NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO

Mchana huu sehemu nyingi za starehe zilikuwa zimefungwa, hii ni kutokana na agizo la Serikali kuwataka watu wafanye kazi kwanza na kustarehe baadaye, kutokana na hali hii tulipata wasaa mzuri wa kukaa hapa Green Pub kumsikiliza Kanali huyu wa Jeshi, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Upelelezi, Benny Emilly. Alikuwa Mzee wa makamo na nywele zake zilikuwa zimebadilika rangi kuwa nyeupe kabisa. Baada ya kufuta machozi ya uchungu yaliyomtoka akiwa mbele yetu, alivuta kiti kilichokuwa karibu akaketi. Tukasogeza viti ili kumsikia atasema nini.

"Wapiganaji wangu shupavu, nyie ndiyo hazina ya nchi yetu, sisi wazee tumechoka, tunaelekea ukingoni, jukumu lenu sasa ni kulinda heshima ya nchi yenu. Mimi sina kawaida ya kutoa machozi mbele ya watoto, lakini leo yamenitoka. Mnajua kwanini yametoka. Nimefurahi sana kuwaona katika hali hii ya umoja, bila umoja hakuna ushindi. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema Umoja ni nguvu, Mzee Kenyatta naye akasema Harambee, maana ni lilelile. Watanzania wanasubiri ushindi kutoka kwenu. Kabla ya kuja mbele yenu nimeongea na Teacher pale ndani ya gari, amenieleza misukosuko na hatari zilizowakuta, nafurahi kusikia mko salama na hakuna aliyekata tamaa. Ndiyo maana nikatoa machozi baada ya kuwaona mkiwa salama. Teacher amenijulisha pia kuwa leo ni siku ya kufa ama kupona kati yetu na vibaraka wa taifa letu. Pia amenifahamisha kuhusu mama huyu jasiri, ambaye kwa kiasi kikubwa amesaidia kuoko maisha yetu. Asante sana mama", Kanali Emilly alieleza huku akimshika mkono.

"Hakika, bila Mama Feka pengine taarifa za habari za ndani na nje ya nchi wakati huu zingekuwa zinasimulia habari nyingine kabisa", Julius Nyawaminza alieleza.

"True. Unachosema ni kweli kabisa", Claud alirukia.

"Mimi sikutegemea kama mama huyu ataimudu kazi niliyomuomba atusaidie, lakini nilitokwa na hofu aliponidokeza kuwa alipitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni Ushindi. Kweli anastahiri kuitwa mshindi", nilieleza.

"Anastahiri kabisa", alieleza Kanali Emilly, halafu akaendelea kwa msisitizo. "WAPIGANAJI. Naomba mnisikilize kwa makini sana. Teacher, Julius, Claud, Peter, Mama Feka kama ambavyo Teacher anakuita na Fred ambaye simuoni hapa, Teacher unazo taarifa zozote kuhusu Fred?." aliuliza kabla ya kuendelea.

"Naam, tunawasiliana, hatuwezi kuwa hapa wote kama wajinga, amenijulisha kuwa yuko pamoja nasi hapahapa karibu kabisa anaangalia usalama wetu, tuko salama bosi", nilimwambia.

"Oh, vizuri sana. Hii ni mesheni ya aina yake, tujitahidi kwa njia yoyote wahalifu hawa wakamatwe na ushahidi, tusifanye makosa kabisa, sheria za nchi hii zinataka mtu akutwe na ushahidi, ili tushinde vita hii lazima adui akamatwe na kielelezo, yaani hayo madawa ya kulevya yapatikane, vingine tutakuwa tumefanya kazi bure, tutawafikisha mahakamani bila kielelezo?", Kanali Emilly alihoji baada ya kushauri.

"Tutajitahidi kufanya hivyo. Lakini Afande, kazi kubwa imefanywa na mama huyu shemeji yangu, leo tunaingia vitani wakati yeye hana kumbukumbu za aina yoyote katika kumsaidia endapo itatokea bahati mbaya. Mkuu vita si lelemama, lolote laweza kumpata na muda huu hakuna nafasi tena. Naomba Mama Feka aingizwe katika kumbukumbu zako", nilimshauri Kanali Emilly akatingisha kichwa kukubaliana na mawazo yangu.

"Hilo halina tatizo kabisa Teacher, kama ulivyotangulia kusema vita si lelemama, tuombe Mungu awasaidie kwa mapenzi yake naamini mtarudi salama, nitafurahi sana kuwaona. Viongozi wote wa serikali wako pamoja nanyi, niwahakikishie tuko pamoja nanyi, niwatakie kila la heri wote".

"Amina", tulijibu kwa pamoja.

"Naomba muwe makini na waangalifu sana, Mama Feka?" Kanali Emilly aliita.

"Naam baba".

"Nimeambiwa wewe ndiye unalifahamu vizuri eneo walilopanga kwa ajili ya kutoroka, saidia tafadhali, msiwape nafasi hata kidogo. Kwa vile muda unakwenda sana sasa niwaache mjipange. Mheshimiwa Rais ameahidi kutoa zawadi nono kwenu".



"Ni kweli baba, mimi si mwenyeji sana katika Jiji hili, hata hivyo nitajitahidi kuwapeleka. Bahati nzuri ni kwamba huyu mzungu Carlos ananiamini sana, niko kwenye orodha ya wanaosafiri. Naweza hata kuwachelewesha ili tufanikiwe", alisema.

"Tutajitahidi huku tukimuomba Mungu", nilisema kwa niaba ya wenzangu wote. Kanali Emilly akasimama baada ya kutushika mikono, akaondoka.

Nilitumia nafasi hiyo kuwajenga vijana wangu kisaikolojia. Baada ya kujiweka vizuri tukajigawa katika makundi mawili tofauti, Peter kama ilivyo ada alianza kuondoka na Mama Feka, akawachukua na vijana wetu kutoka Lugalo, wakaondoka kuelekea eneo la Kunduchi Beach. Mimi Claud Mwita na Julius Nyawaminza tukampitia Fred, tukaanza tukaelekea Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU