NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU

Taarifa za kufungwa jela kwa watuhumiwa wawili wa dawa za kulevya, Hawa Msimbazi na mwenzake Tony Sime, zilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii. Blog ziliripoti habari hii kwa mbwembwe, waandishi wa mitandao wakipishana kwa vichwa cha habari na maelezo yaliyosisimua wengi.

Blog ya MPIGANAJI iliandika. Breaking News, halafu mwandishi akaweka maneno haya. WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA WAKIONA CHA MOTO, WATUPWA JELA MIAKA. 15. Blog ya KAMANDA WA MATUKIO iliruka na kichwa cha habari, DAWA ZA KULEVYA ZAWAPELEKA JELA MIAKA 15, MICHUZI wakaandika, MAHAKAMA YATOA ADHABU NDOGO KWA WAUZA DAWA ZA KULEVYA. Redio zikatangaza habari hii, waliosikia walishangilia.

Shamla shamla ziliendelea mitaani. ulikuwa ushindi mkubwa kwa Serikali. Lakini ghafla habari hii ikagauka msiba. Masaa kadhaa baada ya hukumu, taarifa zikaenea kuwa Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo na kutoa hukumu amepigwa risasi na kuuawa ofisini kwake. Hofu ikatawala. Wakati viongozi wakitafakari kuhusu tukio hili. Habari nyingine inasambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, askari kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya kutokea mapigano makali wakati wakisindikiza wafungwa.

Taarifa hii ilieleza kuwa wafungwa wawili waliotuhumiwa kuingiza dawa za kulevya nchini, Hawa Msimbazi na Tony Sime, waliokuwa wakipelekwa katika gereza moja Jijini Dar es Salaam wametoroshwa wakiwa wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Wananchi wakapatwa na masikitiko, Mzee mmoja wa makamo aliposikia taarifa hizi kwenye vyombo vya habari alitoa machozi. 

Habari zinamfikia Kanali Beny Emilly, anashindwa kuyaamini masikio yake, anasimama sekunde kadhaa mbele ya kiti chake, hofu inamwingia, anajaribu kwa mara nyingine kuinua simu yake ya kiganjani kuwasiliana na Teacher. Bahati mbaya simu hiyo haipatikani anaelekea kuchanganyikiwa, furaha yake inageuka kalaha, machozi yanamlengalenga.

"Nini hii?", Kanali Emilly anajiuliza wakati akielekea nje ya ofisi yake. 

Taarifa hii inawafikia wakubwa wa nchi, vikao vya dharura vinakaa. "Nini kumetokea", anahoji mkuu wa nchi. "Hili haliwezekani katika nchi hii", anasisitiza bila kupata majibu. Wasaidizi wake wanajaribu kueleza msimamo.

Simu zinapigwa huku na huko bila mafanikio, "Nani hasa wameshiriki katika tukio hili", Kanali Emilly anajiuliza kwa mara nyingine.  

*************************************

Nilijaribu bila mafanikio kutambua wapi tulipofichwa. Tulikuwa tumesimamishwa mbele ya watu hawa huku mikono na miguu yetu ikiwa imefungwa barabara kwa kamba ngumu. Pamoja na mazoezi makali ninayofanya karibu kila siku, lakini hapa niliyasikia maumivu kutokana na staili iliyotumika kutufunga hizi kamba. Ukweli hata uwe na mazoezi kiasi gani kwa mtindo huu lazima utasikia maumivu.

Wote watatu tulifungwa kwa mtindo mmoja, yaani miguu yetu ikiwa imefungwa kamba, mikono nayo ikiwa imefungwa vizuri kwa nyuma halafu kamba hizo zimevutwa na kufungwa sehemu ya juu. Kwa maana hiyo mikono yetu ilivutwa nyuma ikaangalia juu na kutusababishia maumivu makali sana.

Kelele za mashine na baadhi ya watu zilisikika, hali hii ilinifanya nikabaini kuwa eneo hili lilikuwa la viwanda. Niliwaza na kujiuliza mambo mengi, nilimuomba mungu angalao awanusuru wenzangu Julius Nyawaminza na Claud Mwita ili mimi nichukue nafasi yao.

Nilijilaumu kwa kuweka tahadhali ndogo wakati naingia pale hotelini, hata hivyo sikupaswa kulaumu sana maana tayari nilikuwa katika mikono ya mauti. Hasira na chuki kwa watu hawa zilinijia, nikatamani kufanya miujiza lakini sikuweza tena.

Mlango ulifunguliwa mtu mmoja mnene ambaye sikuwahi kumuona katika historia ya maisha yangu akaingia ndani, alikuwa mtu makamo, mwenye umri kati ya miaka hamsini na sitini, alivaa mavazi yaliyomkaa vizuri na miwani ya jua, mtemba ukiwa kinywani mwake. Alionekana mtu mwenye busara kiasi, lakini kwa uzoefu wangu nikabaini mtu ni mmoja wa watu washenzi pengine zaidi ya Carlos Dimera.

"Karibu Mzee Mtemba", sauti nzito ya Jackina ilisikika, Mzee huyo alipita taratibu akituangalia kwa tabasam na bashasha, baada ya kushikana mikono na Carlos akaketi.

"Nimekuita ushuhudie vifo vya mbwa hawa. Mzee Mtemba bila shaka unatambua jinsi mtandao wetu ulivyotikiswa, chanzo ni hawa washenzi wanaoamini biashara ya dawa ya kulevya itakomeshwa, ni ndoto ya mchana". Akainua macho. "Poleni sana, ujinga wenu umewakosti, mimi ni mtu mwenye huruma sana lakini kwenu sintakuwa na huruma kamwe", Carlos akasisitiza.

"Wewe ndiye unaona hivyo Carlos, lakini pia tambua kuwa mjinga wa leo ndiye mwelevu wa kesho, kufa ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu, sisi hatuogopi kufa, naamini siku moja utakufa pia, adhabu yako mbele za Mungu itakuliza milele", nilimwambia.

"Mwangalie mpumbavu huyu, wakati wewe unakufa leo mimi nataendelea kula maisha, nitatanua kwa raha zangu, pole sana Teacher, wewe ni miongoni mwa watu waliochelewa sana katika maisha.  Hebu mtieni adabu mbwa huyu", Carlos aliagiza. Vijana wawili wakanijia tena na kuanza kunitwanga.

Wakati wote huo Mama Feka alikuwa akichezea simu yake ya kiganjani, sikujua alichokuwa akifanya nadhani alikuwa akiwasiliana na watu wake fulani. Vijana hawa walinivamia na kunipiga ngumi kadhaa tumboni na kunisabanishia maumivu makali zaidi.  

"Utalipa, iko siku utalipa", nilieleza wakati nakaribia kupoteza fahamu.

"Teacher, kama nilivyokwambia hapo awali mtandao wetu ni mkubwa mno, umesambaa dunia nzima, mijini na vijijini, tunao viongozi wakubwa katika Serikali. Huyu Mzee wa Mtemba ndiye Mkuu wa Operesheni ya wizi wa kutumia noti bandia, ambazo nafikiri ulionyeshwa na bosi wako, wengi wameuza majumba yao kupitia mzee huyu", Carlos alidokeza, sasa nikaelewa sababu za mtu huyu kufika mbele yetu maana niliwahi kumsikia lakini kwa jina la Benny.

Mzee Mtemba akasimama. "Asanteni sana vijana wangu, kama ulivyoelezwa, mimi ndiye kigogo wa opereshani ya noti bandia. Lakini kabla sijaongea nanyi, binafsi nichukue nafasi hii kutoa hongera kwa kazi yenu nzuri, mmejaribu kututia matumbo joto. Mimi ni mfuatiliaji wa siasa za nchi hii, miaka zaidi ya kumi niliyoishi humu, nimegundua kuwa nchi hii haina mwenyewe, ndiyo maana tumeweza kuishi hata bila kufuata taratibu za uhamiaji, nawasikitikia sana vijana hawa ambao umri wenu bado mdogo sana, lakini mtakufa leo, mimi ni mtu wa imani na huruma sana, sipendi kuona mtu akiuawa, lakini nyie mmekitafuta kifo wenyewe, ndiyo maana nimekuja mnijuwe pia nishuhudie vifo vyenu", alieleza mtu huyu halafu akaketi.

"Mzee Mtemba, binafsi nimekuwa nikieleza habari hizi kwa mifano ili adui zangu watambue mimi ni mtu wa aina gani, lakini vijana hawa hawakunisikia eti kwa sababu tu wamekunywa maji ya bendera. Kikosi ninachokiongoza kina nguvu kubwa kushinda dola ya nchi hii, Hawa na Tony wako huru, hebu ingieni ndani", Carlos Dimera alieleza. Mlango ukafunguliwa Hawa na Tony tuliowakamata na dawa za kulevya na kisha kuwafikisha mahakamani wakaingia wakiwa na nyuso za hasira.

"Asante sana bosi. Tuko huru sasa", alieleza Hawa huku akionyesha hasira alizokuwa nazo kwangu. "Ulijisikia jasiri kwa kutukamata, lakini ujasiri wako leo umekwisha", aliongeza.

"Ni kweli, lakini amini utakamatwa tena", nilimwambia kwa mkato.

"Mpaka itokee. Naamini kifo chako kitawaogopesha wengi, hata mashujaa waliokuwa wakijipanga kujiingiza katika suala hili watakaposikia mwili wako umeokotwa kando ya bahari, mmmh watarudi nyuma", Hawa aliongeza.

"Hii ni kuwaonyesheni kuwa hatushindwi kitu, kama mzee Mtemba alivyosema, leo ndiyo mwisho wenu kuishi duniani, tulitaka mhakikishe kuwa Hawa na Tony hawafungwi jela, sasa ni wakati mzuri kwenu kupeleka habari hii huko kuzimu, poleni sana", carlos aliongea kwa kujiamini.

"Tuko tayari kwa lolote, lakini mtambue kuwa hakuna mwenye nguvu zaidi ya dola, sisi tutakufa leo, lakini wapo ambao wataendeleza hapa tulipofika, wengine wamezaliwa tayari, wengine wako katika matumbo ya mama zao", niliwaambia kwa sauti ya kutetemesha na hasira.

"Yawezekana wewe una mapungufu katika kichwa chako, mtu gani wewe usiyeogopa kifo, mbona wengine wamenyamaza", alisema Carlos.

"Kunyamaza kwao si kwamba wanakuogopa kufa, wamekudharau sana, nikwambie ukweli, kabla hamjatoka hapa leo mtakuwa mmekamatwa wote, hii ni nchi ya watanzania, hata hawa vibaraka wako pia ni watanzania lakini wasarti wa nchi iko siku yao", niliwaambia.

"Ombeni Mungu wenu azipokee roho zenu kwa mara ya mwisho, sihitaji kuumizwa kichwa cha.... Carlos alikatishwa na kelele za vishindo na risasi zikasikika kutoka nje. Risasi zikaendelea kulindima, wote tukaingiwa na hofu, ghafla umeme ndani ya chumba hiki ukazimika, kukawa giza.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru