KIKOSI CHA KISASI

SURA YA SITA 

WASIWASI
III

Wakati kikao cha dharura cha 'WP' huko kwenye ofisi za gereji ya G.A.D. kikiendelea. Kikao kingine cha 'KK' kilikuwa nacho kinaendelea nyumbani kwa Robert Sikawa huko Macampagne. Kofi na Ozu baada ya kumpigia Robert simu walitelemka chini na kuchukua teksi iliyowapeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Robert. Waliwakuta wenzao wakiwasubiri kwa hamu na kweli walipoonana walikumbatiana kwa furaha kubwa. Kusema kweli kama ungewaona vijana hawa ungeamini kuwa ni watoto wa mzee mmoja maana walifanana. 

Kweli ni ajabu sana Ozu na Kofi walimfurahia sana Willy kumuona maana sifa zake nyingi walikuwa wamezisikia. Kwa mawazo yao walifikiri ni mtu wa kutisha sana, lakini kwa mshangao wao walimkuta ni kijana wa rika yao na sura ya kupendeza ajabu kiasi kuwa mtu kwa mtu yeyote angempenda. Kweli alikuwa rijali. Willy na Robert nao waliwafurahia wenziwe na katika muda wa dakika chache vijana hawa walitaniana na kuchekeshana kana kwamba walishafahamiana miaka kumi iliyopita. 

Baada ya mazungumzo haya ya kukaribishana, waliingia katika mazungumzo ya kikazi, Willy alieleza kwa kirefu sana mambo yote kuhusu nia na utekelezaji wa kazi waliyopewa. Baada ya maelezo haya aliwaeleza maendeleo waliyokuwa wameyafanya katika shughuli, na kuwafikisha mpaka kwenye tukio la akina Ozu, Mulumba na Kasongo.

"Kwa kifupi ndivyo hivyo mambo yalivyokuwa mpaka sasa hivi. Swali linabaki pale pale hawa watu ni akina nani, na wanawakilisha kundi gani?".Alimalizia Willy. 

"Vizuri sana umetuweka katika hali nzuri ya kujua mambo yalivyo. Kweli suala linabaki ni hilo hilo," Ozu alisema. 

"Hiki kijikaratasi huenda kina maana. Kabeya ni nani na Charles ni nani? Ndilo suala jingine", Willy alijaribu kutafuta mawazo.

"Unajua katika Zaire siku hizi majina ya kizungu hayatumiwi, basi hii inaonyesha kuwa aliyeandika kikaratasi hiki ambaye ni Charles si Mzaire", Robert alieleza.

Willy alikitoa kile kikaratasi ndani ya mfuko wake wa shati na kuanza kukiangalia tena. "Ahaa angalieni mwandiko huu ni wa Kizungu si wa Kiafrika, unajua miandiko ya Kizungu na Kiafrika inatofautiana! Wote walicheka kutokana na jinsi Willy alivyokuwa akieleza.

"Ni kweli, huu ni mwandiko wa Kizungu", walikubaliana wote.

"Hii ina maana hawa watu walikuwa na uhusiano na mzungu. Kwa hiyo itabidi tujaribu kumtafuta Kabeya na huyu Charles, naamini tukiwapata watatueleza zaidi", alizungumza Willy kimatani.

"Tutawapataja na huku kuna Kabeya chungu mzima Kinshasa na akina Charles chungu nzima vile vile", alisema Robert. 

"Ndiyo sababu sisi tunaitwa wapelelezi," Willy alimkumbusha, "Sasa itabidi tupeleleze hata ikiwa ni lazima kuwakusanya watu wote wa majina haya itatubidi tufanye hivyo. Maana maelezo yoyote tuliyonayo sasa ya kuweza kutusaidia ni hayo tu na lazima tuyatumie", alimalizia Willy.

"Majina haya yanaweza kuwa ya bandia na yakawa hayana maana yoyote", Ozu alisema.

"Si kitu, sisi tutajaribu tu, kitu ambacho najua ni kweli kwamba watu hawa wapo hata kama majina haya ni majina ya bandia watu hawa wapo na wana uhusiano mkubwa na watu wale tuliopambana nao mchana. Mimi nina miadi yangu saa moja ambayo sasa imeshafika tayari kwa hiyo itabidi niondoke. Kitu muhimu cha kufanya sasa, inabidi sisi wote sasa tuwe macho hasa wewe Ozu maana wewe tayari wamekwisha kutambua na ni imani yangu kuwa wako mbioni kukusaka. Hivyo wewe ndiwe utakuwa chambo na wewe ndiwe utaweza kutufanya tuwajue watu hawa. Hivi lazima tuwe katika tahadhari kubwa maana kitu chochote kinaweza kutokea wakati wowote. Huu ni wakati wa wasiwasi sana hivi itabidi tuwe na moyo wa utulivu kabisa. Kesho asubuhi nitajaribu kuwaona watu wa STK, ili nipate kujua ni nani aliyekuwa amekodi lile gari walilokuwemo wale majambazi. Mmefikia hoteli gani?" Alimazia Willy kwa kuuliza.

"Mimi niko hoteli Regina chumba nambari 108 na Kofi amefikia Hoteli Intercontinental," alijibu Ozu.

"Chumba nambari 401," aliongezea Kofi.

"Vizuri, kama nilivyokwisha sema kaeni macho. Kama kitatokea kitu chochote habari ziletwe hapa kwa Robert. Mimi nimefikia Hoteli Memling, chumba nambari 240, ikiwa nitahitajika. Ninayo imani kubwa saba baada ya kuwaona, Kuwa Mungu akipenda tutashinda vita hivi. Robert peleka habari Lusaka kueleza kuwa wote tumekwishawasili mjini hapa na shughuli zimeanza. Vile vile gari nililokodi tulifanyia ajali, liweke ndani mpaka kwanza tuone uchunguzi wa tukio hili utafikia wapi, mimi nitaendelea na gari hili ulilokodi wewe. Asanteni mimi naondoka," Willy alimalizia kunena huku akisimama tayari kwa kuondoka.

"Vipi una miadi na mtoto nini?", Ozu alitania 

"Kitu kama hicho", alijibu Willy huku akimwemwesa. 

"Una bahati basi mara hii tayari. Haya starehe njema," Ozu alimwombea.

"Asante." Waliagana Willy akaondoka kuwahi miadi yake na Mwadi ambayo alikuwa tayari amechelewa. Aliingia ndani ya gari alilokuwa amekodi Robert, baada ya kufanya ajali na lile gari jingine, na akaondoka kwenda zake. Robert na wageni wake walibaki na wote kwa pamoja wakakata shauri kutengeneza chakula cha jioni hapo nyumbani kwa Robert wao wenyewe. Kwani Robert hakuwa hata na mfanyakazi hivi ndivyo alivyokuwa akiishi. Mtu aliyekuwa akifika hapa nyumbani kwake mara kwa mara na kumsaidia kusafisha nyumba na mara nyingine kumsaidia kupika alikuwa rafiki yake msichana aitwaye Ebebe, ambaye walipendana sana.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU