KIKOSI CHA KISASI

SURA YA SITA 

WASIWASI

I

Ozu ambaye alikuwa amefikia Hoteli Regina, alimaliza kuoga. Aliangalia saa yake akakuta inakaribia saa kumi na moja za jioni akaona ajitayarishe kusudi awahi ahadi yake na Kofi huko Restaurant Namouna ambako waliagana wakutane mnamo saa kumi na moja na nusu, ili wapate kuelezana mambo yalivyokuwa. Alivaa vizuri akapanga vitu vyake vizuri, kisha akafungua mlango, akachukua kijikaratasi akakibana na mlango, akaufunga akaondoka kwenda zake. Funguo za chumba chake hakuzirudisha mapokezi isipokuwa aliondoka nazo moja kwa moja.  

Restaurant Namouna iko ghorofa ya nne ndani ya jengo maarufu liitwalo Galleries Presidentielles. Na kutoka Hoteli Regina mpaka jumba hili ni karibu sana, kiasi cha mwendo wa dakika tano kwa miguu. Hivi Ozu aliondoka kwa miguu akaelekea kwenye mkahawa huu. Alipofika alimkuta Kofi tayari ameiwasili huku akiwa anakunywa kahawa na Sangweji.

"Katibu", Kofi alimkaribisha.

"Asante", alijibu Ozu huku anakaa. Kofi alimwagizia Ozu kahawa vile vile.

"Ehe, umekata shauri kwenda hoteli gani?" Ozu alimwuliza Kofi.

"Nimefikia Hoteli Intercontinental".

"Mimi niko Hoteli Regina", walielezana.

"Mimi safari yangu kutoka uwanja wa ndege ilikuwa safi kabisa. Maana nilipotoka hapo nje nilichukua taksi na hatukupata tatizo lolote mpaka tulipofika Intercontinental. Baada ya kuchukua chumba nimejitayarisha na kuja hapa, sijui wewe mwenzangu ilikuwaje", aliuliza Kofi.

Ozu alimeza mate, akamwangalia Kofi kwa macho makali kisha akamwambia. "Mimi rafiki yangu mambo hayakuwa mazuri kama yako. Wakati natelemka tu ndani ya ndege, ndipo hapo mambo yalianza. Kulikuwa na watu wanatusubiri. Inavyoonekana wewe hawakuweza kukutambua, hivi umepita bila taabu. Lakini mimi walinitambua na ndiyo sababu walinifuata. Ajabu ni kwamba kulikuwa na makundi mawili. Na walinifuata katika magari mawili tofauti. Nilipotaka kuhakikisha kama kweli nafuatwa nilimwamru taksi dereva achepukie kwenye barabara ya Poids Lourds, na kweli nilikuwa nafuatwa na makundi yote mawili. Sasa sikiliza kitu cha kushangaza. Nilipoona kuwa siwezi kuwakabiri watu hawa peke yangu nilimweleza dereva aongeze mwendo. Magari haya ya nyuma nayo yaliongeza mwendo. Tulipovuka Fiat tu, pale kwenye msitu, niliona lile gari la nyuma aina ya Benz linakuja kasi. Mimi nikajua sasa nitafungiwa kazi, kwa hiyo nikamwamru dereva azidishe mwendo kwa kadri ya uwezo wake. lakini Kofi, ajabu ni kwamba niliona kitendo cha ajabu. Lile gari la nyuma lilipolipita lile la mbele tu likafunga breki, ikabidi itokee ajali maana lile ambalo lilipitwa ilibidi lijigonge kwenye lile la nyuma na hapo hapo watu waliokuwa ndani ya magari haya waliruka nje na kuanza kushambuliana. Mimi kuona hivi nilizidi kumwamrisha dereva akaze mwendo na kuja moja kwa moja mpaka Hoteli Regina. Yaliyotokea hapo nyuma siyaelewi". Ozu alinyamaza kiasi cha kupitisha mate kisha akaendelea.

"Kitu kinachonishangaza sana ni kwamba watu hawa ni akina nani? Na kwanini wameshambuliana? Wamejuaje kuwa sisi tunafika? Nafikiri tukishajibu maswali haya basi tutakuwa tumeshapata jawabu la tukio hili", alimalizia Ozu.

"Ahaa, afadhali wewe maana umeona vituko. Mimi nafikiri makundi mawili ni makundi tofauti katika misingi ya shughuli zao. Tuliarifiwa kuwa tukifika hapa tumwarifu Robert ambaye atamwarifu Willy kuwa tumefika. Inawezekana Willy na Robert walishaletewa habari kuwa tutafika, hivi walifika kutupokea na wakati wanafanya hivi ndipo waligundua kuwa kuna kundi jingine lililokuwa linatusubiri. Kati ya wale watu uliowaona jukwaani lazima Willy na Robert au mmojawapo walikuwemo, lakini kwa sababu hatuwajui kwa sura ndiyo sababu hukuweza kuwatambua. Mimi nahisi kuwa Willy na Robert ndio walikuwa ndani ya Benz na walifanya mashambulizi ya kukunusuru wewe. Lakini tusichoshe vichwa vyetu maana itabidi tuonane na Robert jioni hii", alishauri Kofi.

"Mawazo yako ni sawa kabisa. Hata mimi nilikuwa nashauri katika misingi hiyo hiyo. Swali moja limebaki bila kujibiwa. Hili kundi jingine limejuaje kuwa sisi tunawasili hapa mjini na hali kuingia kwetu ni siri ya hali ya juu ", aliuliza Ozu.

"Kama Willy na Robert wamenusurika katika mashambulizi haya wataweza kutujibu swali hili," Ozu aliangalia saa yake akaona ni kiasi cha saa kumi na mbili unusu.

"Sijui tumpigie simu Robert au tumfuate nyumbani kwake?", Ozu aliuliza.

"Nafikiri tumpigie simu kama yupo, na kama yupo tumfuate", Ozu alitoa kijikaratasi ambacho kilikuwa kimeandikwa simu na sehemu ambayo Robert alikuwa akikaa kama walivyopewa na ofisi ya 'KK' ya Lusaka. Walikuwa wameelezwa kuwa Robert alikuwa akikaa sehemu iitwayo Macampagne mtaa wa Marais nyumba nambari ya kiwanja 2994. Ozu alikwenda kaunta akaomba kama anaweza kupiga simu. Kijana aliyekuwa kaunta alimruhusu apige kwa Robert, "Hallo," Ozu aliuliza simu ilipoinuliwa kule kwingine.

"Hallo, nani mwenzangu", sauti nzito ilijibu.

"Hapo ni nyumbani kwa Robert Sikawa?" Ozu aliuliza. 

"Ndiyo", sauti ilijibu.

"Mwenyewe yupo?".

"Ndiye anazungumza".

"K.K", Ozu alisema.

"Kikosi cha Kisasi," Robert alijibu. Hii ndiyo namna walivyokuwa wanajitambulisha.

"Habari yako Robert? Ozu hapa".

"Nzuri, salama lakini".

"Salama kabisa, sisi tuko hapa Restaurant Namouna, pamoja na Kofi, tuonane wapi?"

"Nafkiri ingekuwa vizuri kama tungeonana hapa maana Willy naye yuko hapa kwa wakati huu. Mimi nakaa..."

"Usiwe na wasiwasi tunapajua mtusubiri tunakuja sasa hivi", Ozu alimkata kauli. 

"Oke, tunawasubiri, fanyeni haraka maana Willy ana miadi yake,"

"Sasa hivi," alijibu Ozu na kukata simu.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru