NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA MBILI
Ilikaribia kuwa saa sita na nusu za usiku, niliposhuka kwenye taksi iliyonitoa katikati ya mji, nilipenya uchochoroni, nikapita nyuma ya Kanisa la KKKT, lililopo Kijitonyama, nikaambaa na ukuta wa kanisa hili nikaibukia kwenye barabara ya vumbi inayoelekea nyumbani kwangu. Nilitembea haraka haraka, nilipoufikia mti ulio karibu na nyumba yangu nikasimama na kuufanya kuwa ngao yangu.

Eneo hili lilikuwa kimya kabisa, ni nyumba yangu pekee iliyokuwa katika hali ya giza. Hii ilitokana na familia yangu kutokuwepo. Baada ya kujiridhisha kuwa hali ilikuwa shwari, nilinyata mfano wa paka, nilipoufikia ukuta wa nyumba, nilitoa funguo za mlango wa siri ulioko nyuma ya ya nyumba, nikaufungua taratibu, nikaurejesha kama ulivyokuwa, nikasubiri kwa sekunde kadhaa halafu nikasogea na kuingia.

Kwa vile hali ya usalama haikuwa nzuri, familia yangu niliihamishia sehemu nyingine, nilitumia nafasi hiyo kukagua usalama wa eneo la nyumba yangu, nilipohakikisha kuwa hakuna dalili zozote za hatari, nikauendea mlango wa nyumba, nikaufungua kwa tahadhari nkajitosa ndani.

Ndani ya Nyumba hii kulikuwa kumepekuliwa sana, kabati ya nguo iliyoko chumbani kwangu ilikuwa imepekuliwa na baadhi ya nguo na vitu vyangu vingine kuachwa bila kuvirejesha mahali pake. Nadhani waliamua kuviacha hivi baada ya kujiridhisha kuwa waliniua katika shambulizi la Posta kwa hiyo waliamini kuwa siko tena duniani. Lakini walikosea jambo moja. Hakuhakikisha nani alikuwa akiendesha gari lile walilolishambulia.

Kiasi fulani nilicheka mwenyewe, maana nilijua sasa kazi imeanza, niliyakumbuka maneno ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa akitangaza vita dhidi ya majeshi dhalimu ya Ndul Iddi Amin Dada wa Uganda. Kilichonisisimua zaidi ni pale Mwalimu aliposema, 'RAFIKI ZETU WALIOKUWA WANASEMA MWALIMU ACHA, SASA WAKAE PEMBENI, WATUPISHE, MAANA HATUTAWASIKILIZA TENA, ILI SASA UBISHI UISHE'.

Maneno haya ya Mwalimu Nyerere yaliniongezea hamasa, nililiendea kabati langu maalumu lenye dhana zangu muhimu za kazi, kabati hili lilikuwa sehemu ya siri, nikalifungua kabati hilo lililoko ukutani, nikatoa fulana mbili maalumu zisizopenya risasi (bletproof), nikazihifadhi vizuri kwenye mkoba wangu, halafu nikatoa bastola mbili aina ya M9 zisizotoa sauti, zote zikiwa zimejazwa risasi kumi na mbili kila moja kwenye magazini zake, nikazifutika kwenye mapaja yangu, moja kulia na nyingine kushoto. Nikatoa magazini zingine nne zenye risasi za ziada, mkasi wa kukata vyuma na kisu kidogo nikaviweka kwenye mkoba wangu.

Kichwa changu kilijawa na mambo mengi, nilijiuliza hili na lile, nikishika hili na lile. Niliwakumbuka wenzangu, Luteni Claud Mwita, Fred Libaba na Julius Nyawaminza, moyo wangu ukajawa na matumaini ya ushindi. Maana kila mmoja alikuwa na hamasa ya kuingia kwenye uwanja wa mapambano.

Baada ya kutoa vifaa hivyo, nilirudi hatua moja nyuma, nikasimama nikitafakari nini kingine kitanisaidia zaidi katika mapambano na watu hawa, nikaikumbuka ngazi yangu ambayo mimi huitumia kupanda au kushuka kwenye majengo makubwa. Pamoja na kwamba nilikuwa na kamba maalumu niliyoinunua Kariakoo kwa ajili ya kazi hiyo, nikalazimika pia kuichukua ngazi. Usidhani ni mzigo mkubwa, ilikuwa ngazi ya kisasa kabisa, unaweza kuiweka hata kwenye mkoba wako na mtu asijuwe ulichobeba.

Sasa nilikuwa tayari kwa mapambano na watu hawa, nilipiga magoti chini nikamuomba mungu wangu, nikawaomba bibi na babu zangu ili wanisaidie. Nikayakumbuka maneno mazuri ya waswahili, 'AKUANZAE MMALIZE' nikaapa kufa au kupona. Ama zangu ama zao.

Baada ya kupiga maombi, nilitoka ndani ya nyumba yangu na kuacha kila kitu kama nilivyokikuta, Hasira na woga vyote vilikuwa ndani ya nafsi yangu, nikajiuliza iwapo nitaishia njiani katika vita hivi nani atakuja kuviendeleza. Imani ikanijia kuwa iko siku atapatikana kijana mkeleketwa wa atakayewasha moto na kuendeleza mapambano hadi kieleweke.

Saa yangu ya mkononi ilinieleza kuwa ni saa nane kasoro dakika chache usiku, nilipenya kwenye uchochoro nikatokea Chuo cha Ustawi wa Jamii, eneo hili lilikuwa na wasichana kadhaa wanaouza miili yao, waliponiona walinigombea, lakini mimi sikuwajali, niliwapita kimya kimya nikatafuta taksi iliyonishusha karbu na taa za usalama barabarani za Morocco.

Muda huu magari yalikuwa machache barabarani, baada ya kushuka kwenye taksi iliyonileta, nilitembea haraka kurudi nyuma, kama Fred alivyokuwa amenielekeza, nilianza kuhesabu nyumba moja baada ya nyingine, nikiitafuta nyumba ya Carlos Dimera, hatmaye nikaiona.

Eneo hili lilikuwa limezungukwa na miti mingi, kwa vile nilikuwa nimevaa nguo nyeusi, nililipita geti kuu la kuingilia ndani. Nilifanya hivi ili kuona kama kulikuwa na mtu yeyote eneo hilo. Baada ya kujiridhisha nilirudi nikinyata taratibu na kwa tahadhari kubwa, nikauparamia mti uliokuwa karibu na ukuta, nikatulia juu kwa sekunde kadhaa, nikiangalia ndani ya ngome hii. Nilipoona hali ni shwari niliifungua ngazi yangu, nikaifunga juu, halafu nikashuka taratibu kwa hadhari, hatimaye nikajitosa ndani. 

Mwanga mkali wa taa ulilifanya eneo hili kuwa la usalama wa kutosha, muziki laini ulisikika ndani ya jengo lililokuwa mbele yangu. Nililala kifudifudi, nikakuloo hadi nyuma ya dirisha lililokuwa na kelele ya muziki, nikautumia mti mkubwa uliokuwa eneo hili kujikinga ili nisionekane.

Chumba hiki kilikuwa kimejaa watu, Carlos Dimera alikuwa ameketi juu ya kiti kikubwa, huku wasichana wawili warembo wakifanya kazi ya kumpepea asipate jasho, vijana kadhaa walikuwa wakicheza muziki, huku wengine wakipata vinywaji.

"Jamani, makamanda wangu, mmeinjoi hamjainjoi?" Carlos aliwauliza vijana wake.

"Tumeinjoi sana bosi, tumekunywa, tumekula, tunacheza muziki", walisema.

"Kama nilivyosema, mzigo unaingia usiku, sasa sitaki mlewe, tuna jukumu kubwa mbele yetu, Teacher amekufa sawa, lakini hatujui nani atafanya nini, au siyo jamani?", Carlos Dimera alieleza.

"Hakika, lakini nikutoe hofu bosi, kifo cha Teacher kitasababisha wengine waogope kabisa, ni mtu mwendawazimu ambaye ameona kilichompata mwenzake, halafu aingie kichwa kichwa, itawachukua muda", Nombo alidakia.

"Ndiyo, lakini mnajua wanaweza kujiuliza kwanini Teacher ameshambuliwa na kuuawa kinyama namna ile?", Carlos Dimera aliuliza.

"Maswali lazima yawepo, nakuhakikishia mzigo utaingia na kusambazwa kwa amani kama ilivyokuwa, huyu mshenzi alikuwa kikwazo kikubwa kwetu, kifo chake ni faraja kubwa katika familia yetu", Hawa Msimbazi alieleza.

Nilikaa kimya nikiwasiliza washenzi hawa, nilijiuliza kwanini hawakuweka ulinzi wa aina yoyote katika eneo hili, lakini nikabaini kuwa hofu ya kuvamiwa na mimi ilikuwa imewatoka baada ya kubaini kuwa niliuawa katika shambulizi lile.

"Kanali Emilly ameagiza lazima wwatu hawa akamatwe wakiwa na ushahidi, vinginevyo tutakuwa tumefanya kazi ya bure", nilijisemea mwenyewe, maana bila hivyo walikuwa katika himaya yangu, ningewaita wenzangu tukawatia mikononi, lakini tutakuwa tumefanya kazi ya bure.

"Wakala anasubiri taarifa kutoka kwangu ili mzigo uondoke Addis Ababa, Ethiopia. Hatutaki kufanya makosa, shehena iliyopo stoo ni ndogo, mzigo unaotarajiwa kuingia ni mkubwa kiasi cha matumizi ya miezi sita, kazi kwenu, kuingia kwa mzigo huu kutawafanya wote kuuaga umasikini", aliwaeleza Dimera.

"Bosi, tumejipanga vizuri mno, waswahili wanasema kila anayetaka cha uvunguni sharti ainame, maana yangu ni kwamba, kila atakayeonekana kuingilia anga zetu, mauti yatamkuta, Teacher ni mfano wa kuigwa na wenzake", Jakna alifafanua.

"Basi, maneno yenu yamenitia nguvu, Jakna, unajua utaratibu wa kupokea mzigo, panga halafu utanijulisha, nitawasiliana na wakala ili kuwajulisha hali halisi ya Dar es Salaam. Kama ilivyo kawaida yetu, Hawa Msimbazi, utasimamia taratibu za kupokea mzigo. Sitaki mpango wetu huu uferi", alisisitiza.

Walizungumza na kujadili mambo mengi huku nikiwasikiliza, nilimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa na kusikia upuuzi wao, ilionekana kuwa hofu yao ilikwisha kabisa baada ya kufanya shambulizi lililomuua kijana wetu David.

Dakika kumi zilikuwa zimenitosha kabisa, baada ya kudaka baadhi ya maneno ambayo niliamini yatanisaidia katika kazi yangu, nilijitoa taratibu, nikapita sehemu ile ile ya awali, nikatoa ngazi yangu na kuondoka eneo hili salama usalimini. Nikiamini kuwa habari hizi zitamshangaza sana Fred.

ITAENDELEA 0784296253   


Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU