KIKOSI CHA KISASI

SURA YA NNE

"WP"

I

"Mabibi na mabwana, kwa niaba ya rubani wetu Godi Kazadi pamoja na wafanyakazi wenzake, ningependa kuwajulisheni kuwa mnamo dakika kumi na tano zijazo tutatua kwenye uwanja wa ndege wa Ndjili wa mjini Kinshasa. Ni matumaini yetu kuwa mmefurahia safari yenu ambayo mmesafiri na shirika la ndege la Zaire ndani ya ndege ya aina ya Boeing 737 ambayo imekuwa ikiruka kisi cha futi 30,000 juu ya usawa wa bahari. Kwa wageni ningependa kuwajulisha kuwa Kinshasa ndio mji mkuu wa Zaire ambao umejengwa pembeni mwa mto wa Zaire magharibi ya nchi. Mji wenyewe ni mtulivu kwa biashara na starehe na ninadiriki kusema kuwa ndio mji wenye anasa zaidi katika Afrika ya kati. Kwa hivi ni matumaini yetu kuwa mtafurahia kuwapo kwenu Kinshasa na tunawakaribisheni tena kusafiri na shirika la ndege la Zaire Mpatapo safari tena. Asanteni sana," ilisikika sauti nyororo na tamu ya msichana ikinena. 

Abiria wote walichangamka kule kusikia walikuwa karibu kutua mjini Kinshasa. Hata waliokuwa wamelala waliamka.

Willy ambaye kwa muda mwingi alikuwa akisinziasinzia alikuwa sasa hivi yu macho. Alikuwa akisinziasinzia maana usiku ule alikuwa hakupata usingizi sawasawa. Alianza kufikiria usiku uliokuwa umepita. Usiku ule baada ya kuondoka na Amanda Ridgeway Hoteli, alimpeleka mpaka nyumbani kwake Kamwala. Alipofika nyumbani kwa Amanda. Amanda alimng'ang'ania aingie ndani. Amanda alikuwa akikaa peke yake kwenye nyumba ya chumba kimoja cha kulala na sebule. Kusema kweli kilitosha sana kwa msichana kama yeye na vyombo vilivyokuwa ndani vilionyesha waziwazi kuwa Amanda alikuwa na kipato cha juu. Haya yote Willy aliyaweka rohoni alipoingia ndani ya chumba hicho. Amanda alileta vinywaji wakaanza kunywa upya kabisa huku hali ya kimapenzi ikizidi kukomaa kati yao dakika hata dakika kiasi kwamba walijistukia ni saa tisa za usiku. Kwa hivi Amanda alimuomba Willy ajipumzishe pale kwa masaa yaliyokuwa yamebaki. 

Kwa vile Willy hakutaka kumvunja moyo mtoto huyu alikubaliana naye na kwenda chumbani tayari kwa kulala. Sina haja ya kukueleza mengi kwani wewe mwenyewe unajua mambo wayafanyayo wawili wapendanao na hasa ikiwa penzi bado changa kama hili la Willy na Amanda. Kusema kweli watu hawa walistukia wale ndege wa asubuhi wanatoa salam zao kabla hata hawajafumba macho yao kusinzia. Hivi ilimbidi Willy aondoke awahi hotelini tayari kwa safari. Willy alikumbuka jinsi Amanda alivyomuaga huku machozi yakimtoka na huku akirudia neno lile anarudia usiku kucha "Willy mpenzi, sijui kwa nini nimekupenda kiasi chote hiki na huku kesho unaondoka tena! Tafadhali sana mpenzi ukienda urudi kuniona." Baada ya kuondoka nyumbani kwa Amanda alirudi hadi hotelini kwake ambapo alianza 
kujitayarisha kwa safari.

Ilipofika saa kumi na mbili na nusu alipata simu toka kwa Chifu. Chifu alizidi tu kumhimiza umuhimu wa kazi aliyokuwa akienda kuifanya akimalizia kwa sentesi hii "Willy ni imani yangu kuwa kwa maadili na hamasa upiganaji wa kimapinduzi mtaweza kabisa kufauli katika jambo hili. Kwa hiyo nendeni mkaitende hii kazi kwa moyo safi na wa kimapinduzi, na Mungu atawasaidia", Willy aliyafikiria yote haya kwa moyo wa uchungu SANA kwani aliweza kuufikiria uzito wa mambo yaliyokuwa yakimngojea kuyakabiri huko Kinshasa. "Funga mkanda wako", alishituliwa Willy na msichana mmoja mfanyakazi, "Tunatua sasa"

"Oho asante bibie, nilikuwa mbali", Willy alijibu huku akijiweka sawa kwa kutua.

Ndege ilipokuwa imetua watu walianza kutelemka hapo kwenye uwanja wa ndege wa Ndjili wa mjini Kinshasa. Willy hakuwa mgeni sana mjini Kinshasa kwani alikuwa amewahi kufika mara mbili ingawaje kwa muda mfupi, hivi alikuwa akijua vipi mambo yalivyokuwa hapo uwanja wa ndege.

Akiwa amebeba mkoba wake Willy alitelemka pamoja na abiria wenzake kuelekea uhamiaji na ofisi ushuru wa forodha.

Willy aliweza kupita ukaguzi wa ofisi hizi bila shida na kutokea nje tayari kwa safari ya kuelekea mjini Kinshasa. Huku akiwa anaangaza huku na kule kuna kama kulikuwa na mtu ambaye alikuwa anaonyesha kumtegemea kuingia mjini Kinshasa. Alipoona hakuna mtu wa namna hii ila abiria waliowasili pamoja na ndugu zao waliokuja kuwapokea na taksi dereva walikuwa tayari kujipatia abiria wa kupeleka mjini. Willy alienda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi za kampuni ya 'Soviete de Transport de Kinshasa' ijulikanayo kwa kifupi kama STK ambayo inashughulikia magari ya kukodisha. Alipofika kaunta ya ofisi hii aliwakuta wasichana waliokuwa wakishughulika.

"Habari yako dada?" Alimsalimia msichana aliyemkaribisha.

"Nzuri karibu, tukusaidie nini?" Yule msichana alimuuliza kwa sauti nyororo.

"Nahitaji gari".

"Oho, hamna taabu tunayo magari mazuri aina ya Mercedes Benz", alimweleza kisha akamwita msichana mmoja aliyekuwa amesimama hapo nje ya ofisi, "Marie, mpeleke abiria huyu mjini", Hii kampuni ya STK madereva wake wa teksi asilimia sitini na tano ni wanawake. 

"Hapana, mimi nataka gari ya kuendesha mwenyewe (Salf drive) Willy alieleza.

"Vile vile hamna taabu", yule msichana alimjibu kisha akaendelea, "Unayo leseni ya udereva?".

"Ndiyo", alijibu Willy huku akitoa leseni yake ya kimataifa ya udereva na kumpa yule msichana. Yule msichana aliangalia leseni kisha akamwangalia Willy halafu akasema. "Bosi, masharti ni kwamba itakubidi utoe amana ya Zaire mia mbili, na malipo mengine utayafanya siku utakaporudisha gari, kwani unategemea kukaa nayo muda gani?".

"Huenda kiasi cha wiki moja au mbili".

"Vizuri, kwa sasa lipa pesa hizo na jaza fomu hii", akampa fomu. "Hebu nipe pasipoti", Willy alimpa pasipoti yake huku akiendelea kujaza fomu ya kukodi gari. Alipomaliza akamuuliza, naweza kulipa katika dola".

"Unaweza, nitakupa risti".

Walipomaliza taratibu zote yule msicha alichukua ufunguo wa gari na kumpeleka Willy kwenye gari moja kati ya yale yaliyokuwa yameegeshwa karibu na ofisi ile. 

"Nimekuchagulia gari nzuri sanana mpya aina ya Marcedes Benz, ina 'redio-cassette' ndani yake, kwa hiyo naamini itakufaa sana, hasa kwa mfanyabiashara kama wewe. Na ukipata matatizo yoyote tafadhali nijulishe, kadi yangu ya kazi hii hapa", alimpa hiyo kadi Willy akaiangalia, ilikuwa na jina la msichana huyu ambaye jina lake aliitwa Ntumba Akanda. Vile vile kulikuwa na namba za simu yake ya nyumbani pamoja na ya kazini.

"Asante sana Ntumba, nikipata shida yoyote nitakujulisha", 

"Hata kama utakosa mahala pa kulala karibuni nyumbani", alitania huku akicheka.

"Lo, afadhali nikose nafasi, ili nikaribishwe kwako," alijibu Willy naye kimatani.

"Bila wasiwasi, haya kwaheri".

"Asante sana bibie tutaonana", wakaagana.

"Kutoka uwanja wa ndege wa Ndjjili hadi mjini Kinshasa ni umbali wa kilomita 30. Hivi, Willy aliwasha gari moto kuondoka kuelekea mjini. Kwa hivo alikata gari lake kulia na kuingia ndani ya barabara ya Patrice Emery Lumumba barabara kubwa itokayo uwanja wa ndege akielekea mjini. 

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU