KIKOSI CHA KISASI


SURA YA SABA 

"GARAGE PAPADIMITRIOU"

Gari hili lilipotoka barabara ya 8 Armee liliingia mtaa wa 30 Juin, Ozu alilifuata kwa mbali akiwa anafuata taa za nyuma na lile gari, kiasi ambacho kisingeweza kuwagutua watu waliokuwa ndani ya gari hilo.

Kofi ambaye sasa mawazo yake yalikuwa yameishatengamaa, aliwaangalia watu waliokuwa wamemvamia. Ndani ya gari hili mlikuwa na watu wanne, yeye wa tano. Dereva alikaa mbele na mtu mmoja, na nyuma walikaa watu watatu pamoja na yeye, yeye akiwa katikati. Watu hawa wawili walishikilia bastola tayari tayari kabisa kwa msukosuko wowote. Hakuna neno lolote lilizungumzwa ndani ya gari hii. Kutoka mtaa wa 30 Juin mtaa wa Victimes de la Rubelion. Ozu alisimama, maana kulikuwa hamna magari yaliyoingia Juin mtaa wa Victimes de la Rubelion isipokuwa gari lililomteka nyara Kofi. Kusudi asije akawagutua, alingojea waende mbali kidogo ndipo yeye akatokeza kwenye mtaa huu wa Juin mtaa wa Victimes de la Rubelion. Gari la mbele lilienda kisha likaonyesha taa ya kuwa lilikuwa linaingia mtaa wa Kabambare. Ozu aliongeza mwendo nae akaingia Kabambare kwa mwendo mdogo sana. Kwa mshangao wake aliona gari lile likipita kwenye lango moja, na kuingia ndani. Ozu alipofika sehemu ile alikuta lango limefungwa na walinzi wasiozidi watatu wakiwa mlango hapo. Alipoangalia jengo lenyewe liliandikwa 'GARAGE PAPADIMITRIOU', aliangalia mambo yote haya huku akiendesha kwa mwendo kasi kabisa, alipokuwa amefika sehemu hii, ili asiweke mashaka yoyote kwa wavamizi wa Kofi ambao alihisi wangekuwa kundi kubwa.

Jengo hili la Garage Papadimitriou lilikuwa karibu na njia panda ya Kabambare inapokutana na mtaa wa Assossa. Kulikuwa na nyumba nyingine tatu kutoka kwenye gereji hii hadi Assossa. Hivi Ozu alipitiliza na kuingia mtaa wa Assossa ambako aliegesha gari na kutoka ndani na kurudi tayari kutaka kujua nini kinaendelea huko'Garage Papa'.

Gari lililokuwa limemteka nyara Kofi, pamoja na abiria wake lilipoingia mtaa wa gereji hii, liliendeshwa moja kwa moja mpaka ndani kabisa ambako kulikuwa na nyumba ambayo ndani mlikuwa na ofisi ya gereji hii. Kofi aliweza kuwaona walinzi watatu waliokuwa kuwenye lango. Ndani ya ngome ya jengo hili ambayo ilikuwa imejengwa kwa matofali ya saruji na yenye urefu usiopungua mita tisa, mlikuwa na uwanja mkubwa sana. Ndani ya uwanja huu mlijaa magari mengi ambayo yalikuwa yamekuja kutengenezwa. Wakati wanayapita magari haya kuelekea kwenye ofisi. Kofi aliweza kuona vivili vya watu waliokuwa wamesimama kando kando mwa njia hii iliyokuwa inaelekea ofisini. Hivi alihisi kuwa kulikuwa na ulinzi kabambe ndani ya ngome ya gereji hii. Kusema kweli kwa mara ya kwanza moyo wake ulipata wasiwasi. 

Gari liliposimama milango ilifunguliwa na watu wengine wawili ambao walijitokeza ndani ya magari mabovu yaliyokuwa yameegeshwa ndani humo huku wakiwa na bastola zao mikononi tayari kwa kuzitumia.

"Teremka, na tafadhali usijaribu ujanja wowote, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaomba kifo chako mapema zaidi," Kofi alielezwa na mmoja wa wavamizi wake.

"sawa bwana mkubwa, mimi niko chini ya ulinzi wako hivyo usiwe na wasiwasi na mimi hata kidogo," alijibu Kofi kwa sauti ya kejeri. Waliandamana chini ya ulinzi mkali sana na kuingia ndani ya ofisi.

Pale mapokezi walimkuta mtu mwingine naye akiwa na bastola mkononi ambaye aliwaeleza, "Nendeni ndani ya chumba cha mkutano bwana mkubwa anawangojea huko". Walienda moja kwa moja mpaka kwenye chumba kilichokuwa kimeandikwa 'CHUMBA CHA MKUTANO', yule mtu aliyekuwa mbele aligonga mara tatu, kisha mlango ukafunguliwa na mtu mwingine kwa ndani ambaye vile vile alikuwa na bastola mkononi.

"Ingieni," mtu huyu aliwaamru. Kundi zima liliingia ndani ya chumba hiki cha mkutano ambako walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia amekaa huku akiwa anazungumza na walinzi wake watatu.

"Haya huyu aliye mbele yako ni Mike Kofi ambaye tumemleta kwa mazungumzo nawe kama ulivyoagiza," alisema mmojawapo wa watu waliokuwa wamemteka nyara Kofi, ambaye alionekana kuwa kiongozi wao.

"Asante sana, karibu bwana Kofi. Samahani sana kwa kuletwa namna ulivyoletwa, lakini natumaini hakukuwa na njia nzuri zaidi ambayo ingeweza kukushawishi uje kuzungumza ila njia iliyotumika peke yake. Karibu keti kwenye kiti," Papa alieleza. Kofi ambaye alikuwa amesimamishwa upande mwingine wa meza, alivuta kiti na kukaa bila kusema kitu. Wale walinzi wake kila mmoja wao alichukua nafasi kwenye ukuta, wakiwa wamezunguka meza kila mmoja wao bastola mkononi. Baada ya kukaa, na mwili wake ukiwa katika tahadhari ya hali ya juu kabisa Kofi aliinua macho yake ambayo yalionana ana kwa ana na macho ya yule waliyekuwa wanamuita Papa. Macho yao yalipoonana wote walitambuana kwa kutokana na ujasiri katika macho yao kuwa wote walikuwa watu katika mchezo mmoja. Kofi alishangazwa sana kupambana na mtu mwenye asili ya Kiasia jambo ambalo hakulitegemea kabisa. Akiwa anasubiri nini atafanyiwa alijiweka tayari kuyakabiri mambo yote yatakayomtokea kiume. Wazo ya kwamba Ozu aliona mambo yaliyompata ilimtia moyo, lakini vile vile alikata tamaa kupata msaada kutoka kwake kwa sababu ulinzi aliokuwa ameuona hapa nje, kwa mtu mmoja kuingia ilikuwa kazi bure.

"Bwana Kofi nina maswali machache ya kukuuliza. Ningependa kukueleza kuwa, sitapenda kutumia njia yoyote ya kukushawishi ila napenda ujibu mwaswali yangu kwa hiari yako. Lakini kama utapenda nitumie kishawishi basi utakuwa umenilazimisha nami sitakuwa na budi kufanya hivyo", alisema Papa taratibu.

"Bwana Papa, ninaomba niulize na mimi swali moja kabla hujaanza kuniuliza," aliomba Kofi.

"Ehe, uliza", Papa alimjibu.

"Wewe ni nani na kwanini niko hapa?" Aliuliza Kofi.

"Baada ya muda mfupi utajua kwanini uko hapa, na vile vile utanitambua mimi ni nani," alijibu Papa kwa jeuri.

Kofi alielewa kwa ufasaha maana ya maneno haya na haikuwa mara ya kwanza kuyasikia hivyo alijibu, "Sawa."

"Bwana Kofi wewe pamoja na mwenzako Petit Osei kwa jina la bandia Petit Ozu, mmefika hapa mjini kwa shughuli gani?" Aliuliza Papa huku akimwangalia Kofi kwa macho makali sana. Kofi kusikia jambo hili la kutambuliwa kiundani kabisa yeye pamoja na Ozu kulimshitua sana ingawaje sura yake haikuonyesha. Alijua kuwa mara hii walikuwa wamepambana na kundi hatari kabisa, lenye upelelezi wa hali ya juu. Mara moja alihisi lazima watu hawa watakuwa ni majasusi wa Shirika mojawapo la kijasusi ambalo ni maarufu sana.

"Bwana Papa, kama utanisamehe ningependa uniulize vitu vinavyonihusu mimi mwenyewe, kwa sababu mimi nimeingia hapa peke yangu na wala mtu unayemzungumzia simjui. Nikijibu swali lako mimi nimefika hapa kwa shughuli za kibiashara," alijibu Kofi kwa sauti ya kutokujali kabisa.

"Kitu ninachotaka ni kunieleza ukweli, kama usiponieleza ukweli utanifanya nitumie vishawishi na nikivitumia utasikitika kwanini hukutaka kushirikiana nasi. Bila kupoteza muda nieleze kwa ufasaha nyinyi mmefika hapa kufanya nini. Maana mimi najua shughuli zenu na kuniongopea kutazidisha hasira yangu bure", alisema Papa kwa hasira.

"Kwanza nataka kujua namjibu nani? Nyinyi mmenileta hapa kwa kikuku. Sasa sielewi nyinyi mnawakilisha serikali au nani. Maana kama mna mashaka na kuingia kwangu hapa mnipeleke polisi na vile vile mnipe nafasi ya kumwarifu balozi wangu". Alijibu Kofi huku akinunua muda.

"Huyu hawezi kueleza chochote bila kishawishi Papa," alishauri yule mtu aliongoza msafara kumteka nyara Kofi.

"Kwa usalama wako jibu swali langu. Na kwa taarifa hapa ulipo huna haki ya kuuliza jambo lolote, ni aidha ujibu kwa hiari yako au utajibu kwa lazima," Papa alimweleza kama onyo la mwisho.

"Sawa kwanini nisiwe na haki yoyote katika nchi huru ya Kiafrika wakati sikufanya lolote. Tatizo ni dogo sana nieleze na mimi nikueleze," Kofi alijibu kwa dharau kubwa. Jambo hili lilimchukiza Papa, na akaona siasi ingempotezea muda mwingi na njia rahisi ilikuwa kupata maelezo aliyoyataka kutoka kwa mtu huyu kwa njia ya nguvu. Aliwaangalia wale wavamizi wa Kofi akawatingishia kichwa. Kofi aliona ishara hii akajua nini kitafuata hivi akaweka mwili wake tayari.

Wale watu walimwendea Kofi wakamvuta toka kwenye kiti. Kofi alisimama wakamshika huku watu wawili na huku wawili na mmoja akasimama mbele yake na kukunja ngumi tayari kwa kumtwanga masumbwi. Mmoja wa walinzi wa Papa alijaribu akiwa ameweka bastola yake tayari kabisa kwa tukio lolote. Kofi aliangalia yote haya na kujiweka tayari kwa kipigo. Alijua kama angejaribu chochote hapa asingeweza maana hawa watu walikuwa wengi na walikuwa na silaha. Kufanya lolote kungekuwa na maana ya kuuawa mara moja, hivyo alionelea aendelee kupoteza muda akitafuta nafasi nzuri kama itatokea jambo ambalo hakulitegemea.

Yule jamaa alianza kumtwanga masumbwi babu kubwa tumboni. Kofi alistahamili kwa muda mrefu mauivu haya haya makali aliyoyapata lakini mwishowe hakuweza kustahamili tena akasema.

"Ngoja ngoja nitawaeleza mnachotaka!"

Papa ambaye alikuwa akiangalia kwa makini kipigo hiki cha kuridhisha aliamru wamuachie ili aweze kuwaeleza.

"Nime... nime... ku... kuja... kufanya... biashara", alijibu Kofi kwa kutetemeka.

"Aa, aa, aa, bado ananitania ongeza mara mbili zaidi", aliamru Papa na kipigo kikaanza tena. 

ITAENDELEA 0784296253


Comments

  1. Safi sana mkuu.
    Ila episodes zinachelewa sana mkuu, au utaratibu wako wa kupost upo vipi.

    ReplyDelete
  2. Hapa hii tamthilia ni mzuri sana ila anaeitoa ni mbaya!! Haiwezekani utupe tamthilia mzuri kama hii kama dozi ya methadone!! Tupe kwa wakati sahihi Hata kama blog ni Mali yako.

    ReplyDelete
  3. Enter your comment...Kaka tunaomba wewe endelea kutuletea hadithi! Baadhi ya maneno yapuuze Kaka!

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

TUTARUDI NA ROHO ZETU?

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru

HOFU