NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI

Hali ya utulivu katika Jiji la Dar es Salaam, kiasi fulani ilikuwa imetoweka, Gabriel na George waliokuwa wamehitimu vizuri mafunzo ya ujasusi, katika nchi mbalimbali duniani, waliingia katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi moja tu, kumsaka Teacher. Majasusi hawa wakiendesha magari mawili tofauti, mmoja akiendesha Toyota Brevis yenye rangi ya Blue, mwingine alikuwa ndani ya Toyota Verosa yenye rangi ya Zambarau. Carlos Dimera aliuamini sana utendaji kazi wa vijana hawa, akasubiri kuona nini matokeo.

Mfano wa panya wa Suwa, wenye uwezo mkubwa wa kunusa na kutegua mabomu ardhini, majasusi hawa Gabriel na George, walianza kunusa harufu. Wakitumia mtambo maalumu wa kunasa mawasiliano, hatmaye walifanikiwa kuingilia mawasiliano ya Teacher, mara tu baada ya kuipata namba yake ya kiganjani. Mtambo huo maalumu uliweza kuonyesha mnara unaotumika kwa mawasiliano ya Teacher, baada ya kufanikiwa kuupata mnara huo, kazi ya majasusi hawa, ilikuwa kufuatilia uelekeo wa mahali mnara huo ulipo.

Carlos Dimera, alikuwa amewaeleza majasusi hawa kila kitu kuhusu Teacher, aliwaeleza jinsi Teacher alivyo mwepesi na mjanja wa kubaini mambo. Dimera alimwelezea Teacher kuwa ni mtu mwenye hisia kali katika tasnia hiyo. Hivyo aliwayaka walijiweka vizuri mara mia zaidi kwa ajili ya mapambano. iwapo hali hiyo itatokea.

Hatmaye mtambo ukawafikisha Kinyerezi, kila wanapotafuta uelekeo, mtambo nao unaonyesha mshale wa mawasiliano ya simu husika. kila waliposogea mlio fulani ulisikika ndani ya mtambo huo, kuashiria uelekeo ulikuwa sahihi. Hatmaye wakaifikia Hotel Bella, iliyoko Kinyerezi, nje kabisa ya Jiji la Dar es Salaam, eneo ambalo dakika chache zilizopita Teacher alikuwa amewasiliana na watu kadhaa. Majasusi hawa waliamini kuwa Teacher atakuwa amekia hotelini hapo kwa vile katika eneo hilo, hakukuwa na Hotel nyingine. wakajiweka sawa, wakapanga kuivamia. 

Ukweli ni kwamba, baada ya Teacher kufanikiwa kuwaburuta mahakamani, Hawa na Tony, alikubaliana na wenzake Fred, Claud na Nyawaminza, kila mmoja apumzishe akili sehemu aliyoona inamfaa, wakisubiri mahakama kutoa hukumu dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, Hawa na Tony. Akatafuta sehemu nzuri ya kupumzisha akili, sehemu ambayo si rahisi adui kuifikia, akajihifadhi Hotel Bella, kwa ajili ya usiku mmoja wa leo, akiisubiri kesho.

Kwa vile Hoteli Bella iko karibu na mitambo ya umeme wa ges ya SONGAS, baada ya majasusi hawa kufanya utafiti kuhusu eneo hilo, waliingia Hotelini hapo mmoja baada ya mwingine, wakikodi vyumba vya kulala, huku wakijisajili katika kitabu cha wageni kwa majina tofauti. George akijiita Mhandisi Hezdori Stephan, kutoka Zimbabwe nae Gabriel, alijiita Mhandisi David John kutoka Comoro. 

Wakati Gabriel anajisajili, alitumia nafasi hiyo kukagua majina ya wageni mmoja baada ya mwingine, kilichomshangaza hakukuwa na jina linaloelekea kuwa la Teacher. Hata hivyo, aliamini kuwa Teacher ni mjuzi katika tasnia hiyo, akaziamini hisia zake.

Kutokana na uzoefu katika mambo ya uchunguzi, Teacher hakupenda kusajili jina lake kwenye kitabu cha wageni, badala yake akajisajili kwa majina ya Mrs Martina Fundi, mhasibu kutoka mkoani Mtwara. Lakini kabla ya kuandika katika kitabu cha wageni alimjulisha mhusika wa Hoteli hiyo kuwa atakuja mgeni mwenye majina hayo, akalipa pesa za chumba halafu akaendelea na mipango yake mingine.

Kulikuwa na idadi kubwa ya wageni katika Hotel hii, wengi walikuwa wahandisi kutoka sehemu mbalimbali ya Tanzania, ambao walifika Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uzinduzi wa bomba la ges lililojengwa na Serikali kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.

Majasusi hawa, George na Gabriel walikuwa tayari wameipata taarifa hii ya uzinduzi wa bomba la ges kutoka Mtwara, wakajiita wahandisi. 

********************************

Ilikaribia kuwa saa mbili kamili za usiku, niliingia bafuni, nikaoga haraka haraka, baada ya kuvaa suluali na fulana iliyokuwa kwenye mkoba wangu, nilitoka na kuelekea sehemu ya bar kwa ajili ya kusikiliza taarifa ya habari ya usiku pamoja na kupata bia mbili za kutafutia usingizi. Si kwamba chumbani kwangu hakukuwa na televishen, la hasha, nilikwenda sehemu ya bar kwa ajili ya kunywa kidogo.

Muziki wa taratibu ulisikika, sauti za magwiji wa muziki nchini, akina Tx Moshi Wiliam, Joseph Maina, Kamanda Mzee Muhidini Gulumo wa OTTU Jazz zilisikia, kiasi fulani nilitokea kuipenda bendi hii, ninapozisikia sauti za watu hawa, huwa nafarijika na kusahau machungu.

Watu wachache walikuwa wameketi kwenye meza wakipata moja moto, moja baridi, baadhi walikuwa wakijadili kuhusu hali ya maisha ya sasa, mimi nilipita karibu yao, nikatafuta meza ya pembeni nikaketi. Mimi hupenda kukaa meza za pembeni, kwa sababu ambazo nitakudokeza ukinitafuta, ukinielewa sawa, usiponielewa shauri yako.

"Karibu kaka, nikusaidie kinywaji gani?" mhudumu wa hoteli hii aliniuliza baada tu ya kuketi.

"Nitashukru, umesema unisaidie kinywaji gani, asante kama hapa mnatoa vinywaji bure, niletee?" nilimtania.

"Hapana, hapana kaka, tunauza, labda nimekosea kiswahili, maana yangu unaagiza kinywaji gani, ulipe pesa nikuletee?"  msichana huyu alijitetea.

"Nitapata Wisky aina ya Tekla, zinazotengenezwa kwa mkonge?".

"Bila shaka zipo, ila bei yake imechangamka kidogo", alibainisha.

"Bei siyo tatizo, hebu niletee hilo Tekla chupa ndogo, usisahau maji ya kunywa, weka barafu nyingi kwenye glasi", niliagiza.

"Usijali kaka", akaondoka.

Watu waliokuwa ndani ya bar hii walikaa kimya wakifuatilia taarifa ya habari ya saa mbili. Habari kubwa ni utumbuaji majipu unaofanywa na Serikali. Watu walianza kuchoshwa na habari hii ambayo imekuwa ya kawaida kwenye vyombo vya habari.

Wakati najaribu kutafakari hili na hili na kazi zangu za kesho, mara kijana mmoja alisimama mbele ya meza yangu.

"Habari kaka?" alisema kijana huyu huku akivuta kiti kwa ajili ya kuketi.

"Salama", nilimjibu kwa mkato, vinywaji vyangu vililetwa, nikaanza kunywa huku nikimtafakari mtu huyu kimya kimya, sikuwa na sababu za kumzuia kuketi, baada ya kushikana nae mikono, akaketi.

"Samahani, naitwa Mhandisi David John kutoka Comoro, nimekuja kama kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa bomba la gesi, ama kweli huu ni uwekezaji mkubwa katika eneo hili", alieleza kijana huyu.

"Inawezekana", nilisema kwa mkato  

Nilijaribu kumtafakari tena kijana huyu, lakini sikuwa na jawabu la haraka, kutokana na uzoefu wa kazi hii kwa muda niliamini kijana huyu hakuwa mtu wa kawaida, mkono wake pekee ulinidhihirishia hivyo. Nilikunywa taratibu huku nikiwa katika hali ya hofu.

"Samahani kaka, kuna umbali gani kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara?", alihoji kijana huyu.

"Sina hakika", nilimjibu kwa mkato.

"Inaweza kuwa kilomita mia sita hivi, au zaidi?" aliuliza kwa mara nyingine.

"Nimesema sijui", niliongea kwa sauti ya kutisha kidogo ili asiendelee kuuliza.

"Nasikia Tanzania kuna bomba la mafuta lililounganishwa na Zambia, hivi ni kweli?" aliendelea kuuliza.

Niliinua glasi, nikanywa wisky yote iliyokuwa ndani ya glasi, "Mimi si Mhandisi. Lakini Wewe umejinadi kuwa ni Mhandisi, kwanini usijue kuhusu hilo bomba la mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia?" akacheka.

Mara nikasikia miguu yangu inaguswa na kitu, nilishituka, lakini nilikuwa nimechelewa. Nilipigwa shoti na kitu ambacho sikukijuwa, miguu na mikono yangu iliishiwa nguvu taratibu nikapoteza fahamu.  

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru