TUNDU LISSU AHOJIWA POLISI

MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki, (Pichani), Tundu Lissu (CHADEMA), ameitwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam leo na kuhojiwa kuhusu uhalali wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika wiki iliyopita na kuhusu kupotea kwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, Bw.Ben Saanane. 

Akizungumza baada ya kuwepo taarifa za kukamatwa kwake, Lissu amesema: “’Sijakamatwa ila nimeitwa leo saa mbili asubuhi, nimefika Polisi saa nne, nimekaa hadi muda wa saa 10.15, nimehojiwa mambo mawili.’’ Amesema Lisu na kuongeza kuwa amehojiwa kuhusu kauli aliyoitoa kwenye mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopita akituhumiwa kutoa kauli ya uchochezi kuwa watu waliokamatwa sehemu mbalimbali na kuletwa Dar es Salaam hufungiwa Mikocheni na kuteswa. 

Amesema jambo la pili ni kuhojiwa kama shahidi kana kwamba ana taarifa zozote kuhusu kupotea kwa Saanane na baada ya mahojiano walimwacha wakimweleza kuwa endapo wakimhitaji watamwita tena. 

Awali kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Lissu alisema Chadema haijui aliko Saanane na kuiomba Serikali ieleze mahali alipo kwani ina jukumu la kulinda raia na mali zao. "Chadema haijui aliko Saanane, haonekani kokote, katika mazingira haya ni vema Serikali ikaeleza kama vyombo vya ulinzi vinamshikilia au kama havijamkamata,

Amezitaka Mamlaka husika za mawasiliano zieleze mara ya mwisho alifanya mawasiliano lini, wapi na nani maana ndio wenye uwezo wa kuamuru mashirika ya mawasiliano kusema. 

Lissu amesema wiki mbili kabla ya kupotea kwa Saanane baada ya kuandika katika mitandao ya kijamii akihoji uhalali wa shahada ya tatu ya Rais John Magufuli, ndipo alipopokea vitisho. Alisema hatua hiyo ilikuja baada ya Rais kuanzisha mchakato wa uhakiki wa vyeti kwa watumishi ambapo yeye aliliendeleza kwenye mitandao ya kijamii.

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU