KIKOSI CHA KISASI

SURA YA SITA 

WASIWASI

V

Usiku huu ambao Willy alikuwa na pilika za starehe, wenzake nao walikuwa na mengi. Baada ya kupika chakula na kula, vijana hawa waliendelea na vinywaji huku wakiangalia 'Televishen' ambako kulikuwa na kipindi cha muziki wa bendi ya Lipua Lipua ambao walifanya na maonyesho.

Waliendelea hivyo mpaka ilipotimia saa sita za usiku.

"Nafikiri sasa twende ili tukapate kupumzika, maana huenda kesho itakuwa siku ya pilika nyingi", Kofi alishauri.

"Hata mimi naona hivyo", Ozu alijibu.

"Si lazima mwende, mnaweza kulala hapa, ili tupate muda zaidi wa kuongea. Nyumba hii ina vyumba chungu nzima, wote wanne tunaweza kuishi hapa", Robert alishauri kutaka kwa vile alivyopendezwa na ugeni wa vijana hawa.

"Haitakuwa vizuri kiusalama", aliasa Ozu.

"Siku moja tutakapokuwa tumemaliza shughuli hii, ni lazima mje tukae wote hapa kwa mapumziko."

"Tuombe Mungu tuvuke salama," alijibu Kofi.

Walimaliza vinywaji vyao na kuondoka. Waliingia ndani ya gari la Robert ili Robert aweze kuwapeleka mahotelini kwao. Walipofika kwenye kona ya 30 Juin na 8 Armee ambapo ndipo Hoteli Tip Top imejengwa. Ozu alimshauri Robert watelemke hotelini hapo wapate bia moja moja ya kulalia.

"Mimi nimeisha tosheka", alijibu Robert, "Huenda niwasindikize nyinyi".

"Kama ni hivyo wewe tuache hapa sisi tutajua namna ya kwenda," alijibu Kofi.

"Ndiyo, wewe tuache hapa, kwa Kofi hapa ni karibu anaweza kwenza kwa miguu mpaka Intercontinental bila taabu na mimi nitachukua teksi mpaka hotelini kwangu," Ozu alikubaliana.

"Haya vizuri, tutaonana kesho," Robert alijibu na kuagana nao hawa wenzake. Ozu na Kofi walitelemka na kungia Hoteli Tip Top na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye kaunta ya baa na kuagiza Primus mbili baridi. Walikunywa huku wakizungumzia hali halisi kama walivyokuwa wakiiona kwa wakati huu.

"Mimi najisikia mchovu sana, ngoja nikalale," Kofi alieleza.

"Sawa hata mimi najisikia uchovu. Mimi nitachukua hapa teksi inirudishe hoteli kwangu," alijibu Ozu.

Waliongozana nje ya hoteli wakaagana.

"Njoo hotelini kwangu asubuhi baada ya chemsha kinywa. Utakuta tayari nimeisha zungumza na Willy au Robert," Ozu alieleza.

"Nitegemee kiasi cha saa mbili hivi. Jihadhari lakini," Kofi alimuaga.

"Na wewe jihadhari vile vile", alijibu Ozu akimwangalia Kofi anaelekea Intercontinental kwenye barabara hii ya Armee. Ozu alibaki akingojea teksi yoyote ambayo ingepita au kufika pale aisimamishe.

"Vipi, mbona umesimama hapa?," askari anayechunga magari hapo nje ya Tip Top alimjia Ozu na kuuliza.

"Mimi nangojea teksi nataka kwenda Regna Hoteli", Ozu alijibu.

"Lo, saa hizi teksi hapa ni shida sana, afadhali uende Intercontinental ambapo kuna teksi masaa ishirini na nne", askari alimshauri, Ozu aliona mawazo haya yanafaa.

"Asante kwa kunishauri, nitafuata teksi Intercontinental", akifuata barabara hii ya 8 Armee. Alimuona Kofi kwa mbele, lakini alikuwa ameshaenda mbali kiasi cha kwamba hata angetembea haraka namna gani asingemkuta. Hivi alikata kshauri kutomharakia.

Kofi ambaye alitembea kwa hatua ndefu, alitembea kwa tahadhari kubwa maana mawazo yake yalikuwa yakifikiria sana kazi hii waliyokuwa wamefikia mjini hapa kushughulikia. Akiwa anatembea pembeni mwa barabara na chini ya vivuli vya nyumba alivuka mtaa wa Asemblee na kuendelea na 8 Armree kwenye upande wa shule ya Athene'e de la Gombe, ambapo magari mengi yalikuwa yameegeeshwa. Gari moja kati ya magari haya yaliyokuwa yameegeshwa liliwasha taa ambazo zilimmulika Kofi usoni na kuzimishwa tena. Kitendo hiki kilimfanya Kofi asimame kuona kama gari lile lilitaka kuondoka. Kwa tahadhari yake alikata shauri avuke barabara kwa upande wa pili tayari kwa kuingia kwenye maegesho ya magari ya Intercontinental, ambayo vile vile kuna mlango wa kuingilia hotelini. Kabla hajavuka alisimama nyuma na akaona kwa mbali mtu anakuja. Alipoangalia vizuri aliona miondoke ile ni ya Ozu, akakata shauri asimame amgojee ajue kwa nini anamfuata, vile vile alikuwa na wasiwasi na lile gari lililowashwa taa, hivi aliweka mkono wake kwenye bastola yale aliyokuwa ameiweka ndani ya mfuko wa ndani ya koti.

Kwa silika, bila kujua kwa nini . Kofi aligeuka nyuma kama umeme huku akiwa ametoa bastola yake lakini mkono ulipigwa karate na bastola yake ikaanguka chini. Kuangalia akajikuta anaangalia ndani ya midomo ya bastola mbili.

"Usifanye lolote la sivyo utauawa mara moja," alielezwa. Gari lile lililowashwa taa lilipiga moto likajitokeza kwenye maegesho na kupiga breki mbele ya Kofi na milango ikafunguliwa. "Ingia ndani," Alielezwa Kofi akisukumwa ndani. Aliingia na wale watu waliokuwa wamemvizia nao wakaingia ndani na gari likaondoka. Tukio hili lilichukua chini ya dakika moja.

Ozu ambaye aliona tukio hili lakini kwa mbali kidogo alikimbia huku akijificha ndani ya vivuli vya michongoma iliyokuwa imezunguka nyumba zilizo sehemu hii, Lakini hakuweza kuwahi tukio lenyewe lilifanywa kwa ujuzi wa hali ya juu kiasi kwamba lilichukua muda kidogo sana. Alipoona Kofi ameingizwa ndani ya gari na gari linaondoka alirudisha bastola yake kwenye mfuko wa 'Jaketi' alilokuwa amevaa, akatoa funguo malaya za gari la Kijapan. Yaani funguo hizi zinaweza kufungua gari lolote lililotengenezwa na kampuni ya magari yoyote ya Japan. Aliharakisha kutafuta gari la Kijapan katika gari zilizokuwa zimeegeshwa barabarani. Gari ya kwanza kuiona ilikuwa Mazda Delux 1800. Alifungua akaingia ndani na kuwasha gari, na kuondoka kama mshale akalifuata gari lililokuwa limemteka nyara Kofi.


ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. kwa ufupi sana mkuu,jaribu kuifululiza

    ReplyDelete
  2. Relax brother...kumbe unafwatilia heee, mi huwa siwezi soma vitu vya hivi mpk vifike mwisho...ngojea ngojea siwezagi eti

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU