KIKOSI CHA KISASI

SURA YA SABA

GARAGE PAPADMITRIOU

II

Ozu ambaye alikuwa ameacha gari mtaa wa Assossa, alirudi kuja kutafuta namna ya kuingia ndani ya gereji hii ajue nini kinafanyika. Alitoa bastola yake tayari tayari. Bastola ilikuwa sailensa. Alipita kwenye vivuli vya nyumba zilizokuwa karibu ya gereji kwa kuvizia. Alipofika kwenye nyumba iliyokuwa inapakana na gereji alisimama na kujibanza sawa sawa na ua wa michongoma iliyokuwa imezunguka nyumba hii. Alipochungulia aliona mlinzi mmoja anazunguka zunguka upande ule aliokuwa yeye yaani kwa nje ya ukuta uliokuwa umezunguka gereji. Hii ilionyesha kuwa zaidi ya kuwa na walinzi ndani ya gereji hii kulikuwa na walinzi wengine nje. 

Hivi Ozu alikata shauri amvizie huyo mlinzi kwanza. Karibu na alipokuwa amejibanza aliona mti mkavu. Alijivuta taratibu halafu akautupa na ukuaanguka katikati ya ukuta na ua wa gereji na ua wa nyumba ambako yeye alikuwa amejibanza. Yule mtu kusikia kishindo hiki aligeuka na kuja kuangalia ni kitu gani kilikuwa kimeanguka. Alikuja bastola mkononi na akitembea kwa uangalifu sana. Ozu alijibanza akiwa ameinama na kufichwa na kivuli cha michongoma. Yule mtu alipofika karibu aliwasha tochi, akamulika ule mti halafu akamulika upande ule aliokuwepo Ozu lakini alimulika kwa juu hivi hakumuona Ozu ambaye alikuwa tayari kabisa kwa mapambano. Alipogeuka kumulika sehemu nyingine na wakati huo akiwa hatua moja toka pale Ozu alipokuwa amejibanza. Ozu alimrukia na kumpiga karate ya shingo na bila hata kupiga kelele mtu huyo alizirai pale pale. Ozu alimgonga zaidi ili kuhakikisha kuwa asingeweza kuamka masaa yasiyopungua kumi. Alimvuta akamlaza kwenye kivuli cha michongoma akachukua bastola yake na tochi akajiweka tayari kwa pambano jingine.

Akiwa anautawala upande huu wa ukuta, alikwenda mpaka kwenye pembe ya kuelekea nyuma nyuma ya ukuta huu wa ua wa gereji. Alipofika hapa alichungulia akamwona mlinzi mwingine aliyekuwa anazunguka zunguka huku nyuma. Ozu alimpigia mlinzi mluzi wa kumwita. Na huyo mlinzi alifikiria kuwa huyo ni mwenzake akaja mbio mbio. Alipokaribia kabisa na kabla hata hajamwangalia Ozu vizuri, Ozu alimuonyesha kidole atazame kule alikokuwa akionyesha. Mtu huyu alipopotea kuangalia kule tu. Ozu alimpiga karate ya shingo nae akazirai pale pale. Baada ya kumhakikisha kuwa hangeweza kuamka mpaka asubuhi. Ozu alimvutia kwenye shimo la taka lililokuwa karibu, yeye akasonga mbele. Alizunguka kwa nyuma mpaka akafika kwenye pembe ya nyuma na ile ya upande mwingine. 

Huku nako alikuta kuna mlinzi, akamfanyia 'ssss'. Yule mlinzi nae akadhani ni mwenzake alikuja upande ule aliokuwa Ozu mbio mbio. Ozu akajibanza kwenye ukuta akajiweka tayari. Vile vile kwa sababu kwenye kona hii kulikuwa na mwanga kidogo alijibanza kusudi mtu huyu asije akamtambua kabla hajafika karibu. Alipokuwa amekaribia alisimama akafungua mdomo wake kutaka kusema kitu lakini kabla hajasema akashtuka, nafikiri alimtambua mtu huyu hakuwa mlinzi mwenzake. Ozu hakupoteza muda, mtu huyu aliposhtuka tu alimpiga risasi na yule mtu akafa pale pale.

Aliangalia huku na kule kama kulikuwa na walinzi zaidi lakini hakuona mtu. Hivi alijua kutakuwa kumebaki wale walinzi watatu wa mbele ambao alikata shauri asiwagutue ila tu lililobaki kuingia ndani ya ngome ya gereji hii kwa kupanda ukuta wa sehemu hii ya nyuma. Kama nilivyokwisha kukueleza ukuta wa ngome hii ulikuwa kiasi cha mita tisa hivi. Ozu alitafuta mti mgumu kiasi cha kuweza kubeba uzito wake, ili umsaidie katika kupanda ukuta. Kwa ufundi na ujasiri mwingi aliweza kupanda na kushika juu kabisa ya ukuta. Alipokwisha kufanya hivi alisukuma ule mti ukaanguka chini. Alipochungulia ndani ya ngome hii akajikuta anaangalia nyuma ya nyumba na kati ya hii nyumba na ukuta wa ngome kulikuwa na nafasi kubwa ambayo ilikuwa tupu. Sehemu hii haikuwa na mlinzi. Alipokuwa anahakikisha kuwa hakukuwa na hatari yoyote, Alivuta mwili wake wote akalalia tumbo juu kabisa ya ukuta kisha akajining'iniza kwa ndani, halafu akajiachia na kuangukia ndani.

Alianguka kwa kishindo, hivyo upesi sana alikimbia mpaka kwenye ukuta wa nyumba akajibanza na kusikiliza kama angesikia lolote. Ghafla alisikia nyayo zinakuja tokea upande wa kulia wa nyumba. Hivyo alikimbia bila kishindo akaenda kujibanza kwenye pembe hii ambayo nyayo zilikuwa zikisikika zinatoka. Mtu akiwa na bastola na tochi mkononi akajitokeza. Mtu huyu bila kumwona Ozu alimulika mbele yake huku akitembea taratibu na kumpita Ozu. Alipompita tuu Ozu alimrukia akamtia kabali kiasi cha kukata roho, alimlaza taratibu chini, halafu akakaa kimya tena kusikiliza kama kulikuwa na kitu kingine. Aliposikia kimya kwa nje alijiweka tayari kwa mapambano zaidi.

Katikati ya nyumba hii mlikuwa na dirisha moja kubwa. Dirisha hili lilikuwa la vioo na mapazia makubwa ambayo yalifunika dirisha hili kwa ndani. Ndani ya chumba ambacho dirisha hili lilikuwa mlikuwa mnawaka taa, hivi Ozu alihisi, huenda mngekuwa na watu. Alienda mpaja nyuma ya dirisha hili akasikiliza. Alisikia watu wanazungumza. Alipilichunguza dirisha hili lilikuwa limefungwa kwa ndani. Kuona hivi, alivua peke yake ya almasi ambayo alikuwa amepewa na mchumba wake siku waliyochumbiana, akaishika vizuri halafu akaitumia kukata kioo cha dirisha hili. Alikata kipande cha kutosha na kwa uangalifu kisije kikaanguka, alikitoa na kukiweka chini taratibu.

Kisha pole pole alivuta sehemu ndogo ya pazia ambayo ilimwezesha kuona ndani. Ndani aliona watu wawili ambao walikuwa wamekaa kwenye meza wameelekeza migongo yao kwake.Alipoona hivi alivuta pazia zaidi aweze kuona hasa chumba hiki kilikuwa na nini zaidi, akakuta kilikuwa chumba cha simu. Watu hawa walikuwa ni maopereta wa simu na 'radio-call'. Alimsikiliza mmoja wao akizungumza na 'radio-call'na alipomaliza kuzungumza akamwambia mwenzake,

"Nenda kamwambie Papa kuwa mpaka sasa hivi Ozu hajafika hotelini kwake na wala hawajui yuko wapi", Yule mwenzie alisimama na kuondoka. Ozu alisisimkwa aliposikia maneno haya. Aliinua bastola yake ghafla akavuta pazia kwa nguvu yule mtu kugeuka ili kuangalia nini kinatokea Ozu alimpiga risasi katikati ya paji la uso akafa pale pale. Kwa sababu bastola yake ilikuwa na sailensa tukio hili halikuwa na sauti yoyote. Haraka haraka Ozu alipitisha mkono ndani ya sehemu ya kioo aliyoikata akafungua dirisha lote, akapanda na kutumbukia ndani ya ofisi hii ya simu. Kisha alirudisha dirisha halafu akavuta pazia na kuweka sehemu ile katika kawaida yake.

Alipokwisha kufanya hivi aliangalia ofisi hii, mlikuwa na taa mbili moja ilining'inia katikati ya dari na nyingine ilikuwa kwenye ukuta karibu na meza ya kupokelea simu. Ozu alitafuta swichi ya taa hizi akakuta zote ziko karibu na mlango wa kutokea nje. Alienda akajaribu swichi hizi kuona ni ipi inawasha taa ipi. Alipokwisha gundua, alizimisha taa ile ya karibu na meza, kisha akatoa pakiti yake ya sigara mfukoni akaifungua halafu akatoa karatasi la ndani  
linalong'aa kama fedha. Halafu akatoa balubu ya taa hiyo ya mezani akaizungushia karatasi hili la sigara, ambalo alikuwa amelikunja kiasi kwamba ile sehemu ing'aayo ndiyo ilizunguka sehemu yote ya chini ya balubu kisha akairudisha ndani ya soketi yake. 

Mambo yote haya aliyafanywa haraka haraka, huku akimsubiri yule mtu aliyekuwa ametumwa. Ile maiti ya yule mtu aliyempiga risasi alimwinamisha vizuri kwenye meza halafu akaenda kwenye mlango kumsubiri yule mtu mwingine. Haukupita muda mrefu akasikia mtu anakuja akajiweka tayari. Mtu huyo alifungua mlango wa nguvu, na kuingia moja kwa moja. Alipogutuka kuona damu zilizokuwa zimetapakaa mle ndani Ozu alimwekea bastola sikioni akamwambia. "Usijitingishe tafadhali".

Ozu alirudisha mlango. "Papa ni nani?". Ozu aliuliza.

"Ndiye mwenye gereji hii", alijibu yule mtu huku akiwa anatetemeka vibaya sana.

"Yule mtu aliyetekwa amewekwa wapi?"

"Yuko chumba cha mkutano wanamhoji".

Ozu kusikia hivi moyo wake uliingiwa na matumaini kuwa Kofi alikuwa bado yuko hai.

"Sasa utafanya kama nitakavyokuambia la sivyo hayo yaliyomkuta mwenzio, na wewe yatakupata", Ozu alimtisha.

Kwa vile mtu huyu hakuzoea mambo kama haya alikubali amfanyie lolote mtu huyu asije na yeye akauawa, naye alikuwa akiogopa sana kifo. 

"Usiniue mimi nitakufanyia lolote unalotaka.

"Ndani ya chumba cha mkutano mna watu wangapi?"

"Yumo Papa, walinzi wanne na yule mtu waliyemleta.

"Na wewe kazi yako ni nini?"

"Mimi ni karani tu. sijui mambo yoyote ya kupigana, tafadhali usiniue," yule kijana alizidi kuomba, na aliyokuwa akisema ilikuwa ni kweli.

"Walinzi wengine wako wapi?".

"Wako nje, ila mmoja yuko mapokezi".

"Anaweza kumuona mtu akiwa anatokea huku, usinidanganye."

"Hawezi maana yeye analinda mtu asiingie ndani bila ruhusa."

"Sasa wewe na mimi tutatembelea chumba cha mkutano, na tutaingia kwa kufuata sheria za hapa na wewe unazijua. Kumbuka ukijaribu ujanja wowote nitakuua, lakini ukifuata masharti yangu hutapata taabu yoyote."

"Sawa," alijibu yule mtu akiwa bado yuko katika hofu kubwa. Ozu alifungua mlango, alimtanguliza yule mtu kisha akarudisha mlango. Akiwa anashikiria bastola yake mgongoni mwa huyu mtu waliongozana ukumbini kana kwamba hakukuwa na kitu kibaya kati yao. Walipopita vyumba viwili na kufika cha cha tatu, yule mtu akanong'ona, "Chumba chenyewe ni hiki." Ozu alikiangalia kilikuwa kimeandikwa. 

"Chumba cha mkutano".

"Najua mna namna yenu ya kugonga ili kujitambulisha, usije ukagonga vingine unasikia?" Ozu alimweleza.

"Ndiyo", alijibu.

"Haya gonga sasa", Ozu alimwamrisha.

Ndani ya chumba Kofi alikuwa anaendelea kunyukwa. 

"Nimekwambia sasa hivi, ongeza mapigo mara mbili," Papa aliamrisha. Yule mtu aliyekuwa anampiga Kofi, alibadilishana na mwenziwe ili apumzike maana alikuwa naye amechoka. Yule aliyebadilishana naye, alikuwa ni mpigaji stadi zaidi.

"Sema Ozu unafikiri yuko wapi sasa?" Papa alimuuliza Kofi.

"Simjui Kofi na wala sielewi unasema nini!" alijibu Kofi ambaye sasa alikuwa ameanza kupata maumivu na akiwa anatafuta njia ya kuweza kuanzisha sarakasi ya kujiponyesha. Alipoendelea kupigwa alijifanya amesikia uchungu sana na karibu azirai akasema tena. 

"Ime... tosha... imeto... sha nitawaeleza chochote mnachotaka.

"Mwacheni, mwacheni ajibu maswali yangu," Papa aliamru na wakamwachia. 

"Unamjua Ozu?," Papa alimuuliza Kofi. 

"Ndi... ndi... ndiyo," alijibu Kofi huku anatingisha kichwa chake kutuliza akili yake.

"Ni nani".

"Ni... ni... mwenzangu," Kofi alijibu huku anaweka viungo vyake katika hali ya ukakamavu na katika tahadhari ili akipata nafasi kidogo ya kuanzisha rabusha akili zake na mwili uwe tayari.

"Sasa naona tutaelewana, unafikiri sasa hivi yuko wapi?".

"Atakuwa hotelini kwake!"

"Hotelini kwake nimepata habari hajafika, unafikiri atakuwa mahali gani pengine saa hizi?" Kusikia hivi mwili wa Kofi ulisisimkwa zaidi kuona ya kwamba kumbe Ozu naye alikuwa akingojewa kama yeye. Lakini kwa vile mpaka saa hizi alikuwa bado hajafika alifikiri lazima aliona kutekwa kwake nyara na inawezekana atakuwa amempasha habari Robert na huenda Ozu na Robert walikuwa wakifanya mbinu za kumtafuta.

"Itakuwa vigumu kujua maana tuliachana Hoteli Tip Top na akachukua teksi ya kwenda hotelini kwake.

"Una... u... Papa alikatwa kauli na mtu aliyegonga mlango. Mlango uligongwa mara tatu, kitu ambacho Kofi alitambua kuwa ndiyo ilikuwa ishara yao kuonyesha kuwa aliyetaka kuingia alikuwa mmoja wao.

"Kafungue", Papa alimwamrisha mlinzi wake mmoja. Kofi alijiweka vizuri maana kila wakati mlango ulipokuwa ukifunguliwa, ndipo alipokuwa akitafuta mwanya wa kuanzisha sarakasi ya kuweza kujiokoa. Hivi alijiweka tayari kama angeweza kupata mwanya safari hii kuufikia mlango kabla haujafungwa, maana walikuwa kama hatua nne  kutoka waliposimama mpaka kwenye mlango. Yule mlinzi alikwenda akafungua mlango. Kufungua mlango tu Ozu ambaye tayari alikuwa ameshikilia bastola mbili mkononi, alimsukuma yule mtu aliyegonga mlango kwa nguvu sana kiasi kwamba aligongana na yule mlinzi aliyekuja kufungua wote wawili wakaanguka ndani. Ozu alijirusha ndani ya chumba na wakati ule ule akapiga risasi mfululizo na kuweka chumba kizima katika hadhaa, halafu akapiga taa risasi chumba kikawa giza. Kofi ambaye alikuwa tayari tayari alipoona yule mlinzi anagongana na yule mtu aliyegonga mlango, aliwatia mateke wale walinzi waliokuwa karibu naye kisha akarukia pale watu wale walipokuwa wamerukia na kuidaka bastola ya yule mlinzi na kujiviringisha kukwepa risasi zozote ambazo zingekuwa zinamfuata. 

"Wapige risasi", sauti ya wasiwasi ya Papa ilisikika. Papa ambaye alikuwa hategemei kabisa kuingiliwa kiasi hiki kwa kufuatana na ulinzi uliokuwa nje, aliingiwa na hofu. Wale walinzi wa Papa nao hawakutegemea kabisa shambulio kama hili, hivi hofu iliwafanya wachelewe hata kutumia silaha zao vizuri na walipoanza kuzitumia walipiga risasi ovyo bila kujua wanapiga wapi na kwa nini. Ozu alipopiga taa na kuwa giza alikuwa ameisha muona Kofi alikorukia na Kofi naye alikuwa ameshatambua kuwa ni Ozu, hivi shambulio likawa limekamilika. Taa kuzimika katika chumba hiki kuliwafanya wababaike zaidi. Ozu aliwashambulia kwa risasi wale walinzi waliokuwa wamemshikilia Kofi. Wakati Kofi yeye alishambulia kule alikokuwa Papa na walinzi wake. 

Ozu aliwaua walinzi hawa watano na Kofi aliwawahi wale walioanguka pale chini na huku akiendelea kumvizia Papa na walinzi wake wasije huku mlangoni, kwani alichokuwa wanatafuta ni nafasi ya kutoka chumbani humu na hatimaye kutoka ndani ya ngome hii. Papa akitumia ujuzi wake na akiwa ni jasusi maarufu, alijaribu kila njia kuweza kuwazuia watu hawa wasije wakaondoka, kwa kupiga risasi huku na kule katika giza ili kuongeza nazaa ndani ya chumba na wakati ule ule aweze kupata msaada kutoka nje. Jambo hili ndilo vile vile lilikuwa likiwaogopesha Kofi na Ozu, kwa hivi walipopata mwanya tu iliwabidi watoke. Kofi ndiye alijiviringisha kwanza na kurukia sebuleni, huku Ozu akimzuia Papa na walinzi wake kwa risasi nyingi wasije wakapata nafasi ya kumjeruhi Kofi. Kofi naye alipofika sebuleni alikuta kuna walinzi wawili wanakuja mbio sebuleni huku, basi akawawahi mara moja na kuwaua. Akiwa sasa analinda sebule Ozu naye alipata nafasi ya kuruka toka mle mchumbani mpka sebuleni huku risasi za Papa na walinzi wake wawili waliobaki zikimkosakosa. 

Walinzi waliokuwa nje walikimbia kuingia ndani ili kusaidia katika mapambano yaliyokuwa yakiendelea ndani. Kwa sababu kulikuwa hakuna mtu wa kuwaongoza watu hawa, kila mtu alifanya alivyoamua, kiasi kwamba wote walikuwa wanakimbilia ndani walikosikia mlio wa basitola na kujua ya kwamba kulikuwa na mapambano ndani ya chumba. 

"Twede huku," Ozu alimwambia Kofi, alipokuwa tayari amesimama. Walikimbia kwenye chumba kile cha simu huku wakipiga risasi kuzuia Papa na walinzi wake wasitoke mlangoni pa kile chumba na vile vile kuwazuia wale walinzi waliokuwa wanatoka nje. Walipofika kwenye chumba hiki Ozu alimwambia Kofi, "Endelea kuwazuia," Ozu alifungua mlango akaingia ndani, Kofi akabaki amejibanza kwenye mlango huku anajibizana risasi na kundi la Papa. Ozu alienda akafungua dirisha, halafu akamwambia Kofi. "Ruka dirishani halafu panda ukuta," Kofi alikimbia akaruka nje kupitia dirishani. Ozu alienda akawasha taa ile ya karibu na mezani ambayo alikuwa ameifungia karatasi ya kung'aa ya sigara. Alipowasha tu, taa zote za umeme za gereji zililipuka na gereji yote ikawa giza.

"Watatoka nje wazuieni kwa nje, nyuma ya nyumba kwenye dirisha la nje la ofisi ya simu", aliamrisha Papa kwa kelele kubwa. Lakini walikuwa wamechelewam Ozu na Kofi walikwea ukuta kama nyani na kujitupa nje kabisa ya ngome ya 'Garage Papadimitriou'.

Papa akiwa anajigonga ovyo gizani aliingia ndani ya chumba cha simu na kutambua kuwa watu hawa walikuwa wamemzidi maarifa na walikuwa wamekwenda zao.

"Mama yangu mzazi watu hawa wameniadhiri sana lakini wataniona na watajua kwa nini 'BOSS' inaniita 'EXCUTIONER' alitamba Papa.

Ozu na Kofi walikimbia mpaka pale Ozu alipokuwa ameliacha gari alilokuwa ameliiba wakalikuta bado liko pale pale na hakukuwa na mtu wa kulitilia mashaka. Waliingia ndani ya gari wakalitia moto na kuondoka.

"Umefunga kazi takatifu Ozu, bila wewe sasa hivi mimi ningekuwa maiti!" Kofi alimshukuru Ozu.

"Usiseme, bila wewe mimi vile vile nisingetoka ndani humo. Sikutegemea ungekuwa mwepesi katika vitendo kama ulivyokuwa," Walicheka pamoja kwa furaha na kupeana mikono ya kuonyesha wako bega kwa bega.

"Tusirudi mahotelini kwetu, wewe wanakusubiri hotelini kwako mpaka sasa hivi," Kofi alieleza.

"Ala, sasa tutaenda wapi?" Ozu aliuliza.

"Kuna hoteli moja sio hoteli hasa ila ni kijihoteli kinaitwa Hoteli Mazeza; kiko kwenye kona ya mtaa wa Kasavubu na Victoire. Twende pale kijana anayefanyakazi pale ninamfahamu sana maana nilipokuwa mjini hapa mara ya mwisho miezi mitatu iliyopita nilimfanyia msaada fulani ambao aliahidi kuulipa wakati wowote atakaponiona. Tukifika pale mahali atatupatia mahali pa kupumzika mpake kesho. Kazi iliyofanyika leo inatosha," Kofi alishauri.

"Sawa, naona shughuli hii inaanza kuwa tamu. Gari hili nimeliiba hivi twende tukaliache katikati ya magari mengine pale Vatican Klabu, maana sasa hivi klabu hiyo bado watu wanaendelea na starehe. Kutoka pale tutatembea kwa miguu mpaka kwenye hoteli ya rafiki yako," Ozu alishauri. 

"Sawa na tufanye hivyo," Kofi alikubali.

ITAENDELEA 0784296253

Comments

  1. kazi nzuri mkuu,nasubiri kwa usongo haswa

    ReplyDelete
  2. Mkuu unakawisha sana mpaka vinaboa wafwatiliaji, au ungetoa ratiba kua utakua unaziachiaje

    ReplyDelete

Post a Comment

HABARI ZILIZOPITA

HEKAYA ZA ABUNUWASI

HISTORIA YA VITA VYA KAGERA 1978 - 79

PATA HADITHI ZA UPELELEZI ZA KUSISIMUA

HOFU

Vifaa vya Kijeshi vilivyotia fora maonesho ya miaka 50 ya Uhuru