NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI

"Teacher, sasa tunawasaidiaje wazee hawa?", lilikuwa swali kutoka kwa Kanali Emilly. Kutokana na swali hili, nilitembea hatua tatu kutoka nilipokuwa nimesimama, halafu nikarejea tena kwenye kiti nilichokuwa nimeketi awali.

"Inategemea...", nilijibu kwa mkato,

Baada ya kutafakari kwa muda, huku tukiangaliana kama mabubu, nililazimika kumweleza Kanali Emilly kuhusu mkakati wangu wa kazi zilizokuwa mbele yangu.

"Afande..., kabla sikaingia kazini rasmi, naomba utambue kuwa kujiingiza katika jambo hili, ni sawa na kuanzisha vita, nasema hivi kwa sababu watu waliofanya uhalifu huu wana mtandao mkubwa mno. Hawa ndio wahusika wakubwa wa dawa za kulevya, ndio wahusika wa uhalifu wa kila aina. Swali langu ni kwamba, uko tayari kwa mapambano na watu hawa?", nilimuuliza.

"Potelea mbali, lolote liwe, dunia itatukumbuka kwa hili, tukilimaliza salama tutashukru, tukiishia njiani naamini wapo watakaokuja kuliendeleza", Kanali Emilly alisema huku akisimama kuonyesha msisitizo. "Niko tayari kabisa".


Nililazimika kumweleza Kanali Emilly, kuhusu shambulizi la jana usiku uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, akaonekana kushangazwa, nami nikatumia nafasi hiyo kumweleza jinsi nilivyojipanga kukabiliana na watu hawa, maana walikuwa wamenianza.

"Afande, kutokana na umuhimu wa jambo hili, nimelazimika kuwaita vijana wetu wawili, Luteni Claud Mwita kutoka Morogoro na Sajenti Julius Nyawaminza kutoka Zanzibar, hawa ni makomandoo wenye uwezo mzuri, bahati nzuri wako karibu na eneo hili.  Hapa ofisini nimeamua kuwatumia Luteni Fred Libaba na Sajenti Peter Twite tu, nina sababu za kufanya hivyo", nilidokeza.

"Sababu gani hiyo Teacher, wakati idara yetu hapa inao vijana wenye uwezo mzuri tu, wangeweza kukusaidia kwa karibu zaidi, jambo hili linahitaji ushirikiano wenu", alishauri.

"Afande, nimelazimika kufanya hivi kwa sababu, sielewi ilibainika vipi kuwa nimesafiri, ilifahamika vipi kuwa niko kwenye ndege nikirejea Dar es salaam, na sijui nini kilisababisha hata watu hawa wakanishambulia baada ya kutoka kwenye ndege, hilo linanitia shaka", nilimwambia. "Hawa vijana tutawashirikisha kwa kazi nyingine, kuhusu hii watuache kwanza. Kama utapenda operesheni hii iwe na mafanikio utaniwia radhi kwa hilo".

"Umesomeka, hakuna ubishi katika hilo. Kuna la ziada?".

"Hapana", nilimwambia, baada ya ukimya wa sekunde kadhaa nilimwambia kuhusu ujio wa shemeji yangu Mama Feka. "Afande, kama ulivyosikia nikiongea na simu, shemeji yangu tunayeshibana sana yuko njiani kuja Dar es  Salaam, pamoja na kwamba anakuja kwenye mahafari ya chuo kikuu, kwa vyovyote vile atapenda kufikia kwangu, kama unavyojua familia yangu nimeihamisha kabisa ili sasa vita vianze, itakuwa vita ya kufa au kupona", nilisema kwa hasira.

"Sasa kuhusu huyu shemeji yako utafanyaje, maana nyumbani kwako sasa si sehemu salama kama ulivyosema?", alihoji Kanali Emilly.

"Nafikiria kumshirikisha katika vita hivi, maana ujio wake unaweza kuwa faida au hasara, lolote laweza kutokea", nilimwambia Kanali Emilly akaonekana kunishangaa.

"Kwanini umeamua kufanya hivyo Teacher?. Huyu shemeji yako ataweza kumudu hali ngumu ya vita ambavyo hatujui nani adui na rafiki?".

Nilitumia dakika mbili tatu kumweleza Kanali Emilly, kuhusu uhodari wa Mama Feka. Nilimweleza jinsi mama huyu alivyo na msimamo imara katika kutekeleza majukumu yake, nilieleza historia yake fupi, kuwa kabla ya kujiunga na chuo kikuu huria cha Tanzania, alifanya kazi kama mwalimu wa michezo katika shule kadhaa, lakini kabla ya hapo alikuwa ameshiriki mafunzo mbalimbali ya kijeshi kwa mjibu wa sheria.

"Kuhusu hilo nakuachia utaamua mwenyewe. sasa umepanga kumtumiaje huyo shemeji yako, au ni siri yako?".

"Hapana, ndiyo maana nikakushirikisha kuhusu jambo hili. Afande, Mama Feka ni mwanamke mrembo sana, ni mwanamke ambaye anaweza kumshawishi mwanaume yeyote akaingia katika himaya yake. Labda nikudokeze jambo moja".

"Itakuwa vizuri".

"Hapa Dar es Salaam, kuna mtandao wa uhalifu ukiongozwa na mzungu mmoja aitwae Carlos Dimera, kama unavyojua taratibu na sheria za nchi yetu huwezi kumkamata mtu bila kuwa na ushahidi wa kutosha. Taarifa nilizonazo ni kwamba huyu Carlos anapenda sana wanawake warembo, kwa Mama Feka ataingia, akiingia amekwisha", nilifafanua.

"Ni mpango mzuri Teacher, tufanye kila iwezekanavyo watu hawa wakamatwe na ushahidi, hii itasaidia kuwafikisha mahakamani, nikutakie kazi njema, tuwasiliane kila hatua utakayofikia, ukihitaji msaada wa aina yoyote usisite kunijulisha, kuanzia sasa ofisi hii itaacha mambo mengine yote ili tushughulikie jambo hili", Kanali Emilly alisema.

"Nikutakie kazi njema, tuombe mungu ndiye mwenye dhamana ya uhai wetu, lolote likitokea itakuwa kwa mapenzi yake, lakini pia tuko tayari kufa kutetea wengi", nilisema huku tukisimama. Tukashikana mikono.

Muda ulikuwa umeyoyoma sana, nilitoka ofisini kwa Kanali Emilly, huku mawazo mengi yakiwa yamenizonga juu ya jambo hili, nilijiuliza kuhusu mbinu walizotumia watu hawa, kiasi fulani nilijikuta nikicheka mwenyewe na kuwasifu kwa jinsi walivyoweza kufanikisha mpango wao wa wizi na kuwaacha wazee hao kwenye mataa. Nilifungua mlango nikatokea mapokezi. Linnah aliponiona akasimama.

"Pole sana bosi wangu, naona kikao kilikuwa kirefu kupita maelezo", alisema, mama huyu askari mwenye cheo cha Staff Sajenti, lakini aliheshimiwa sana kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka.

"Ndiyo mambo ya kazi. Sikiliza Linnah, naomba nisaidie kazi moja muhimu sana, niitie Sajenti Peter Twite aje ofisini kwangu haraka, ikiwezekana aingie kwa siri. mtu zaidi yako asijue", niliagiza halafu nikaingia ofisini kwangu.

Nilipanga kumtumia Peter kufanya kazi maalumu, kazi ya kimafia, ambayo ingetusaidia kumaliza jambo hili haraka. Baada ya muda mfupi Peter aliingia ofisini kwangu.

"Jambo Afande?" alinisalimia.

"Jambo. Habari ya toka usiku wa jana, Peter ujumbe wako ulinisaidia sana, maana sikujua lolote litatokea, sijui ingekuwaje?", nilimuuliza.

Peter akatumia muda huo kueleza mambo yalivyokuwa uwanja wa ndege, akaeleza jinsi alifika uwanja wa Julius Nyerere kwa ajili ya kunipokea, uwanja wa ndege alikutana na watu ambao aliwatilia shaka, kutokana na uzoefu wake wa kazi baada ya kuwawafanyia utafiti alibaini kuwa walikuwa katika mpango wa kumsubiri mtu.

"Ilikuwa vigumu saba kuwabaini, baada ya kutulia na kusoma mazingira ya uwanja wa ndege, nilibaini magari mawili aina ya BMW, moja likiwa limeegeshwa karibu kabisa na sehemu ya kutokea abiria na lingine liliegeshwa sehemu ya kutokea magari. Ulipoanza kutoka wewe watu wawili walilikimbilia gari la mbele, ambalo lilianza kuondoka, lingine likasuri gari ulilopanda liondoke ndipo wao walifuate gari hilo kwa nyuma. Haraka nikakutumia ujumbe wa tahadhari".

"Ama kweli ulifanya kazi ya ziada, sikuwa na mashaka kabisa, bila wewe pengine siku ya leo ingekuwa ya maombolezo kwangu, asante Peter", nilimshika mkono.

"Usijali mkuu, haya ni matunda yako, kumbuka wewe ndiye uliyenifundisha haya, ulinifundisha jinsi ya kunusa harufu mfano wa mbwa, Nikushukuru kwa kunifikisha hapa", alisema Pete.

"Tuachene na hilo, sasa nataka ufanye kazi moja ya muhimu sana, nimemwambia Mzee Emilly kuwa mapambano yameanza, ni mapambano makali ambayo yafaa tuyapigane sasa, hakuna jinsi, kazi yako tafuta vijana watano, wawe raia wa kawaida tu, lakini waendesha bodaboda jijini, ingia nao mkataba, lakini wapatie pamit na alama ili wasisumbuliwe na migambo. Pikipiki zao waziegeshe kwenye barabara kubwa tano za jiji. Yaani Morogoro road, Ali Hassan Mwinyi, Nyerere road, Kilwa road na Bibi Titi Mohamed, ukimaliza hilo tuwasiliane nitakuelekeza kazi nyingine", niliagiza.

"Nitalifanya hilo haraka sana bosi", alisema Peter.

"Ok, usikose kunijulisha, kumbuka kuwafahamisha kuhusu matumizi ya pikipiki hizo, maana tumepanga kuwatumia wao katika kazi fulani, isifike wakati wakatushangaa, kazi kwako".

Niliwasiliana na Luteni Claud Mwita kumuuliza kama uwepo wake eneo hilo umebaini nini akanidokeza kuwa watu ni wengi, pamoja na kufanikiwa kufahamiana na Sajenti Julius Nyawaminza, wameimalisha ulinzi katika eneo hilo.

Simba, Nyati na Chui, wao walikuwa eneo hilo wakitembea hatua kadhaa kwenda upande mwingine na kurejea kwenye pointi huku silaha zao ndogo, zikiwa tayari zimeondolewa usalama. Risasi zikiwa chemba tayari kwa lolote.

ITAENDELEA 0784296253  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru