NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Baada ya sisi wote kupata chakula cha jioni kwenye Mghahawa huu wa YWCA, tulitoka mmoja baada ya mwingine kama tulivyoingia, lakini tukiwa nimewapa ishara ya kukutana sehemu nyingine ambayo tutafanya mazungumzo na kupanga mipango yetu kwa siri. 

Kabla ya kutoka ndani, niliwasiliana na Mama Feka, ili kujua wapi amefika, akanifahamisha kuwa amefika salama Jijini Dar es Salaam. Nilimfahamisha kuwa nitamtafuta kesho, hivyo atafute hoteli itakayomfaa apumzike kwani alikuwa amesafiri kwa muda mrefu.

Wakati tunatoka ndani ya Mghahawa huu wa YWCA, nilisikia kelele za risasi, zilizosikika kutoka upande wa pili, zikafuatiwa na harufu ya baruti. Kwa sisi wazoefu wa mambo ya silaha, mara moja nikahisi jambo. Watu walikimbia kuelekea upande tuliokuwa, ghafla kwa muda mfupi hali ya usalama ilikuwa imetoweka katika eneo la Posta Mpya.

Tuliangaliana na wenzangu, moyo wangu ukaingiwa na hofu, nikahisi jambo la hatari limemtokea David. Tulianza kusogea taratibu eneo la tukio. Nilifungua mkoba wangu nikatoa moja ya kofia zangu za kuficha sura, nikaivaa ili kuficha sehemu ya uso wangu.  

"Tukimbie, majambazi yamevamia na kuua watu, mwenyezi mola tusaidie", mama mmoja wa makamo alisikika huku akikimbia kuyanusuru maisha yake.

"Sijawahi kuona unyama kama huu, binadamu kumuua binadamu mwenzao tena mbele ya watu utadhani wanaua mnyama", alieleza mzee mmoja aliyekuwa amelala kwenye mfereji wa barabara ya Azikiwe.

Toyota Carina TI, ambayo David alikuwa akiendesha kutoka kwenye maegesho ya magari ghorofa ya kwanza, ishambuliwa na kuteketezwa vibaya kwa kombora ambalo halikujulikana, David aliuawa katika shambulizi hilo. Waliofanya shambulizi hilo hawakufanya makosa. Nilisikitishwa sana, lakini kwa kiasi fulani nilijiona mwenye bahati, maana kazi yangu sasa ingekuwa rahisi au ngumu zaidi.

Polisi hawakuchelewa kufika eneo la tukio, waandishi wa habari pia waliwasili na kamera zao, mimi na wenzangu Claud Mwita, Julius NYawamizna na Fred Libaba tuliangalia tukio hilo kwa dakika kadhaa tukiwa mbali kiasi, halafu tukapeana ishara ya kuondoka eneo hilo. Hata kama ungekuwa mtaalamu wa hisia kiasi gani hakika usingeweza kubaini ishara zetu, labda uwe mmoja kati yetu.

Kutokana na uzito wa tukio hilo, niliwasiliana na Peter Twite, nikamfahamisha klichotokea, nikamwelekeza mambo ya matatu ya kufanya, afike haraka eneo la tukio na kutoa taarifa kwa Kanali Emilly, ahakikishe majina ya marehemu hayaripotiwi kwenye vyombo vya habari, ofisi anayotoka marehemu iwe siri na mwili wake uhifadhiwe mahali salama mpaka tutakapomaliza kazi.

Baada ya kutoa agizo hilo kwa Twite, tulikubaliana kuonana kwenye Mghahawa wa Chief Pride, uliopo mtaa mdogo wa Chaga, katikati kabisa na barabara za Jamhuri, upande wa kushoto na Libya, upande wa kulia. Tulipanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza, hapakuwa na wateja zaidi ya meza na viti. Wakati tunapanda ngazi, muhudumu alitufuata kwa nyuma, tulipoketi akawa tayari kutusikiliza. Tuliagiza vinywaji kila mmoja alichoona kinamfaa.

"Nadhani hapa patatufaa kwa mazungumzo, au mnasemaje bosi?", Fred alihoji baada ya muhudumu wa Mghahawa huu kuondoka.

"Pamoja na kwamba sijaelewa lolote kuhusu kilicho mbele yetu, lakini kwa utulivu huu, nashauri tuifanye sehemu hii iwe kwa ajili ya kukutana tukiwa na dharura. Naamini kazi tuliyoitwa kuifanya itakuwa ngumu, lakini tutashinda", alieleza Claud.

"Sikilizeni, naamini mpaka sasa adui zetu wanasherehekea ushindi wakidhani nimekufa, David ameuawa kinyama, wamemuua wakidhani ni mimi, sasa kabla jua la kesho halizachomoza, yatupasa kufanya kazi ya ziada, kujua wauaji wanapatikana wapi, wanafanya nini? Sababu zilizowasukuma kutushambulia, tukilijua hilo, kazi yetu itakuwa rahisi, tofauti na hapo tutakuwa tunajisumbua kutwanga maji ndani ya kinu", niliwaeleza.

Vinywaji vililetwa mezani, tukaanza kunywa huku kila mmoja akieleza mpango kazi wake. Baada ya kila mmoja kutoa mchango wake huku Fred akijaribu kuweka kumbukumbu ya maandishi, nikakumbuka kuhusu, Carlos Dimera.

"Wakati mwingine linapotokea tukio la kushitua kwa aina hii, akili yangu hulazimika kufanya kazi ya ziada. Fred..., unaweza kumfahamu mzungu mmoja anaitwa, Carlos Dimera?".

"Yaa. Ndiyo, Carlos Dimera namjua, huyu jamaa ndiye tajiri mwenye kile kiwanda cha kutengeneza tembe za malaria, Huyu jamaa anatajwa kuwa mtu safi na mwaminifu kwa serikali, pia anatajwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii, ana nini?", Fred alihoji.

"Yatupasa kumchunguza haraka iwezekanavyo. Nimewahi kusikia minong'ono kuhusu yeye, lakini nisimchumie dhambi, nataka kujua anaishi wapi, anapendelea mambo gani?", nilimuuliza Fred.

"Huyu Carlos, anaishi Mikocheni A, ukiziacha taa za usalama barabarani za Morocco, barabara ya kwanza kabisa ingia kulia, nimewahi kuonyeshwa na rafiki yangu mmoja Inspekta wa polisi. Anasema walikwenda kupokea msaada wa Pikipiki kumi za kuwasaidia polisi kufanya doria, ndipo nilipobaini kuwa ni mtu safi. Ni matajiri wachache sana wenye moyo wa kusaidia suala la usalama wa raia", alifafanua Fred.

"Siyo sababu, yafaa achunguzwe, na kazi hii lazima tuifanye usiku huu, huyu jamaa kwa nyakati fulani, binafsi nilijaribu kufuatilia nyendo zake, sikupata mambo makubwa sana, lakini nilipata mashaka kidogo, sasa nitamfuatilia kwa undani zaidi ili nijiridhishe", nilisema.

"Inspekta Judith, aliyenionyesha nyumbani kwake alinidokeza kuwa wakati anawakabidhi Pikipiki hizo, Carlos mwenyewe aliwaeleza polisi kuwa binafsi anachukia sana vitendo vya uhalifu, akaahidi kutoa magari mawili maalumu kusaidia doria, ndiyo maana najiuliza", Fred alieleza.

"Siyo sababu, wahalifu wana mbinu nyingi, hujaona wachawi walivyo wakarimu, anakufanyia vitendo vya ushirikiana huku akikuonyesha wema. Hata ukielezwa kuwa huyu ndiye mchawi wako huwezi kuamini, kutoa msaada haitoshi kukufanya uwe mwaminifu", Nyawaminza alieleza.

"Hakika", Claud alisapoti.

"Ndugu zangu, Claud na Julius, kwanza poleni kwa safari, niwaombe radhi kwa safari ya kushitukiza, nimelazimika kuwaita ili tusaidiane kupigana vita iliyoko mbele yetu", nilitumia nafasi hiyo kuwaeleza kila jambo, kuanzia wazee walioibiwa kwa mtindo wa noti bandia na jinsi dawa za kulevya zinavyoingizwa nchini na kuchangia kuharibu maisha ya ambani ni nguvu kazi ya taifa na kizazi cha sasa.

"Tuko pamoja". 

"Kuanzia sasa, mtaziacha kazi zenu zote, mtayaacha majukumu yenu yote, tukabiliane na jambo hili, si kazi rahisi kama tunavyodhani, kuwakabiri watu hawa ni sawa na kuwa mkononi na tiketi ya kwenda ahera, kwa vile tuliapa kuilinda Jamhuri yetu, hatuna budi kuifanya kazi hii", niliwaambia huku wote wakiniangalia kwa macho makavu.

"Hakuna shaka kuhusu hilo Kamanda", alieleza Claud, Julius akatikisa kichwa kuunga mkono. 

Nikatumia nafasi hiyo pia kuwaeleza wenzangu kuhusu ujio wa shemeji yangu Mama Feka, nikawaeleza nilivyopanga kumtumia mwana mama huyu. 

"Ataweza?", alihoji Nyawaminza huku akicheka. 

"Naamini ataweza, Mama Feka ni mmoja kati ya wanamke jasiri sana", niliwahakikishia, halafu nikamgeukia Fred, "Sikiliza Fred, hawa jamaa watafutie mahali pa kulala leo, kuanzia kesho hatutakuwa na muda wa kulala, lakini iwe maeneo ya Sinza, Kinondoni au hata Kijitonyama, mimi nitakwenda nyumbani kwangu wakati huu, kuna vifaa vyangu vya kazi nitachukua halafu nitamtafuta Carlos, hata wewe pumzika maana kesho utakuwa na kazi nyingi zaidi".

"Asante", Fred alishukuru.

"Angalizo, jambo hili bado ni siri, pale ofisini hakuna anayejua mpango huu zaidi ya Mzee Emilly, Twite na wewe Fred, hatuna sababu ya mtu mwingine kujua, ndiyo sababu ya kuwaita hawa jamaa, Claud na Nyawaminza. Of rekodi", nilionya. 

"Nimekusoma", alieleza Fred.

"Fred, wakati unakwenda kulala, hakikisha unapata ratiba ya huyu Carlos, ujuwe ni mtu wa aina gani, anapenda nini, ana msimamo gani, nani rafiki zake wa karibu na hiki kiwanda chake kinakidhi haja? tumia akili zaidi kuliko nguvu".  

Wakati huo kulikuwa na sherehe kubwa nyumbani kwa Carlos Dimera, vinywaji vya kila aina vilikuwa mezani, nyama za kila aina zilitafunwa, muziki laini ukipenya katika masikio ya watu hawa, kila mmoja akiyatafakari maisha baada ya kazi nzito.

"Umefanya kazi nzuri sana Nombo, kuanzia sasa mshahara wako unaongezwa mara mbili zaidi, lakini hata, Simba, Nyati na Chui pia posho zenu zimeongezwa, mmefanya kazi nzuri sana. Kumfuatilia adui kuanzia usiku wa jana, leo asubuhi, mpaka jioni mnamaliza kazi ni jambo kubwa mmefanya. Kuondoka kwa mbwa huyo ni ushindi kwetu", Carlos Dimera alieleza.

"Wakati mwingine lazima ujifanye kama mwendawazimu ili kazi yako iwe nzuri. Nguvu ya Nombo kwenye uwanja wa mapambano imesaidia sana, milango yote ya kuingia na kutoka ilikuwa chini yetu, tulisubiri mpaka mwisho, alipotoka tu akakutana na kifo, wakati ndugu zake wakiomboleza sisi tunakula raha", Nyati alieleza.

"Sasa ni wakati wa kula na kunywa, kazi yenu imenifurahisha sana, sina budi kuwaambia nawapenda sana, shehena kubwa ya dawa za kulevya yenye utajiri, itaingia Dar es Salaam, kesho alasiri, taratibu zote za kupokea mzigo huo zimefanyika, kunyweni lakini msilewe", Carlos alishauri. Wakaendelea kunywa huku wengine wakicheza muziki.

Wakaendelea kula, kunywa na kucheza muziki.

ITAENDELEA 0784296253


Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU