NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA TANO

Wakati vyombo vya ulinzi na usalama nchini vikifuatilia kwa makini na karibu matukio ya kutisha ya uhalifu yaliyokuwa yakiendelea Jijini Dar es Salaam. Watu kadhaa walifika vituo vya polisi kutoa maelezo ya jinsi walivyo tapeliwa.

Mfanyabiashara John Roman, afika Kituo Kikuu cha Polisi, Sokoine Drive, baada ya kuibiwa kwa njia ya mtandao, Shaaban Ismail, baada ya kubaini kuwa ameibiwa, alifika haraka kituo cha polisi Oysterbay, ambapo maofisa wa polisi walichukua maelezo yak.

John Roman ni mmiliki wa klabu ya 'Toroka Uje' ambaye aliibiwa pesa nyingi kwa njia ya mtandao. Alifika polisi akionyesha namba za simu za nje zilizotumika kuwasiliana nae na kumfanya atume pesa nyingi, akiwaomba polisi watumie uwezo kuzifuatilia namba hizo.

Akihojiwa na polisi wa zamu waliokuwa kituoni hapo, John Roman alieleza kuwa, awali alipokea ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB, ukimweleza kuwa ameteuliwa kuwa mrithi wa Hayati John Bryson wa Uingereza, aliyekuwa na akaunti katika benki hiyo, lakini alifariki dunia na kuacha pesa nyingi..

Maelezo ya John Roman yalimshawishi Afisa wa Polisi kumhamishia chumba maalumu cha mahojiano, afisa huyo alifanya hivyo baada ya kuvutiwa na taarifa hiyo. Alipoingia ndani ya chumba hicho, askari huyo alimtaka bwana John Roman kulielezea vizuri kuhusu tukio hilo.

"Nimekuleta katika chumba hiki ili tuweze kuzungumza kwa uwazi zaidi, tukio hili ni moja ya matukio ya uhalifu yanayotokea karibu kila siku, naomba uanze kueleza toka  mwanzo wa tukio hili mpaka sasa, usifiche kitu na usione aibu. Eleza mpaka ulivyofika hapa", Inspekta Judicate alieleza, akijiweka sawa kuandika maelezo yake.

"Ni hadithi ndefu Afande, lakini nitahitahidi kueleza kama ilivyo, naamini polisi mba mbinu zetu ambazo zitasaidia kuwakamata watu hawa. Maana kichwa changu hakifanyi kazi vizuri, nimevurugwa", John Roman alieleza.

"Usijali, maji yakimwagika hayazoleki, lakini maelezo yako yataisaidia polisi katika upelelezi wa tukio hili, cha msingi usifiche jambo", Inspekta Judicate alimhakikishia.

"Asante sana Afande, nakumbuka siku tatu zilizopita nilipokea ujumbe kupitia email yangu, ukiuliza kama mimi ndiye John Roman raia wa Tanzania Bara, nilipojibu ndiyo, nilipokea ujumbe mwingine ukiniuliza nahusika na biashara gani, nilipojibu kuwa namiliki klabu. Hawakutuma ujumbe tena, isipokuwa walinipigia simu wakitumia namba za nje ya nchi", alinyamaza kidogo ili kumeza mate, baada ya kutafakari aliendelea.

"Afande, watu hawa ni wajuzi wa hali ya juu, aliyenipigia simu alijitambulisha kwa majina ya Roggers Peter, akidai kuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambayo Makao Makuu yake ni Ouagadougou nchini Bukinafaso, Afisa huyu alinieleza kuwa benki imenichagua mimi kuwa mrithi wa mali za marehemu John Bryson, raia wa Uingereza aliyekuwa na pesa nyingi katika benki hiyo, nilipohoji inakuwaje niteuliwe kuwa mrithi wa mali za mtu nisiyemjua, Afisa huyo alinieleza kuwa huo ni mpango wa siri wa benki na kwamba watanitumia nyaraka mbalimbali za marehemu John Bryson, ikiwa pamoja na hati ya kifo ili nizitumie kupokea pesa hizo kama urithi alioniachia. Lakini akaniasa kuwa mwaminifu, akidai kuwa kuna dola milioni sita za kimarekani ambazo zitaletwa Tanzania kwa jina langu, nitazipokea uwanja wa ndege, halafu tutagawana", alieleza.

Inspekta Judicate aliyekuwa akiandika maelezo hayo kwa haraka na kwa umakini, aliuliza "Kumbe Makao Makuu ya Benki hii yako Bukinafaso?"

"Hata mimi ndiyo nafahamu hivyo, maana sikuwa na uhakika". 

"Oke. Kwa jinsi inavyoelekea ni kweli watu hawa ni wajuzi katika kutenda uhalifu, ehee, ikatokea nini sasa?".

"Nilishawishika kwenda kwenye mtandao, kama unavyojua dunia sasa ni kijiji, sikuchelewa nikaandika neno Mtendaji Mkuu wa ADB, likatokea jina la Roggers Peter, nikaanza kuyaamini maneno ya mtu huyo, baada ya muda nikapokea taarifa na nyaraka mbalimbali za marehemu John Bryson, ikiwa pamoja na hati ya kifo, ikieleza kuwa alifia nchini Uingereza na kuzikwa huko", alinyamaza kidogo kupisha kama kuna swali.

"Hizo nyaraka ulizipokea kwa njia gani?", Inspekta Judicate alihoji.

"Documenti zote za tukio hili zilitumwa kwa njia ya mtandao, na kweli zilikuwa zinaendana na tukio lenyewe, ilifika wakati nikaanza kuwaamini, mimi ni mtu makini sana lakini sijui nilipatwa na jinamizi gani?", alieleza John Roman huku akitoa nyaraka hizo na kuzikabidhi kwa Inspekta Judicate. 
   
Inspekta Judicate alizipitia documenti hizo moja baada ya nyingine, akiziangalia kwa makini, halafu akaziweka kando.

"Ehee, nini kikatokea sasa, maana unanieleza hadithi ambayo hakika ni tamu masikioni mwangu, endelea?".

"Jana asubuhi, nilijulishwa kuwa benki imewatuma maofisa wake wawaili, Mohamed Mussa na Seif Mtigino kusafirisha pesa hizo hadi Dar es Salaam, nilitakiwa kufika uwanja wa ndege saa sita mchana kwa ajili ya kupokea pesa hizo. Kwa kuwa pesa zina mambo mengi, nilimuomba Afisa wa Jeshi la Ulinzi, Kapteni Masey anisimamie kupokea pesa hizo, lakini alinikatalia, akidai kuwa huo ulikuwa utapeli, kiasi fulani nilimlaumu, lakini sasa nimeamini kuwa alikuwa na nia njema", alieleza John Roman. 

"Afisa huyo wa Jeshi hakukueleza chochote zaidi ya kusema uache ni utapeli, kama wewe mwenyewe ulivyosema hapa?".

"Afisa huyo yeye alikataa tu, akidai kuwa hao ni matapeli na kwamba hawezi kupoteza muda wake kunipeleka kwa matapeli eti nikatapeliwe, lakini pia alinisihi niachane na mpango huo, lakini sikumwelewa, ndiyo nazinduka usingizini sasa baada ya kuwa tayari nimeibiwa, tena nakumbuka alinieleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi za Afrika tu, haiwasiliani na mtu mmoja mmoja, pia alieleza kushangazwa na mtindo wa kusafirisha pesa hizo kuja Tanzania, ningemsikiliza hakika nisingekutwa na jambo hili", alieleza machozi yakimtoka.

Inspekta Judicate alikuna kichwa cheke, huku kalamu yake ikiwa mdomoni kwa mshangao, alimwangalia John Romani kwa macho makali. "Kumbe ulipewa darasa la kutosha na bado ukaendeleza ujinga wako, aisee wewe ni kichwa maji kweli, lazima ufahamu kuwa maofisa wa Jeshi wana mbinu nyingi, kama alivyokushauri ungemsikiliza, au ungetoa taarifa kituo chochote cha polisi".

"Ni kweli, hata mimi najiuliza sasa, sijui niliingiwa na tamaa au shetani gani, maana wakati wote mimi ni mtu makini sana", alieleza John Roman.

"Wewe si mtu makini, ungekuwa makini usingekaidi ushauri wa Afisa wa Jeshi", Inspekta Judicate alieleza kwa sauti ya kukatisha tamaa. Alimwangalia John Roman kwa macho yake makali, macho ya mwanamke Afisa wa polisi, aliyewiva katika utendaji kazi wake.

"Ni kweli Afande, unajua linapotokea jambo kama hili ndiyo mtu unajifunza, kwa kuwa limetokea sina jinsi kujifunza". alieleza John Roman kwa unyenyekevu.

"Ehee, kwa hiyo hizo dola ndiyo zikaletwa Dar es Salaam au ilitokea nini tena?", alihoji Inspekta Judicate kwa shauku.

"Ilipofika saa tano jana, nilipokea simu nyingine kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kwa majina ya Mohamed Mussa, akadai kuwa yeye Afisa kutoka ADB, akanijulisha kuwa ndege iliyokuwa ikitoka Bukinafaso kuelekea Dar es Salaam, Nchini Tanzania imepata hitlafu ikiwa angani na kutua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Entebe, Nchini Uganda, hivyo, akashauri nitume haraka dola elfu ishirini za Marekani ili waweze kuondoka Entebe kuja Dar es Salaam, wakidai kuwa visa zao zikiisha kabla ya kufika Dar es Salaam, itabidi warudi tena Bukinafaso, jambo ambalo wao binafsi hawapendi litokee".

"Ukatuma pesa hizo?".

"Mdiyo, ikanilazimu kuwatumia hizo pesa".

"Kwa nini hukuwaambia watumie pesa walizokuwa wakisafirisha kuleta Dar es Salaam. Maana kama ni pesa walikuwa nazo tena nyingi. Dola milioni sita ni pesa nyingi, ni zaidi ya shilingi bilioni kumi za Tanzania, inakuwaje utume pesa?", Inspekta Judicate alihoji.

"Niliwashauri watumie pesa hizo walizokuwa wakisafirisha, lakini wakadai kuwa taratibu za Benki haziruhusu pesa hizo kufunguliwa mpaka zifike sehemu husika, nikawaeleza kuwa mimi ni mlengwa wa pesa hizo, naruhusu zitumike, lakini hawakunielewa, wakadai kuwa zikifunguliwa itakuwa vigumu kupokelewa na wakala wa Dar es Salaam, atakayethibitisha kama pesa hizo zimefika salama Tanzania, ikanilazimu kutuma kiasi hicho haraka iwezekanavyo", alieleza.

"Mama yangu, baada ya kutuma pesa hizo ikatokea nini?", Inspekta Judicate alihoji.

"Baada ya kutuma pesa hizo. Simu zao hazikupatikana, kuanzia ya aliyejiita Mtendaji Mkuu wa ADB, pamoja na maofisa wote waliohusika kunipigia simu, lakini pia nilipotoa taarifa kwa mamlaka zingine ili kuzuia pesa hizo zisichukuliwe, nilikuwa nimechelewa, hali halisi ndiyo hivyo Afande", alieleza John Roman.

"Mmmm, iko kazi, maana inawezekana watu hawa wako hapa hapa Dar es Salaam, naamini pia wanakufahamu, ndiyo maana wakaweza kupata hata namba zako za simu na majina yako, ok, ngoja tujaribu jinsi ya kukusaidia, pia taarifa hii tutaipeleka kwa wenzatu wa usalama ili nao waifanyie kazi", Inspekta Judicate alieleza huku akisimama.

"Nitashukru", John Roman nae alisema huku akimshika mkono wa wakaagana.

Wakati huo, Mama Feka alikuwa amewasili kwenye maegesho ya magari ya Msasani Shopaz Plaza, alifika eneo hili mapema kwa ajili ya kazi moja, kumshawishi Carlos Dimera ampende. Alikuwa ameketi ndani ya gari aina ya Ford Pick Up yenye rangi ya kijani, ambayo vioo vyake vilikuwa vyeusi, hivyo si rahisi kuonekana kwa mtu anayepita nje. 

Aliketi kwenye viti vya nyuma vya gari hii Doble Cabine, huku wakiteta mawili matatu na Peter Twite, aliyemleta hapa. "Cha msingi uwe makini sana na watu hawa, naamini Teacher hawezi kumtuma mtu asiyemwamini, amekuamini ndiyo maana amekutuma katika kazi hii", Peter Twite alimwambia Mama Feka.

"Nitajitahidi sana, naamini siwezi kuwaangusha, sijui kitokee nini, lakini nitajitahidi kupambana, najiamini", Mama Feka alimwambia Peter. Alichukua picha ya Carlos Dimera iliyokuwa kwenye mkoba wake, akaingalia kwa mara ya mwisho, halafu akairejesha mahali ilipokuwa. 

"Baadaye", Mama Feka aliaga.

"Kila la heri, usiogope, maana kila utakapokuwa tutakuwepo pia", Peter alieleza, Mama Feka akashuka kwenye gari na kuingia upande wa Supermaket hii kubwa iliyoko Barabara ya Kawe, Dar es Salaam.

Dakika kadhaa baadaye, Carlos Dimera aliwasili eneo hilo, akifuatana na mpambe wake, Jackna, walipoukaribia mlango wa kuingilia ndani, Jackna alikimbia na kuufungua mlango huo, ili Dimera aweze kupita. kama ilivyo kawaida yao, Walipoingia ndani haraka Jackna, alianza kusukuma tololi, akiwa nyuma ya bosi wake, ambaye wakati huo alikuwa akichagua vitu kadhaa anavyopenda kununua katika Supermaket hii. 

Mama Feka aliyekuwa upande huo, akitafuta jinsi ya kuwasiliana na watu hawa, alibeba kikapu mkononi, akasogea mpaka kwenye pembe ya mwisho ya Supermaket, mapigo ya moyo yakamwenda mbio, akajiuliza mawili matatu, akapata jibu. Haraka akazunguka upande wa pili, alipofika sehemu ya makutano, hakuchelewa, akamgonga Jackina kama bahati mbaya, vifaa vyake zikamwagika chini.

"Vipi wewe kaka unatembea kama kipofu?", Mama Feka alihoji.

Jackina alihamaki, haraka akainua mkono wake juu ili aushushe katika mashavu ya Mama Feka, lakini Carlos Dimera alikuwa mwepesi akaudaka mkono wa Jackina na kumzuia.

"Jackina, acha bwana, usipende kuwapiga watoto wazuri kama huyu, Mungu aliwaumba ili waupendezeshe ulimwengu", Carlos Dimera alisema huku akitembea taratibu kuelekea kwa Mama Feka. "Pole sana, usijali kwa lililotokea", hakafu akamgeukia Jackina, "Haraka okota vitu vyake, nitamlipia bili". Jackina aliinama na kuokota vitu vilivyokuwa vimemwagika na kuvirejesha katika kikapu.

"Utaongeza nini malkia ili nikulipie bili?", Carlso Dimera alimuuliza Mama Feka aliyekuwa amesimama akiwaangalia kwa hasira.

Alichukua kikapu chake, akatembea hatua mbili, halafua akawageukia na kusema, "Sikiliza kaka, mimi sibabaiki na rangi yako, kwetu si masikini kama unavyodhani, sina shida ya kulipiwa bili, tunajiweza ndiyo maana nikaja hapa, kaa na pesa zako, lakini pia mwambie huyu bwege wako avae miwani ili siku nyingine aweze kuona".

"Shika adabu yako we malaya", Jackina alifoka.

"Malaya ni wewe unayetembea kama kipofu",

"Nyamaza Jackina, mbona hunielewi, usipende kugombana na wasichana", Carlos alimtuliza Jackina huku Mama Feka akiondoka. "Ni msichana mzuri sana", aliongeza Carlos.

"Lakini, anaonekana kuwa hana adabu bosi". 

ITAEBDELEA 0784296253  

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU