KIKOSI CHA KISASI

SURA YA TATU

KIKOSI CHA KISASI

Kwa mara nyingine tena chumba hiki cha mkutano ambamo jana yake walikutana wanakamati wa kamati ndogo ya usalama ya kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, kilikuwa kimekawa tena na watu wale wale jioni hii. Kila mmoja alipokwisha keti, Mwenyekiti alianza kusema, "Ndugu wanakamati nashukuru kuwaona wote mmehudhuria tena katika kikao chetu hiki cha pili cha mkutano huu wa maana sana katika Afrika. Nimatumaini yangu kuwa Wakurugenzi wa upelelezi wameweza kupata muda wa kukutana na kuzungumza kikamilifu juu ya utekelezaji wa suala hili. Vile vile ni matumaini yangu kuwa Ndugu Willy Gamba ameweza kupashwa habari na kuwasili mjini hapa ingawaje simuoni hapa," alimaliza Mwenyekiti wa kamati ya ukombozi.

Bila kusita Mkurugenzi wa Upelelezi wa Zambia alisimama na kuanza kueleza. 

"Ndugu wanakamati, nachukua fursa hii kwa niaba ya Wakurugenzi wenzangu, ili nipate kuwaelezeni ingawaje kwa muhtasari tu mambo tuliyoafikiana juu ya jambo hili. kwanza tumekubaliana kuwa ifunguliwe ofisi ya muda itakayo shughulikia operesheni hii na iwe hapa Mjini Lusaka chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Tanzania akisaidiwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Zambia. Huenda wengi wenu mnajiuliza kwa nini kama kiongozi wa ofisi ya operesheni hii ni kutoka Tanzania, Ofisi yenyewe isiwe mjini Dar es salaam. Kwa sababu makao makuu ya kamati ya ukombozi yako mjini Dar es salaam, tumeonelea ili kupoteza lengo ofisi hii ni ya muda isikae mjini hapo. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Tanzania amechaguliwa kuongoza ofisi hii ya muda kwa sababu kiongozi wa 'kikosi cha kisasi' ambaye ndugu wanakamati mmemchagua anafanya kazi chini yake kwa hiyo itakuwa rahisi kwao kuelewana vizuri kuliko ikibidi mpelelezi huyu awe chini ya kiongozi ambaye hakumzoea. Kama nilivyokwisha tamka hapo awali sisi tumeendelea kuunga mkono uamuzi kuwa Ndugu Willy Gamba ndiye apewe rasmi jukumu hili kubwa. Kwa taarifa yenu ndugu Gamba ameisha wasili hapa mjini na huenda muda si mrefu atafika kuhudhuria kikao hiki kama ilivyokuwa akitakiwa. Juu ya kikosi chenyewe kitakavyokuwa tumeamua kuwa kikosi hiki kiwe na watu wanne. Yaani Gamba akisaidiwa na wapelelezi wengine wa hali ya juu watatu. Wapelelezi hawa wengine watatu majina yao yameisha pendekezwa na mara tu taratibu fulani fulani zitakapo malizika wataelezwa jinsi ya kuungana na mwenzao huko mjini Kinshasa na ofisi hii ya muda itakavyokuwa ikishughulikia suala hili kuanzia sasa. Kwa kifupi, ndugu wanakamati, utekelezaji wa suala hili litakuwa jukumu la ofisi hii ya muda ikishirikiana na 'Kikosi cha Kisasi. Kwa niaba ya Wakurugenzi wenzangu ninadiriki kusema kuwa kama kuna watu watakaoweza kulifanya jambo hili lifaulu basi watu hawa waliokwisha pendekezwa ndio pekee wanaweza kulifanya lifaulu. Kwa hiyo ninalowaomba ndugu wanakamati, ni kukaza roho, tumuombe Mungu, yeye atawasaidia hawa vijana wetu hadi kufaulu, asante, alimaliza.

"Imenipa matumaini makubwa," alisema Mwenyekiti, "Kuona kuwa kwa muda mfupi huu mmeweza kupanga jinsi ya kulikabili suala hili. Kwa vile nyinyi ndio wataalamu sisi hatuna budi kuchukuwa ushauri wenu na kuacha yote mikononi mwa ofisi hiyo ya muda ya kushughulikia suala hili. Nasi tunatumaini Mungu kuwa atakuwa pamoja nasi hadi tupatapo ushindi. Mimi nitaendelea kukaa hapa kusudi niweze kuwa karibu na mambo yanavyokwenda. Wanakamati wengine mnaweza kurudi kwenu, jinsi mambo yatakavyokuwa yakiendelea hii ofisi ya muda itawajulisheni. Kitu kikubwa ni kutoa shukrani zangu nyingi kwa jinsi mlivyoweza kufika na kutoa uamuzi kwa suala lililo gumu kuliko yaliyowahi kutokea katika bara letu hili la Afrika. nawaombeni mzidi kukaa na moyo wa namna hii. Kwa hivi ni..."

Alipokuwa amefikikia hapo, ghafla mlango wa chumba ulifunguliwa na Willy Gamba akaingia ndani. Wajumbe wote macho yao yalimwangaza kijana huyu nadhifu aliyeingia na kuanza kumchunguza toka chini hadi juu. Mkutano ni kama ulikuwa umepigwa bumbuazi, wakati vile vile Gamba alikuwa amepigwa na bumbuazi kutokana na jinsi alivyokuwa akiangaliwa.

"Asante," walijibu kwa pamoja. 

"Karibu," Mwenyekiti alimkaribisha kwa kumuonyesha kiti kilichokuwa wazi karibu naye. Gamba alienda akakaa huku bado macho yake yako kwake. Wajumbe wengi ambao walikuwa bodo hawajamuona hata mara moja, walishangaa kuona kuwa kijana nadhifu na mwenye sura nzuri hivi ndiye alikuwa Willy Gamba ambaye sifa zake za ujasiri zilifana na kutapakaa Afrika nzima.

"Ndugu wajumbe huyu ndiye Willy Gamba tuliyekuwa tukimzungumzia. Na ndugu Gamba hawa ni wajumbe wa kamati ndogo ya usalama ya kamati ya Ukombozi ya Nchi huru za Kiafrika," Willy alitingisha kichwa huku akiwaangalia wajumbe kwa makini mmoja baada ya mwingine, "Sidhani kama unajua kwa nini umeitwa hapa." 

"Sijui maana sijaambiwa kwa nini, mimi habari nilizozipata ni kuwa nifike hapa Lusaka. Na nilipofika hapa nimeamriwa nifike jengo hili na chumba hiki ambamo nitamkuta mkuu wangu wa kazi. Kwa mshangao mkubwa najikuta uso kwa uso na kamati ya usalama, sijui na mimi nimepandishwa cheo kiasi cha kuwa mwanakamati wa kamati mojawapo ya OAU." 

"La hasha, kwa taarifa yako ndugu Gamba umeitwa hapa na kikao hiki kwa jambo maalumu", alimweleza Mwenyekiti kwa uso mzito, "Jambo uliloitiwa hapa ni kuwa, bara zima la Afrika limekuhitaji ukalisaidie kupigana vita dhidi ya wapinga mapinduzi wa Afrika. Nafikiri umepata habari za tukio la kifo cha Rais wa Shirikisho la vyama vya wapigania uhuru Kusini mwa Afrika Ndugu Edward Mongo kilichotokea siku mbili mjini Kinshasa Zaire".

"Nimepata habari, nimesikia kwenye redio na nimesoma magazetini". 

"Kwa kifupi mkutano huu umekuita ili ukapeleleze kifo cha ndugu huyu. Jambo hili ni kubwa sana maana kifo hiki ni mojawapo ya vifo vingi ambavyo vimewahi kuwatokea ndugu zetu wapigania uhuru. Kwa hivi jukumu ulilopewa na Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika ni kuongoza kikosi kitakachopeleleza na kuwasaka hawa maadui wa Afrika wanaoua vijana wanamapinduzi wa Afrika eti kwa sababu wanapigania haki za nchi yao. Kwa hivi utaongoza kikosi kitakachoitwa "KIKOSI CHA KISASI" ambacho habari zake zaidi utapata kutoka kwenye ofisi ya muda inayoshughulikia suala hili. Nasema tena jukumu hili ni kubwa na tunakuomba ukalitekeleze kwa kadri ya uwezo wako, maana kushinda kwako ndiyo kushinda kwa Afrika. Mimi sina maelezo zaidi, maana maelezo haya utayapata kutoka kwa Mkurugenzi wako ambaye ndiye vile vile atakayeongoza ofisi hii. Una swali?". Mwenyekiti alimuuliza Willy huku akimkazia macho.

"Ndugu Mwenyekiti mimi nikiwa mwana wa Afrika sina budi kuitika mwito niitwapo. Sina la kuuliza bali ningependa kusema tu kwamba jukumu mlilonipa nitalitekeleza kwa kadri ya uwezo wangu. Kwa vile umesema habari zenyewe juu ya jambo hili, maswali zaidi nitayauliza huko. Kwa hiyo hapa nasema tena msiwe na wasiwasi mimi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu" alimazizia.

"Asante sana, tunapokuwa na vijana kama nyinyi, nasi hatuna budi kujivunia na kusonga mbele mapambano dhidi ya wapinga mapinduzi. Ndugu wanakamati sina budi kuwaageni tena. Mambo yote tunayaacha mikononi mwa ofisi ya muda, na nina imani kuwa mambo yatakwenda vizuri. Tufunge mkutano tukitegemea mafanikio mazuri, kama tulivyoanza na mafanikio mazuri," alimaliza Mwenyekiti na Wajumbe waliondoka ndani ya chumba cha mkutano, walipofika chini kwenye maegesho ya magari. Mkurugenzi wa Usalama wa Zambia na wa Tanzania waliingia ndani ya gari moja halafu wakamweleza Gamba awafuate."Tangulieni", huku akiendesha gari lake la kukodi alilokuwa ameliegesha hatua chache. Aliingia ndani ya gari na kuanza kuwafuata japokuwa kwa mbali. Ndani ya mawazo yake Willy alijua mara hii alikuwa anakwenda kwenye tume kubwa kuliko zote alizowahi kwenda. Alifikiria upinzani ambao angeupata na kubashiri kuwa utakuwa mkubwa kutokana na habari walizokuwa nazo tayari juu ya hawa wauaji waliokuwa wakiwaua wapigania uhuru sehemu mbali mbali katika Afrika. Hata hivyo alipiga moyo konde na kungojea kusikia zaidi kutoka kwa Chifu kabla hajasumbua sana mawazo yake juu ya suala hili. Huku mawazo yote yakipita kichwani mwake aliendelea kuwafuata Chifu na mwenzake ambao walikuwa wakiingia barabara iliyokuwa ikichepuka na kuingia sehemu ya Lilanga. Kwa mawazo yake alifikiri kuwa huenda walikuwa wakielekea nyumbani kwa mwenziwe na Chifu kwa ajili ya chakula cha jioni. Punde si punde akaliona gari la akina Chifu likitoa ishara ya kuingia kwenye nyumba moja naye akafanya vile vile. Baada ya kungoja magari yaliyokuwa kwenye barabara kuu kupita walipiga kona na magari yote yalielekea kwenye nyumba hii iliyokuwa hatua chache tu kutoka barabarani. Nyumba hii ilikuwa imezungukwa na ua na ilikuwa na mlango mkubwa uliokuwa umefungwa na lango kubwa. Gari ya akina Chifu ilipiga honi na lango likafunguliwa na askari ambaye baada ya kulifungulia alikuja mpaka kwenye gari na kuinama akazungumza na mwenziwe na Chifu ambaye ndiye alikuwa akiendesha. Baada ya kuzungumza kidogo aliwaruhusu wakapita na Willy naye aliruhusiwa kupita bila kusimamishwa. Baada ya kulipita lango hiligari la Willy liliangaza nyumba moja nzuri iliyokuwa ikiwaka taa. Chifu na mwenzake wakaegesha gari lao karibu tu na mlango wa
mbele ya nyumba hii na Willy naye akafanya vile vile. Chifu na mwenziwe alitoka na kusimama nje ya gari lao huku wakimsubiri Willy. Willy alipokuwa ameungana nao walimkaribisha ndani. 

Kwa kuangalia mazingira ya nyumba yenyewe mara moja Willy alitambua kuwa haikuwa nyumba iliyokuwa ikikaliwa na watu bali ilikuwa nyumba iliyokuwa ikitumiwa kwa shughuli fulani fulani. "Karibu ndani ndugu Gamba,"

"Asante", alijibu Willy. 

Walipoingia ndani Willy ndipo alitambua hasa kuwa hii haikuwa nyumba ya kuishi kama inavyotegemewa kwa sehemu ya Lilandabali ilikuwa ni ofisi. Baada tu ya kuingia, walifika sehemu ya mapokezi ambako walikuta kuna wasichana wawili mmoja akiwa yule aliyewafungulia na mwingine alikuwa amekaa kwenye kiti huku kulia kwake kukiwa na mashine ya teleksi na kushoto kwake kulikuwa na "Swichi-bodi" ya simu. Hawa wasichana wote walikuwa wakishughulika sana maana yule aliyekuwa akifungua mlango baada kuwafungulia tu alienda kwenye mashine ya kupiga taipu. Huyu mwingine alikuwa akihangaika, huku akijibu simu na huku akijibu au akipokea habari zilizokuwa zikitokea kwenye teleksi.

Willy aliwaangalia wasichana hawa kwa mara moja huku akiendelea kuwafuata Chifu na mwenzake ambaye walipita sehemu hii ya mapokezi kana kwamba hapakuwa na Kitu. Wale wasichana nao waliwahi kumwangalia Willy ingawaje kwa wasiwasi na kuendelea na kazi zao kanakwamba hakuna aliyekuwa ameingia ndani humo. Hii nidhamu ya kazi wasichana hawa imemuelewesha Willy kuwa hii ilikuwa ofisi maalumu. Mwenziwe na Chifu alitoa funguo mfukoni mwake na kufunguwa cha kwanza walichofika na kuingia ndani. Kilikuwa chumba kikubwa cha kutosha kiasi cha kuweza kuwa na meza ya mkutano. 

"Karibu", aliwakaribisha tena kwa kuwaonyesha viti vya kukaa.

"Hizi ndizo zitakuwa ofisi za ofisi ya muda itakayoshughulikia shughuli za "Kikosi cha Kisasi", aliwaeleza.

Ziko mahala pazuri sana, maana panaonekana kama nyumbani kwa mtu tu" aliongeza Chifu.

"Kwa kweli ni sehemu nzuri na huwa inatumiwa kama ofisi yangu ya siri, na ni maofisa wa hali ya juu sana katika ofisi yangu wanaoijua ofisi yangu hii iko wapi. Na tokea sasa ofisi hii itafungwa kwa shuguli zake za kawaida na itatumiwa tu na shughuli hii mpya. Hao wasichana mliowaona hapo mapokezi ni waandishi wangu wa siri na nimeonelea vizuri kuwaweka kama waandishi wetu kwa shughuli hii mpya." Mkurugenzi wa Zambia alisema.

"Chifu, Maselina angefaa kuwa hapa, unaonaje ?" Aliuliza Willy kimatani.

"Anafaa huko huko aliko", alijibu chifu naye kimatani.

"Ndugu Chifu, kama Gamba anavyokuita, hii ndiyo ofisi yetu karibu tuanze kazi", alisema mwenyeji wao huku akiinua mkoba wake na kuanza kutoa makaratasi na kuyasoma taratibu. Willy yeye alichukuwa paketi yake ya sigara aina ya Benson & Hedges (B & H) na kutoa sigara na kuanza kuvuta taratibu huku akiwaangalia hawa mabosi wake waliokuwa wakisoma hayo makaratasi yao huku wakikunja uso utafikiri mwanamke anayejisikia uchungu wa kujifungua. Ilichukuwa zaidi ya nusu saa kumaliza kuyapitia makaratasi yao kabla hawajaanza kumhutubia Willy. Chifu mara tu baada ya kusoma makaratasi haya uso wake ulibadilika kama kawaida yake anapokuwa karibu kuzungumzia kitu ambacho hakimpendezi.

"Willy sidhani kama kuna haja ya kukueleza jinsi suala hili lilivyo la muhimu, maana wewe mwenyewe umesikia umuhimu wake kutoka kwa kinywa cha Mwenyekiti mwenyewe. Kwa hivi sisi katika maelezo yetu tutakazia juu ya namna suala lenyewe inabidi lishughulikiwe", alieleza Chifu huku mwenziwe naye akiwa ameishafunga jalada huku akimsikiliza kwa makini. Willy naye alikaa kimya huku akimsikiliza Chifu kwa makini sana alipokuwa akiendelea na maelezo yake, "Tatizo linalo tukabili ni kuhusiana na mauaji wanayofanyiwa wapigania uhuru. Kwa vile naelewa unajua kwa kirefu juu ya mauaji yaliyotokea hapo awali na bidii zilizofanywa na idara za upelelezi za kila Nchi iliyousika na mauaji haya, maelezo yangu yatasimama juu ya nini unatakiwa ufanye kwa sasa hivi. Kitu ambacho unatakiwa wewe pamoja na wenzio mtakaounda hiki "Kikosi cha Kisasi ni kukisaka kikundi kinachohusika na mauaji haya na kukifutilia mbali. Kikundi hiki ambacho tunaamini kumeundwa na Serikali za wapinga mapinduzi wa Afrika ni lazima kisakwe na kufutiliwa mbali kabla madhara yake hayajawa makubwa sana kiasi cha kuwakatisha tamaa wapigania Uhuru wa Kusini mwa Afrika. Haya mauaji yaliyofanyika juzi mjini Kinshasa, imeamuliwa upelelezi wake ufanywe moja kwa moja chini ya Kamati ya Ukombozi ya OAU badala ya kuiachia serikali ya Zaire kufanya upelelezi huu. Hii haina maana kuwa hii itaikataza Zaire isifanye upelelezi wake, na wala haina maana kuwa serikali ya Zaire inajua uamzi wa Kamati ya Ukombozi ya kufanya upelelezi chini yake yenyewe. Kwa hivi wewe tokea sasa utafanyakazi chini ya Kamati ya Ukombozi mpaka hapo tutakapojua mwisho wa jambo hili.

Kwa vile mauaji haya yametokea huko Kinshasa itakubidi uondoke ukaanzie huko huko Kishasa upelelezi wako. Mauaji haya bado yako moto kwa hivi tunaamini kuwa ukifika na kuanza upelelezi kwa wakati huu tunatumaini unaweza kupata mwanzo mzuri. Kwa vile nimekueleza kuwa serikali ya Zaire haina habari juu ya uamuzi huu wa Kamati ya Ukombozi kwa wakati huu itabidi upelelezi wenu ufanyike kwa siri mpaka hapo itakapobidi serikali ya Zaire ipate habari. Dhamira yetu ni kutaka uwe Kinshasa kabla ya mazishi ya marehemu ili uweze kuyahudhuria. Hii itakupa nafasi ya kuwahi harakati zote zinazofanyika na vikundi mbali mbali juu ya tukio hili.

"Huko Kinshasa utamkuta kijana mmoja aitwaye Robert Sikawa, ambaye ni mpelelezi wa idara ya upelelezi ya Zambia lakini anafanya kazi katika ofisi ya OAU iliyopo hapo mjini Kinshasa kama katibu mwenezi. Kijana huyu alipelekwa kwenye ofisi hii toka mwaka jana baada tu ya mauaji ya Meja Komba Matenga yaliyotokea huko Kinshasa. Tokea wakati huo mpaka sasa amekuwa huko na anaweza kuonyesha kuwa anafanya kazi yake. Kwa hivi itakubidi ifanye kazi bega kwa bena naye na vile vile ameamriwa akueleze habari zote anazozijua mpaka sasa. Ni imani yetu kuwa kutokana na habari utakazozipata kutoka kwa Sikawa zitakupa mwanga mkubwa jinsi gani ulishughulikie jambo hili. Vile vile utapata msaada kutoka kwa wapelelezi wengine wawili mashuhuri sana katika Afrika. Mmoja ni Kapteni Petite Osei kutoka Nigeria na mwingine ni Michael Degaro kutoka Msumbiji. Wapelelezi wote hawa wawili wameishapata habari na wameshauriwa wafikapo Kinshasa wafanye mipango ya kukuona kwani kazi yote watakaiyofanya itakuwa chini yako. Kwa hivi wewe Willy pamoja na hawa vijana wengine watatu ndiyo mtaunda "Kkosi cha Kisasi". Wewe ndiye utakuwa kiongozi wa kikosi hiki na hawa vijana na vijana wengine wameamriwa kufanya kazi chini amri yako. Wewe ndiye utakuwa wa kwanza kufika Kinshasa hawa wengine wawili watafuata, nawe utapata habari zao za kuingia Kinshasa kwa kupitia kwa Sikawa ambaye upashanaji wote wa habari utapitia kwake ila tu kwa habari ambazo utaziona muhimu na ungehitaji kuziwasilisha mwenyewe moja kwa moja kwetu. Katika upashanaji wetu wa habari juu juu ya suala hili utajulikana kama "KK". Utapewa nambari za simu na za teleksi zilizomo ndani ya ofisi hii kwa hiyo wakati wowote utakapoona inabidi kutupasha habari unaweza kuzituma.

Kwa vile shughuli mtakazozifanya huko ni za kisiri basi itabidi nanyi muingine nchini na mjini hapo kwa siri. Wewe itaingia mjini hapo kama mfanyabiashara kama ilivyo kawaida yako. Kwa mara hii utakuwa Mkurugenzi wa Wakala wa makampuni ya nchi za nje katika Zaire ambaye yuko mjini Kinshasa kwa mapumziko ya kibiashara. Na hasa kusudi la kuwa kwako mapumzikoni kibiashara mjini Kinshasa ni kutafuta wakala kwa makampuni yaliyo mjini hapo ili yaweze kufanya biashara na makampuni ya hapa Zambia. Sina haja ya kukueleza zaidi maana wewe mwenyewe unajua vizuri kuwa na kazi hiyo. Jina utakalotumia ni Willy Chitalu, kabila Mnyanja wa Zambia. Wenzako nao wataingia Kinshasa kama wafanyabiashara. Wote wawili wataingia kwa pamoja kama wafanyabiashara kutoka Nigeria ambao vile vile wamefika mjini Kinshasa katika shughuli za kukuza biashara yao nchi za nje. Wao nao watakuwa wakitumia majina ya bandia. Kapteni Petite Osei atakuwa akitumia jina la Petit Ozu, Michael Degero atakuwa akitumia jina la Mike Kofi", Chifu alipofika hapa alitoa picha mbili ndani ya bahasha na kumpa Willy. "Hiyo picha niliyokupa mwanzo ndiyo ya Petit Ozu na ya pili ya Mike Kofi, nafikiri utawakumbuka ukiwaona uso kwa uso", Willy alikuwa mtu mwenye akili ya kunasa sura za watu ya hali ya juu sana. Kwa hivi aliziangalia sura hizi kwenye picha kwa makini sana na baada ya kuziangalia sana akazirudisha kwa Chifu.

"Asante, nitawakumbuka", nilimwambia.

"Unaweza kuziweka kwa ukumbusho wako", Chifu alimwambia.

"Hapana nitawakumbuka, si vizuri kusafiri na picha za watu ambao inabidi usiwe umewafahamu tangu awali".

"Vizuri kama unaona si lazima. Nafikiri ulipata ujumbe wangu kutoka kwa Maselina kuwa uchukue zana zako zote tayari kwa safari".

"Ndiyo nilipata na nimechukua kila kitu ninachohitaji kwa safari kama hii".

"Nafikiri maelezo niliyokupa yanatosha, mambo mengine yote tunayaacha mikononi mwako na wenzako. Wewe utaondoka hapa kesho asubuhi na ndege ya Shirika la Ndege la Zaire" kisha akafungua tena mkoba akatoa pasipoti na tikiti ya ndege "Hii hapa ni tikiti yako ya kusafiria hai Zaire na hii ni pasipoti utakayotumia kwa jina la Willy Chitalu". Alifungua tena mkona na kutoa hundi za kusafiria na noti za dola ya Kimarekani. "Hizi pesa za matumizi na ukihitaji pesa zaidi wakati wowote Sikawa ameelekezwa akupatie. Nafikiri mimi kwa upande wangu nimemaliza, kwa hivi ninamwachia mwenzangu kama ana zaidi ya kukueleza", alimaliza Chifu.

"Mimi sina mengi ya kueleza nadhani yote Chifu amekueleza kwa ufasaha. Sisi hata kama tukikuambia nini, haifai kitu, ngoma utaiona wewe mwenyewe, kwa hivi sasa tunabaki tukikutegemea wewe huku tukipiga mioyo yetu konde na kumuomba Mwenyezi Mungu aweze kuwasaidia hadi kufaulu hadi kufaulu katika suala hili. Kitu mnahitajiwa kuwa nacho ni ujasiri na kupigana hadi mwisho, maana tutakuwa tumeanguka sana mkishindwa vita hivi dhidi ya wauaji katili hawa. Vijana ambao utashughulika nao ni vijana jasiri na ni matumaini yangu kuwa chini ya uongozi wako shupavu ujasiri wao utaziidi. Sasa inakaribia saa nne za usiku, nafikiri tukuache ukapumzike kwani siku zitakazofuata zitakuwa hazina mapumziko ya kutosha. Mungu akusaidie.

"Asante sana wazee wangu" Willy alisema. Mimi nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu. Tuombeeni tu Mungu aweze aweze kutusaidia kwani sisi tunachokifanya ni haki yetu kwa hivi katuna budi kupata baraka za Mwenyezi Mungu katika mapambano yetu. Asanteni sana", alisema huku akinyanyuka kitini. "Haya Willy nadhani nitakupigia simu hapo hotelini kwako kabla hujaondoka kesho asubuhi". Alijibu Chifu.

"Kwani amefikia hoteli gani? Maana nasikia alikataa nafasi aliyowekewa huko Lusaka Hoteli", alieleza mwenzake na Chifu.

"Yuko Ridgeway Hoteli", alijibu Chifu. 

"Siyo kuwa nilikataa kukaa Lusaka Hoteli, bali tu kwa sababu ya kawaida. Mara nyingi mimi nikiwa hapa Hoteli yangu ya Ridgeway. Oke Chifu nitangojea simu yako na kwaheri kesho asubuhi", alisema Willy huku akiagana nao kwa kushikana mikono.

Willy alifungua mlango wa chumba na kutoka kisha akarudisha mlango na kuwaacha mabosi wake waendelee na mambo yao. Willy alijitokeza kwenye mapokezi ya hii ofisi ya waandishi wa siri wa Mkurugenzi wa upelelezi wa Zambia. Willy alipotokeza kwenye ofisi hii alikuta bado wale wasichana wapo. Yule msichana aliyekuwa anashughulika na simu pamoja na teleksi alikuwa bado anashughulika huku yule msichana mwingine aliyekuwa akipiga mashine alikuwa amekaa juu ya meza huku ameshika mkoba wake akionyesha kuwa amemaliza kazi. Walipomuona Willy anatokeza yule msichana aliyekuwa amekaa kwenye mezaa alitelemka haraka haraka na kujiweka sawa. 

"Nafikiri tunaweza kusalimiana sasa, habari zenu?" Willy aliwasalimu.

"Habari zetu ni nzuri", walimjibu kwa pamoja huku yule msichana wa simu akionyesha dalili kuwa alikuwa bado anazongwa na kazi.

"Poleni sana mpaka sasa bado mko kazini? Kusema kweli wasichana kama nyinyi saa hizi mnafaa muwe mko mahali mkistarehe, moyo kama huu ni wa kizalendo na mnastahili pongezi zangu."

Wale wasichana walitabasamu tu bila kumjibu kitu. Kisha yule msichana mpiga mashine akamwambia mwenzake, "Mwambie mzee, mimi nimemaliza kazi naomba anifanyie mpango wa usafiri kurudi nyumbani," Wakati yule msichana mwingine akizungumza na bosi wao, Willy ambaye sasa alikuwa karibu akiwaangalia vizuri wale wasichana, alimtolea yule msichana aliyekuwa akiomba usafiri tabasamu la haiba kisha akamwambia, "Hamna haja ya kuomba usafiri, kama hautajali sana mimi nitakupa msaada mpaka mahali popote unapotaka kwenda."

"Asante sana, sisi tunao usafiri wetu, kwa hiyo hamna haja ya kukusumbua", yule msichana alijibu.

"Hapana siyo kwamba kukupa msaada utakuwa unanisumbua, kusema kweli moyo wangu utafurahi sana kukupa msaada huo. Na kama kweli utanikatalia utakuwa umenisikitisha sana,"

"Yule msichana akiwa anasita kujibu huku yule mwenzake akiwa anamtolea jicho la pembeni naye akingojea mwenziwe atajibu nini, bosi wao alifungua mlango na kutokea hapo ofisini kwao. Mara moja wote wakawa wamejiweka vizuri, wakati bosi wao anamwangalia Willy kwa mshangao. 

"Wewe bado unafanya nini hapa?" alimuuliza Willy.

"Mzee, unajua sisi vijana lazima tufahamiane, isiye siku moja tukagongana mitaani na hawa dada zangu tukafanyiana ubaya na hali sisi ni ndugu." Jibu hili la Willy lilionekana kumtosheleza bosi kwa hivi akaanza kumweleza yule msichana aliyekuwa akiomba usafiri, "Unaweza kwenda ila kesho asubuhi sana utakuja kuchukuliwa kuna kazi, kwa hivi kapumzike mapema upate kuamka mapema. Joyce piga simu kwa dereva alete gari," alimwamru yule msichana mwingine.

"Hamna haja ya kumwita dereva mzee, kama amemaliza kazi na kwa vile mimi ninaondoka sasa hivi sioni kwanini tusiondoke pamoja," Willy alishauri.

Bosi alimwangalia yule msichana halafu Willy akatingisha mabega yake kuonyesha kuwa yeye naye alikuwa haoni sababu kama Willy anakwenda huko kwanini wasiondoke pamoja. 

"Haya kama unaona hatakusumbua unaweza kwenda."

"Bila taabu mzee". alijibu Willy huku anamshika yule msichana mkono na kumwongoza nje. Bosi na yule msichana mwingine wakabaki wanaangaliana kwa shauku.

Willy na yule msichana waliingia ndani ya gari na kuelekea mjini. 

"Sijui mwenzangu unaitwa nani?" aliuliza Willy.

"Mie naitwa Amanda".

"Jina zuri sana, unakaa sehemu gani?".

"Nakaa hapa karibu, sehemu ya Kamwala karibu na sokoni."

"Oho, nafikiri hutajali tukipita mara moja hapo Ridgeway ukapate kinywaji kidogo kabla hujaenda kupumzika."

"Hapana, nafikiri umemsikia mzee alivyosema, itabidi nikalale mapema.

"Mimi najua ndiyo sababu nikasema kidogo," Willy alimwangalia tena na kutoa tabasamu la kukata na shoka. 

"Uh... sijui kwa nini inakuwa vigumu kukukatalia kitu, haya twende ndugu..."

Ndugu Willy, ndilo jina langu". 

"Nafurahi kuwa na wewe, kusema kweli nimesoma habari zako jana, na ninasisimkwa kila nikifikiri niko na wewe," Amanda alieleza huku akimwangalia kidogo na kuangalia pembeni. Muda huu Willy ndipo alipokuwa anaanza kutambuwa kuwa msichana huyu aliyekuwa nae alikuwa msichana mzuri sana lakini uzuri wake ulikuwa hauwezi kujulikana kwa mara moja. 

"Hata mie nafurahi kuwa nawe," Willy alijibu huku akiwa anapiga kona kuingia Ridgeway Hotel. Aliegesha gari lake vizuri na kutoka nje. 

"Mimi sijawahi kuingia hapa hotelini," alisema Amanda.

"Wacha kwa nini?" Aliuliza Willy kwa mshangao. 

"Basi tu, kwanza sina mtu wa kuweza kunileta hapa, maana tangu nianze kazi mwaka mmoja sasa kazi yangu imenitinga kiasi kuwa ni vigumu kupata mtu wa kuweza kuvumilia kiasi kile." Willy aliweza kuelewa maana hata Maselina aliwahi kuwa na tatizo kama hilo. Kidogo alisikia huruma maana msichana huyu alikuwa bado mbichi kiasi cha miaka ishirini na moja au mbili hivi.

"Kama mimi ningekuwa hapa siku zote amini nakwambia ningepata muda tu." alimjibu huku wakikaa kwenye meza moja kando ya bwawa lililotengenezwa hapo Ridgeway Hotel. Mtumishi alikuja akaagizwa vinywaji. Vinywaji vilipokuja walikunywa huku wakielezana mambo mbalimbali katika maisha yao ambayo yaliwafanya kustukia ni saa sita na kuhitaji waondoke.

"Asante sana Willy, umenifanya kuwa msichana wa furaha sana leo kwani kwa mara ya kwanza maishani nimepata mtu ambaye nimeweza kuzungumza naye na kunielewa. Tafadhali ukirudi toka Kinshasa rudi unione. Mungu atakusaidia najua utarudi salama kwa hiyo tafadhali rudi hapa unione eh Willy. 

"Mungu akipenda nikiwa salama nitakuja usiwe na shaka", Alijibu Willy wakiingia ndani ya gari. Amanda alimvuta na kuanza kumpiga busu. "Tafadhali urudi." Alibwebweta.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. Enter your comment...Duuuh! .........Kazi sasa inakaribia kuanza! Telemka nayo!

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU