NOTI BANDIA

SEHEMU YA NANE

Sajenti Julius Nyawaminza aliwasili bandarini, Dar es Salaam kwa Meli ya Kilimanjaro II majira ya saa moja na dakika ishirini asubuhi akitokea Visiwani Zanzibar. Baada ya kuwasili Dar es Salaam, kutoka bandarini, Nyawaminza alitembea kwa miguu yake hadi eneo la Posta mpya kama alivyokuwa ameelekezwa.

Kijana huyu alikuwa na shauku ya kufanya kazi aliyokuja kuifanya Dar es Salaam, alifikiria mambo mengi aliyozungumza na Teacher usiku, akajiona mwenye bahati kipindi hiki kuitwa kufanya kazi katika mazingira aliyokuwa akiyasubiri kwa siku nyingi.

Baada ya kuhitimu kozi mbalimbali za kijeshi ndani na nje ya nchi, Sajenti Julius Nyawaminza alipangiwa kazi katika vikosi vya Zanzibar. Akiwa Visiwani Zanzibar, alifanya mazoezi yake ya kawaida kila siku akisubiri hali mbaya itokee. Yeyote angemuona barabarani kwa bahati mbaya asingeamini kuwa kijana huyu ni moto wa kuotea mbali, kama huamini mtafute umchokoze ili uamini haya niyasemayo..

Begani, Nyawaminza alining'iniza mkoba wake mdogo wenye vifaa vyake kadhaa vya kazi. Alipofika eneo la Posta mpya alinunua gazeti la michezo, akaketi kwenye mojawapo wa vibanda vya abiria wanaosubiri usafiri vilivyoko mbele ya jengo la Benjamini Wiliam Mkapa na Benki ya CRDB.

Luteni Claud Mwita, kutoka mkoani Morogoro, naye pia alikuwa amewasili katika eneo hilo, yeye alitumia usafiri wa bodaboda kutoka Ubungo, alifanya hivyo kutokana na hali ya barabara za Dar es Salaam asubuhi kuwa na msongamano wa magari mengi, hususan wakati wa kuelekea katikati ya Jiji.

Kama alivyofanya Sajenti Julius Nyawaminza, Claud Mwita alitafuta gazeti ya michezo, baada ya kupitia vichwa vya habari vya gazeti hili, akatafuta uelekeo akaweka makazi yake ya muda akisubiri taarifa kutoka kwa Teacher.

Pamoja na kusoma magazeti, vijana hawa walifika hapa kwa kazi maalum, kuangalia aina ya watu wanaofika eneo hilo na muda wa kukaa kusubiri usafiri wa daladala ama taksi zilizoegeshwa katika eneo hilo. Kila mmoja kwa wakati wake alituma ujumbe mfupi wa maneno kumfahamisha Teacher kuwa tayari amefika na yuko kwenye pointi ya kazi.

Nao Simba, Nyati na Chui kama wanavyofahamika, walifika eneo hilo mapema zaidi, hawa waligawana njia za kuingia na kutoka katika jengo hilo, Simba akiulinda mlango mkuu wa mbele unaoangalia kituo cha daladala, Nyati akajiweka upande wa kuingia na kutoka magari, Chui akaimalisha ulinzi kwenye mlango mdogo unaotokea sehemu ya maduka kama unatokea barabara ya Jamhuri.

Teacher aliingia ofisini kwa Kanali Emilly na kuonyeshwa karatasi zilizoandaliwa mfano wa noti, lakini zilikuwa bandia.

"Karibuni", Kanali Beny Emilly alisimama kuwakaribisha wageni hawa. Kwa sheria za kijeshi ilinilazimu mimi pia kusimama ili kumuunga mkono bosi wangu. Baada ya wageni hawa kushikana mikono na mzee huyu, wakanishika mkono.

"Karibuni, karibuni sana, mnaweza kuketi", Kanali Emilly alirudia kusema huku akiwaonyesha sehemu za kuketi. 

"Shukrani sana", walisema wageni hawa kwa pamoja huku wakiketi taratibu kwenye viti vilivyokuwa mbele yangu. Kutokana na uzoefu wangu wa kazi nikabaini kuwa wageni hawa walikuwa na tatizo zito linalosumbua nafsi zao.

"Karibuni tena ndugu zangu, karibuni sana hapa ofisini kwangu, huyu kijana ndiye Teacher ambaye niliwafahamisha amesafiri, nikaona ni vizuri tumsubiri awepo ili tuzungumze wote kuona namna ya kusaidia jambo hili", Kanali Emilly alisema akiwaangalia wageni hawa.

Halafu akanigeukia, "Teacher, hawa ni wageni wetu, nimefarijika kukuona umerejea wakati muafaka kabisa, dunia ya sasa hakuna siri, jana niliitwa Ikulu kwa mheshimiwa Rais, nimeulizwa maswali mengi ambayo nimekosa majibu, nikaamini kuwa ukirudi tutajadiliana na majibu yatapatikana, ndivyo ninavyoamini", alisema huku nikimwangalia kwa makini.

Aliinua simu yake ya mezani akampigia Katibu Mahsusi wake Linnah, akamwambia atuletee vinywaji juisi, soda, maji na sambusa. Haikupita hata dakika tano, vinywaji vililetwa, tukaanza kunywa huku kila mmoja akiliweka tayari koo lake kwa mazungumzo.

"Mko tayari kwa mazungumzo yaliyowaleta, ni muda muafaka sasa kuzungumza?", Kanali Emilly aliwauliza watu hawa.

"Naam, tunaweza kuanza mazungumzo yetu", alisema mmoja wa watu hawa huku akimwangalia mwenzake usoni, mfano wa mtu anayeomba ridhaa ama kibali kwa ajili ya kuanza kutoa maelezo.

"Itapendeza kama mtaeleza kuanzia mwanzo ili tuwe pamoja na Teacher katika mazungumzo haya", Kanali Emilly aliwaeleza watu hawa, halafu akanigeukia mimi", "Teacher jana nilikutana na watu hawa, walinisimulia kwa undani kuhusu jambo hili lakini itapendeza zaidi wakirudia mbele yako ili upate picha kamili" aliniambia.

"Kijana au Teacher kama mzee wetu anavyokuita. Naamini utaelewa vizuri nikianza kwa kujitambulisha, sisi ni nani tunatoka wapi na tumefika hapa kwa sababu gani?".

"Naam", nilijibu kwa mkato.

"Asante. Mimi binafsi naitwa Enock Nyanda, mkaazi wa Msasani ni mfanyabiashara maarufu hapa Jijini Dar es salaam", alisema huku akiniangalia, nikamuonyesha ishara aendelee. 

"Huyu mwenzangu anaitwa mzee Sadik Tagazi, makazi yake pia ni Msasani, ni mfanyabiashara wa siku nyingi... Kijana wangu, naamini nitaeleweka vizuri kwako nikisema wazi kuwa tamaa ya kupata mali nyingi imeniponza mimi, imemponza hata huyu mzee mwenzangu, tumeingizwa mjini, nimeibiwa kiasi kikubwa cha pesa, huyu mzee mwenzangu pia amefanyiwa hivyo hivyo, tumeumizwa", alisema huku machozi yakianza kumtoka, jambo ambalo kwa kiasi fulani liliushitua sana moyo wangu.

"Ehee, ilikuwaje mpaka mkaibiwa kiasi kikubwa cha pesa kama ulivyosema", nilihoji huku akili yangu ikibadilika, maana tukio hili ni moja ya matukio ya kawaida ambayo huwatokea watu kila siku, mawazo yangu yakarejea shambulizi la usiku, nikajiuliza ni wizi huu wa pesa uliosababisha nishambuliwe na kuponea chupuchupu.

"Labda, niseme wazi kuwa watu hawa wametumika teknolojia ya kisasa sana, naamini kwa teknolojia hii hata nani angeibiwa, mimi ni mtu makini sana, lakini huwezi amini nimeibiwa kirahisi mno", anaeleza mzee Sadik ambaye kwa muda mrefu alikuwa kimya.

"Ni teknolojia ipi hiyo, mbona mnazunguka tu hamsemi wazi?", niliwauliza.

"Nimewapa nafasi ya kuzungumza, ndiyo maana nikasema uwanja ni wenu, tusipoteze muda, cha msingi elezeni nini kilitokea mpaka mkaibiwa, jambo hili ni kweli linaweza kumpata kila mtu, lakini mengine ni uzembe wa mtu", alisema Kanali Emilly kwa hasira.

"Si kusudi letu kupoteza muda, tunataka kueleza jambo hili kwa kinagaubaga zaidi ili muone jinsi ya kutusaidia pia kuwanusuru ndugu wengine wanaokusudiwa kuibiwa kama sisi, nashauri mwenzangu aanze maana yeye ana taarifa nzuri na muhimu zaidi", alisema mzee Enock.

"Leo ni tarehe ngapi", alihoji mzee Sadik.

"Leo... Jumatatu ya Machi 21, unataka kusema nini?", Kanali Emilly alieleza na kuhoji.

"Ehee ni jambo zito lakini nitafanyaje, Machi 13, mwaka huu watu wawili nadhifu sana walifika ofisini kwangu... Nitaeleza kwa kifupi, utaniuliza maswali itakapobidi", alisema mzee Sadik. "Baada ya watu hawa kufika ofisini kwangu, tulianzia mbali sana, niliamini ni watu safi, tena waungwana sana, wakajitambulisha kuwa wanafanya kazi katika ubalozi mmoja nchini Tanzania, baada ya kujitambulisha walitoa karatasi fulani kuwa hizo ni dola za Kimarekani ambazo hazijasafishwa", alinyamaza kidogo ili kumeza mate.

Linnah aliingia ofisini kwa Kanali Emilly akiwa amebeba faili kubwa, aliliweka sehemu ya mafaili yanayoingia halafu akaniangalia na kufinya jicho lake, nikatabasamu akatoka.

"Ehee, leta habari, baada ya kuonyeshwa karatasi hizo ambazo walidai ni dola wewe kama wewe uliamini kuwa ni dola?", nilimuuliza. Alionekana kupagawa, kiasi fulani alionekana mwenye aibu kiasi.

"Teacher, ukweli ni kwamba hawa jamaa zetu wameibiwa lakini inashangaza jinsi wanavyoona abu kueleza ukweli kuhusu tukio hili, kwa uzoefu wangu, baada ya kukutana nao na kuzungumza nao jana, nimeamini kuwa hawapendi jambo hili litoke nje, yaani kwenye vyombo vya habari, hilo tumelizingatia, sasa watueleze kwa undani jambo hili lilivyotokea", Kanali Emilly alieleza. 

"Kama ulivyosema, itakuwa fedheha iwapo tukio hili litarushwa kwenye vyombo vya habari, vinginevyo hakuna tunachoficha, ndio maana nikasema tumeibiwa, wezi wametumia teknolojia ya kisasa kabisa, hata hivyo mimi na mwenzangu tunakiri kuwa tamaa ya kupata utajiri zaidi imetuponza. Kama ambavyo nilivyotangulia kusema, watu hawa walijitambulisha kuwa wanatoka ubalozi wa Marekani na walifika kwangu wakidai kuwa wanatafuta mtu mwaminifu ili wamkabidhi hizo dola azisimamie wakati wa kusafishwa, na kwamba mtu waliyemuona ni mimi", alisema mzee Sadik.

"Uliwauliza, walikufahamu vipi?", nilimuuliza.

"Naam, niliwauliza wamenifahamu vipi, pia niliwauliza wanajuaje kuwa mimi ni mwaminifu katika masuala ya pesa, mmoja wao alisema amepata kusikia sifa zangu na ndiye aliyependekeza waje kwangu, mara moka nikayaamini maneno yake", alisema mzee Sadik.

Nikajiweka vizuri kwenye kiti ili niweze kusikia habari hii, maana kwa kiasi fulani ilianza kuusisimua mwili wangu, "Baada ya hapo nini kiliendelea?".

"Baada ya kuongea mambo kadhaa na watu hawa, nikiuliza maswali nao wakijibu, hatmaye walinidokeza kuwa baada ya tukio la wizi wa dola milioni mbili za Kimarekeni, lililotokea Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, usafirishaji wa dola, paundi na pesa zingine zinazoingizwa nchini Tanzania ulibadilishwa, sasa zinaingia kama karatasi halafu zinasafishwa kwa dawa maalumu ili zianze kutumika kama dola", alinyamaza kidogo ili kupisha swali, alipoona nimekaa kimya akaendelea.  

"Nilihoji pia, ili kujuwa kama ni tukio hilo la wizi tu lililopelekea pesa zote zinazoingizwa nchini Tanzania kuchafuliwa, pia nilitaka kujuwa hali hiyo ni kwa Tanzania peke yake, watu hao ambao walikuwa wakiongea taratibu kwa kujiamini sana, walisema uhalifu umeongezeka sana duniani hivyo mamlaka za fedha zimeona hiyo ndiyo njia salama zaidi ya kusafirisha pesa", alieleza.

Aisee ni stori tamu sana, endelea nakusikiliza", nilisema huku Kanali Emilly akitabasamu.

"Baada ya majadiliano ya muda mrefu, maofisa hawa waliodai kuwa wanatoka Ubalozi, walitoa mfano wa karatasi kadhaa zikiwa na rangi nyeusi, wakadai kuwa hizo ni dola orijino ambazo huletwa nchini na baadaye kusafishwa kwa dawa maalumu ambayo walisema pamoja na kupatikana kwake kuwa vigumu, wao wanajua mahali pa kuipata na kazi hiyo ikafanyika vizuri. Una swali?", aliuliza huku akiniangalia usoni, macho yetu yalipokutana, alionekana wazi kuwa mwenye aibu. 

"Teacher, karatasi anazoeleza mzee Sadik nimekuonyesha kabla hatujaanza mazungumzo", alisema Kanali Emilly nikatikisa kichwa kukubaliana naye.

"Sasa ilikuwaje ukaamini kuwa hizi karatasi ni dola?", nilimuuliza baada ya kusimama, nikazichukua zile karatasi alizonionyesha Kanali Emilly, nikamuonyesha, maana maelezo haya yaliniingia vizuri, nikasahau kama nilikuwa likizo.

"Lo, sijui shetani gani aliniingia, mwanzo sikuwaanini kabisa, nilipanga kupiga simu kuwajulisha polisi kuhusu watu hawa ili wakamatwe, lakini baadaye nilishawishika kuwaomba vitambulisho vyao, hakika vilikuwa vitambulisho vya ubalozi wa Marekani, nikaanza kuyaamini maneno yao, nikaingia kwenye mtego baada ya mmoja wa maofisa hawa kutoa dawa na kusafisha karatasi kadhaa ambazo ziligeuka kuwa dola halali kwa matumizi. Hakika nilianza kusadiki, baada ya kudai kuwa dawa waliyonayo ni kidogo haiwezi kusafisha zaidi ya karatasi ishirini", alinyamaza kidogo akachukua glasi yake ya juisi akanywa kiasi huku midomo yake ikimcheza mfano wa mtu aliyekutana na baridi kali.

"Teacher, nakuhakikishia kuwa, kazi ya kusafisha karatasi hizo na kuwa dola ilifanyika mbele ya macho yangu, nilifuatilia tukio hilo kwa umakini wa hali ya juu. Karatasi kumi ziliingizwa kwenye dawa nikiona, baada ya sekunde kadhaa zikatolewa zikiwa tayari zimebadilika na kuwa dola mia mia za Kimarekani, wakati huo boksi kadhaa zilikuwa kando zikiwa zimesheheni karatasi hizo, hakika nikauona utajiri mkubwa mbele yangu, nikajua sasa nimeukata", alisema mzee Sadik, alinyamaza kupisha kama kuna mtu mwenye swali, alipoona kimya akaeleza. 

Baada ya karatasi hizo kusafishwa na kila moja ilikuwa dola mia za Kimarekani kuonekana, walinikabidhi, halafu wakaanza kusafisha karatasi ambazo walidai ni paundi za Uingereza ambazo pia zilipotakata zilikuwa paundi mia kila moja. Wakadai dawa hiyo imeisha nguvu, wanatafuta watu wa kusaidia ili karatasi hizo zisafishwe na kuwa dola. Wakanipatia dola zilizosafishwa ili niende sehemu ya kubadilishia pesa kuthibitishe kama ni dola halali, nikafanya hivyo, hakika zilikuwa dola halali kabisa, nikajiona mwenye bahati kuonana na watu hawa".

"Aisee, kweli hapo hakuna ujanja, lazima utaibiwa tu", nilimwambia akacheka kidogo huku akisisitiza kuwa huo ni wizi ambao si rahisi mtu kukwepa, labda uwe fukara. Na jamaa hawa hawamfuati mtu asiye na kitu.

"Tamaa ya kupata pesa nyingi imeniponza", alisema akitoa kitambaa cha jasho mfukoni akafuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.

"Karatasi walizokuja nazo ofisini kwako na kudai kuwa ni dola ambazo hazijasafishwa, waliziacha kwako?". niliuliza. 

"Yes, waliziacha karatasi hizo kwangu huku wakisisitiza kuwa nisitoe taarifa hii kwa mtu yeyote, wakadai kuwa wangerudi kesho yake mapema kuangalia kama nimebadili dola, ili tuangalie uwezekano wa kupata pesa za kununua dawa kwa ajili ya kusafisha karatasi zilizobaki, ambazo walidai iwapo zitasafishwa zote ni zaidi ya shilingi bilioni tano za Tanzania, nilifurahi sana", alisema mzee huyu.

"Kama ndivyo, mbona wewe umefaidika", nilimwambia.

"Hapana, nimeumia sana Teacher, waliporudi mara ya pili walinieleza kuwa karatasi hizo zina thamani kubwa sana, ni mapesa ya kigeni yanayosubiri kusafishwa, kwa hiyo waliniomba mimi kama mwenyeji wao niwatafutie mtu mwenye pesa ili tununue dawa na kusafisha karatasi hizo, ambazo wao walidai kuwa waliziiba ubalozini", anabainisha.

"Ndipo wewe ulipotoa pesa?", nilimuuliza.

"Hapana, kwa vile walinieleza kuwa dawa ya kusafisha karatasi hizi inauzwa kwa bei mbaya, nilimfuata mzee mwenzangu, Enock Nyanda, baada ya kumshawishi alikubali tushirikiane kutoa pesa ili dawa ipatikane, ndipo kazi ya kutafuta dawa ilipoanza".

"Hapo ndiyo patamu sasa, ehee?", niliteka masikio.

Baada ya utaratibu wa pesa kupatikana, maofiosa hawa kutoka ubalozi walituambia kuwa, sehemu ambayo tunaweza kupata dawa ni kwenye maabara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Walishauri kuwasiliana na Profesa waliyedai kuwa anahusika na maabara ya chuo, baada ya kuwasiliana naye kwa simu yake ya mkononi, alitupangia muda ya kwenda kumuona", alitulia kidogo, akaonesha hasira iliyokuwa katika nafsi yake, halafu akacheka.

""Watu hawa walijipanga vizuri", nilijisemea.

"Hakika, kwa mchezo huu walijipanga vizuri kuhakikisha wanafanikiwa", alirukia Kanali Emilly.

"Inaonyesha hivyo. Maana siku iliyofuata tulifika eneo la chuo kikuu, tukakutana na Profesa mmoja anaitwa Davis Magajimbo, kwa vile alikuwa ametuelekeza sehemu ya kumuona, Baada ya kumfahamisha kuwa tunahitaji dawa ya kusafisha dola, alitueleza kuwa dawa hiyo inauzwa bei mbaya na ili kuipata lazima zipatikane shilingi milioni mia moja za kitanzania", alisema, baada ya kutafakari kidogo akaendelea.

Kutokana na thamani ya dola na wingi wa karatasi zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kusafishwa, tulikubali kutoa kiasi hicho cha pesa kwa Profesa, ambaye alitukabidhi dawa huku akidai kuwa dawa hii ni nyingi sana, akashauri kama ikibaki tutaitumia wakati mwingine. Haraka tuliwasiliana na maofisa wa ubalozi kuwajulisha kuwa dawa imepatikana, nao hawakuchelewa kufika". 

"Walipofika ikawaje?", niliuliza.

"Kufika kwa maofisa hawa kulitupa faraja, walishauri dawa hiyo ihifadhiwe vizuri kwenye jokofu, ili kazi ya kusafisha dola kwa vile ni nzito ifanyike kesho yake mapema alfajiri, kwa madai kuwa kuna kazi nyingine wanaifanya wakati huo ili kesho yake wasiwe na ratiba nyingine", alisema mzee Enock ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu.

"Ah, jambo hili lilipangwa kwa ustadi wa hali ya juu, tulihifadhi dawa hii vizuri kama watu hawa walivyoagiza, siku ya pili walifika mapema alfajiri kama walivyoahidi, walinihimiza nitoe dawa ili kazi ya kusafisha dola ianze", alipofika hapo machozi yakaanza kumwagika.

"Usilie tafadhali, hii ni hali halisi ya dunia, unaweza kulala masikini ukaamka tajiri, ama ukalala tajiri ukaamka masikini, yote ni mipango ya Mungu", niliwaambia ili kuwatia moyo.

ITAENDELEA 0784296253


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru