KIKOSI CHA KISASI

SEHEMU YA TANO

VI

Wakati ndege hii ya Shirika la Ndege la Nigeria ikitelemka, huko Limete kwenye gereji iitwayo 'Garage du Peuple' aliingia kijana mmoja wa kizungu ambaye alionekana kuwa na wasiwasi sana. 

"Bwana Pierre yupo?", aliuliza.

"Ndiyo yupo. Nenda moja kwa moja ndani". Alimjibu kijana mmoja aliyekuwa mlangoni. Alipofika ndani ya maofisi ya gereji hii, alimwendea msichana mmoja aliyekuwa anapiga mashine na kumweleza. "Nataka kumwona Bwana Pierre."

"Nenda chumba cha tatu toka hiki upande huu huu." Alijibiwa. Alipoingia hiki chumba alikuta kuna wasichana wawili ambao alihisi ni waandishi mahsusi wa Pierre.

"Bwana Pierre yupo." Aliuliza bila hata kuwasabahi.

"Yupo. Unamhitaji kwa jambo gani?". Aliulizwa na msichana mmojawapo.

"Mwambie nimetumwa na wakala."

"Yule msichana aliinua simu na alipokwisha kuzungumza na Pierre alimwambia apite ndani.

"Karibu, lete habari," Pierre aliuliza upesi upesi kijana yule alipoingia. Bila kujibu kitu kijana yule alitoa karatasi ya teleksi na kumpa Pierre. Pierre alipoisoma sura yake ilibadilika akasema, "Haya asante kwa heri", Kwa maneno haya ya mkato yule kijana aliondoka. Pierre aliinua simu na kuanza kupiga yeye mwenyewe moja kwa moja.

"Jean".

"Ndiyo".

"Pierre hapa".

"Ehe".

"Nimepata habari, kutoka Wakala. Wamesema habari kutoka kwa wateja wetu wanasema kuna spea zinawasili hapa toka Nigeria kwa ndege ya shirika la ndege la Nigeria ambayo inaingia sasa hivi tunavyozungumza. Ni spea za aina mbili. Moja ni ndefu kama futi 5inchi 10, nyeusi, imefunikwa kwa suti nyeusi. Nyingine nayo ni ndefu futi 5 inchi 6, maji ya kunde, imefunikwa kwa suti nyeusi vile vile. Spea hizi ni za hatari sana lazima zikaangaliwe zinapelekwa duka gani ili iwe rahisi kuzinunua. Kwa sababu ni za hatari, lazima watu wenye ujuzi wa juu ndio wapelekwe kuzitambua. Umenielewa?"

'Hakuna taabu, tayari nina watu wenye ujuzi wa hali ya juu katika spea huko uwanja wa ndege nitawapasha habari mara moja".

"Wapashe habari mara moja, maana saa zenyewe ni hizi".

"Oke, nitapiga baada ya kuwapasha habari," alijibu Jean na kukata simu.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU