NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA

Baada ya mimi kuachana na wenzangu usiku ule, kila mmoja alitafuta uelekeo wake, Luteni Claud Mwita alipanga Elegant Lodge iliyoko kando ya barabara kuu inayotoka Majumba Sita kwenda Segerea. Julius Nyawaminza hakuona sababu ya kwenda mbali, akajihifadhi FQ Hoteli iliyoko hatua chache kutoka Elegant, katika barabara hiyo hiyo ya Segerea. Fred Libaba yeye aliingia Kilimani Lodge akaweka makazi yake ya muda,

Baada ya kufanikiwa kuwatoroka watu hawa, nilitembea kwa tahadhali kubwa, giza lilikuwa bado limetanda kwa nje. Kutoka kiwanda cha Blanket Keko, niliambaa na barabara ya Chang'ombe hadi, hapo nilikodi Bodaboda iliyonipeleka Segerea.

Ilikuwa saa kumi na moja kasoro dakika kidogo za alfajiri, nilipobisha hodi kwenye mlango wa chumba cha Luteni Claud Mwita, Elegant Lodge kama tulivyokuwa tumeelekezana awali. Niligonga haraka haraka kwenye mbao za mlango huu mara tatu, halafu nikasubiri kidogo. Giza lilikuwa bado limetanda kwa nje, taa zenye mwanga hafifu zilileta nuru sehemu ya kupita kuingia ndani ya jumba hii la kisasa. Baada ya kugonga nilisubiri kwa muda, Wakati najiandaa kugonga tena, ghafla nilisikia shingo yangu ikiwa baridi, chuma kizito kilinigusa vizuri shingoni, nikatulia na kujiandaa kugeuka kwa mzaha.

Kwanza nilidhani ni utani wa Claud. Wakati najaribu kugeuka nyuma yangu ili nifanye mzaha, sauti nzito ilisikika. Haikuwa sauti ya Claud kama nilivyoizoea. "Tulia kaka, inua mikono yako juu, halafu ugeuke taratibu upande wangu. Onyo, usithubutu wala kujaribu kufanya ujanja wa aina yoyote, maana jaribio lako lolote litakusababishia hasara".

Utabiri wangu haukuwa umebashiri vizuri kama nilivyoanza nikidhani ni Claud, matumaini yangu ya kutoka salama kwenye mahabusu ya awali yalitoweka. Jasho jembamba lilinitililika. Nilitii amri hiyo na kuweka mikono yangu juu kama nilivyoagizwa kufanya, niligeuka nyuma, macho yangu yalikutana na macho makali yanayong'ara mfano wa jini. Mtu mrefu mnene aliyeshiba vizuri, Bastola yake ikiwa mikononi mbele yangu, alikotoke sikujua.

"Pole sana Teacher, labda nisema leo una bahati mbaya mno, siku ya kufa kwako imefika, hata utende miujiza ya aina gani leo ni siku ya hukumu yako, ni kweli umefanikiwa kutoroka mikononi mwa  Carlos Dimera, lakini umeishia mikononi mwangu, Naitwa Ninja Mweusi asiyeshindwa", alisema mtu huyu aliyefunika uso wake kwa kofia nyeusi na kuruhusu macho yake tu kuona.

Nilimwangalia mtu huyu kwa tahadhari kubwa. Akili yangu ilianza kufanya kazi haraka, nilijiuliza ilikuwaje mtu huyu afike eneo hili la siri, ambalo hata Kanali Emilly hakuweza kulijua. Baada ya kujiuliza na kutafakari, nikabaini kuwa inawezekana mtindo waliotumia kuniteka usiku kule Hotel Bella Vista waliutumia kuwatafuta wenzangu.

"Nimekukosea nini mpaka unitangazie kifo, kwani wewe ni Mungu?" nilimuuliza.

"Usiniulize maswali magumu ya kipuuzi, kwa taarifa yako sikuja hapa kujibu mwaswali, wewe na mpuuzi mwenzio uliyempangishia chumba hiki mmefanikiwa kwa kiasi fulani kurudisha jitihada zetu nyuma, lakini baada ya vifo vyenu, naamini tutaanza kwenda mbele", alisema mtu huyu kwa sauti ya kutisha na kukatisha tamaa.

"Mwenzangu ni nani?" nilimuuliza tena.

"Bila shaka nimekwambia naitwa Ninja Mweusi. Lakini utanifahamu vizuri baada ya kifo chako, malaika watakuletea sura yangu utanifahamu. Haya, haraka geuka nyuma", alisema tena kwa sauti ya kutisha, haraka nilitii amri hii nikageuka nyuma.

"Sikiliza, hivyo hivyo ulivyoweka mikono yako juu, tembea kuelekea upande wako wa kushoto, baada tu ya kushuka ngazi utaelekea tena kushoto, mbele kidogo kuna ngazi fupi, baada ya hizo ngazi utaelekea tena kushoto, fungua mlango utakaokuwa mbele yako, utakapotoka nje utaona gari ndogo BMW yenye rangi ya blue, utafungua mlango wa nyuma upande wa dereva itangia ndani, bila shaka utafurahi kuonana na mwenzio", alisema mtu huyu mimi nikaanza kutembea kufuata maelekezo yake.

Kama nilivyoelekezwa, nilitembea hadi kwenye gari hili, lililokuwa nje. Pamoja na kuingia kwa tahadhali kubwa katika eneo hili, nilijilaumu sana mimi kukamatwa kama kuku. Nilifungua mlango wa nyuma ya dereva, nikaingia ndani. Taa ndani ya gari hili iliwashwa. Claud alikuwa amefungwa mikono kwa nyuma, jasho jingi lilimtoka mwilini, nadhani kwa sababu ya mateso na kipigp alichopata kutoka kwa watu hawa baada ya kumteka. Nilipoingia ndani ya gari hili, haraka mtu mmoja aliifunga mikono yangu kwa kamba ngumu, nikavishwa soksi kichwani ili nisiweze kuoma, mtu mmoja ambaye sikumuona vizuri aliingia na kukaa juu yangu.

"Mnatupeleka wapi? Kama kutuua hata hapa inawezekana", niliwauliza kwa shauku.

"Sehemu ambayo ni nzuri nyinyi kujibu maswali yetu na baada ya hapo vifo vyenu vinafuata, ni kosa la jinai maiti zenu kuonekana baada ya kuuawa", alisema mmoja wa watu hawa.

"Mnadhani sisi tutawajibu nini zaidi ya kusubiri vifo vyetu?", niliwauliza huku dereva akiondoa gari eneo hili.

"Tunakujua kabisa kuwa wewe una kichwa na roho ngumu kama ya paka, lakini leo umekutana na watu wenye vichwa na roho mbaya sana. Tunaweza kuongea na wewe kirafiki, lakini pia tukiona huelewi maana ya urafiki, tutakufanya uongee kwa lazima. Uwezo huo tunao", alisema mtu huyu.

"Unaweza kumfanya marehemu aseme?".

"Ikibidi atasema".

Nilijaribu kutuliza akili yangu ili niweze kuisikia sauti ya mtu huyu vizuri. Alijitahidi sana kuongea kiswahili, lakini hakikuwa kiswahili cha mtanzania halisi. Matamshi ya mtu huyu anaweza kuwa raia wa Congo ama Uganda.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, gari lilisimama, dereva alipiga honi, tukasikia lango la chuma linafunguliwa. Sauti kutoka ndani ya gari ikahoji. "Bosi yupo?".

"Bosi ameingia muda si mrefu, anawasubiri", sauti kutoka nje ya gari ilisikika.

"Tumewaleta hawa washenzi wengine wawili. Idadi yao sasa imefika watatu, huyo mmoja naamini tutamtia mikononi leo", alisema mmoja wa watu hawa kwa kujiamini. Mapigo ya moyo wangu yalibadilika, akili yangu ilihama, nikaamini kuwa mwisho wetu umefika, nikajiuliza mwenzetu mwingine kati ya Julius Nyawaminza Fred Libaba, nani atakuwa ametekwa kama sisi.

Lango lilifunguliwa, gari likaingia ndani, baada ya mwendo wa sekunde kadhaa lilisimama tena, milango ikafunguliwa watu hawa wakatoka nje. Sisi tulikuwa tumefungwa vitambaa machoni hivyo hatukuweza kuonana kinachoendelea, wala kujua tulikuwa wapi.

"Imekuwaje?" nilimuuliza Claud baada ya watu hawa wote kutoka ndani ya gari na kutuacha peke yetu.

"Hata mimi sijui, nasikia maumivu makali sana kifuani, watu hawa ni wajuzi katika mambo ya ujasusi, inawezekana leo ikawa mwisho wa maisha yetu", Claud alisema kwa sauti ya kukata tamaa.

"Katika maisha, usiogope lolote Claud, kila lililopangwa na Mungu litatimia, acha watuue, wataua wangapi?. Sisi ni binaadamu wa kupita kama ilivyo wao, tukifa leo tutakuwa tumekufa kwa jambo jema, watatokea wengine wataendeleza hapa tulipofikia, mimi naamini hivyo", nilimwambia. 

"Lakini tutakuwa tumeacha pengo kubwa sana, vifo vyetu nadhani vitarudisha nyuma kasi ya mapambano, siogopi kufa ila naumia kuona jitihada zetu zinaishia njiani", Claud alilalama.

"Siku zote Mungu husikia kilio cha wengi, sisi tunapigana kuokoa wengi, hata tukifa leo, siku moja majina yetu yatasikika miongoni mwa mashujaa... Hayati Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema askari shujaa ni yule anayefia vitani, akirudi nyumbani, anarudi na ushindi, tusikate tamaa, nafasi ya kuishi bado ipo, japo ni finyu sana", nilimwambia.

"Asante kwa kunitia moyo bosi", Claud alisema kwa sauti ya kujiamini. "Nikiwa na wewe siogopi". Milango ya gari hili ilifunguliwa tukatolewa ndani kama kuku. Baada ya kushushwa tulisukumwa kupelekwa sehemu isiyojulikana. Eneo hili lilikuwa kimya kabisa, kwa vile tulikuwa tumefunikwa nyuso zetu kwa kofia nyeusi hatukuweza kujua mahali tulipokuwa.

Kofia nyeusi tulizovalishwa wakati tunaletwa hapa ziliondolewa vichwani mwetu, tulijikuta mbele ya Carlos Dimera, alikuwa ameketi kwenye kiti kikubwa akivuta sigara kubwa iliyosokotwa kwa karatasi ngumu. Sekunde chache baadaye Julius Nyawaminza aliunganishwa nasi, alikuwa amechoka sana, nilipomwangalia niliamini kuwa alikuwa katika mateso makali.

"Ulijitia mjanja, ukanikimbia. Lakini waswahili wanasema ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu, kuku hata awe mjanja kiasi gani anategwa kwa mahindi na punje za ulezi tu, nikusifu kwa kuweza kutoroka sehemu ambayo si rahisi mtu kutoroka, hongera sana", Carlos Dimera alisema huku akiniangalia kwa hasira.

Mama Feka aliketi upande wa kushoto karibu kabisa na Carlos, aliniangalia kwa macho ya wizi halafu akasimama na kuelekea upande wangu. Alivaa mavazi yaliyompendeza sana, suluali nyeusi, fulana ya kijani, raba miguuni na kofia nyeusi. Hakika alionekana kuvutia zaidi.

"Wewe ni binadamu wa aina gani?. Usiku wa kuamkia leo nusura uniue kwa risasi, isingekuwa mipango ya Mungu labda sasa ningekuwa maiti, sasa kabla ya kifo changu, utaanza kufa wewe", Mama Feka alisema huku akitembea kuelekea kwangu. Alinitandika kibao, nikaona nyita.

"Teacher, kabla hamjaingizwa kwenye chumba cha mateso kama huyu mwenzio alivyofanyiwa, nikuulize swali moja rahisi sana, ukijibu nitawaruhusu muondoke", Carlos alisema.

"Niliulize", nilimjibu kwa sauti ya kutojali.

"Yupo mwenzenu mmoja anaitwa Fred, yuko wapi kijana huyu?" Lilikuwa swali kutoka kwa Carlos.

"Simjui", nilijibu kwa mkato.

"Humjui Fred Libaba?" alihoji.

"Nimesema simjui", nilijibu kwa msisitizo.

"Kama humjui Fred, basi ina maana hata hawa uliosimama nao hapa mbele yangu... Huwajui?". 

"Hakika siwajui, nimeshangazwa kuunganishwa na watu ambao sijawahi hata kuwaona katika historia ya maisha yangu", nilisema.

"Usinitie hasira, mpumbavu mkubwa, tafadhali usinifanye nikavua hili gamba la ustaarabu nilililovaa leo, kama utapenda kuliona jua la saa nne leo, jibu maswali yangu", Carlos alieleza.

"Nitajibu maswali ambayo nayafahamu, lakini usinilazimishe kujibu maswali ambayo binafsi siyajui".

"Mpumbavu mkubwa, mlipowakamatwa vijana wangu, Hawa na Ton eneo la Kipawa wakiingiza dawa za kulevya, mkawapeleka haraka mahakamani, mliona fahari sana kufanya vile?". 

"Unapomkamata mhalifu wa aina ile lazima ufarijike, mimi kama mimi nilijisikia vizuri, pamoja na kwamba wewe ilikukera, lakini wengi walifurahi sana kukamatwa kwa dawa za kulevya ambazo ni hatari kwa matumizi ya watu".

"Ahaa, una hakika ni hatari kwa matumizi ya watu. Wewe na hao wengi unaosema mmenufaika nini baada ya watu wangu kukamatwa?".

"Tumenufaika sana, kuzuia uchafu kuwafikia vijana wetu ni faida kubwa", nilijibu swali hili kwa kujiamini, maana nilijua nitakufa.

"Mussa hebu mtie adabu huyu paka", Carlos aliagiza. Kijana mmoja aliyeshiba vizuri alisimama na kunijia, aliponifikia alinipiga ngumi kadhaa nzito tumboni. Aliendelea kunipiga kwa hasira. Sikuweza kumfanya kitu kwani mikono yangu ilikuwa nimefungwa kwa kamba. Nilisikia maumivu makali tumboni, nikavumilia.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru