TUTARUDI NA ROHO ZETU?

SURA YA PILI

II

Joram alikuwa ni mtu ambaye halewi kwa urahisi, tunaweza kusema kuwa alikuwa amechangamka pindi Kombora alipokuwa amekaribia meza yake na kuketi.

"Karibu sana Inspekta, karibu uketi", Joram alisema kwa uchangamfu huku akimwita muhudumu wa hoteli hiyo. "Leo naweza kusema kuwa ni siku tukufu sana kwangu kutembelewa na Inspekta Mkuu. Habari za siku nyingi mzee?".

"Polepole kijana", Kombora alisema. "Wanasema siku hizi hata kuta zina masikio".

"Kwani kuna lolote la siri tunaloongea hapa mzee?, Siku hizi mambo yote ya siri nimeachana nayo mzee. Nimeamua kuwa raia mwema na mtulivu kama ulivyokuwa ukinitaka niwe", Lilikuwa jibu la Joram.

Kombora hakutia neno. Akamgeukia Nuru na kumsalimu, "Bila shaka huyu ndiye yule dada ambaye alikuwa na balaa la kulazimishwa kushirikiana na yule mwuaji ambaye alikusudia kuangamiza viongozi wengi wasio na hatia?", Joram na Nuru waliitika kwa vichwa. "Ni msichana shujaa sana. Msichana wa kawaida angeweza kupoteza kichwa chake mara baada ya kukabiliwa na mkasa mkubwa kama ule", alimaliza na kupokea kinywaji chake akaanza kunywa.

"Sivyo mzee", Nuru alijibu. "Kila nikifikiria kile kitendo naona aibu kubwa sana. Nisingestahili kukubali kulazimishwa kushiriki katika mauaji ambayo yangekuwa ya kinyama kama yale. Ingawa yule jasusi Proper alikuwa kanilaghai kuwa ungekuwa mzaha wa kawaida bado sikustahili kuafikiana naye. Uzalendo wangu ulitiwa dosari na kitendo kile. Najaribu kutafuta nafasi ya kuudhihilishia moyo wangu lakini sijafanikiwa...".

"Joram ananinyima nafasi hiyo", Nuru aliongeza baada ya kusta kidogo.

"Ni hilo tu ulilotaka kusema Nuru", Joram alidakia. "Nadhani hata Inspekta amefuata kujadili hilo, au sivyo mzee.

"Inspekta Kombora aliimeza bia iliyokuwa kinywani mwake. Kisha alijibu.

"Kiasi ni kweli niko hapa kujadili hilo, kiasi siyo kweli". Alisita kidogo na kuendelea. "Unajua hatujaonana kwa muda mrefu? Tangu ulipoondoka Arusha kwa hasira baada ya kuitupa bastola yako hatujaonana tena. Nilifika katika chumba cha dada huyu nusu saa baadaye na kuukuta ubongo ule na bastola. Nilidhani umemuua wewe. Lakini bastola yako haikuwa imefyatuliwa walau hata risasi moja. Mara kikatokea kile kitabu ambacho kilinifanya nielewe yote yaliyotokea. Ndipo nikaelewa kwanini umekasirika na kuamua kuwa mnywaji".

"Niite mlevi Inspekta, vyovyote sijali".

"Hapana. Wewe si mlevi na wala huwezi kuwa mlevi. Ni mnywaji tu. Mnyaji ambaye hanywi kwa ajili ya kupenda kunywa, isipokuwa kwa hasira baada ya kunyang'anywa fursa ya kukitia risasi kwa mkono wako kichwa cha yule mshenzi. Sivyo Joram?" Kombora alitulia akimtazama Joram. Mara Joram akakumbuka kuwa hajavuta sigara kwa muda mrefu. Alitoa sigara moja na kuiwasha baada ya kuwataka radhi jirani zake.

"Kuacha hadhi yako ipotee kwa sababu ya kukosa kumuua mtu mmoja tu duniani!", Kombora aliendelea, "Sioni kama ni haki. Ziko nafasi nyingi za kufumua vichwa vya watu wenye haki kabisa ya kufumuliwa. Hati maalum inatayarishwa ambayo itakuruhusu kufanya lolote kama afisa yeyote wa usalama mwenye jukumu maalumu. Zaidi kimetengwa kifungu maalumu cha fedha ambacho kitaingizwa katika akaunti yako ili pesa zisiwe kipingamizi..." 

"Taratibu Inspekta", Joram alimkatiza. "Vipi, mbona mema mengi hivyo, kama sikosei unachotaka kusema ni kwamba unaniomba nishiriki katika kutafuta kiini cha maafa haya yanayotendeka katika nchi za mstari wa mbele. Na kama sikosei nadhani mtu uliyemtuma kwangu amekupa majibu yangu rasmi. Msimamo wangu ni uleule. Na utaendelea kuwa uleule. Kama mngefahamu Joram ambaye alikuwa mpenzi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla, lazima muelewe kuwa Joram huyo amekufa. Aliyeko hai mbele yako, ni Joram mpya. Joram ambaye hana na wala kiu ya kushiriki kwa njia moja ama nyingine katika masuala yoyote ya nchi. Aliyeko mbele yako ni Joram wa mastarehe, Joram wa kutumia. Hata dada yangu Nuru hapa nadhani anaelewa".

Ndipo Kombora alipoona ugumu wa kazi iliyoko mbele yake. Kumshauri Joram ilikuwa sawa na kulilazimisha jabali lielee juu ya maji. Akiwa mtu ambaye hakuzoea kuwabembeleza binadamu wengine, hasa wanaume, Kombora alisema kwa sauti ambayo ilificha hasira na unyonge.
"Pengine unajua unachokifanya. Lakini nadhani hujui ni kiwango gani cha madhara yanayolikabiri taifa hili endapo tutashindwa kuukomesha uovu huu unaotunyemelea. Niruhusu nikusimulie mambo ya kutisha ambayo hayajavifikia vyombo vya habari".

"Haitasaidia", Joram alimjibu Inspekta Kombora, "Utaupoteza bure muda wako. Ninachohitaji kusikia ni habari za burudani tu. Kama kuna burudani mpya ambayo sijaiona, kinywaji kipya ambacho sijakinywa au muziki mpya ambao sijausikia, nitafurahi endapo utanisimulia. Juu ya vifo vya marais na raia wasio na hatia na wenye hatia, si kazi yangu tena".

"Hata hivyo sauti yako haifanani kabisa na madai yako Joram. Kuna watu ambao silika yao ni kukesha katika mabaa na kwenye madansi, wewe si mmoja wao. Kuna wanaostarehe kusubiri maafa ya kusikitisha, wewe si mmoja wao Joram. Kuna wanaofurahia radha ya pombe na utamu wa muziki zaidi ya kazi na ushujaa, wewe si mmoja wao vilevile".

"Zamani, Inspekta. Sasa hivi mimi ni mmoja wao. Na kama huna maongezi mengine zaidi ya hayo mzee, nitashindwa kuendelea kukusikiliza", Joram alimaliza na kutoa sigara yake na kuiwasha.

Kombora hakuona kama angeweza kufanya lipi la kumshawishi Joram. Alimtazama Nuru kama aliyehitaji msaada wake. Akayaona macho yake mazuri yaliyojaa uzuri katika hali yake ya kukata tamaa. Hilo kiasi lilimfariji Kombora. Alifahamu kuwa anaye msaidizi ambaye angesaidia katika juhudi zake za kumrejesha Joram Kiango katika dunia ya Joram Kiango. Kombora hakuwa mgeni katika dunia hii alijua kuwa mwanamke mzuri ni silaha. Hivyo akamtupia Nuru jicho la kumtaka aelewe kuwa anautegemea msaada wake. Kisha aliinuka na kuaga bila ya kumaliza kinywaji chake.

"Hukufanya vizuri, Joram", Nuru alimwambia.

"Mfuate mkazungumze vizuri".

"Hivyo tu, sikia...".

Nuru akavunjika moyo. Uchungu ukamwingia rohoni. Alijilazimisha kuendelea kunywa pombe, lakini haikumuingia. Baada ya jitihada nyingine alimtaka Joram radhi, akaondoka kutangulia chumbani.


"Samahani, naweza kuketi hapa", alisema mtu mmoja akimsogelea Joram baada ya Nuru kuondoka.
********************************************

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru