KIKOSI CHA KISASI

SEHEMU YA NNE

"WP'

II

Wakati huo Willy akielekea mjini kutoka uwanja wa ndege katika nyumba ya Mzungu mmoja iliyoko mtaa wa Gitronir sehemu ya kuishi ya Limete kulikuwa na watu wanne wakiwa na fikra ya jambo hilo hilo ambalo alikuwa akilifikiria Willy lakini kwa hali tofauti. 

Kati ya watu hawa wawili walikuwa Wazungu, mmoja Muasia na mmoja Mwafrika. Watu hawa ambao saa sita hizi za mchana walikuwa wamekusanyika kwa kikao cha dharura, walikuwa ni viongozi wa kikosi cha siri kilichokuwa kikijulikana kama "WP" kirefu cha 'White Power' yaani 'Nguvu ya Mweupe' ambacho kilikuwa ni kikosi kilichoundwa na Shirika la ujasusi la Afrika Kusini liitwalo 'Boss' kwa madhumuni ya kuwapiga vita wanamapinduzi na wapenda maendeleo wa Afrika. Kikundi hiki kilikuwa kimeundwa kwa ujuzi wa kijasusi wa hali ya juu kiasi kwamba mbali na 'Boss' hakuna shirika lingine la ujasusi pamoja na Idara zote za upelelezi na polisi duniani ambazo zilijua kuwepo kwa kikundi hiki. Kikundi hiki kilifanya shughuli zake makao yake makuu yakiwa mjini Kinshasa na kikiongozwa na Pierre Simonard ambaye ndiye alikuwa mwenye nyumba hii ambamo mchana huu alikuwa akikutana na wasaidizi wake hawa watatu.

Pierre Simonard alikuwa mtu mwenye umri wa miaka 52, mjini Kinshasa alijulikana kama Mbelgiji na alifahamika kwa watu wengi sana maana alikuwa na gereji ya magari ambayo ilitokea kupendwa sana na watu wa hali ya juu kutokana na utengenezaji wake mzuri wa magari. Gereji yake hii ambayo ilikuwa barabara ya tisa (9) sehemu ya Limete ilikuwa ikiitwa Garage Du Peuple!. Kutokana na hali hii ilikuwa vigumu kumfikiria Pierre kwa shughuli zinginezo mbaya. Jina lake la kweli aliitwa Peter Simon na alikuwa ofisa wa juu katika 'Boss'. Kabla ya kutumwa Kinshasa kuongoza 'WP' alikuwa kiongozi wa idara ya mateso na mauaji ya 'Boss'. Hii inaonyesha waziwazi Pierre alikuwa jasusi katili wa hali ya juu, na kuchaguliwa kwake kuja kuongoza kikundi hiki kulitokana na uongozi wake wa kikatili katika idara hii. 

Pierre aliingia mjini Kinshasa mnamo mwaka kama mfanyabiashara wa Kibelgiji. Kusema kwelie Pierre hakuweza kutambulika kuwa si Mbelgiji kwa sababu hati zake zote za kusafiria zilionyesha kuwa yeye ni Mbelgiji kwa kila hali. Hati zake zilionyesha kuwa yeye alikuwa ni mhandisi wa magari na hivi aliomba leseni ya funguo gereji alipewa bila matatizo. Kwani jila lake lilipopelekwa Brussels kwa uchunguzi na idara ya uhamiaji ya Zaire majibu yaliyorudi yalionyesha kweli kuwa kulikuwa na Pierre Simonard ambaye alikuwa mhandisi na mzaliwa wa Ubelgiji. Hivyo mwishoni mwa mwaka 1968 Pierre alianzisha 'Garage Du Peuple huku akiendelea na harakati zake za kuunda 'WP' huku akisaidiwa na wateja wake. Baada ya kuwa amejiweka katika hali ya usalama mwaka 1969 ndipo 'WP' hasa iliundwa.

Mwanzoni mwa mwaka huu wa 1969 Jean Vergeance aliingia nchini Zaire naye akitokea Brussels Ubelgiji. Jean naye kama Pierre alikuwa jasusi wa hali ya juu katika 'Boss'. Baada ya Pierre kutoa taarifa kwa wateja wake kuwa mambo yalikuwa yakienda sawasawa na hakukuwa na wasiwasi, ndipo 'Boss' walipomtuma Jean Vergeance ambaye hasa jina lake ni John George mwenye umri wa miaka 36 kwenda Kinshasa. Jean alipoingia Kinshasa aliingia kama mtaalam na kuajiriwa na kampuni ya Fiat kama mtaalamu. Naye baada ya miezi sita alikwisha jijenga kwa wakubwa aliacha kazi hii na kuanzisha gereji yake binafsi ijulikanayo kwa jina ya 'Garage Auto Diesel' au kwa kifupi GAD ambayo iko sehemu ya Gombe barabara ya T.S.F, wakati wote huo walikuwa wakionana na Piere kwa siri, na hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa akijua kama watu wawili hawa wanafahamiana ila tu kwa vile wote wawili walikuwa na gereji. Na huku kuwa na shughuli hii ndiyo ilikuwa mbinu ya Pierre katika mfumo wa kuunda 'WP'.   

Katikati ya mwaka huu 1968, Mpakistan mmoja aitwaye Papadimitriou kwa kifupi akijulikana kama Papa aliomba leseni ya kufungua gereji sehemu za Lingwala. Mpakisitan huyu ambaye alikuwa ameingia Zaire kutoka Zambia kama mfanyabiashara wa duka kubwa sana la madawa. Lakini baada ya kukaa na kuanza kujulikana, naye katikati ya mwaka 1969 aliomba leseni ya gereji na bila matatizo akafanikiwa. Mpakistan huyu vilevile alikuwa ni jasusi wa shirika hili la ujasusi 'Boss', Yeye kweli alikuwa Mpakisitan aliyekulia mjini Johannesburg ambako alikuwa akifanya shughuli za biashara. Na wakati wakikaa Johanneburg ndipo 'Boss' ilipomchagua na kumfanya mmoja wa majasusi wake latika nchi za nje. Na baada ya mafunzo ya hali ya juu katika ujasusi Papa alijulikana ndani ya 'Boss' kama 'Executioner'yaani muuaji kwa kutokana na uwezo wake wa kuweza kumwinda mtu hata kama analindwa kiasi gani, na kumuua. Hivi 'Boss' alionelea vizuri kumtumia Papa katika 'WP' na mnamo mwisho wa 1968 wakamfanyia mpango wa kumwamru aende Kinshasa Zaire ambako angasubiri maelezo. Naye katika ya 1969 alipata amri aripoti kwa Pierre kwa siri na afuate maagizo yake. Na kwa kutokana na maagizo ya Pierre, Papa ilimbidi kuuza shughuli zake za duka la madawa na kuanzisha gereji iliyoitwa 'Garage Papadimitriou' ambayo iki barabara ya Kabambare sehemu za Lingwala.

Mwisho wa mwaka 1969 kijana mmoja ambaye kwa wakati huo alikuwa akiitwa Muteba Andre ambaye kwa sasa anaitwa Muteba Kalonzo aliingia mjini Kinshasa akitokea jimbo la shaba. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 aliingia Kinshasa na pesa nyingi kutoka jimbo la Shaba, na kuomba leseni ya kuendesha biashara ya magari ya kukodisha, Akiwa mzalendo haikuwa taabu kwake kupata leseni hii, hivyo baada ya kupata leseni hiyo alinunua magari ishirini ya aina ya Fiat 124 na kuyafanya teksi. Kwa sababu vijana wengi mjini Kinshasa wana uwezo wa kufanya hivi, jambo hili halikumshangaza mtu yeyote hasa akiongezea kuwa kijana huyu alikuwa akitokea jimbo la Shaba. Mwanzoni mwa mwaka 1970 Muteba aliomba leseni ya kufungua gereji kwa sababu aliyoitoa ya kwamba kwa vile ana magari mengi yake binafsi ingekuwa vizuri kuwa na gereji yake ambayo ingeweza kuhudumia magari yake na vile vile magari ya watu wengine. Sababu hii ilitosheleza sana kwa hiyo alipewa leseni ya gereji na kufungua gereji moja iitwayo ' Garage Baninga' katika sehemu ya Kintambo barabara ya Bangala. Ukweli ni kwamba Muteba naye alikuwa ameajiriwa na 'Boss' kama muuaji wao. Uhusiano wake na makaburu ulianza wakati bado akiwa na umri wa miaka 18, wakati kijana huyo alipokuwa akipigana na majeshi ya kukodishwa ya Tshombe huko Katanga. Muteba alionekana kijana jasiri sana katika mapigano haya, kwa hiyo wakati askari wa kukodishwa walipokuwa wakiondoka Katanga walimuomba afuatane nao. Na kwa sababu wakati huo Muteba alikuwa bado mdogo na mwenye uchu wa kuona ulimwengu ulivyo alikubali na kuondoka nao. Kwa bahati nziri au mbaya askari aliyetokea kumpenda sana alikuwa kaburu, hivyo alisafiri naye kuelekea Afrika Kusini. Na wakati akiwa na askari huyo ndipo 'Boss' alimgundua na kumuona kuwa yu kijana mwenye akili nyingi za kuzaliwa na wangeweza kumtumia kwa mambo yao maovu kama wangeweza kumpatia ujuzi zaidi katika mambo ya ujasusi. Hivi Muteba alikuwa amefanya maovu mengi katika Afrika kwa niaba ya makaburu. Kwa hiyo wakati mipango ya kuunda 'WP' inaendelea, ilionekana jambo muhimu kumshirikisha. Hivyo Muteba ambaye alikuwa Tanzania kwa wakati huo aliamriwa kwenda Kinshasa na kuripoti kwa siri kwa pierre ili aweze kupata maelekezo zaidi. 

Hivi ndivyo viongozi wa 'WP' walivyoingia mjini Kinshasa mmoja mmoja na hatmaye kukamilika na kuunda kikosi cha 'WP' ambacho tokea wakati huo kimeweza kufanya madhara ambayo hayatasahaurika kwa wanamapinduzi wa Afrika na kwa watu wenye fikra za kimaendeleo kote Ulimwenguni. 

Wakati huu Pierre, Jean, Papa na Muteba wakiwa wamekaa kwenye mkutano wa dharura ndani ya nyumba ya Pierre, 'WP' ilikuwa imekomaa sana na ilikuwa na matawi katika nchi zote za kimapinduzi.

Kikosi hiki kilikuwa na watu wengi sana na chenye uwezo wa kufanya madhara yasiyo kifani. Kama nilivyokwisha kusema Kinshasa ndipo palikuwa makao makuu, na magereji haya manne ndiyo yalikuwa makambi na viwanja vya mafunzo kwa wapinga mapinduzi hawa ambao tayari walikuwa wameweza kuwaua wapigania uhuru wenye sifa za juu sana.

"Jamani karibuni," Pierre aliwakaribisha wageni wake, huku akiwawekea kinywaji cha 'Whiski' ndani ya bilauli zao. 

"Asante," walimjibu kwa pamoja. Alipokwisha kuwapa kinywaji alijiwekea na yeye halafu akaa chini tayari kwa mazungumzo.

"Nimewaiteni hapa ghafla kwa sababu nimepata habari ambazo nisingeweza kukaa nazo hata kwa muda wa saa moja. Nadhani mmeshangaa sana mimi kuwaiteni wakati majuzi tu ndipo tumeweza kufanya tukio la maana kiasi kwamba Ulimwengu wote unapiga kelele, huku tukiwa tumewapa pigo kubwa makafiri hawa ambao itawachukua muda kupona pigo hili. Naelewa waziwazi kuwa ni amri yetu kuwa kuwa baada ya tukio kama hili tusionane mpaka hapo mambo yanakapokuwa yamepoa lakini kwa sababu ya umuhimu wa mambo niliyoyapata imenibidi nichukue jukumu hili la kuitisha mkutano huu. Nafikiri tumeelewana."

"Tumeelewa". walijibu tena kwa pamoja huku wakiwa na shauku la kusikia jambo hili muhimu.

"Nimepata habari kutoka 'Boss' muda wa saa moja iliyopita. Habari hii imeeleza kuwa, 'Boss' imepata habari kutokana na Shirika la Ujasusi la Marekani 'CIA' kuwa juzi Mawaziri wa Ulinzi na Wakurugenzi wao wa Upelelezi wa nchi saba zilizo wanakamati wa kamati ndogo ya usalama ya Kamati Kuu ya Ukombozi ya Nchi Huru za Kiafrika, wameingia Lusaka kisiri. Jambo hili si la kawaida maana kwa mara ya kwanza wanakamati hawa wameandamana na wakurigenzi wao wa upelelezi na safari yao ilikuwa ya kisiri. Hivi ni bayana kuwa wamewasili Lusaka kuzungumzia tukio hili la majuzi. Hivyo 'Boss' imetujulisha jambo hili kusudi tuwe katika hali ya tahadhali. Bado hawajajua ni uamzi gani umefikiwa bali tu wamepata habari kuwa walifanya vikao viwili, lakini bado hawajaona kitu chochote kinachoweza kuonyesha ni uamzi gani wamefikia. Hivyo 'Boss' pamoja na 'CIA' ziko macho kuangalia hatua gani itafuata. Kwa hivi si..." kengere ya simu ilimkata kauli, "Samahani," aliinuka na kwenda kuzungumza kwenye simu. "Hello Pierre hapa,"

"Aha Patron," sauti ilijibu. Mara sura ya Pierre ilibadilika na kuwa nzito.

"Nakupata endelea," alijibu.

"Nimepata habari, spea zimeondoka Lusaka," alielezwa kutoka upande mwingine wa simu.

"Zote?".

"Ziendazo Tanzania nusu zimeondoka nusu zimebaki."

"Ina maana zimekoswa usafiri".

"Haijajulikana bado, lakini tutapata habari karibuni. Ni hivyo tu. zilizobaki ni zile chache".

"Habari zingine hizo", aliwaeleza wenzake, "Hawa wanakamati wote wameishaondoka Lusaka kuelekea makwao isipokuwa mkurugenzi wa upelelezi wa Tanzania ndiye amebaki. Tutapata habari zaidi kwanini amebaki baadae,"

"Hakuna mpelelezi yeyote aliyeingia Lusaka kutoka nchi huru za Kiafrika?" aliuliza Papa. 

"Jambo hili nimeulizia lakini mpaka leo asubuhi hakuna hata mmoja kwa wale wanaojulikana aliyeonekana kuingia Zambia," alijibu Pierre.

"Ni lazima ijulikane upesi kwanini mkurugenzi wa upelelezi wa Tanzania amebaki. Kwa kutokana na rekodi zilizopo 'Boss' pamoja na utafiti wangu nilioufanya wakati nikiwa Tanzania, Mkurugenzi huyu ni mshauri sana katika kazi yake, si mtu wa kumrahisisha", alieleza Muteba.

"Sawa kabisa", Pierre alisema, "Nitatuma habari wapate kushughulikia jambo hili kikamilifu. Vile vile inatubidi na sisi tuwe macho, kwa hivi lazima kwa wakati huu tuchukue jukumu lote la usalama wa 'WP' sisi wenyewe. Mpaka hapo tutakapoona vingine kuhusu amri zote juu ya tukio hili tunazitoa wenyewe na habari zozote lazima zitufikie sisi wenyewe moja kwa moja, kama mmoja wenu akipata habari zozote kuhusu tukio hili hata likiwa dogo kiasi gani lazima aniletee ripoti, maana 'Boss' inafikiria huenda 'OAU' ikaamua kulipiza kisasi jambo hili, kwa sasa hivi nchi huru za Kiafrika zemeanza kufikia maendeleo makubwa katika mambo mbalimbali hivi hatuwezi kuwapuuza," aliwaeleza Pierre.

"Kuna jambo moja ilitubidi tuwe tumelifanya, kuwa na mtu wa kuchunga uwanja wa ndege, kuona kama kuna mtu yeyote ambaye kuingia kwake Kinshasa kunatia wasiwasi," Jean alitoa oni.

"Sawa kabisa Jean, nilikuwa naelekea huko. Itabidi Jean usimamie kikundi chako ambacho kitaangalia usalama kwa ujumla, itabidi sehemu zote muhimu kama uwanja wa ndege na mahoteli yashughulikiwe kikamilifu. Vilevile itabidi utume mtu kwenye mazishi ambayo yameahilishwa mpaka kesho asubuhi ambapo huenda akapata fununu yoyote."

"Hamna taabu, mambo yote juu ya usalama nitayashughulikia pale patakapohitaji msaada nitawajulisheni," alijibu Jean kwa sauti ya uthabiti.

"Itabidi tusionanenane isipokuwa tu kwa lazima sana kama hivi. Kama kuna maelezo yoyote tunaweza kuwatumia vijana wetu kama kawaida", alisema Pierre.

"Ok Patron, sisi tutajiweka katika hali ya tahadhali, lakini sidhani kuna kitu chochote, 'WP' imejificha kiasi ambacho hakuna idara ya upelelezi Afrika inaweza kugundua. Sidhani vilevile kuwa wanaweza kuwekea mashaka Kinshasa, saana wakaiomba Serikali ya Zaire kufanya upelelezi wa kinaganaga jambo ambalo Zaire haiwezi kufika popote Zaidi ya hapo sidhani kuna haja ya kuhangaika sana. Lakini hata hivyo hatutaacha njia yoyote wazi ikiwa 'OAU' itaamua kufanya matata," alizungumza Papa.

"Kiusalama ni vizuri kuzuia kuliko kuponya", alijibu Jean ambaye alikuwa amesomea sana mambo ya usalama katika shule za kijasusi za 'Boss'.

"Nakubaliana kabisa nanyi nyote, hivi hatuna budi kuwa na usalama wa hali ya juu. Inawezekana kifo hiki cha Mongo kimewapiga vibaya sana. Lakini hata wakiamua kufanya utafiti 'OAU' wenyewe sidhani watafika popote. Sidhani 'OAU' kiupelelezi inao uwezo wa kuingilia 'Boss' kabla 'Boss' haijaweza kuwasaga wapelelezi wake wote", alijigamba Pierre.

"Ni kama Papa kupigana ngumi na Mohammed Ali", alitania Muteba huku wote wakiangua kicheko. 

"Oke jamani, kawawekeni watu wenu katika tahadhali, tukingojea nini kitatokea. Mambo mengine yanaendelea kama kawaida. Mimi nitajaribu kukusanya habari nyingi iwezenavyo, nyinyi tumieni majina yenu mazuri kupata habari, maana huenda kwa mara ya kwanza tukapata upinzani toka 'OAU' kutokana na tukio hili la juzi,"  aliendelea kuasa Pierre.

"Patron, mbona unakuwa kama mtu mwenye wasiwasi. Usiwe na wasiwasi sisi tuko macho hakuna kitu kinachoweza kuingia 'WP' ambapo sasa ndipo iko imara kama chuma cha pua," Papa alimhakikishia Pierre. Pierre aliagana na wageni hawa maarufu ambao waliingia ndani ya magari yao na kwenda zao, bila kujua kuwa Willy Gamba mpelelezi mashuhuri katika Afrika alikuwa ameingia mjini Kinshasa saa hizo hizo tayari kutafuta chanzo cha tukio hili.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru