NOTI BANDIA

SEHEMU YA KUMI NA SITA

Kama ilivyo kawaida yake, Carlos Dimera, aliwasili katika Hoteli ya Seaclif, ambako hukutana na wageni kutoka nje ya nchi, ambao hufika nchini kwa ajili ya biashara haramu ya dawa za kulevya. Mara hii alifika hapa ili kuonana na mtu maarufu sana duniani, mtu ambaye vyombo vya habari vya dunia humtaja karibu kila siku.

Hakuwa mwingine, huyu ni Emilio,
mtoto wa Pablo Escoba, aliyekuwa mwanasiasa, mbabe wa dawa za kulevya, raia wa Colombia ambaye historia inaonyesha hakuwa na mfano. Kijana huyu Emilio, alikuwa amewasili nchini kwa ajili ya kuonana na Carlos Dimera. Alimtambua Carlos kama mtu wa karibu, kutokana na historia zao.
 

Mtoto huyu wa mbabe wa dawa za kulevya, ambaye baba yake alitoka katika familia ya mwalimu na mkulima, aliambatana na msichana mrembo, Serina Wilson.

Jakna hakuruhusiwa kusikiliza mazungumzo ya Carlos na mgeni wake Emilio, hivyo aliketi katika meza nyingine karibu akisubiri. Wakati wote Carlos alikuwa hafanyi kosa, alijua kufanya kosa moja kunaweza kumgharimu. Aliwatumia hawa kupokea na kusambaza dawa, lakini mambo yake ya ndani, hakupenda kuwashirikisha kabisa.

"Karibu sana, hii ndiyo Tanzania", Carlos alimwambia Emilio, wakasimama na kushikana mikono.

"Asante sana Carlos, vipi hali ya biashara hapa?", Emilio alihoji.

"Tuko vizuri", Carlos alijibu kwa mkato.

"Si kweli Carlos, nimelazimika kuja hapa, ili tuzungumze kwa kirefu kidogo, nini tatizo, haiwezekani mzigo ukwame Adis Ababa kwa muda mrefu kiasi hicho, halafu unasema uko vizuri?", Emilio aliuliza.

"Kuhusu hilo tumelimaliza, ni kweli kulikuwa na tatizo kidogo kwa wenzetu wa uwanja wa ndege, lakini jambo hilo limekwisha, kila kitu kimekaa vizuri, mzigo unaweza kuwasili Dar es Salaam leo, kuhusu hilo, ondoa shaka, tumelimaliza".

"Nini kilikwamisha huo mzigo kuingia hapa, kama ni pesa mnazo za kutosha, mnaweza kumnunua mtu yeyote, au unasemaje Carlos?".

"Hilo halina ubishi, ilitokea tatizo ngazi za juu, huko serikalini, mtu mmoja alipewa cheo akajiona tayari amekuwa Mungu, akahamia uwanja wa ndege, baadhi ya watu wamekamatwa, lakini si wa upande wetu, hata hivyo pesa imefanya kazi yake, mtu huyo ameondolewa, mzigo unaingia leo, mamlaka zote zina taarifa kuhusu mzigo huo kuingia", Carlos alieleza.

"Nilitaka kujua hivyo, haiwezekani nchi ndogo kama Tanzania kuwe na usumbufu wakati wa kuingiza mzigo, wakati nchi kubwa kama Marekani, China, Japan na South Afrika mzigo unaingia haraka na bila shaka. Nimekuelewa Carlos, nitaondoka leo, hakikisha biashara yetu inashamili na kupata watumiaji wengi zaidi, huo ndio msimamo wetu", alieleza Emilio huku akisimama kwa ajili ya kuaga na kuelekea kwenye helikopita iliyomleta eneo hili.

"Hatutalala, amini hivyo", alidokeza Carlos huku wakipeana mikono ya kwaheri,
akaaga na kuondoka, akiacha maswali mengi kwa Carlos. .

Baada ya Emilio kuondoka, Carlos alimwita Jakina.

"Tukiendelea kucheza ngoma za sindiba, tunaweza kupoteza kazi, unamfahami huyu jamaa?", Carlos alimuuliza Jakina.

"Hapana", Jakina alieleza.

"Huyu ni Mkurugenzi wa Shirika la Tuwezeshe, anatoka Marekani, alipenda kuonana na mimi kwa ajili ya mambo fulani, tukimaliza kazi hii salama, nitamuomba twende wote, yaani mimi na wewe tuishi Marekani, ukaishi huko Jakina", Carlos alidanganya.

"Hakuna kitakachoharibika bosi, tumejipanga vizuri mno, naamini mzigo utaingia usiku huu, Hawa amefanya kila jambo, hakuna wa kuzuia", Jakina alijinasibu.

Wakati huo, Mama Feka alikuwa ameketi upande wa pili kwenye kona akiwaangalia. Alipoona sasa ni wakati mwafaka, alitoka na kujipitisha mbele yao. Mama Feka alipita mbele ya meza waliyoketi Carlos na jakina, kama hajawaona vile akatafuta meza akaketi.

"Bosi, umemuona yule dada mshenzi wa Supermarket?", Jakina alimuuliza Carlos.

"Na wewe husahau, kama alikukela msamehe, nenda mwambie aje aketi na sisi hapa", Carlos aliagiza.

"Achana na huyo mshenzi, atatupotezea muda wetu, mbona wasichana wapo wengi tu bosi", Jakina alieleza msimamo wake.

"Hapana, nimesema nenda mwambie aje hapa".

"Mkorofi yule bosi".

"Jakina, elewa kuwa si ombi, nasema nenda mwambie aje aketi na sisi hapa, ni wakati wa kumuomba msamaha kwa yaliyopita", Carlos alieleza huku Jakina akisimama,

Huku mapigo yake ya moyo yakimwenda kasi, Jakina alitembea hadi mahali alipoketi Mama Feka. Aliona njia pekee ni utani, hivyo alimtokea kwa nyuma na kumshika bega.

"Helo, hujambo mrembo", alisema Jakina huku Mama Feka akigeuka. Macho yao yalipokutana, Mama Feka akaonyesha mshangao wa uongo.

"Haaa, wewe ndiye yule kipofu wa Supermarket?", Mama Feka alihoji.

"Hapana, ilikuwa bahati mbaya".

"Ilikuwa bahati mbaya, mbona ulikusudia kunipiga?".

"Ibilisi tu dadangu, bosi amenituma kwako".

"Bosi amekutuma kwangu, anasemaje?".

"Anaomba uhamie kwenye meza yake, tupate chakula pamoja".

"Tupate chakula pamoja, nikikuita kipofu unachukia, hapa unaona nakula, halafu unasema tukapate chakula pamoja na bosi wako, mbona siwaelewi?".

"Tunaweza kuhama na chakula chako, tafadhali niruhusu nikubebee chakula", Jakina aliomba.

"Hapana, mwambie bosi wake sina muda huo", Mama Feka alieleza.

"Sawa, lakini unapoteza bahati yako", Jakina alimwambia.

"Acha ipotee", Mama Feka alieleza kwa kujiamini.

Jakina alirejea kwenye meza ya Carlso.

"Yule msichana ni jeuri sana, anasema hana muda wa kuonana na wewe, nimemwambia anapoteza bahati amesema acha ipotee, anajiamini sana, yawezekana ni mtoto wa kigogo", Jakina alieleza.

"Achana naye, iko siku atanasa", Carlos alieleza, baada ya kupata vinywaji na chakula, Carlos na mpambe wake Jakina waliondoka.
                                ****************

Niliendesha gari kwa mwendo wa kasi ili tuwahi kufika. Wakati huo nilikuwa nikiendesha gari aina ya Isuzu Troupe steshen wogan yenye rangi ya kijani, Fred alikaa kimya akiniangalia, bila shaka aliuhofia mwendo wangu. Tulipofika kwenye taa za kuongoza magari zilizoko katikati ya Barabara za Mandela na Uhuru, eneo la Buguruni, nilisimama ili kusubiri ruhusa ya taa hizi.

Kila mmoja alikaa kimya akitafakari nini hatma ya jukumu lililokuwa mbele yetu, magari yalipoanza kuondoka, niliongeza mafuta nikayapita baadhi ya magari yaliyokuwa mbele, tulipofika kwenye taa za Tazara, zinazoruhusu magari yanayotumia Barabara za Nyerere na Mandela, tulisimama tena hadi zilipoturuhusu kuendelea na safari.

Dereva wa gari lililokuwa mbele yetu alinionysha ishara ya taa, nikalipita gari hili kwa mwendo wa kasi, nadhani dereva huyu alitambua haraka tuliyokuwa nayo, akaamua atupishe. Ni madereva wachache sana barabarani wenye uelewa kama huyu, nilipiga honi ya asanye, nikaongeza mwendo.

"Uko vizuri", nilimwambia Fred aliyekuwa kimya.

"Niko sawa", alisema huku akiniangalia.

"Lolote laweza kutokea, lazima tukubaliane na hali hiyo", nilimwambia Fred.

"Najua hivyo bosi, lolote laweza kutupata, lakini naamini kuwa tutashinda, wewe ukisimamia jambo sidhani kama linashindwa", alinipamba.

"Ni kweli, lakini kila jambo na wakati wake", nilisema wakati nikiingia kwenye maegesho ya magari ya Uwanja wa Ndege. Nilitafuta mahali pazuri nikaegesha gari.

"Fred... Hapa tumekuja kufanya kazi moja tu, kumkamata Afisa Ukaguzi, tukifanikiwa kumkamata huyu, kazi yetu itakuwa rahisi, vinginevyo itategemea kudra za Mwenyezi Mungu".

"Atakamatwa tu", Fred alisema kwa kujiamini.

"Sikiliza Fred, ingia ndani omba kuonana na Mr. Raymond Kenoko, ndiye Afisa Ukaguzi mwandamizi. Utakapomuona, mwambie kuna mgeni wake ndani ya gari, akifika hapa tumemaliza kazi", nilimwambia Fred. Aliniangalia kwa sekunde kadhaa halafu akavuta shati na kutoa bastola yake ndogo, akaigagua.

"Iweke hapo kwenye droo ya gari, hapa si mahali pake", niliagiza, akafungua droo ya gari akahifadhi silaha yake, akafungua mlango wa garu na kutoka taratibu kama ilivyo kawaida yake.

Kwa wasiomfahamu Fred, ni mmoja wa vijana watanashati, mtaratibu, hata vitendo vyake huvifanya taratibu, ukimuona ghafla unaweza kudhani ni mtu zoba, lakini ukihitaji undani wake, unaweza kuingia kwenye mto wenye mamba ili asikutie mikononi mwake.

Wakati nikimsubiri Fred, niliwasiliana na Kanali Emilly, kumuomba ajiweke tayari kuonana nasi wakati wowote kuanzia sasa. Niliwasiliana pia na Claud Mwita na Julius Nyawamiza kuwatahadharisha na hali ya sasa pia kuwaandaa kwa kazi.

Nikiwa ndani ya gari niliweza kuona kila mtu aliyekuwa karibu yangu, nikisaidiwa na aina ya vioo ya gari hii, kwani mtu akiwa ndani haonekani kabisa, lakini unaweza kumuona mtu wa nje kwa ufasaha zaidi. Mara Fred alifungua mlango akaingia.

"Huyu jamaa ametoka hapa dakika ishirini zilizopita, wanasema amekwenda kupata chakula pale Transt Motel, tumsubiri hapa au unasemaje bosi?", Fred alihoji.

"Hapana, hapana twende haraka", nilisema huku nikitoa shilingi elfu moja ili Fred akalipie ushuru wa maegeshi ya uwanja.

Haraka nikaliweka gari barabarani, nilipoona taa za Barabara ya Nyerere zitatuchelewesha kupita, niliamua kuliingiza gari huku madereva wa magari mengine wakitupigia honi, nikapenya na kuliegesha gari mbele ya Transt Motel, karibu kabisa na Reli ya kati.

Nilitoa picha ndogo ya Raymond Kenoko nikaiangalia kwa mara nyingine, haikuwa rahisi kumfahamu moja kwa moja hivyo ilitulazimu kutumia akili zaidi. Mara nikawaona watu wawili wakitoka ndani ya Transt Motel, walifanana urefu na maumbo yao, akili yangu ikacheza.

"Atakuwa mmoja kati ya hawa. Shuka muite kwa jina, atakayeitika ndiye", nilimwambia Fred akafungua mlango na kuita, "Habari ya kazi Mr. Ray?".

"Nzuri kaka, habari yako", Raymond alisema huku akisogea ili kumshika Fred mkono, mwenzake alitembea hatua chache akasimama kumsubiri. Bahati nzuri alivaa kitambulisho chake shingoni, kikiwa na jina la RH Kenoko.

"Samahani kwa usumbufu, naitwa Jabir Idrisa, nimefika ofisini kwako nikaelezwa kuwa umetoka kwa ajili ya chakula, nikaona nikufuate, kwa ufupi ni kwamba nina mzigo umekwama, lakini nimeelezwa kuwa nikikuona waweza kunisaidia, sasa tunafanyaje kaka?", Fred alidanganya.

"Nani kakutuma uje kwangu?" Alihoji kwa sauti nzito.

"Carlos", Fred alidanganya.

"Ahaa, sawa sawa, ni mzigo tofauti na unaoingia leo?", alihoji.

"Ndiyo, ni aina nyingine, labda tuingie ndani ya gari ili tuelekezane vizuri, uangalie uwezekano".

"Hakuna shaka", Raymond Kenono alisema huku akimuelekeza mwenzake atangulie ofisini. Fred alifungua mlango wa gari wakaingia.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru