UCHUSURA YA KUMI NA MOJA

KAMPALA

II

Ilikuwa yapata saa moja asubuhi Willy aliposhituka kutoka usingizini baada ya kuota ndoto mbaya ya vita ambayo aliota Bibiane akipigwa risasi sita kifuani na kupoteza maisha, alipotaka kupiga kelele alishituka kutoka usingizini, akamwona Bibiane amemlalia kifuani wakiwa kitandani akakumbuka kuwa kumbe walikuwa Hoteli ya Sheraton, iliyoko mjini Kampala, baada ya kuletwa hapa jana jioni kwa ndege ya serikali ya Rwanda baada ya kuchukuliwa na helikopita ya jeshi ya akina Col. Rwivanga kutoka kule porini Kibumba walikolala baada ya usiku wa kasheshe walipofanikiwa kuiteketeza ngome ya Akazu. Taratibu Willy alimwondoa Bibiane kwenye kifua chake na kumlaza kwenye mto. Alichukua chombo cha kuwashia televisheni ili kusikia taarifa ya habari ya saa moja.

Baada ya kuwasha televisheni mtangazaji alisoma taarifa ifuatayo.

"Zaire. Vikosi vya wapinzani wa serikali ya Zaire, vikiongozwa na mpinzani mkuu Bwana Mpinda vimeanzisha mapigano makali dhidi ya serikali hiyo vikisaidiwa na vikosi vya waasi wa kabila la Banyamulenge vikiongozwa na Meja Tom Kabalisa Mubanyamulenge, aliyeasi kutoka jeshi la Zaire. Bwana Mpinda amekaririwa na vyombo vya habari kuwa nia yao ni kuuondoa utawala wa kidikteta wa serikali iliyoko madarakani Kinshansa. Wamejigamba wakisema usiku wa kuamkia jana walishambulia kambi kubwa ya kivita iliyoko Kibumba, karibu na Goma na kuteketeza silaha nyingi, vikiwemo vifaru, ndege za kivita, mizinga mkibwa na midogo na kuua askari wapatao elfu kumi".

"Pamoja na kwamba habari hizi hazijathibitishwa na vyombo vingine vya habari vya ndani na nje, raia wa sehemu hiyo wamethibitisha kutokea kwa milipuko mkubwa ya ajabu ambayo hawajawahi kuisikia katika kambi hiyo. Na wanasema wanajeshi karibu wote na silaha zilizokuwa kwenye kambi hiyo zimeteketezwa kwa milipuko hiyo iliyosikika mpaka Gisenyi na Goma".

"Habari zilizotufikia hivi punde katika chumba chetu cha habari zinasema waasi tayari wamekamata miji wa Goma na Bukavu na bado wanasonga mbele kuchukua maeneo mengine. Vilevile, kuna habari ambazo hazijathibitishwa kuwa vikosi hivyo vya wapinzani vinasaidiwa na vikosi vya jeshi la RPF la Rwanda".

"Hii ina maana kuwa wapinzani wamekusudia kuung'oa utawala wa sasa ambao umedumu madarakani kwa zaidi ya miaka thelethini sasa ambao wameupachika jina kuwa utawala wa mabavu, unyanyasaji uliojaa rushwa na udikteta. Bado hakuna taarifa yoyote ya kukanusha habari hizo kutoka kwa serikali ya Zaire, mji Kinshansa".

"Na huko Jijini Dar es Salaam, Tanzania kuna habari kuwa waziri wa ngazi ya juu nchini humo kwa jina maarufu la JKS amefariki dunia akiwa katika benki moja huko Geneva, Uswisi baada ya kupatwa na shinikizo la damu. Kiongozi huyo aliondoka nchini Tanzania siku mbili zilizopita na kuelekea London kwa ajili ya matibabu ya moyo, bado haijabainika kwa nini alikwenda Geneva, na alifuata nini kwenye benki hiyo. Waziri huyo ndiye aliyekuwa akitegemewa kuwania urais wa Tanzania baada ya rais wa sasa kumaliza muda wake".

Willy alitabasamu baada ya taarifa hii iliyonoga. Kisha, akachukua simu na kumpigia Mzee Musoke na kumwomba waonane mchana kama walivyokuwa wamepanga wakati akiwa mjini Kigali ili ampatie ripoti ya kazi yake aliyoifanya kwa mafanikio.

"Nimefarijika kusikia kazi yako kwenye taarifa ya habari ya asubuhi hii, wewe ni mwanaume wa shoka", Musoke alimsifu Willy.

"Asante mzee, tutaonana hiyo saa nane", Willy alimjibu Musoke na kukata simu. Kisha akapiga simu nyingine.

"Pepe mpenzi".

"Uko wapi", Pepe aliuliza.

""Niko Kampala narudi kesho".

"Ooh Mungu wangu, toka umeondoka sijapata usingizi. Njoo mume wangu nina hamu sana na wewe, nakupenda sana".

"Na mimi zaidi, kesho mama, kwaheri", Willy akakata simu.

Bibiane alikuwa akisikia lakini alijifanya kama hamsikii alimgeukia Willy na kusema. "Uko wapi Willy?, njoo ulale, najua siku yangu ni leo tu, hivyo lazima niitumie siku hii kikamilifu".

"Katika nafsi yangu hupenda mtu anayeelewa mambo kama wewe", Willy alijibu huku akirudi ndani ya shuka na kumkumbatia Bibiane.  


MWISHO wa HADITHI YA UCHU

WAPENDDWA WASOMAJI, MNARUHUSIWA KUTUMA MSG KUCHAGUA HADITHI GANI YA KUSISIMUA NIWALETEE KUPITIA BLOG YETU YA MPIGANAJI. KARIBUNI 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru