SURA YA TATU
Alikuwa mtu
wa umri wa kati. Sura yake ilionyesha dalili zote za kutocheka, macho yake
yakionyesha dalili ya kuelemika. Kiasi alionekana kama pombe ilianza kumshinda
nguvu, japo alitembea kwa uhakika.
Joram
alimtazama kwa makini kabla ya kumjibu, "Una haki ya kukaa popote. Nchi
huru hii".
"Asante",
alijibu mtu huyo huku akijiweka kitini. Baada ya dakika mbili tatu za kunywa na
kuvuta kwa utulivu alimgeukia Joram na kumwambia, "Samahani. Sina budi
kulitoa dukuduku langu. Siku zote nimekuwa na hamu ya kuipata fursa hii ya
kuketi nawe. Kama sikosei u Joram Kiango".
Joram
alimtazama kwa makini mtu huyo. Alipochelewa kumjibu mgeni wake aliendelea.
"Tumekuwa
tukikutana mara kwa mara katika majumba ya starehe. Kilichonifanya nikufahamu
ni huyu msichana mzuri unayefuatana nae. Kwa kweli sina budi kukupa pongezi
zako. Wazuri nimewaona na aina yake lakini huyu sijapata kuona. Ulimpataja yule
dada Joram". Jambo moja lilikuwa limemvuta Joram katika kumsikiliza mtu
huyu. Jambo la pili lilijitokeza. Sauti. Ilikuwa sauti ya kawaida, ikizungumza
kiswahili cha kawaida katika masikio ya watu wa kawaida. Lakini katika masikio
ya Joram Kiango, Joram ambaye alikuwa sasa amekaa chonjo, sauti hiyo ilificha
uhalisia fulani.
"Unadhani
una haki gani ya kunifahamu, na kumfahamu msichana wangu wakati mimi binafsi
sikufahamu hata kidogo", Joram alimuuliza. Kama ambaye alilitegemea jibu
lile yule mgeni alijibu mara moja japo kwa kusitasita.
"Mimi
kwa jina naitwa ISmail Chonde. Ni mfanyabiashara wa siku nyingi. Nimezaliwa na
kukulia hapahapa ingawa siku hizi naishi Nairobi".
"Na
unawezaje kunifahamu kwa urahisi kiasi hicho?".
"Nasoma
vitabu, nasoma magazeti. Hakuna asiyekufahamu Joram". Sauti iliendelea
kuwa na walakini katika hisia za Joram.
"Inaelekea
bado huna maswali ya kuniuliza bwana Chonde. Nataka kumuwahi huyo msichana
unayemwita mzuri".
"Kweli.
Inaonyesha aliondoka hapa akiwa amechukia", Joram alitabasamu.
"Naona
umeona mengi zaidi ya hilo".
"Ndio,
nimeona na kusikia mengi. Kwa kweli endapo utaniona mlevi, nilichokusudia
kuongelea ni yule mzee aliyekuacha muda. Nafahamu yule ana madaraka makubwa
serikalini. Kama sikosei alikuwa akikushawishi utoe mchango wako katika
kupeleleza kuhusu matukio haya. Na niliona akiondoka bila furaha. Inaelekea
umemkatalia. Hivi kweli umekataa katakata", Joram alimtazama kwa makini
zaidi.
"Sielewi
maswali yako yanaelekea wapi?", alihoji Joram.
"Inashangaza",
Chonde aliongeza. "Joram ninayemfahamu mimi hawezi kuipoteza nafasi nzuri
ya kuonyesha ushujaa wake. Afrika iko katika mashaka makubwa. Watu wanakufa
hovyo. Majumba yanalipuka hovyo. Bara zima la Afrika liko mashakani. Joram
ninayemfahamu mimi angetoa hata roho yake kupambana na hali hii", Joram
alisikia na kupima sauti ile, akiilinganisha na uso wa msemaji. Ingawa aliongea
kama mtu mwenye uchungu wnchi na hisia ya bara lake, bado hisia fulani
zilimfanya Joram aone kitu kama kebehi katika macho yake. Kana kwamba alikuwa
na hakika kuwa Joram na U Joram wake asingeweza kufanya lolote. Wazo hilo
lilimuongezea Joram hamu ya kuendelea kumsikiliza.
"Bado
sijaelewa unachotaka kusema", Joram alichochea.
"SIdhani
kama wewe ni mzito wa kuelewa kiasi hicho", wakatazamana. Kila mmoja
akimsoma mwenzake. Kisha Chonde aliangua kicheko kirefu kilichomwacha Joram
akitabasamu. Baada ya kicheko hicho aliongeza, "Samahani endapo umeniona
mhuni au mlevi. Sikuwa na nia mbaya zaidi ya kuzungumza nawe na kufahamiana.
Kwa kheri". Aliinuka na kuondoka akielekea maliwatoni. Mwendo wake ulikuwa
wa kilevi zaidi ya sauti yake.
Joram
aliendelea kunywa taratibu. Alipomuona rafiki yake huyo mpya anayeitwa Chonde
akitoka nje ya hoteli na kusikia mlio wa gari ukiondoka, Joram alielekea
mapokezi ambapo alimsalimu tena msichana aliyekuwa hapo na kumuuliza kwa upole,
"Samahani dada. Hivi huyu bwana aliyetoka sasa hivi anakaa katika hoteli
hii?".
"Yule,
hakai hapa. Huwa anatokeatokea tu. Kila mara huja na msichana wake. Leo ndio kwanza
nimemuona akiwa peke yake. Sijui wamekosana nini na msichana huyo. Maana huyu
bwana inaonekana pesa si moja ya matatizo katika maisha yake", msichana
huyo alieleza.
"Pengine
hawajakosana", Joram alimchokoza.
"Wamekosana.
Bila hivyo asingenikonyeza mara mbili", Joram alicheka. Maongezi yao
yalikatishwa kwa simu ambayo msichana huyo alikuwa akijibu. Alipotaka kuanza
tena maongezi iliingia simu nyingine. Hii msichana huyo alionekana kuifurahia
zaidi. Alizungumza kwa furaha huku akitabasamu. Baada ya kutoa chombo cha
kuongelea alimgeukia Joram na kusema.
"Unaona,
nimekwambia leo hana mtu. Ananiambia nikimaliza kazi nimkute hoteli ya New
Afrika, chumba namba 104".
"Ndipo
anapokaa?", Joram alihoji.
"Bila
shaka".
Baada ya
mazungumzo hayo Joram aliirudia meza yake na kuendelea kunywa. Mawazo yake
yalikuwa yakimfikiria mtu huyo Chonde. Hakuelewa nini hasa ilikuwa dhamira ya
maongezi yake yale. Alishuku kuwa pengine alikusudia kupata undani wa Joram na
uamzi wake. Kwanini?, zaidi Joram alishuku kuwa mtu huyo hawakukutana
kuzungumza kiajaliajali, bali alikuwa akimfuata yeye au Kombora kwa ajili hiyo.
Juu ya yote hayo hisia za Joram kuhusu mtu huyo zilizidi kujiimarisha akilini.
Aliona kama ulikuwemo walakini fulani katika sauti ya kiswahili chake ambayo
iliutia dosari Utanzania wake. Hayo na kile alichoona katika macho ya mtu huyo
zilimtia Joram hamu ya kumfahamu mtu huyo zaidi.
Hivyo dakika
tano baadaye alijikuta mitaani akielekea New Afrika. Alipofika hapo alimwendea
mfanyakazi wa mapokezi na kuzungumza naye hili na lile huku macho yake yakiwa
kazini kutazama kama funguo namba 104 ulikuwepo. Aliuona akauliza juu ya mtu wa
chumba fulani ambacho aliona ufunguo wake haupo.
"Yuko
ndani, ameingia sasa hivi".
"Ngoja
nikamuone", baada ya kwenda chumba hicho, Joram alipanda ghorofani hadi
chumba namba 104 ambacho kilikuwa kimefungwa. Kuacha kwake tabia ya kutembea na
bastola hakukuwa kumemfanya aache kutembea na vifaa vyake vidogo vidogo kama
funguo malaya ambazo hazishindwi kulifungua kufuli la aina yoyote. Hivyo kitasa
hicho cha mlango wa Chonde kilimpotezea nusu dakika tu.
Chumbani
humo, Joram aliurudisha mlango na kuufunga kwa ndani. Kisha aliangaza huku na
kule kwa makini. Kilikuwa chumba cha kawaida kama vilivyo vyumba vingine vya
hoteli. Hivyo Joram hakuwa na kazi kubwa ya kupekuwa magodoro na viti. Hakuna
chochote. Ndipo alipoliendea Kabati na kulifungua. Ndani ya kabati hilo
kulikuwa na sanduku kubwa ambalo Joram alilifungua. Kulikuwa na pesa za kutosha
pamoja na mavazi. Vitu hivyo havikumvutia Joram. Macho yake yalivutiwa na
nyaraka mbalimbali ambazo alizipekua kwa umakini. Mengi yalikuwa makaratasi ya
kawaida yaliyomuonyesha kuwa aliitwa Afith Chonde. Baada ya kupekuwa zaidi
aliipata hati yake ya kusafiria. Aliifungua haraka haraka huku akianglia mihuri
iliyogogwa katika nchi mbalimbali ambazo Chonde alikuwa amezitembelea. Alikuwa
anatembea sana. Mihuri ya Nairobi, Lagos, Lusaka, Harare, London, New York,
Hong Kong, Tripol na nyinginezo ilikuwa ikionekana waziwazi. Hilo lilimfanya
Joram azidi kuvutiwa na mtu huyo. Hakuonekana kama mfanyabiashara mkubwa kiasi
hicho. Zaidi ya vipindi alivyokuwa akitumia kutoka mji mmoja kwenda mwingine
kwa muda mfupi, hivyo Joram alimshuku kuwa hakuwa mfanyabiashara wa kawaida.
Hivyo akaongeza umakini katika upekuzi wake.
Kama
alivyotegemea Joram aligudua mifuko ya siri katika begi hilo. Mifuko ambayo
maafisa wa forodha wasingeweza kuiona bila ujuzi maalumu. Katika mifuko hiyo,
Joram alikuta bastola moja aina ya Rivolver, maandishi mbalimbali ambayo
alipojaribu kuyasoma hakuweza kwani yalikuwa yameandikwa kimafumbo mafumbo kwa
hali ya kijasusi kamili, pamoja na kijaruba kimoja cha chuma kilichokuwa
kimefungwa kwa ufunguo. Kijaruba hicho kilimvutia zaidi Joram. Alihisi kuwa kilikuwa
kimeficha mengi zaidi ya yale aliyokuwa ameyaona. Hivyo alianza kujaribu funguo
zake malaya. ilimchukua dakika kadhaa alipogundua kuwa asingeweza kukifungua
kisanduku hicho. Kilitengenezwa maalumu kufunguliwa na mtu mwenyewe. Kiu ya
Joram juu ya kumjua mtu huyu ikazidi. "Vipi awe na kisanduku kama hicho,
kimeficha nini, na maandishi haya ya siri yanasema nini?, siyo bure. Liko
jambo", Joram aliropoka.
"Ndio.
Kuna jambo", sauti ilizungumza nyuma ya Joram. akageuka hima na kukutana
na uso wa Chande akimtazama kwa kebehi. alikuwa kaketi juu ya kochi.
alivyoingia chumbani kwa ukimya kama jini na kuketi kwa utulivu kipindi chote
ni jambo ambalo lilimuongezea hofu Joram akaamini kuwa yule hakuwa binadamu wa
kawaida. Akageuka kumtazama Chonde huku akiruhusu tabasamu zake kishujaa.
Tabasamu ambayo ilifuatwa na sauti yake tulivu.
"Tumesema
nimefumaniwa".
"Ndio
umefumaniwa. Na bahati mbaya ni kwamba umefumaniwa na kifo. Binadamu hanichezei
mimi na akaendelea kuishi", Chonde alisema huku akiinuka taratibu kutoka
kitini. "ulijifanya umeacha mambo yako ya kuingilia mambo yasiyokuhusu.
Kumbe ulikuwa ukijiburudisha kwa kujidanganya mwenyewe. Umekosea sana".
"Huwa
nafurahia zaidi kuwaua watu wangu kwa mikono yangu", alisema Chonde
akizidi kusogea.
Mzaha
haukuwemo katika macho na sauti ya Chonde kisha alionekana ni mtu anayejua nini
anachofanya. Jambo ambalo lilimfanya Joram asogeze mkono kuiendea ile bastola
iliyokuwa imelala kando yake. kama alikuwa ameuhisi wepesi wa Chonde basi
alikuwa hajauona. Mara tu mkono huo ulipoifikia bastola mguu wa Chonde ulitua
juu ya mguu huo. Wakati huo huo Joram alipokea ngumi mbili nzito zilizomfanya
Joram asahau bastola. Chonde hakuwa na roho mbaya kiasi hicho. Alimpa muda wa
kujiandaa. Joram akavuta pumzi kwa nguvu na kuanza kumwendea Chonde. Alimshitua
kwa mkono wa kulia, Chonde aliudaka na wakati huohuo akamkata Joram judo ya
mgongo na kumfanya aanguke kifudifudi. Alipoinuka Chonde alikuwa akimsubiri
huku akicheka.
"Wanasema
Tanzania kuna mtu mmoja tu wa kujihadhari nae, ambaye anaitwa Joeam Kiango.
Niko naye chumbani, sioni ujoram wake".
Maneno hayo
yalimuuma Joram zaidi ya kipigo alichopokea. Akainuka ghafla na kumwendea
Chonde akitumia mitindo na mbinu zake zote za kupigana. Vipigo kadhaa alimpata
Chonde. Lakini kwa jinsi vipigo hivyo alivyompiga kwa hasira havikuwa na
madhara kwa Chonde dakika chache baadae Joram alijikuta yuko chali sakafuni
kasalimu amri. Chonde akaendelea kutabasamu.
Sasa Joram
alimtazama Chonde kwa mshangao zaidi ya hasira. Ni mtu wa aina gani anaweza kumwadhibu
kama mwanae, bila shaka si mtu wa kawaida. Amejifunza mengi kama anavyoonekana
kujua mengi. Pamoja na kwamba kipindi kirefu kilikuwa kimepita bila Joram
kufanya mazoezi ya viungo na akili, pamoja na kule kuzoea starehe za mahotelini
na ulevi mwingi, bado hakuna kama binadamu yeyote angeweza kumfanya kama Chonde
alivyokuwa amemfanya.
Ile hamu
iliyokuwa imelala usingizini ikaibuka upya katika moyo wake. Hamu ya mapambano,
vitisho, maafa, damu, na mikasa, hamu ya kuwatia adabu watu ambao wanependa kuwafanya
vibaya binadamu wenzao. Chonde alionekana kama mmoja wao. Joram alimtazama tena
na kutabasamu kwa uchungu huku akisema, "Haya umeshinda.
Kinachofuata?".
"Ni
kifo chako", Chonde alijibu kijeuri. "Siwapendi vijana watundu kama
wewe. Kufa huna budi.
"Kosa
langu".
"Unapenda
kufa?".
Joram
alifikiri kwa makini lipi angefanya kuahirisha hukumu hiyo ya kifo. Alihitaji
muda ili ikiwezekana itokee njia moja ama nyingine ya kuyaokoa maisha yake.
Akaanzisha maongezi kwa sauti ambayo aliifanya dhaifu kuliko alivyokuwa
akimuuliza Chonde hili na lile. Chonde alikuwa mgumu wa kutoa habari kama
jabali. Kati ya maneno ya kashfa na matusi kwa Joram, nchi na bara zima la
Afrika hakutamka neno lolote litakalomfanya Joram ajue kuwa yuko katika
ulimwengu wa ujasusi. Alichoambulia ni zile hisia tu kuwa Chonde hakuwa raia wa
kawaida tu.
"Umeahirisha
sana kifo chako", Chonde alisema baadae kama aliyekuwa akizisoma fikira za
Joram. Sasa iliyobaki ni kazi ndogo ya kukutoa uhai. Nitakuua kwa mkono wangu
wa kushoto. Maiti yako itaokotwa kesho ikiwa imevunjikavunjika kama mtu
aliyeanguka kutoka ghorofani. Kwa jinsi ulivyobadilika kitabia hakuna
atakayejuwa kuwa umeuawa", baada ya maneno hayo, Chonde aliinuka na
kumwendea Joram kama alivyofanya awali, lakini macho yake yalitangaza kitu
kimoja tu, kifo.
Joram alijiandaa.
Akijua kuwa vita vilivyokuwa mbele yake vilikuwa vita vikubwa pengine kuliko
alivyowahi kupambana navyo. Vita vya kuitetea roho yake. Akaikusanya akili yake
yote na kumsubiri Chonde kishujaa.
Mara mlango
ukagongwa.
Chonde
aligutuka kwa mshangao na kuutazama mlango. Joram hakuipoteza nafasi hiyo.
Aliruka na kuufanya mguu wake utue katika shingo ya Chonde. Lilikuwa pigo
ambalo Chonde alilitegemea. Akalihepa na kuachia judo ambalo Joram aliikinga.
Papo hapo mlango ukagongwa tena na kufunguka na kuruhusu msichana mzuri
kuingia.
Alikuwa yule
msichana wa mapokezi pale Embassy hoteli. Alitokwa na macho ya mshangao kuona
miili yenye jasho, michubuko na damu, ya wanaume hawa, ilikuwa tayari
kuvamiana. Wote walimtazama msichana huyo. Chonde akimlaani, Joram akishukru.
Akiwa kama hajui lipi la kufanya msichana huyo aliduaa mlangoni, Midomo wazi.
"Karibu
ndani. Tulikuwa tukifanya mazoezi ya viungo na huyu rafiki yangu", Chonde
alimwambia yule msichana huku akivaa tabasam ambalo lilificha kabisa tabasam la mauaji.
"Karibu ndani. Na wewe ndugu yangu nenda zako sasa. Tutakutana siku
nyingine".
Joram
hakuamini, aliyarekebisha mavazi yake na kutoka chumbani humo taratibu. Hakuwa amesahau
kumwachia msichana huyo tabasam la shukrani.
*************************************************************
ITAENDELEA
0784296253
Comments
Post a Comment