KIKOSI CHA KISASI

SURA YA TANO

MWANZO WA MAPAMBANO

Yule kijana alipoangalia usoni mwa Willy mara moja alijua huyu mtu hakuwa na mzaha. Hivi akiwa mikono yake ikiwa imeshika kwenye usukani wa gari na mwili wake mzima akiwa amekauka kama mti uliopigwa radi alimjibu Willy, "Tafadhali niache, mimi ni Robert Sikawa."

"Nitajuaje kama wewe ni Robert Sikawa?" Aliuliza Willy hali uso wake ukiwa bado mzito.

"Maana wewe ni Willy Gamba, kiongozi wa 'Kikosi cha Kisasi' kwa kifupi KK, ambacho makao yake makuu yako Lusaka..."

"Oke, siku nyingine ujiangalie unaweza kupatwa na matatizo bure. Vile vile unapofuata mtu, inabidi ufunye vizuri kuliko ulivyofanya hasa unapofuata mtu mwenye ujuzi katika mchezo wetu huu," Willy alimweleza Robert huku akiwa ameisharudisha bastola yake na tayari uso wake ukiwa unaonyesha urafiki, na vile vile akiwa amempa nafasi Robert kutoka ndani ya gari na kusimama wote nje ya gari la Robert.

"Ama kweli ndiyo sababu umechaguliwa kuongoza 'KK'", alieleza Sikawa. "Mimi nilishangaa nilipoambiwa inabidi nichukue amri toka kwako tangu wakati utakapofika, maana mimi mwenyewe najiamini sana. Hivi sikuona kwanini tena aje mtu nichukue amri kutoka kwake badala yake yeye kuchukua amri kwangu. Hivi nilikuwa uwanja wa ndege kukupokea na vile vile kukujaribu una ujuzi kiasi gani. Jaribio langu dogo hili linanidhihirishia kuwa kweli wewe ni mjuzi katika mchezo wetu huu, maana mimi ninapomfuata mtu huwa ni vigumu sana kunigundua. Kule kwetu Lusaka katika idara yetu huwa wananiita 'Nyoka wa kijani' sababu hii hii. Hivyo bosi wangu ninakukaribisha mjini Kinshasa," alieleza Robert.

"Ulijuaje kama ninakuja?".

"Chifu wako alinitumia habari jana pamoja na picha yako ambayo ingeweza kunifanya nikutambue".

"Picha, bado unayo?"

"Ndiyo".

"Tafadhali itatue sasa hivi. Si vizuri kiusalama mpelelezi kutembea na picha ya mpelelezi mwenziwe, kitu anachobidi kufanya ni kuhakikisha kuwa anaangalia picha mara moja na kuiweka sura yake ndani ya kichwa chake kisha anaitatua hiyo picha hapo hapo", Willy alimshauri.

"Vizuri", alijibu Robert huku akitoa picha ya Willy ndani ya mfuko wa koti lake na kuwasha kibiriti na kuichoma hiyo picha pale pale.

"Utafikia hoteli gani?", aliuliza Robert.  

"Nafikiri Memling Hoteli itanifaa".

"Yaa, hoteli hiyo ni tulivu itakufaa. Sijui tuonane muda gani ili niweze kukupa habari nilizonazo kikamilifu?"

"Tuonane jioni saa mbili hivi na kuendelea, maana sasa hivi itabidi nipumzike kidogo".

"Sawa basi tuonane Vatcan Klabu huko Matonge saa hizo.

"Sijui unaifahamu?".

"Hamna taabu, naifahamu." Alijibu Willy.

"Oke basi tuonane huko saa hizi".

"Oke Robert, asante sana, tutaonana", alijibu Willy huku akiondoka na kuelekea kwenye gari lake. Robert alibaki amesimama pale penye gari lake akimwangalia Willy kwa shauku.

Willy alipanda gari lake akalitia moto na kuondoka kuelekea Memling Hoteli. Alipofika Memling Hoteli alikuta kuna nafasi.

"Karibu," alikaribishwa na mfanyakazi mmoja msichana aliyemkuta hapo kwenye mapokezi ya hoteli hii.

"Naweza kupata chumba?", aliuliza Willy.

"Bila shaka, unakaribishwa kwa dhati. Una mzigo?".

"Nina mkoba mmoja uko ndani ya gari".

Yule msichana alimwita mchukuzi ili akachukue ule mzigo.

"Acha tu nitakwenda kuuchukua mwenyewe", Willy alieleza huku akienda kwenye gari.

"Tunavyo vyumba wazi kwenye ghorofa ya pili, tatu na tano, sijui ungependelea ghorofa ipi?", yule msichana alimuuliza Willy, aliporudi na mkoba wake.

"Wewe unafikiri ghorofa ipi ni nzuri?".

"Hii inategemea na uchaguzi wa kila mtu binafsi".

"Uchaguzi wako ndiyo utakuwa wangu", Willy alimwambia yule msichana huku akimtolea bonge la tabasamu.

"Chumba nambari 240 kwenye ghorofa ya pili kitakufaa," yule msichana alimjibu Willy naye akitoa tabasamu.

"Asante sana, hicho hicho chumba kitanifaa." Willy alijaza fomu kama ilivyo desturi, kisha akapelekwa na askari wa hoteli mpaka chumbani kwake. Chumba alichokuwa amepewa kilikuwa kwenye sehemu nzuri sana na chumba chenyewe kilikuwa kimepangwa na kuwekwa vyombo vizuri saana. Askari alipokuwa amekwishaondoka, Willy alianza kukipekua kile chumba, na kukikuta salama. Alipokwisha kufanya hivyo alifungua mkoba wake na kuanza kupanga vitu vyake. Alipomaliza alienda akaoga kisha akatelemka chini kwenda kupata chakula cha mchana. Alipomaliza kula alipita pale kwa yule msichana wa mapokezi. 

"Haya kisura bado unaendelea na kazi!" 

"Ndiyo, heri nyinyi wenye bahati ya kutembea nchi mbali mbali na kustarehe. Sijui lini mimi nitapata nafasi kama hii!", alijibu yule msichana kwa masikitiko.

"Siku ipo itafika usiwe na shaka, ya Mungu mengi sana. Fanya kazi yako kwa bidii, tumia mapato yako kwa mpango, huku ukiweka akiba kwa ajili ya safari kama hii, ukifanya hivi nina imani siku moja ndoto zako za kutembea nchi mbali mbali zitakuja kweli," alimshauri Willy.

"Ndivyo wewe ulivyofanya?" Yule msichana alimuuliza.

"Lazima, hamna dawa nyingine," alijibu Willy huku akitoa pesa ili kubadilisha kutoka kwenye dola ili apate Zaire. Msichana yule alipombadilishia pesa zake, Willy alitoa Zaire kumi akampatia yule msichana.

"Za nini?" Yule msichana alimuuliza.

"Asante yako kwa kunipokea vizuri. Wewe unaitwa nani?"

"Naitwa Mwadi," yule msichana alisema huku akionekana kuwa na mshangao.

"Jina zuri 'Mwadi', haya asnate Mwadi tutaonana jioni".

"Jioni nitakuwa nimeishamaliza kazi, namaliza saa tisa mchana, hivi nitakuwa nyumbani."

"Basi tutaonana kesho,"

"Haya asante," alijibu Mwadi, huku akimwangalia Willy kwa macho malegevu. Willy alipoondoka alimwacha yule msichana moyo wake unapiga haraka haraka. Maishani mwake alikuwa ameishaona wavulana wengi sana, hasa ukitilia maanani kazi yake hii, lakini alikuwa hajaonana na mvulana mwenye kusisimua kama huyu. Pale pale alijawa na moyo wa kimapenzi juu ya Willy.

Willy naye alienda chumbani kwake na kupumzika.

ITAENDELEA 0784296253


Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru