NOTI BANDIA

SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA

Baada ya kufanikiwa kuuruka mtego wa kukamatwa na vijana shupavu wa Peter Twite pale karakana ya  Reli ya Tazara, Carlos Dimera na kundi lake walikimbia na kufanya harakati za kuihama Dar es Salaam. Wakijua mambo sasa yametibuka.

Haraka, Carlos aliwasiliana na Emilio Pablo, kiongozi wa vikundi vya wasambazaji wa dawa za kulevya duniani, bila kupepesa maneno Carlos alimfahamisha kigogo huyo kuwa hali ya hewa ya Dar es Salaam, imegeuka. Akaeleza jinsi walivyopata ushindani kutoka kwa vijana ambao mpaka sasa hawajafahamika.

"Huo ni uzembe wako Carlos, sharti letu unapomkamata adui yako hana budi kuishi hata kwa sekunde moja, maneno gani umefanya. Ok, sasa unahitaji msaada gani zaidi?", Emilio alihoji.

"Kama nilivyojulisha awali, vijana walifanikiwa kuiba shehena yote ya dawa iliyokuwa imekamatwa na kupelekwa kwa mkemia, mzigo uko salama na sasa tuko katika maandalizi ya kuondoka Dar es Salaam leo mchana kwa boti kubwa sana ambayo tayari iko ufukweni mwa bahari ikisubiri safari.

"Safi, niwapongeze hao vijana kwa kufanikiwa kuufikisha mzigo ndani ya boti salama, lakini unawapeleka wapi, huo ni mzigo kwetu, una hakika mzigo uko salama?'.

"Naam bosi, hilo halina shaka, mzigo uko salama kabisa. kuhusu hao maisha yao yatakoma baada ya kuondoka, Tunaondoka Dar es Salaam mchana tukabiliwa na changamoto moja, Tunaelekea wapi baada ya Dar es Salaam?". Carlos alihoji. Baada ya kuelezana hili na lile, alikata simu.  

Madawa mbali mbali ya kulevya, vifaa kadhaa vya kutengeneza noti bandia, silaha na dhana nyingine zilihamishwa na kuhifadhiwa ndani ya boti kubwa iendayo kasi sana. Boti hii iliyoandaliwa kwa ajili ya safari, kuelekea mahali kusikojulikana. Carlos mwenyewe alipanga kwenda ama Stontown ya Unguja, Visiwani Zanzibar ama Malindi ya Mombasa, nchini Kenya. Lakini pia alijiuliza Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, itakuwaje.

Hakuwa tayari kuwaacha vijana wake, lakini agizo la Pablo Emilio ni lazima wateketee, alionekana kuwathamini, kuanzia wasambaza dawa za kulevya na kundi la watakatishaji wa noti bandia. Ukweli ni kwamba aliagizwa na wakubwa kuwatosa katikati ya bahari na kutokomea kabisa.

"Tumefanya makosa makubwa kuruhusu hali hii. Kutoroka kwa Teacher na wenzake ni changammoto kubwa kwetu, niseme kuwa kazi kubwa iko mbele yetu, nani kati yetu amewahi kumuona nyati aliyejeruhiwa?" Carlos alihoji.

"Ni hatari, nyati anapojeruhiwa haangalii Simba wala Chui, usicheze kabisa na Nyati aliyejeruhiwa, anatwanga kila kilicho mbele yake, miti, mawe", Jakina alieleza.

"Sasa hiyo ndiyo changamoto iliyo mbele yetu. Nyati aliyejeruhiwa ni hatari zaidi ya Chui, ndiyo maana nimeamua tuhame Dar es Salaam kwa muda, upepo mbaya ukipita tutarudi, sawa jamani", Carlos alieleza.

"Sawa bosi, kama tunaihama Dar es Salaam, tunakwenda wapi?" Hawa Msimbazi alihoji. 

"Tunakwenda kuanzisha makazi mapya na maisha mapya kwa muda. Kuhama sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni jambo la kawaida. Ndiyo maana nikasema tunaanzisha makazi mapya na maisha mapya, nawaahidi kuishi maisha mazuri zaidi huko. Kama nilivyosema huu ni upepo, ukipita tutarejea", Carlos alieleza.

"Tuko pamoja nawe bosi Carlos, kila neno lako kwetu ni sheria. hiki ni kikosi chenye nguvu kubwa zaidi ya vikosi vya jeshi. Hata majeshi ya Marekani huhamisha kambi, kama ni silaha tunazo za kisasa na kila aina". alisema Jakina kwa kujiamini.

Carlos akainua simu yake ya mkononi. "Hallo Sweety wangu, uko wapi baby?. Wakati wa safari umewadia", Carlos aliuliza.

"Oh baby, bado niko saloon baby wangu, natengeneza nywele, si umesema tunaihama Dar es Salaam leo?. Nipendeze kwanza", Sweety alijibu kwa sauti ya nyepesi ya mahaba. 

"Tumebakiwa na nusu saa tu kuihama Dar es Salaam, mwambie huyo msusi aongeze bidii, usiniangushe Sweety wangu". Carlos aliagiza.

"Nimemwambia ajitahidi baby".

"Uko pande zipi?"

"Maeneo ya Riverside saloon ya rafiki yangu".

"Ok, sasa nisikilize Sweety wangu, ukimaliza tafuta taksi, mwambie dereva akulete Kunduchi Beach Hoteli, ukifika hapo nijulishe nitakupa maelekezo, usiingie ndani ya hoteli".

"Asante baby, nitajitahidi kuwahi".

"Ok", akamaliza.  

*************************

Ilikuwa saa nane na dakika ishirini hivi nilipoegesha gari kwenye maegesho ya kituo cha mafuta cha GAPCO kando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi huku tukiangalia barabara iendayo nyumbani kwa Carlos Dimera, Peter na Mama Feka walikuwa wametudokeza kuwa Carlos alikuwa akifanya maandalizi mwisho kwa ajili ya kutoroka. Tulisubiri waanze safari hapo saa nane na nusu kama tulivyoelezwa. Gari la Carlos aina ya BMW nyeusi lilikuwa nje kabisa ya geti na kutufanya tuamini kuwa yupo.

Magari kwenye barabara hii yalikuwa mengi kiasi. Kwenye kituo cha Mafuta cha GAPCO, niliegesha gari sehemu ambayo tuliweza kuona vizuri mwanzo na mwisho mwa barabara hii. 

Ilipofika saa sane na nusu kamili, lango la  nyumba hiyo lifunguliwa, gari moja ndogo rangi nyekundu Pick Up aina ya Isuzu Deep ilitoka ndani taratibu na kuegeshwa mbele ya gari lililokuwa nje. Jakina alikuwa wa kwanza kutoka ndani akiwa amevalia suti nyeusi. Roho yangu ilianza kuingiwa na hofu, nikajua mapambano na vibaraka hawa yameanza. Dakika chache zikapita, Carlos naye akiwa amevalia suti ya aina kama ile alitoka, wote wawili waliingia ndani ya gari iliyokuwa nje. Jakina aliingia upande wa dereva. Carlos akakaa kwenye viti vya nyuma.

Niliinua simu yangu ya mkononi kuwasiliana na Kanali Emilly, "Kamanda, ndiyo tunaelekea kwenye uwanja wa mapambano, uwe tayari tukikuhitaji ufike kwa wakati, ukituona tena ujuwe tumerudi na ushindi, usipotuone basi, ujuwe makubwa yametupata".

""Nimeacha kazi zote kwa ajili ya jambo hili, Teacher kama nilivyosema tulipokutana, Mungu yuko upande wetu, unajua kwa nini?. Kwa sababu tunapigania haki ya wengi". Kanali Emilly alieleza, kabla hajaendelea nikakata simu.

Magari haya mawili yaliondoka taratibu, gari la mbele lilipokuwa hatua chache kabla ya kufika kwenye barabara kubwa ya Ali Hassan Mwinyi lilisimama na kulifanya gari la nyuma pia kusimama. Vijana wawili walioshiba sawa sawa walishuka juu ya miti wakaingia ndani ya gari la mbele safari ikaanza.

Watu waliokuwa eneo hilo walishangazwa na tukio hilo, lakini sisi tulijua hiyo ni mojawapo ya kazi za majasusi.  Tulisubiri mpaka wafike kwenye makutano ya Ali Hassan Mwinyi ama Old Bagamoyo na Kawawa, tukaanza kuwafuata kwa nyuma. Unapowafuata watu wa aina hii lazima ujipange sawasawa, vinginevyo itakula kwako. Tuliwafuata kwa siri, walipofika kwenye taa za usalama barabarani za Morocco walichepuka na kuingia barabara iendayo Kawe.

Mchana huu magari yalikuwa mengi kwenye barabara hii, kiasi kwamba haikuwa rahisi mtu kubaini kama anafuatwa. Baada ya mwendo wa kilomita nne ama tano hivi wakaufikia mzunguko unaogawa barabara zinachepuka moja kwenda Kawe na ile ya Mbezi Beach, gari lao lilipunguza mwendo sana, nadhani walifanya hivi kwa kusudi maalum. Walipovuka kwenye mzunguko huu mbele kidogo walisimama. Mtu mmoja aliibuka akitokea kwenye uchochoro, akazungumza na Carlos. Mimi niliwapita kama siwajui nikasimama mbele ya mtu anayeuza mamatunda  kwenye baiskeli. Dakika chache baadaye magari hayo yalitupita tukasubiri kidogo halafu tukaanza kuyafuatana tena.

Tuliendelea kuwafuata kwa makini hadi walipofika kwenye mzunguko mwingine unaogawa barabara tatu, iendayo White Sends Hoteli na Africana. Magari bado yalikuwa mengi kwenye barabara hii, wakati huo mimi nilikuwa nikiendesha gari ndogo aina ya Golf VW Combi iliyoonekana kuchoka kidogo, waliiacha barabara ya kulia inayokwenda White Sends hoteli, wakaifuata inayokwenda Afrikana. 

Tuliendelea kuyafuata magari haya kwa umakini wa hali ya juu sana, walipofika njia panda ya Africana waliingia kulia, wakaendelea na barabara ya Tegeta. Tuliendelea kuwafuata hivyo hivyo. Walipofika kwenye makutano ya barabara iendayo Kunduchi, Salasala na Tegeta, eneo la Mtongani, walipunguza mwendo halafu yakachepuka na kuingia tena barabara ya kulia, nami pia nikaingia kwenye barabara hiyo. Baada ya mwendo wa dakika chache, dereva wa gari la mbele alionyesha ishala ya taa kuwa wanaingia kulia.

"Sasa nimeelewa, wanakwenda Kunduchi Beach hawa. hakuna sababu ya kuwafuata tena", niliwajulisha wenzangu ambao waliokuwa kimya wakijitafakari. Halafu nikawasiliana na Twite. "Mko wapi Peter na vipi hali ya usalama huko?".

"Mipango inakwenda vizuri bosi, kama tulivyokujulisha Carlos amepiga simu kwa mara nyingine akimwambia Mama Feka ajitahidi kuwahi ili safari yao ianze, sisi tuko sehemu tunasubiri mjipange kwanza, halafu Mama Feka anachukua taksi kama alivyoelekezwa na Carlos, bahati nzuri ni kwamba eneo hilo nalifahamu kiasi, ukiiacha Kunduchi Beach Hoteli, mbele kidogo kuna wafanyabiashara wa samaki wengi sana", Twite alinijulisha.

"Mwambie Mama Feka avae ile fulana ya bletprof niliyompa, wakati wowote kazi inaanza, mwambie karibu tunaingia kwenye hatari kubwa zaidi, kuna magari mawili yanaelekea hapo, sisi sasa tunasubiri taarifa kutoka kwako".

"Taarifa kama nilivyokudokeza kuwa eneo hilo kuna wavuvi, vijana wetu Wilson na Edger tayari wako huko kama wachuuzi wa samaki, wanasema ulinzi ni mkali sana kila gari ama mtu anayeelekea huko anachunguzwa, bahati nzuri leo wageni wengi wanaokwenda Kunduchi Beach Hoteli, Wilson anasema mnaweza kuegesha gari kwenye maegesho ya hoteli halafu mkajua cha kufanya."

"Umesomeka Peter," nilisema halafu nikawageukia wenzangu, "Jamani, Peter anasema Wilson na Edger wako kwenye pointi. Vijana hawa wanasema ulinzi ni mkali sana eneo hilo, Sisi tutaingia Kunduchi Beach Hoteli, halafu tutatafuta njia zandani kwa ndani, hata ikibidi kuvunja milango na madirisha vita si mchezo", niliwajulisha wenzangu.

"Iwe isiwe, leo lazima kieleweke, Teacher tusiwape nafasi tena watu hawa ama zao ama zetu", Claud alisema.

"Nina usongo na watu hawa, walivyotutesa pale Karakana ya Tazara, ole wao waingie kwenye anga zetu", Nyawaminza nae alisema.

"Sikilizeni, tunakwenda kuuza roho zetu, lolote laweza kutokea, lazima tujipange sawasawa kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Fred utabaki sehemu hii kama akiba yetu, ukiona kimya utajua cha kufanya, pia wasiliana na Kanali Emilly, mwambie asogee eneo hili. Nyingi wengine twendeni kwenye uwanja wa vita", niliagiza.

"Tuko pamoja", Fred alisema.

Baada ya kujipanga vizuri, tulikubaliana na wenzangu kuwa tuliache gari letu kwenye maegesho ya magari ya Chuo cha Maofisa wa jeshi pale Kunduchi, tulikubaliana nianze kuondoka, ili wao wafuate. nilitafuta taksi iliyoniacha Kubnduchi Hoteli. Mkoba wangu mdogo uliosheheni vifaa vyangu muhimu vya kazi ukiwa begani nilitembea taratibu nikitafuta sehemu ya vyoo vya upande wa mashariki, nilipovipata niliingia na kujimwagia maji kiasi, halafu nikafumua sehemu ndogo ya juu ya paa nikapanda na kuangalia eneo lote la bahari.

Hali ya eneo hili ilikuwa tulivu kabisa, kwa mbali ndani ya bahari kulikuwa na meli kubwa na ndogo zimeegeshwa katikati ya bahari, bila shaka zinazosubiri kushusha mizigo bandarini, baada ya kujuiridhisha kuwa hali ni salama nilipenya kwenye tundu hili na kushuka upande wa pili kwa tahadhali kubwa. Claud na Nyawaminza nao wakitumia njia hiyo, wote watatu tukafanikiwa kuruka kiunzi hiki salama.  

Ndani ya dakika kumi, tayari tulikuwa tumelizunguka eneo lote la bahari. Boti iendayo kasi ilikuwa imeegeshwa ufukweni ikisubiri kuondoka, ilikuwa boti kubwa ya injini mbili, yele magari na mengine kadhaa yalikuwa yameegeshwa kwa mbali kidogo na boti, "Mwambie Mama Feka anaweza kuja sasa", nilimwambia Peter.

"Kuko salama?".

"Ndiyo maana nikasema anaweza kuja", nilimwambia.  

"Nafikiri wote tumeona ulinzi ulivyo. Kitu ninachotaka ni kufanya mashambulizi kimya kwanza mpaka tutakapolazimika kuwashambuliwa walioko ndani ya boti. Walinzi sita wanaonekana upande huu. Mimi nitapita kushoto, Nyinyi mtashambulia upande wa kulia. Nawatakia heri".

Tulipeana mikono kimya kimya kwani hatukujua nini kitatokea. Mimi nilikuwa wa kwanza kujitokeza kwenye kimsitu nikabana kama hatua tatu hivi kulikuwa na mlinzi anavuta sigara, mikononi ameshika bunduki kubwa aina ya AKA 47 huku akiangalia kwenye magari. Sikuona sababu ya kutoa silaha, nilimsogelea kimya kimya nikitembelea tumbo. Nilipokuwa karibu kabisa niliibukia na kuziba midomo, akataka kupiga kelele lakini mimi nilikuwa mwepesi zaidi nikazima kelele zake kwa kumnyonga. 

Tulikuwa tumekwenda haraka sana, Claud alinyoosha mkono wake wa kulia na kunionyesha ishala kuwa hali ilikuwa shwari. wao walipita wakajibanza kwenye mapango ya mawe ya bahari, mimi nikaendelea kutumia miti kuwasogelea tukiona kila kinachotendeka. 

Mlinzi mwingine alikuwa hatua kumi hivi lakini hakujua nini kimetokea. Kwa vile nilikuwa nimevaa mavazi ya mtu niliyemuua mwanzo alifikiri mimi ni mwenzao hivyo nilimfuata nikiangalia chini kama mmoja wao mpaka nilipomfikia.  

"Vipi kuna wasiwasi wote?", nilimwuliza.

Aliinua kichwa.

"Hakuna....."

Kabla hajamaliza nilimkata karate ya katikati ya kichwa akafa palepale. Nilimwegemeza vizuri kwenye mti nikamwacha kama mtu aliyekaa hai. Claud na Nyawaminza nao walikuwa wamekwenda kasi wakiwa wameua walinzi kadhaa.

Tulikuwa tumefanikiwa kuizingira boti hii kutoka kila upande. Mara nikamuona Mama Feka anawasili katika eneo hili, akitembea taratibu kuelekea kwenye boti. Kama ilivyo kawaida Jakina alitoka ndani ya boti ili kumpokea.

Karibu yangu niliweza kuaona walinzi wawili wakilanda huku na huku, nikaanza kuwanyatia. Kabla sijawafikia nilisikia mlio wa risasi upande wa akina Nyawaminza. Nikajua mambo yametibuka. Nami nikainua bunduki AK 47 niliyoichukua kwao na kuanza kuwateketeza walinzi waliokuwa karibu yangu. Kwa kuwa vita vilikuwa vimeanza rasmi nilikimbia nikirusha risasi bila mpangilio.

Hali ya hewa katika eneo hili ilikuwa imechafuka, kumbe kulikuwa na askari wengi ufukweni, sijui hata walitokea wapi tukaanza kupambana, milio ya risasi iliendelea kusikika. Hali hii ilimfanya Mama Feka akimbie kurudi upande wa magari.

Tuliendelea kupambana na watu hawa kishujaa. Mara nikaona askari wawili wakianguka kutoka juu ya miti, bunduki zao zikiwa mikononi. Kumbe walikusudia kunirushia risasi, wakati wanajiandaa kufanya hivyo Claud, alikwisha kuwaona hivyo akawaua kabla hawajanimaliza.

Nilisikia injini za boti zikiwashwa, nikajuwa wanataka kuondoka, nikamfanyia ishara Claud akaiona na yeye akanifanyia ishara ya kuonyesha kuwa Nyawaminza alikuwa chini ya maji anajaribu kuingia ndani boti. Kuona hivyo nilimfanyia ishara kuwa na mimi nakwenda ndani ya boti hivyo atuchunge wote. Tulikuwa tumeuwa idadi kubwa ya askari waliokuwa wamebaki ni wachache tu.

Niliruka chini huku nikiachia risasi ovyo nikafika kwenye boti. Nilikajitupa kwenye mlango na kujiviringisha mpaka ndani, kama umeme nikarukia na kumpiga risasi nahodha wa boti hii aliyekwa kwenye injini akaanguka ndani ya maji. Huko nje nilisikia bado Claud anaendelea kumimina risasi ili kuwazuia walioko ndani wasitoke nje.

Nilipoinuka niliona kama wamebaki kumi tu ndani; wengine wote tulikuwa tumewateketeza. Nilimwona Nyawaminza nae anaviringisha na kuingia ndani. Wale watu walimwona na kabla hawajapiga risasi niliwahi wawili, wengine wote wakarudi kujificha nyuma.

Nyawaminza aliruka mpaka nilipokuwa.

"Asante bosi umeniponya",

"Usinishukru ndio sababu tuko wote. Kwanza kazi uliyoifanya wewe na Claud sikuitegemea. Kazi imekuwa rahis kabisa".

"Kuna watu kama wangapi humu ndani?".

"Hawazidi kumi, na wote wako upande huu wamejificha. Nafikiri wanamlinda Carlos Dimera".

Huko nje kulikuwa kimya; Tukajua Claud anasubiri sasa kashi kashi kutoka kwetu.

"Sikiliza Nyawaminza, lazima tuwafanyie ujanja ili tuwapunguze. Mimi nitasimama juu ili niwadanganye. Walivyo wajinga watainuka ili wanipige risasi. Mimi nikiita jina kaa tayari na silaha yako kisha anza kumimina risasi. Mimi nitaruka kitambo, hivyo utawapata kama mchezo. usiogope".

Niliinuka kama umeme nikawaona wote mara moja.

Nikaita 

"Carlos Dimera?".

Hapo hapo kama umeme nikaruka nyuma ya upande mwingine. Walinzi wanne wainuka ili kunitupia risasi huku wakiwa wamejitokeza hadi vifua. Nyawaminza aliwamiminia risasi na kuwashindilia wote risasi katikati ya vifua vyao wakafa pale pale. Nilimwonyesha ya vidole kuwa wamebaki watatu, kwani nilipokuwa nimeruka niliona wako saba. 

"Teacher, nilisikia sauti ya Carlos anaita.

"Unasemaje?", nilimwuliza.

"Naomba tuzungumze".

"Kuhusu nini tena Carlos, lazima ujuwe kuwa Tanzania haiko tayari kuchezewa, biashara ya dawa za kulevya peleka huko kwenu kusiko na maadili mema katika jamii, watu wanavaa nguo fupi, wanaume wanaoana, hizo imani zibaki kwenu", nilimwambia. 

"Tafadhali tuzungumze?", aliomba kwa mara nyingine.

"Umechelewa sana Carlos, maana umeigharimu nchi hii, hivyo tutakupeleka mbele ya vyombo vya sheria ndivyo vitakavyo kuhukumu, umeua ndugu zetu wengi, umesababisha vijana wetu kujiingiza katika matumizi ya dawa haramu za kulevya, hufai kuonewa huruma".

"Huwezi kunichukua hapa nikiwa hai".

Kumbe wakati huu tunajibishana Mzee wa Mtemba naye na askari wao mwingine nao walikuwa wamejivuta karibu kabisa na mimi. Ghafla nikahisi kuna kitu karibu nami.

"Teacher", Nyawaminza aliita ambaye pia alikuwa amewaona.

Kusikia tu hivyo, niliruka pale nilipokuwa na wakati huo nikawaona Mzee wa Mtemba na yule kijana mwingine karibu kabisa na mimi wameinua bastola tayari kufyatua. Nilijiviringisha hewani namna ambayo hata wao walishangaa risasi zao zote zikanikosa, wakati ule ule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao wakaanguka chini. 

Carlos aliinuka akasimama juu, akachukua bastola akataka kujipiga risasi. Bunduki tatu zililia kwa wakati mmoja na kuupiga mkono wake. Kumbe Claud nae alikuwa amefika mlangoni na kuona kitendo alichotaka kukifanya akakizuia. Nyawaminza nae aliona akazuia wakati na mimi niliona nikazuia asijipige risasi.

"Bado tunakutaka ukiwa hai ili ukajibu maswali ya watanzania", nilimwambia huku bado anashangaa jinsi risasi tatu zikitoka pande tofauti zilivyoweza kupiga kiganja chake tu.

Mara tunasikia kelele za milio ya magari ya polisi. 

"Kanali Emilly yuko njiani", niliwaambia wenzangu ambao sasa tulikuwa tumemzunguka Carlos.

Baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa saa kadhaa, tukibishana kwa risasi na watu hawa, hatmaye tulifanikiwa kuiteka boti hii, Carlos Dimera, Hawa Msimbazi, Jakina, Mzee wa Mtemba na baadhi ya masalia ya askari wao walijisalimisha mbele yetu.

Mama Feka alikuja na kunikumbatia, "Hongera sana Teacher, kazi yenu mliyonituma nimeimaliza", alisema huku akinibusu na kujiegemeza kwenye kifua changu, nikambusu pia. carlos Dimera na wenzake wakabaki wameduwaa.

"Mnamfahamu malkia huyu, anaitwa Sweety, bila huyu kazi ya kuwakamata ingekuwa ngumu, asante sana Mama Feka", nilisema.

Kanali Emilly alifika akiwa na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu Serikalini, Mawaziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani, pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo. Kanali Emilly alitushika mikono na kutuangalia sehemu mbali mbali za miili yetu kama tumepatwa na majeraha. Tulikuwa salama kabisa.

"Wakuu, boti hiyo imebeba vifaa vyote vya hujuma, kuanzia dawa za kulevya, vifaa vilivyotumika kutengeneza noti bandia na baadhi ya silaha za vita ambazo hatujui ziliingiaje hapa nchini", nilieleza kwa uchungu.

Baada ya taratibu zote kufanyika, askari kutoka idara zote tuliwaacha wazee waendelee na mambo yao sisi tukaondoka kishujaa.

MWISHO

Comments

  1. hatimae imekwisha,asante kwa kutujali,tuletee kikosi cha kisasi,ombi usiwe unachelewa sana angalau iwe mara 1 kwa wiki

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU