KIKOSI CHA KISASI

SEHEMU YA TANO

VII

Wakati mlango wa ndege unafunguliwa ili abiria wapate kutoka ndani ya ndege, Mtu mmoja ambaye ni mfanyakazi wa Idara ya Uhamiaji ya Zaire alikuwa akipokea simu. Mtu huyu alikuwa kwenye orodha ya mishahara ya 'WP' kwa ajili ya kutoa habari na vile vile kuwa kiungo kati ya ofisi ya 'WP' na wafanyakazi wa 'WP' ambao wanaweza kuwa kiwanjani. Mtu huyu alikuwa akipata maagizo moja kwa moja kutoka kwa Charles wa G.A.D. gereji. Hivi simu hii aliyokuwa ameipokea ilikuwa imetoka kwa Charles ikiwa na maagizo kwa wafanyakazi wawili wa 'WP'ambao walikuwa wamepelekwa hapo uwanja wa ndege ili kuchunguza watu wote waliokuwa wakiingia Zaire kwa njia ya ndege. Baada ya kupata simu hii aliinuka na kupanda ngazi haraka haraka kwenda kwenye sehemu ya kuagia ambapo alijua ndipo Mulumba mmoja wa wafanyakazi wa 'WP' waliokuwa hapo uwanjania alikuwa. Watu walikuwa wengi sana, lakini kwa bahati Mulumba alikuwa amesimama kando kwenye sehemu ambayo mtu alimwona moja kwa moja.

"Mulumba, nina maagizo yako", huyu mtu alimwambia alipofika.

"Nitakuja ofisini kwako," Mulumba alijibu.

"Ni ya haraka sana inatoka kwa Charles." Alimweleza huku akimvuta kando.

"Ehe anasemaje?".Mulumba aliuliza kwa makini.

"Kati ya watu wanaotelemka ndani ya ndege hii, mna wapelelezi wawili mashuhuri wa Afrika.  Mmoja ni mweusi kiasi cha futi 5 inchi kumi kwa urefu amevaa suti nyeusi na mwenzie ni maji ya kunde kiasi cha furi 5 inchi 6 nae amevaa suti nyeusi. Wanatoka Lagos Nigeria. Anasema ni watu ambao hamuwezi kuwakosa, lazima mtawatambua. Vile vile ameonya kuwa ni watu hatari sana hivi msiwafanyie jambo lolote ila tu muwafuatie mjuwe wamefikia wapi na mripoti moja kwa moja kwake. Vile vile lazima mlinde mahali watakapofikia mpaka hapo watu wengine watakapokuja kuchukua nafasi zenu. Amesema kuwa msiwaache wakawapotea hata kidogo hiyo ni amri."

"Oke, hao abiria wanaanza kutoka, nenda kwenye chumba cha kufikia ukamweleze Kasongo yuko huko", Mulumba alieleza.

"Oke, bahati njema", Mulumba alijiweka sawa kwenye nafasi ambayo angeweza kuona vizuri kila abiria anayetelemka bila kujua kwamba hatua tu kwenye jukwa hilo hilo walikuwa wamesimama wapelelezi mashuhuri wa Afrika waliokuwa wamefika kungojea watu wale wale ambao yeye naye alikuwa akiwangojea.

Willy na Robert walikuwa wakiwaangalia abiria waliokuwa wanatelemka kwa makini sana vile vile bila kujua kuwa hatua chache tu kutoka sehemu waliyosimama kulikuwa na mtu wa 'WP' kikundi ambacho ndicho alikuwa hasa ametumwa kuja 
kukitafuta.

"Huyo ni Kofi", Willy alimweleza Robert wakati kijana mmoja aliyevalia suti nyeusi na huku akitembea kifahari alipokuwa akitelemka kutoka katika ndege.

"Ahaa," aliitikia Robert huku akimwangalia Kofi kwa makini ambaye alikuwa akielekea chumba cha kufikia pamoja na abiria wenzake. Ozu ndiye alikuwa mtu wa mwisho kutelemka ndani ya ndege, na mara alipojitokeza tu Willy alimtambua na hata Robert ambaye alikuwa bado hajawahi kumwona alihisi ya kuwa huyo ndiye alikuwa Ozu kutokana na miondoko yake ilivyokuwa.

Mulumba naye alipomwona Ozu naye alihisi mara moja kuwa ni mmojawapo wa watu aliokuwa ameelezwa, ingawaje Kofi alitelemka bila yeye kumtambua. Hivi baada ya kumhisi huyu mtu Mulumba alitelemka upesi upesi ili akambonyeze Kasongo kuwa amemtambua mtu huyu.

"Huyo ndiye Ozu", Willy alimweleza Robert.

"Hata mimi nilihisi ndiye yeye, miondoke na umbo lake la kimwanariadha limemfanya aonekane waziwazi".

"Telemka chini tukawasubiri," alishauri Willy wakaanza kutelemka.

"Mpango utakuwa ka ule uliofanya. Sisi tutabana mahali ambapo mtu yeyote hatatuona na kuwaacha watangulie kuondoka, halafu sisi tutawafuata. Mimi nitatangulia wewe utanifuata nyuma. Kama kutatokea kitu chochote cha kutaka cha kutaka wewe usihusike nitatoa mkono wangu nje na kuuonyesha juu. Nikifanya hivyo nipite moja kwa moja ukanisubiri hotelini. Na kama kuna kitu nataka tusaidiane nitatoa mkono wangu nje na kuuegesha kwenye dirisha, nikifanya hivyo jiweke katika hali ya tahadhari," alishauri tena Willy.

"Kwani unadhani kitu chochote kinaweza kutokea?". Aliuliza Robert. 

"Huwezi kujua maana inabidi ujuwe kuwa Ozu na mwenzake ni wapelelezi mashuhuri".

Ozu ambaye alitelemka mwisho alifanya hivyo kwa sababu maalumu. Alikuwa amevaa miwani, na miwani hii haikuwa ya kawaida ingawaje ilionekana kama miwani ya jua ya kawaida. Miwani hii ilikuwa na kioo maalumu kinachovuta vitu vilivyo mbali na kuvileta karibu. Hivi Ozu alipotokea kwenye mlango wa kutokea wa ndege aliiweka miwani hii na kuangalia moja kwa moja kwenye jukwa ambapo watu wanasubiri wageni hukaa. Na mara moja aliweza kutambua kitu ambacho alikuwa akihisi. Baada ya kutambua kitu hiki alitoa hiyo miwani na kuendelea kutelemka ngazi za ndeeg.

Mulumba ambaye aliingia ndani ya chumba cha kufikia wasafiri, alionekana mtu mwenye wasiwasi sana na mara Kasongo alipomwona katika hali hii alijua lazima kuna kitu hivi alimsogelea.

"Vipi?", Kasongo aliuliza. 

"Nimemtambua mmoja wao lakini mwingine bado, kwa sababu wako safari moja itakuwa rahisi kuwatambua. Maana itabidi wawe pamoja", alijibu Mulumba.

"Kwa hiyo tuwe macho na huyu mtu uliyemtambua, tusimuachie hata kwa dakika moja".

"Huyo anaingia", Mulumba alimtambulisha Kasongo.  

Kasongo alimwangalia kwa chati kijana huyu ambaye alipita sehemu za uhamiaji bila wasiwasi wowote. Walijaribu kuchunguza katika abiria wote kama wangeweza kumtambua huyu wa pili ambaye alikuwa ameelezwa, lakini bila mafanikio, kwani kulikuwa na abiria wengi waliokuwa na maelezo sawa na yale yaliyotolewa juu ya mtu huyu wa pili, hivi ilikuwa vigumu sana kumtambua.

"Itabidi tumg'ang'anie huyu ndiye atatuonyesha huyu wa pili", alishauri Kasongo.

"Sawa, twende nje tukamsubiri kule", Mulumba alikubaliana/

"Hapana siye tukae hapa hapa kwenye makochi kwa vile tutaona kila kitu nje itakuwa rahisi kumwona na atakapochukua gari ndipo sisi tutamfuata bila mtu kushuku", alishauri Kasongo.

Mulumba alikubaliana na jambo hili wakaketi kwenye makochi kama watu wengine waliokuwa wakisubiri wageni.

Willy na Robert walipotelemka chini walienda moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha kupokelea wageni ambao husafiri ndani ya Zaire tu. Walichagua sehemu hii maana ilikuwa sehemu nzuri ambayo mtu anaweza kuangalia mambo yote yanayoendelea kwenye sehemu ya nje ya uwanja wa ndege, na vile vile kuangalia kitu kinachofanyika ndani ya chumba cha kupokelea wageni watokao nchi za nje. Maana sehemu zote hizi ni vioo vitupu. Hivi Willy na Robert walipoingia walichanganyikana na kundi la watu ambao walikuwa wamefika kuwapokea ndugu zao lakini macho yao yakiwa katika tahadhari ya kuangalia mambo yote ambayo yangeweza kutokea hapo nje.

Bila kujua nini kinatendeka. Kofi alikuwa katika kundi la kwanza lililomaliza kukaguliwa. Akiwa katikati ya kundi hili la wenzake aliweza kuingia kwenye chumba cha kupokelewa na kisha kutoka nje bila ya Mulumba na mwenzake kumtambua ingawaje alipita mbele yao. Kofi na Ozu walikuwa wamepanga kuwa wafikapo Kinshasa kila mtu achukue njia yake ila tu waonane baadae wakishafika mjini. Kwa sababu hawakuwa wageni sana mjini Kinshasa jambo hili lilionekana safi kabisa kiusalama.

Wakati Kofi anatoka nje, Willy na Robert alimwona, "Huyo Kofi anatoka", Robert alimweleza Willy ambaye alikuwa akiangalia mambo mengine. Walimwangalia Kofi ambaye alikuwa pamoja na abiria wengine, akienda na kuingia ndani ya teksi iliyokuwa karibu na kuondoka huku wakipita mbele ya Willy na Robert kuelekea mjini. Willy alichukua namba ya teksi na kuiweka kichwani.

"Ngoja mimi nimfuate Kofi, halafu wewe utamfuata Ozu akitoka maana naona wamekata shauri kila mmoja wao kuchukua njia," Robert alishauri.

"Hapana tusiwe na haraka tumsubiri Ozu mpaka naye atoke", Willy alieleza.

Ozu ambaye kama nilivyokwisha eleza hapo nyuma alikuwa amevuta sura za watu waliokuwa jukwaani wakati anateremka katika ndege kwa miwani yake, na katika sura zilizokuwa hapo sura tatu kati ya hizo alizitilia mashaka kwani macho ya sura hizi yalionekana yakimwangalia yeye moja kwa moja. Naye mara moja sura hizi akaziweka kichwani mwake, hivi alipomaliza kukaguliwa na kuingia kwenye chumba cha kupokea wageni, alizungusha macho yake kwa chati kwa watu wote waliokuwa humo. Macho yake yalipomwangalia Mulumba yalimtambua moja kwa moja lakini wale wengine hakuweza kuwatambua. Hivi akijifanya kama hakuna kitu aliendelea na abiria wenzake na kutoka nje. Baada ya Ozu kutoka nje. Mulumba na Kasogo walisimama na kwenda hadi karibu na mlango na kumwangalia Ozu ambaye alikuwa akizungumza na dereva wa teksi. Kisha alipanda ndani ya teksi na kuondoka kuelekea mjini.

Willy na Robert nao walikuwa wakimwangalia OZu kwa uangalifu kabisa. Baada ya gari la Ozu kuzunguka na kupita mbele yao tayari kwa kuelekea mjini walikata shauri kutoka nje ili wapate kumfuata. Walipokuwa wakifungua mlango ili watoke, waliona watu wawili nao wanafungua mlango wa chumba cha kupokelea wageni watokao nchi za nje na kutembea haraka haraka nusu wakikimbia kuelekea kwenye maegesho ya magari.

"Hebu ngoja," Willy alimsukuma kidogo Robert na kurudi ndani, "Unawaona wale watu?"

"Ndiyo,"

"Hebu tuone wanataka kufanya nini".

Watu hawa walikuwa ni Mulumba na Kasongo ambao waliingia ndani ya gari lao na kuondoka kwa kasi sana kumfuata Ozu.

"Sasa Robert itabidi tuondoke ndani ya gari moja, maana inaonekana watu wawili wanamfuata Ozu kutokana na jinsi walivyoondoka. Unasemaje?".

"Sawa, twende zetu tusije tukawapoteza. Lo, kweli subira huvuta heri."

Willy na Robert waliingia ndani ya gari la Willy alilokodi na kuondoka zao kuwafuata hawa watu waliotangulia.

Mulumba na Kasongo walikwenda kasi kwenye hii barabara ya P.E. Lumumba ili wapate kuisogelea teksi iliyokuwa imembeba Ozu. Ingawaje magari yalikuwa mengi wakati kama huu wa mchana lakini walifanya kila ujuzi kuyapita magari mengine na kulisogelea gari la Ozu. Walipokuwa wameacha gari moja kati ya gari lao na gari la Ozu, walituliza mwendo wao na kufuata wakiwa nyuma ya gari hili jingine.

Ozu ambaye wakati wanaondoka uwanja wa ndege alipata fursa kumwona tena huyu kijana aliyekuwa amemwona kwenye jukwa akiwa amesimama kwenye mlango wa kutokea ndani ya chumba cha kupokelea wageni watokao nchi za nje, alihisi kuwa lazima alikuwa anafuatwa hivi mara kwa mara aliangalia nyuma kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa anafuata.

Willy na Robert nao walitumia kila ujuzi wao mwenye msululu huu wa magari mpaka wakawa wameacha magari mawili kati yao na gari la akina Mulumba na kutuliza mwendo wao.

"Hawa watu ni watu gani?" Aliuliza Robert.

"Tutajua tu, usiwe na haraka", alijibu Willy bila wasiwasi.

Walipokaribia njia panda ya barabara ya P.E. Lumumba na barabara ya 'Poids Lourds', Ozu ili kusudi aweze kuhakikisha kama kweli anafuatwa alimwambia dereva teksi.

"Tuingie barabara ya 'Poids Lourds'.

"Likambo te!" Alijibu teksi dereva katika Kilingala, maana yake 'hamna taabu', na kuonyesha taa za gari kuwa anachepuka kuingia barabara nyingine. Mulumba na Kasongo kuona hivi nao wakaonyesha taa kuwa na wao walikuwa wanachepuka kuingia barabara hiyo.

"Kwanini anaingia barabara hii?", Kasongo aliuliza.

"Kaa macho, huyu mtu ujue ni mpelelezi maarufu kama tulivyoelezwa kwa hivi ni mtu hatari anaweza kuwa ametuhisi, hivi anatafuta njia ya kujihami. Hivyo weka bastola yako tayari, maana hii barabara haina watu wengi ni ya upweke sana, anaweza kuanzisha kitu chochote", alieleza Mulumba huku akiwa na wasiwasi kidogo.

Willy na Robert walipoona gari la Ozu na la hawa watu wengine yakichepuka na kuingia Poids Lourds hawakuwa na budi ila nao kuingia barabara hii.

"Kwanini Ozu anaingia barabara ya upweke namna hii na huku anafuatwa?". Aliuliza Robert.

"Inawezekana amehisi kitu na anataka kuhakikisha," alijibu Willy huku akiwa tayari ameingia ndani ya barabara hii ya Poids Lourds.

"Lakini barabara hii ni ndefu sana na ya upweke sana kiasi kwamba jambo lolote likikutokea kupata msaada ni vigumu."

"Ngoja tuone nia yake ya kufanya hivi ni nini".

Ozu alipoona magari mawili yanamfuata nyuma huku yakiwa yameweka umbali ambao hayakuwa yanauzidi kati yao, aliridhika kuwa alikuwa anafuatwa na vile vile alihakikisha kuwa wale watu wawili aliokuwa amewaona kwenye jukwaa lakini hakuwa amewaona ndani ya chumba cha kupogkelea wageni, nao walikuwa wanamfuata ndicho kisa cha kuwepo magari mawili yakifuatana. Alifikiri afanye nini, lakini moyo wake ulimkataza asifanye chochote maana upinzani ungekuwa mkali sana kwake. Hivi akaamua kuendelea hivi hivi mpaka mjini ambako huenda angeweza kupata nafasi ya kuwakwepa watu hawa. Kwa hiyo alimwambia dereva, "Hebu ongeza mwendo kwa kadri ya uwezo wako".

"Barabara hii ina mashimo mengi sana lakini nitajitahidi", alijibu dereva huku akiongeza mwendo.

Mulumba na Kasongo walipoona gari iliyombeba Ozu inaongeza mwendo, nao wakaongeza mwendo. Akili yao ilikuwa imejawa na kumfuata Ozu kiasi cha kwamba hawakutilia maanani gari lililokuwa linawafuata nyuma.

"Inaonekana Ozu ametambua kuwa anafuatwa angalia jinsi gari lake ambavyo limeongeza mwendo", Robert alisema.

"Naona hata mimi. Ili kusudi tuhakikishe kuwa watu hawa wanamfuata Ozu ni lazima sisi tuwasimamishe. Maana inaonekana haja yao ni kumfuata tu wala si kumsimamisha na kumfanyia chochote. Kwa vile pia tumetambua kweli kuwa wanamfuata litakuwa jambo la maana kuwakamata watu hawa tujuwe ni akina nani na kwanini wanafanya hivi. Hasa ninapofikiria ya kwamba Ozu na Kofi wameingia hapa mjini kisiri, hili jambo la watu kuwafuata linatia wasiwasi," Willy alieleza wasiwasi wake.

"Sawa, mimi niko tayari kwa kitendo chochote utakachoamua".

"Vizuri, una silaha?".

"Sina", alijibu Robert.

"Kwanini unatembea bila silaha nawe unajua uko kazini?"

"Mimi ninatumia silaha inapokuwa lazima sana. Kawaida yangu katika kashikashi ya kawaida judo, karate na kung fu ambayo nina ujuzi wa hali ya juu sana, wewe mwenyewe utachoka ukiniona niko kazini," Robert alieleza kwa sauti ya kujiamini sana. 

Willy ambaye alimwamini moja kwa moja alimweleza, "Kwa sababu hujui watu hawa ni watu wa namna gani lazima uwe tayari kwa yote. Mimi nitalitia gari mwendo wa kasi kiasi cha kuwapita hawa jamaa. Nikishawapita tu nitapiga breki mbele yao kiasi cha kwamba watatugonga nyuma. Hapo ruka mara moja na kumteka jamaa wa upande wako, nami nitamteka wa upande wangu. Kwa sababu tutawashtua nafikiri kazi itakuwa rahisi sana", Willy alitoa bastola ndani ya koti na kumpa Robert, "Chukua hii".

"Asante, kwa upande wangu hamna taabu, sijui wewe dereva".

"Kwangu ndiyo hamna kabisa," alijibu Willy huku akiongeza mwendo.

Walipopita gereji ya Fiat tu. Willy aliweka mwendo wa kasi sana kwa gari hili la aina ya Mercedes Benz na gari likapaa. Sehemu hii waliyokuwa wamefikia ilikuwa sehemu ya upweke sana, na Willy aliiona ndiyo sehemu safi ya kufungia kazi.

Mulumba ambaye ndiye alikuwa akiendesha gari lao aina ya Fiat 124 aliona kwenye kioo chake cha kuendeshea, gari lililokuwa nyuma yao linakuja kasi sana. Mara moja akaingiwa na wasiwasi na kumwambia Kasongo aweke silaha tayari.

Gari hilo sidhani lina usalama," alimalizia na huku gari la akina Willy linaanza kuwapita. Willy aliwapita kwa mwendo huo huo, alipopita mbele yao tu, akaliingiza gari sawasawa na gari la akina Mulumba, huku akiwa kana kwamba ameona shimo. Alifunga breki ghafla na kuliacha gari lijililie. Mulumba alishindwa kulikwepa gari hili na akaligonga kwa nyuma kama vile Willy alivyotaka. Willy na Robert waliruka toka ndani ya gari lao, na huku wakati ule ule, Mulumba na Kasongo nao waliruka toka ndani ya gari lao, Kasongo ndiye alikuwa wa kwanza kufyatua, lakini risasi yake ikamkosa Robert ambaye alikuwa amekwisha jirusha toka alipoangukia na kuangukia karibu na Kasongo, na kufumba na kufumbua akaipiga teke bastola ya Kasongo na kuangukia upande. Robert kuona hivi alirudisha bastola yake ndani ya koti ili amkabiri Kasongo mikono mitupu.

Naye Willy aliporuka alijiviringisha na alipoinuka tu akakuta Mulumba naye anajiweka tayari kufyatua risasi, lakini Willy alikuwa mwepesi zaidi akawahi kufyatua risasi ya kichwa na kumuua pale pale. Alipoona hivi aliruka mara moja kwenye upande ule ambako Robert na Kasongo walikuwa wanazipiga na kumkuta Kasongo amepigwa ile mbaya mpaka hajiwezi kabisa. 

"Basi, basi, inatosha, mwingize ndani ya gari yetu, twende naye, huyu ndiye atatupa habari".

Wakati Robert anamwingiza Kasongo ndanu ya gari. Willy aliangalia lile gari kwenye karatasi za bima akakuta ni gari la kukodi la S.T.K. Kisha akajaribu kunyoosha gari lake kwa nyuma ambako lilikuwa limebonyea kiasi cha kugusa kwenye tairi. Alipolinyoosha kiasi cha gari kuweza kwenda, alipanda ndani ya gari akalipiga moto na kuondoka. Tayari Robert na mtu wake walikwisha starehe nyuma ya gari. Mambo yote haya hayakuchukua zaidi ya dakika mbili. Willy alifikiria wapi wampeleke mtu huyu kumhoji, mara akapata wazo. Aliendelea moja kwa moja mpaka akaingia barabara ya 30 Juin kisha akaingia barabara ya Kasavubu halafu akaingia barabara ya Sendwe halafu barabara ya Universete. Alipoingia ndani ya barabara hii akaenda moja kwa moja mpaka Chuo Kikuu. Alipofika hapa Robert ambaye alikuwa anashangaa wanakwenda wapi aliuliza, "Wapi tunakwenda?".

"Sehemu ambayo huyu ndugu yetu anaweza kutueleza vizuri mambo tunayotaka kuyajua", Willy alijibu Robert naye alihisi sehemu gani Willy alikuwa amefikiria.

Walipofika kwenye msitu ulio karibu na Chuo Kikuu na shule ya sekondari ya wasichana ya Kimwenza, Willy alienda taratibu na kuyaacha magari yampite. Yalipokuwa yamempita magari yote alisimama na kutoka. "Bado amezirai?", Willy aliuliza.

"Anaanza kupata fahamu".

"Tumbebe, hapa ndipo mahali petu ambapo tunaweza kuzungumza na huyu mtu", walimbeba na kuingia naye ndani ya msitu huu. Kwa vile Kasongo alikuwa bado hajapata fahamu vizuri, Willy alichukua galonoya maji iliyokuwa ndani ya gari na walipopata mahali pazuri ndani ya msitu huu walimweka chini Kasongo na kuanza kumwagia maji. Kasongo alipopata fahamu vizuri Willy alitoa bastola yake na kuilenga kichwani mwa Kasongo na kuanza kumhoji.

"Wewe ni nani?", Willy aliuliza.

"Kwani nyie ni nani?", Naye Kasongo aliuliza.

"Tafadhali kijana kama unataka usishi tafadhali sana jibu maswali yetu tutakuacha uende nyumbani, la hutaki leo ndiyo mwisho wako.

"MSipoteze muda wenu. Mimi sintawaeleza lolote, kama ni kuniua basi niueni mwende zenu."

"Lakini tuna njia nyingi za kuweza kukushawishi ujibu maswali yetu, lakini sisi tusingependa kuzitumia njia hizi kama utatujibu moja kwa moja".

"Nimesema nimesema, kama kuniua mniue neno hata moja hamtapata kutoka kwangu", alijibu Kasongo kwa ujasiri mwingi sana.

"Wewe unamkawiza", Robert alimwambia Willy, "Majitu kama haya hayafai kubembelezwa maana yamezoea taabu", Robert alimfungua Kasongo suruali, halafu akamtelemsha suruali pamoja na chupi, kisha akawasha kiberiti chake cha gesi na kuanza kumchoma kwenye sehemu zake za siri. Kasongo alianza kupiga kelele maana alipata uchungu mwingi sana.

"Niache, niache, aaa mnaniua", alilia Kasongo.

"Jibu wewe ni nani na nani amekutuma?".

"Sijui... aaa... sijui", aliendelea kupiga makelele, Robert alisogeza moto, Kasongo aliachama na kuzungusha zungusha ulimi wake halafu kitu kama peremende ndogo sana kikatokea mdomoni mwake na kukazana kukimeza. Willy alipokiona tu alimrukia kusudi asikimeze lakini kwa bahati mbaya hakuwahi. Kwani Willy alikitambua kitu hiki kuwa ni kidonge cha sumu ambacho hutumiwa hasa na majasusi ya hali ya juu sana wanaposhikwa ili wajiue wasiweze kutoa siri.

"Ni kazi bure tumefanya Robert, atakufa sasa hivi, amemeza kidonge cha sumu. Inaonekana hawa ni majambazi ambao wanalifanyia kazi kundi la hali ya juu sana, maana kundi la kawaida haliwezi kutumia njia hizi", alisema Willy kwa huzuni sana.

"Mimi kwanza nilikuwa na wasiwasi nikijua tumepambana na vijana wa CND, lakini hii imehakikisha kuwa kuna kundi la kijasusi mjini hapa na leo tumelitonesha kidogo, sasa tusubiri tuone nini kitafanyika", Robert alieleza. Willy alikagua mifuko yote ya Kasongo, kitu cha kutatanisha alichokipata kilikuwa kikaratasi kidogo kigumu kilichoandikwa, "Muone Kabeya Charles", Willy alikiangalia sana kikaratasi hiki kisha akampa Robert ambaye naye alikiangalia sana.

"Kitatue, lakini majina hayo yaweke kichwani, huenda yakawa na maana sana", alishauri Willy.

"Lazima ni ya maana sana, lakini tukiweke kwanza," alijibu Robert.

Waliondoka sehemu hii na kurudi mjini huku wakiwa na mawazo mengi sana juu ya tukio hili la kushangaza. Kwani huenda walikuwa kwa bahati mbaya wameligusa kundi linalohusika na mauaji ya wapigania uhuru, hivi ndivyo waifikiri wakati wakirudi mjini.  

ITAENDELEA 0784296253


Comments

  1. asante mnoooo kwa kusikiliza maoni yetu broo keep it up yan kila inapoisha ndo tunatamai iendeleee

    ReplyDelete
  2. nimekupata mkuu usichoke kutuburudisha

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU