KIKOSI CHA KISASI

MWANZO WA MAPAMBANO 

SEHEMU YA TANO
IV

Asubuhi yake Willy alipoamka alikuwa mchovu sana, maana usiku ule alikunywa pombe za kutosha, kwani walikaa Vatcan mpaka saa saba za usiku huku wakinywa na kucheza dansi. Alipoangalia saa yake alikuta ni saa moja unusu, basi aliamka na kuelekea maliwatoni. Baada ya kukoga, alinyoa ndevu, kisha akavaa vizuri kabisa na kuonekana mtu wa amani, tayari kamili kwa shughuli za siku hiyo. Kisha alitelemka chini ili kuwahi chemsha kinywa. Alipokuwa anapita pale mapokezi alimwona Mwadi tayari yuko kazini, hivi aliamua kumsabahi.

"Hallo Mwadi, Sango nini?", alimsabahi kwa kilingala kiutani. Mwadi ambaye alikuwa akishughulika na kujaza rejesta ya wageni aliinua kichwa na kumwona Willy, alipomuona tu mwili wake ukasisimka.

"Ohoo Willy malamu", alimjibu huku akiwa amemjengea tabasamu kubwa. Willy alirudisha tabasamu hilo na kuendelea zake kwenda kwenye chumba cha chakua.

Baada ya kustafutahi, Willy alirudi chumbani mwake, akajitayarisha tayari kwa kwenda kwenye mazishi.

Ilikuwa saa tatu kamili alipotoka hotelini kwake kuelekea mazishini. Alipopita pale mapokezi alimkuta Mwadi akiwa na shughuli nyingi hivi alienda akapanda gari lake na kuondoka. Robert alikuwa amemwambia kuwa mazishi yatafanyika kwenye makaburi yaliyoko mtaa wa 30 Juin. Alipofika kwenye makaburi haya alikuta watu wamejazana kibao. Alirudi nyuma na kuegesha gari lake kwenye maegesho ya jengo liitwalo INSS. Alipomaliza kufunga milango alirudi na kuja kungojea maiti pamoja na wananchi wengine.

Kusema kweli mazishi haya yalikuwa yametayarishwa kitaifa. Kulikuwa na gwaride la askari wa jeshi la Zaire, wakiwa tayari kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu huyu ambaye alikuwa mwanamapinduzi imara wa Afrika. Ilipokaribia saa nne, watu wenye vyeo vikubwa wakiwa mawaziri, mabalozi na viongozi wengine wa serikali waliwasili. Saa nne kamili ndipo maiti ya marehemu ilipofika. na pale pale bendi ya jeshi ikaanza kupiga wimbo wa kimapinduzi ambao uliwafanya maelfu ya wananchi waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu wakitokwa na machozi. Mkuu wa majeshi ndiye aliongoza mazishi haya ambayo hayatasahaurika katika historia ya mjini Kinshasa. 


Uchungu huu uliwapata hawa wananchi wa kawaida mpaka wale watu wa vyeo vya juu waliohudhuria mazishi haya, ndiyo uchungu ule ule uliompata Willy. Kwani mtoto mmoja aliyekuwa amesimama karibu na Willy alimuuliza, "Mzee kama mtu huyu alikuwa anapendwa na watu wote hivi kwanini wamemuua", Willy alimwangalia mtoto huyu asiyezidi umri wa miaka nane akajibu, "Mtu hakosi adui, unaweza kupendwa na watu maelfu lakini ukachukiwa na mtu mmoja tu".

"Kama ndio hivyo kwanini watu wengi hawa wasimpate mtu huyo na kumuua? Maana mama ameniambia asubuhi eti mtu aliyemuua hawamjui!"

"Tutamtafuta tukimpata tutamuua vile vile", alijibu Willy huku akizidi kupandwa na uchungu."

"Kweli, ukimpata ukamuua nitafurahi." Yule kijana alijibu. Mtoto huyu alimzidishia mawazo Willy hivi akaamua kutoka pale na wazo moja.

Ampate huyu muuaji wa Mongo, amuue ili watoto wa Afrika waweze kufurahi na kuzidisha mapambano dhidi ya wapinga maendeleo. Kwa sababu watu walikuwa wengi sana aliona kuwa asingeweza kuona jambo lolote la maana hivi akaamua kurudi hotelini kwake ili akajitayarishe kwenda kuwapokea akina Ozu.

Alipofika hotelini alimkuta Mwadi akiwa peke yake.

"Hallo Willy, ulitoka saa ngapi? Maana sikukuona wakati ukitoka".

"Wakati ninatoka ulikuwa na shughuli nyingi usingeweza kuniona", alijibu Willy huku kwa mara ya kwanza tangu amuone Mwadi alianza kutambua kuwa msichana huyu alikuwa na kitu fulani ambacho kilikuwa kinagusa moyo wake. Si kwamba Mwadi alikuwa msichana mzuri sana la hasha, alikuwa msichana mzuri kiasi cha kawaida tu, lakini kitu hiki alichokuwa nacho kilichokuwa kikigusa moyo wa Willy, kilimfanya Willy aamue kuwa karibu na msichana huyu ili aweze kukijua ni kitu gani hiki.

"Ulishawahi kufika Kinshasa au hii ni mara yako ya kwanza?", Mwadi aliuliza.

"Nilishawahi kufika ingawaje sikukaa sana". Alijibu  Willy. "Ahaa..." Mwadi alionekana anataka kusema kitu, halafu akasita.

"Leo unatoka saa ngapi?". Aliuliza Willy. Huku macho yake yakitoa mwanga wa kuonyesha furaha ya kuulizwa swali hili Mwadi alijibu, "Kama jana tu, nitaondoka saa tisa na kuingia tena kesho asubuhi saa moja".

"Una muda mwingi sana wa kupumzika", alisema Willy halafu akatania, "Sijui nani anakusaidia kuusukuma muda wote huo?".

"Aka, sina mtu maalumu anayenisaidia kuusukuma muda wangu. Hata wewe unaweza kusaidia kuusukuma ukitaka!" Alijibu Mwadi kwa sauti ya utani. Willy aliona hapa hapa ndiyo ulikuwa muda wa kuanzisha urafiki na huyu msichana.

"Na kweli kabisa, maana sina msichana wa kusaidia kuusukuma muda wangu hasa ukitilia maanani kuwa mimi niko mapumzikoni ingawaje na kazi".

"Karibu basi nyumbani jioni, nitakupikia 'Maboke'. Umeisha kula maboke ya hapa Kinshasa?". Aliuliza Mwadi.

"Kwanza sijui maboke ni nini", alijibu Willy.
Mwadi aliangua kicheko kisha akasema, "Hii inaonyesha kuwa kweli bado hujaifahamu Kinshasa. Maboke ni chakula kinachopendwa na watu wote hapa mjini, ni samaki na nyama ambayo hupikwa ndani ya majani ya ndizi. Vipi utakuja?".

"Nitakuja", alijibu Willy, "Sijui unakaa wapi?"

"Ninakaa huko Bandalugwa mtaa wa Kimbondo nyumba nambari 79, utapajua?".

"Usiwe na shaka nitakuja, nisubiri saa moja hivi jioni".

"Haya asante, tutaonana saa hizo", alijibu Mwadi kwa moyo wa kuridhika sana, maana alikuwa ameweza kirahisi sana kumpata kijana huyu ambaye alikuwa akimsisimua sana.ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru