NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI

Ilikaribia kuwa saa mbili za asubuhi ya Jumatano, siku ambayo ilikuwa rasmi kwa ajili ya mahakama kutoa hukumu dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya. Viongozi kadhaa wa Chama na Serikali walifika mahakamani hapa ili kusikiliza hatma ya kesi hii. 

Vijana wa Polisi kutoka kikosi maalumu cha kutuliza ghasia walipita huku na huku kuimalisha ulinzi katika eneo hili. Huku magari kadhaa ya Jeshi la Magereza yakiwa na askari wengi kutoka kikosi maalumu wakisubiri.  Wafanyabiashara wa dawa za kulevya nao walituma vijana wao kadhaa, ambao walifika mahakamani hapa kusubiri hatma ya Hawa Msimbazi na Tony Sime. 

Carlos Dimera, alikuwa amepinga wazo la vigogo wa ngazi za juu katika kundi hilo, waliokutana katika jiji la Bogota, nchini Colombia na kuafikiana kuwatosa watuhumiwa hawa kwa ajili ya kulinda maslahi yao. Dimera alipinga vikali wazo hilo kwani aliwaamini sana vijana hawa. Inasemekana kabla hawajajiunga naye aliwanywesha maji yaliyochanganywa na damu yake.

Katika kikao cha dharura kilichofanyika usiku, Dimera na vijana wake walipanga mikakati ya kila aina ili kuwaokoa Hawa na Tony, kutoka katika mikono ya sheria. Hii ilikuwa siku ya tatu kwa watuhumiwa hawa kuwa mikononi mwa vyombo vya sheria, wakisubiri na kuamini nguvu ya pesa itawaweka huru.

Kutoroka kwa Teacher usiku ule kuliwaumiza sana. waliamini kuwa mipango yao haitafanikiwa. Faraja iliwajia baada ya Teacher kutekwa tena alfajiri, wakaamini kuwa mipango yao itakuwa swa. 

Mahakama ilifulika watu, kila mmoja akiwaza hili na lile. Ilikuwa imeahilishwa jana kutokana na hoja mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo, kufuatia malumbano ya kisheria na leo ilikuwa siku rasmi ya kutoa hukumu. baada ya taratibu zote za kimahakama, kama kawaida, askari maalum alipaza sauti kuashiria kuingia kwa mheshimiwa Hakimu, watu wote alisimama.

Kanali Benny Emilly, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, alikuwa mmoja wa watu waliofika hapa, Mzee huyu alikuja kusikiliza hukumu ya kesi hii akiwa na baadhi ya wasaidizi wake kadhaa. Kabla ya kufika mahakamani hapa alifanya kila njia kuwasiliana na Teacher, hakubahatika kupata mawasiliano yake. Baada ya Hakimu kuingia na kuketi katika kiti chake, alichukua baadhi ya mafaili yaliyokuwa mezani hapo na kuyapitia moja baada ya jingine, baadhi aliyaweka kando, hatmaye akabakiwa na faili moja mkononi.

"Kutokana na umuhimu wa kesi ya uhujumu uchumi iliyo mbele yangu, nimelazimika kuahilisha kesi zingine zote zilizokuwa zitajwe leo, wahusika katika kesi hizo wafike chumba cha kumbukumbu kwa ajili ya maelekezo zaidi ikiwa pamoja na kupangiwa tarehe nyingine ya kesi, nitasikiliza kesi ya kuhujumu uchumi inayowahusu Hawa Msimbazi nana Tony Sime, bila shaka wapo?", Hakimu alihoji baada ya kueleza. 

"Naam mheshimiwa, wateja wangu wako mbele yako", alieleza Kyaruzi, ambaye ni mwanasheria upande wa utetezi.  akaandika maelezo, baada ya kujiweka sawa, akasema.

"Mwendesha mashitaka".
 "Mheshimiwa Hakimu, kesi iliyoko mbele yako ni Kesi namba 208 ya mwaka huu, kama ilivyosomwa hapo awali, washitakiwa Hawa Msimbazi na Tony Sime, wanashitakiwa kwa pamoja kuwa mnamo tarehe 15 ya mwezi huu, huko Uwanja wa Ndega wa Dar es Salaam, walikamatwa na askari wakijaribu kuingiza dawa za kulevya aina ya heroine, ambalo ni kosa la kuhujumu uchumi", akageuka. 

"Mheshimiwa, baada ya watuhumiwa hawa kukamatwa kwanza walikaidi amri halali waliyopewa na askari, wakidai kuwa mzigo wao si dawa za kulevya isipokuwa ni malighafi kwa ajili ya kiwanda chao cha kutengeneza tembe za kutibu malaria. Ili kujiridhisha, malighafi hizo zilipelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali. Ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa mzigo uliokamatwa ukiingizwa nchini ni dawa hatari za kulevya aina ya heroin ambazo zimepigwa marufuku na Serikali ya Tanzania kuingizwa hapa hapa nchini".

Haraka mwanasheria wa utetezi akasimama na kugonga meza, "Mheshimiwa Hakimu, suala la dawa za kulevya si jambo la kufanyia mchezo, kama wateja wangu walivyoieleza mahakama yako tukufu jana kuwa hawahusiki kabisa na dawa za kulevya, inashangaza sana mwendesha mashitaka wa Serikali kung'ang'ania kuwa ripoti ya mkemia mkuu wa Serikali imethibitisha wateja wangu walibeba dawa za kulevya jambo ambalo si kweli".

Mwendesha mashitaka wa Serikali akasimama tena. "Kama si dawa za kulevya... naomba uieleze mahakama, wewe unadhani watuhumiwa hawa waliingiza nini hapa nchini?. Mheshimiwa kama ishu ni kuagiza mizgo kwanini wasitumie cargo kusafirisha mizigo yao?".

"Mheshimiwa Hakimu, maelezo ya wateja wangu yako wazi kabisa, wameieleza mahakama yako tukufu kuwa mzigo wao ni maalum kwa ajili ya kutengeneza tembe za kutibu malaria. Tena wakasisitiza kuwa kama mzigo huo ni dawa za kulevya si wao, inawezekana wamefanyiwa njama za kibishara mambo haya yapo. Mheshimiwa, kinachoshangaza ni kwamba mzigo uliokamatwa umepelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali bila wateja wangu kuhusishwa hii haikubaliki. Inawezekana wakafanyiwa hujuma, ndivyo inavyoonekana. Mheshimiwa, mahakama ni chombo cha haki, kisitumike kuwaonea wateja wangu", mwanasheria wa utetezi alieleza.

"Mheshimiwa, kama nilivyoileza mahakama yako tukufu jana. Narudia, haiwezekani watu hawa wasafiri kutoka hapa nchini, waende nje ya nchi, watumie pesa nyingi kwa ajili ya kufuata malighafi za kutengeneza tembe za malaria. Mheshimiwa, mzigo uliokamatwa ni mali ya washitakiwa hawa. naamini hata wewe unasafiri nje ya nchi, lakini huwezi kuchukua mzigo usioujuwa, hawa ni wafanyabiashara wazoefu wa bishara chafu, wakiachiwa wanaweza kuligharimu taifa", aliketi baada ya kusisitiza.

"Mheshimiwa, inawezekana kabisa mwendesha mashitaka wa Serikali ana sababu zake binafsi kwa wateja wangu, jambo hili lisichukuliwe kijuujuu, taratibu ziko wazi mheshimiwa, tusitumike vibaya kwa sababu mkemia mkuu wa Serikali, mwendesha mashitaka wa Serikali ndiyo iwe njia ya kuwaumiza wateja wangu, haitawezekana mheshimiwa, kwanza walipaswa kuitwa ili washuhudie vipimo husika, lakini hili limefanyika bila wateja wangu kuhusishwa", mwanasheria wa utetezi alilalama kwa mara nyingine.

Hakimu aligonga meza, ukimya ukatawala kwa dakika kadhaa. "Hukumu. Nimesikiliza hoja za pande zote mbili kwa makini na kupitia maelezo ya pande zote kwa umakini mkubwa. Hivi niwaulize, inawezekanaje mtu ubebe mzigo usioujuwa kutoka huko nje, ukibadili ndege hii na hii hadi unaingia nchini, mzigo huo huo ukaubeba kwenye magari kuelekea nyumbani bila kujua umebeba nini?", Hakimu alihoji.

"Kama umefanyiwa njama au watu wanataka kuharibu biashara yako ama sifa yako, inawezekana kabisa mheshimiwa, wengi wamekutwa na kashfa za aina hii, naiomba mahakama yako tukufu iwatendee haki wateja wangu", mwanasheria wa utetezi alirudia kusihi. 

Dakika kadhaa zilipita kukiwa kimya, hakimu akiichezea kalamu yake kwa meno, ..."Usinifundishe kazi. Naam, Mwendesha mashitaka wa Serikali ameieleza mahakama hii kuwa mnamo tarehe 15 mwezi huu, watuhumiwa wawili, Hawa Msimbazi na Tony Sime, mlikamatwa huko Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, mkiwa na mzigo ambao ripoti ya mkemia mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin. Jambo hili ni zito, bila shaka unajuwa kuwa dunia nzima imepiga marufuku matumizi ya dawa hizi, sijui hata mmewezaje kutoka huko nchi za mbali, mkavuka ukaguzi pale Uwanja wa ndege, hatmaye mkaingia nchini na kutiwa mbaroni na vijana waaminifu katika taifa hili", Hakimu alieleza huku wengine wakitazamana. 

"Mmmh wamekwenda na maji hawa", kijana mmoja aliyekuwa mahakamani hapo alimnong'oneza mwenzake.

"Mwanasheria wa utetezi anasema inawezekana wateja wake walibeba mzigo wasioujuwa, lakini wamekiri kuwa walisafiri kwa ajili ya kuingiza malighafi za kutengeneza tembe za malaria, walipoulizwa na mwendesha mashitaka inawezekanaje watu watumie gharama kubwa kusafiri nje ya nchi ili kuingia mzigo wa gharama ndogo ambao haukidhi matumizi, hawakutoa jibu. Walipoulizwa tena kwanini wasitumie njia ya cargo kusafirisha mizigo yao hawakutoa majibu. Hii inaonyesha kabisa watuhumiwa hawa walikusudia kuingiza dawa za kulevya hapa nchini", Hakimu alieleza.

"Baada ya kusikiliza kesi hii na kupitia vingu mbalimbali vya sheria, nimethibitisha bila kutia shaka kuwa watuhumiwa hawa wana kesi ya kujibu. Kabla sijatoa hukumu, mnaweza kujitetea.

"Mheshimiwa Hakimu, tunaomba huruma yako, kwa upande wangu nina jukumu la kuwalea wazazi wangu ambao ni wazee sana, nina watoto wadogo wanahitaji msaada wangu mheshimiwa, wakinikosa wataathirika sana, naomba huruma unifikirie kwa hilo mheshimiwa, pia nasumbuliwa na tatizo la kifua", Hawa Msimbazi alijitetea.

"Tunaomba msaada wako mheshimiwa, kimsingi hili ni kosa la kwanza, tunaomba mahakama yako itupunguzie adhabu", Tony Sime alieleza huku hakimu akiandika maelezo yao kwa makini.

"Kuwa na wazazi wazee, watoto wanakutegemea haikupi tiketi ya kukufanya utende makosa, mbona wewe hukuwaonea huruma watoto wa wenzio, dawa za kulevya ni hatari kubwa. Naam ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye mawazo na tabia kama yenu, nawahukumu kwenda jela kila mmoja miaka kumi na mitano", wote wakaanguka chini wakati hakimu akitoka mahakamani. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru