TUTARUDI NA ROHO ZETU?SURA YA PILI

Kati ya watu ambao wameisumbukia sana nchi hii, wakiziweka roho zao katika minada ya maafa na kwato za mauti wakiilinda nchi isimezwe na jangwa la misukosuko inayosababishwa na majasusi hatari wa Afrika, ni Mzee huyu Mkwaju Kombora.

Tangu utoto wake baada ya kumaliza kidato cha sita, alijikuta akitoka chuo hadi chuo, huku akifundishwa mbinu mbalimbali za kupambana na adui. Baada ya kuhitimu vizuri alijikuta akivaa magwanda ambayo mabega yake hayakukoma kubadilikabadilika hadi alipojikuta Inspekta wa kikosi hiki maalumu. Kupanda kwake ngazi mara kwa mara kulitokana na moyo wake wa kishujaa na juhudi zisizo kifani katika kuwakabili adui wa nchi. Mara kwa mara alikuwa akiwashinda adui zake isipokuwa safari chache ambazo alielekea kukata tamaa. Hata hivyo asingekosa kumshukuru Mungu kwani nyakati hizo alitokea kijana yule ambaye alisaidia kuwanasa adui kwa hila zake za kutatanisha. Kijana ambae jina lake lisingeweza kumtoka akilini, huyo ni Joram Kiango.

Kombora asingesahau mchango wa kijana huyu katika mikasa ile ambayo Mswahili mmoja ameamua kuandika vitabu ili apate chochote kile na kuviita Dimbwi la Damu, Mikononi mwa Nunda, Nasikia kuua tena na Salamu kutoka Kuzimu. Hata hivyo, kama polisi wengine, Kombora asingeweza kutamka hadharani kuwa Joram alifanya lolote la haja isipokuwa alibahatisha na kuhatarisha maisha yake. Lakini leo Kombora alitamani kumbembeleza Joram, hata kwa kumuangukia miguuni, endapo ingebidi, amsaidie katika kuutatua mkasa huu ambao ulikuwa ukimtoa jasho yeye na polisi wenzake wote wa nchi zilizo mstari wa mbele kwenye ukombozi Kusini mwa Afrika.

Yalikuwa yakitokea mambo mengi. Mambo mazito na ya kutisha zaidi ya walivyoyafahamu wananchi wa kawaida ambao wanategemea gazeti, radio na televisheni ziwape habari. Kila mmoja alikuwa ameshika mikasa ya kuteketea kwa mamia ya maisha ya watu wasiokuwa na hatia ambao walipata ajali ya kutatanisha katika uwanja wa mpira huko Nigeria. Pia ni wengi waliosikia juu ya kuungua kwa maghala ya chakula bila sababu mahususi inayoeleweka huko Harare. Zaidi, hakuna mtanzania ambaye hakupata kusikia kuungua tena kwa jengo la Benki kuu ambalo lilikuwa likijengwa upya.

Hayo ni maovu ambayo yalisikika katika vyombo vya habari na mitaani. Hayakumtisha sana Kombora. Lakini kulikuwa na haya ambayo yalikuwa bado siri mioyoni mwa wakubwa wa idara ya usalama wa taifa. Haya ambayo hayasemeki wala kutangazwa.

Viongozi wanane wa vyama kadhaa vya wapigania uhuru wa Afrika Kusini na mwakilishi wa PLO hapa nchini ambao walikuwa wakikutana kwa faragha katika jengo moja jijini Dar es Salaam walikuwa wamefariki ghafla katika moja ya ajali zisizoeleweka. Hakuna anayefahamu kikamilifu chanzo cha vifo hivyo, isipokuwa kwamba walikufa kwa kuungua moto uliolipuka ghafla katika chumba chao cha mkutano. Juhudi zote za kutafuta chanzo cha moto huo hazikufanikiwa.

Zaidi ya hao, kuna wale mawaziri wa nchi zisizofungamana na upande wowote ambao walinusurika kufa katika ajali ambayo haikutofautiana na hii ya Dar es Salaam. Mkutano wao ulikuwa umeandaliwa kufanyika katika chumba fulani katikati ya jiji la Lusaka. wakati wakijiandaa kwenda huko lilitokea suala jipya ambalo lilichelewesha msafala wao zaidi ya nusu saa hivi. Kuchelewa huko kuliyaokoa maisha yao. Kwani chumba hicho kililipuka kwa moto na kupoteza maisha ya wafanyakazi wawili wa chumba hicho na kuharibu vifaa vyote. Kama awali, chanzo cha moto huo hakikupata kufahamika mpaka leo.

Hayo ni baadhi tu ya mambo yaliyotokea. Kulikuwa na hisia kuwa mkono wa makaburu wa Afrika Kusini ulikuwamo katika vitendo hivyo. Lakini hisia hizo hazikuwa na uhakika kamili sasa baada ya ushahidi mdogo ambao ulikuwa ukielekea kutoweka kwa njia nyingine ya kusikitisha.

Ushahidi huo ulikuwa ukielekea kuchipuka baada ya ule moto ambao uliteketeza benki kuu. Yuko askari mmoja ambaye alisema aliamini moto huo ulisababishwa na mtu mmoja ambaye alifika katika jengo hilo usiku na kujiita kuwa ni mmoja kati ya mafundi ambao walikuwa wakishughulikia jengo hilo. Jengo lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa askari huyo ambaye alimwamru mtu huyo kusimama na mikono yake iwe juu. Mtu huyo alitii amri na kumsihi askari kwa maneno mengi kuwa amesahau kitu cha muhumu sana kwake katika jengo hilo, jambo ambalo lilimfanya askari amruhusu kuingia ndani baada ya kumpekua kwa umakini mkubwa. Mtu huyo aliingia harakahara na baada ya dakika kadhaa alirudi huku akiwa ameshikiria hirizi mkononi na kusema kwa furaha. "Nilikuwa nimesahau hii, ndugu yangu. Bila kuwa na hii mfukoni siwezi kuishi zaidi ya masaa ishirini na nne", mtu huyo alisema akimuonyesha yule askari ile hirizi.

Askari huyo hakuwa amemwamini sana mtu huyo, kutokana na jinsi alivyomuona mkakamavu maana hata alipoelekezwa mtutu wa bunduki hakuonekana kubabaika. Hivyo jengo hilo lilipolipuka moto masaa kadhaa baadaye, askari huyo alilieleza tukio hilo kwa wakubwa zake ambao walimweka kati ya watu ambao walilazimika kuongea na Kombora ana kwa ana. Baada ya kumsaili kwa mapana na marefu, Kombora alielekea kuamini kuwa mtu huyo aliyeingia katika jengo hilo usiku alihusika kwa njia moja au nyingine katika janga hilo. Lakini pindi walipobuni mbinu za kuanzisha msako wa kumtafuta mtu huyo, askari huyo ambaye ni mtu pekee aliyewahi kumuona mtu huyo, alikutwa akielea baharini pwani ya Magogoni akiwa maiti. Hakuna aliyeweza kueleza kilichomtoa kwake Magomeni Mikumi na kuja kuogelea kwa mara ya mwisho Magogoni.

Ilikuwa dhahili kuwa askari huyo aliuawa.

Jambo ambalo lilimfanya Inspekta Kombora na wenzake wazidi kuamini kwamba kulikuwa na namna katika ajali hizo zilizotokea katika miji mbalimbali ya Afrika huru. Juhudi zao za kutafuta chanzo na watendaji wa maafa hayo hazikuelekea kuzaa matunda yoyote zaidi ya hisia tu, kwamba Afrika Kusini ilihusika. Hisia ambazo ziliongezewa uzito na vitisho ambavyo vililetwa kwa njia mbalimbali zikitishia uhai wa maisha ya watu na nchi ambazo eti zingeendelea na msimamo wao wa kuibana Afrika Kusini. Vitendo ambavyo, licha ya kusababisha hofu na mashaka, vingeweza kupunguza hamasa za moyo wa kimapinduzi katika fikra za mashujaa endapo zingeachiwa kuendelea. Ni hapo ndipo Inspekta Kombora alipozikumbuka silaha zote na kutamani zielekezwe Afrika Kusini. Ni hapo pia alipowakumbuka mashujaa wote na kutamani waelekee Afrika Kusini. Na kati ya mashujaa hao jina la Joram Kiango lilitangulia kumjia rohoni.

Hiyo ilikuwa baada ya kuwasiliana na wakuu wa vikosi vyote maalumu vya upelelezi katika nchi zote zilizokwisha husishwa na maafa hayo ya kutatanisha. Walishauriana kuwa kila nchi ifanye juu chini kuhakikisha kisa cha maafa hayo kinafahamika na ikiwezekana maafa hayo yakomeshwe. Ndipo Inspekta Kombora alipoanza kufanya kila juhudi. Tumaini pekee ambalo lilielekea kumpatia walau fununu, yaani yule askari mlinzi wa benki kuu alikuwa sasa ameuawa kwa hila. Harakati za kupeleleza nani alihusika katika kumuua askari huyo hazikuwa zimezaa matunda yoyote. Hivyo Inspekta Kombra alijikuta hajapiga hatua yoyote katika jukumu hilo. Badala yake alijiona kama kiwete ama mtu aliyepooza ambaye anasubiri maafa ya moto unaomjia kasi.

"Joram lazima ashirikishwe", Kombora alifoka kimoyomoyo.

Alikuwa na habari zote za Joram, kuwa tangu baada ya mkasa wa salamu toka kuzimu alikuwa ameiacha ofisi yake na kuanza maisha ya kiupuuzi ya kustarehe katika mahoteli na mabaa akijistarehesha na yule msichana mzuri wa Arusha aitwaye Nuru.

"Yeye si mtu wa kuupoteza muda wake katika mabaa. Kipaji chake kinahitajika sana katika vita hii. lazima apatikane", Inspekta Kombora alisema huku akiinuka kutoka kitini.

Alimtuma mtu ambaye alizunguka katika mahoteli makubwa na kumpata Joram. Lakini, kama Inspekta Kombora alivyotegemea, majibu ya Joram yalikuwa ya kijeuri kiasi kwamba mtu huyo alijiona mjinga na kurudi kwa Inspekta Kombora akiwa amechukia. Jambo ambalo lilimfanya jioni hii Inspekta Kombora mwenyewe ayavue magwanda yake na kuvaa mavazi ya kawaida, kisha akajitosa katika ukumbi wa Embassy ambao aliambiwa kuwa Joram alikuwemo akistarehe.
*************************************************************
ITAENDELEA 0784296253 

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru