watutsi hata kama ukiona Mtutsi amezaa na wewe lazima atatembea na
Mtutsi mwenzie ili azae Mtutsi, kazi yako wewe itakuwa ni kukuza damu isiyokuwa
yako. Na wamehakikisha wanawake wao wamesambaa dunia nzima, lakini kila
mwanamke wa Kitutsi ahakikishe mahali alipo anapewa mimba na Mtutsi mwenzie tu.
Huku wanawake wao kusambaa ni njia mojawapo ya kujipanua ili waweze kufanya
kampeni yao kwa kuhurumiwa na mataifa mengine. Hivyo, mauaji haya tuliyofanya
ni kwa niaba ya wabantu wote na sasa hivi tuko tayari kuurudisha utawala wetu
Rwanda na Burundi ili heshima ya mbantu katika eneo hili ipatikane. Baada ya
kuichukua tena Rwanda mara hii tutataka viongozi wote katika eneo hili waelewe
ukweli huo na watuunge mkono kuwatokomeza Watutsi hawa. Vinginevyo nakwambia
Willy Gamba watatawala tena sehemu yote hii, la sivyo hakuna amani katika eneo
hili. Vita vitaendelea kwa miaka mingi. Sisi Akazu ndio tumaini pekee la sehemu
hii, bila sisi kesho tawala zote za sehemu hii zinazotawaliwa na wabantu
zitatikiswa na kumalizwa. Hivyo, wewe Willy ni msaliti, unawasalti wabantu kwa
kuwasaidia Inyenzi ili waweze kutawala ardhi halali ya wabantu. ndio sababu
tumekuhukumu kifo. Na, wote wawe wabantu au taifa lingine, wakibainika
wanasaidia Inyenzi lazima wauawe. Na sasa wewe utauawa ili Akazu ifanye kazi
yake ya kuwakomboa wabantu", Kabuga alisema kwa sauti nzito iliyoashiria
hasira ya ajabu ambayo kila mtu pale ndani alihisi kapagawa.
"Yote
hayo uliyoyasema yanaweza kuwa na ukweli mwingi tu, lakini ukweli huwa hautoi
uhalali wa kuangamiza kabila zima. Hii ni kinyume na haki za binadamu. Njia
nyingine itafutwe kuwadhiti na si kuwaangamiza", Willy alijibu huku kidole
chake cha karibu na gumba kwenye mkono wa kulia kikiwa kimefika kwenye ufunguo
wa saa yake na kukandamiza ufunguo wa saa na kusubiri kuona kifo chake ama kifo
cha jeshi la Akazu.
"Unasema
haki za binadamu, sisi wabantu hatuna haki mbona............", Kabuga hakumaliza
sentensi yake teknolojia ilianza kufanya kazi yake.
ITAENDELA
0784296253
Comments
Post a Comment