NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI

Baada ya kupanga mipango yangu, niliyoofanya kimya kimya, nilifungua mkoba wangu mdogo, nikatoa kamba niliyoinunua Kariakoo. Ilikaribia kuwa saa moja ya usiku, giza lilianza kuifukuza nuru, niliwasiliana na wenzangu. Claud Mwita, Julius Nyawaminza na Fred Libaba nikawaomba tuonane kwenye Mghahawa wa YWCA uliopo hapo Posta Mpya kwa ajili ya chakula cha jioni.

Pamoja na kwamba Mghahawa huu uko karibu kabisa na kituo cha Daladala cha Posta Mpya, wengi hawakupajua, lakini pia niliwahadharisha wenzangu kuwa makini. Nilishauri kila mmoja achukua chakula na atumie meza tofauti, baada ya hapo tutakuwa na mazungumzo yetu binafsi nje ya eneo hilo.

Taratibu nilifungua mlango wa ofisi yangu nikachungulia kwa nje, nilitafuta sehemu ya siri nikazificha funguo za gari, halafu nikawasiliana na David, mmoja wa vijana wanaofanya kazi karibu yangu, nikamfahamisha mahali nilikohifadhi funguo hizo ili azichukue na kuipeleka gari kwa aliyeniazima, rafiki yangu Edgar.


Hapakuwa na dalili yoyote ya kuwa na mtu, hata Linnah alikuwa ametoka na kufunga ofisi yake, nilitoka haraka na kuivamia lifti iliyonishusha ghorofa ya kwanza. Nilitembea haraka hadi kwenye maegesho ya magari, sikutaka kupoteza muda, nilichungulia upande wa pili lilipo jengo la ofisi za benki ya CRDB. Baada ya kujiridhisha kuwa hakukuwa na mlinzi eneo hilo wakati huo, nikairejesha kamba yangu kwenye mkoba, baada ya kujiridhisha kuwa hakuna kikwazo cha kunisumbua.

Niliangalia nyuma na upande wangu wa kulia na kushoto, sikumuona mtu, lakini kwa vile jengo hili linalindwa kwa  kamera maalumu za usalama, nililazimika kufanya jambo moja ili kamera hizo zisinione. Nilisogea kwenye kivuli, nyuma ya magari kadhaa yaliyoegeshwa hapa, nikatumia nafasi hiyo kujirusha chini, upande wa jengo la CRDB. Haikuwa shida kwangu kuruka sehemu kama hiyo.

Lango la kutokea bado lilikuwa wazi na kwa vile kuna ofisi zingine juu ya ghorofa hili, nilitoka na kuwapita walinzi na baadhi ya askari polisi waliokuwa kwenye kibanda chao cha ulinzi. Nielekea shell ya Gapco, nikakavuka barabara na kuingia YWCA, Wenzangu wote walikuwa wamefika na tayari walikuwa wamepata chakula.

Tulisalimiana na kupeana ishara, kwa vile Mghahawa huu ni wa kujihudumia mwenyewe, na njaa ilikuwa karibu iniue nilielekea kwenye dirisha la huduma, nikaagiza chakula, ambacho nilikula haraka haraka, ili kwenda sawa na wenzangu, ambao kila mmoja alikuwa na hamsini zake.

Wakati huo Carlos Dimera alikuwa akiwasiliana na wakala wa kusafirisha mizigo kutoka Bogota, nchini Corombia, wakala akimjulisha kuwa baada ya masaa ishirini na nne mzigo huo ambao ni dawa za kulevya, utakuwa umewasili kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

"Tunahitaji maelezo kutoka kwenu, hivi tunavyoongea hapa shehena ya dawa za kulevya imetua salama katika uwanja wa ndege Addis Ababa, nchini Ethiopia. Tumelazimika kupitishia mzigo nchini Ethiopia badala ya Ouagadougou, nchini Burkina Faso kama ilivyokuwa awali kwa sababu za usalama, taratibu zote za mzigo kuondoka Ethiopia kesho zimekamilika, kazi kwenu, vipi hali ya usalama huko?", Carlos Dimera aliulizwa.

"Dar es Salaam, Tanzania hali si mbaya sana, japokuwa kuna mawingu na mvua za hapa na pale, lakini haziwezi kutuzuia kuendelea na majukumu yetu. Kuna wingu moja limetanda angani kuashiria mvua, lakini wataalamu wa hali ya hewa hapa Tanzania wanasema wingu hilo halina madhara, waganga wako kazini kuhakikisha wingu hilo halidondoshi hata tone moja la maji, kuhusu hali ya uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ni nzuri sana, tunausubiri", alieleza Carlos Dimera kwa simu ya mkononi.

"Oke, lakini kuweni makini sana katika jambo hili, nasikia serikali ya Tanzania sasa hailali?."

"Kuhusu hilo ondoa shaka kaka, niko na mtandao unaoeleweka, mtandao wa vijana wa mjini ambao nimewafundisha mbinu za kila aina, hata hili wingu lililotanda angani mwisho wake wa kutanda na kuleta hofu ni leo, wingu hili halitakuwepo tena", alisisitiza Carlos.

Baada ya Carlos Dimera kumaliza kuongea na simu hiyo, aliingiwa na hofu kidogo, alisimama akatembea hatua mbili, halafu akajiuliza maswali kadhaa, akainua simu yake ya mkononi na kuongea na Nombo.

"Uko wapi Mr. Nombo?", alihoji Carlos Dimera.

"Niko katikati ya mji bosi, nimelazimika kuja huku kuongeza nguvu kwa vijana, kazi hii lazima iishe leo bosi, kuna habari mpya?", Nombo alihoji.

"Hakuna habari mpya, isipokuwa wakala wa kusafirisha mizigo anauliza, hatua gani tumefikia, mzigo umewasili salama Addis Ababa, Ethiopia, yamebaki masaa ishirini na nne tu mzigo uwasili Dar es Salaam, na wingu bado limetanda angani, unadhani kuna uwezekano wa kuliondoa?", Carlos Dimera aliuliza.

"Tulia bosi, tumuombe Mungu atasaidia, maana uwezekano ni mkubwa mno, kwa vile hujafika kwenye uwanja wa mapambano, ungeshuhudia adui alivyowekwa kati, hakika jengo lote la Benjamin Mkapa liko chini ya usalama wetu, kila anayetoka na kuingia anaonekana, kuhusu hilo usijali, leo ndiyo mwisho wa wingu hili, labda utokee muujiza gani".

"Niwatakie kazi njema, jitahidini bwana jambo hili liishe mapema leo, vinginevyo nitume kikosi kazi?, hawa jamaa zetu wapo tu wanasubiri kazi kama hizi, mkishindwa semeni", aliuliza Carlos.     

"Hakuna sababu, mapambano ya mchana yangeleta shida kidogo, maana watu walikuwa wengi eneo hili, lakini sasa hali iko shwari, hili giza litatusaidia pia. Kunywa, kula ukiamini kuwa kazi hii imekwisha", Nombo alieleza, Carlos akapata faraja na matumaini.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU